Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Bafu la Mvuke Zamani na Leo

Bafu la Mvuke Zamani na Leo

Bafu la Mvuke Zamani na Leo

KWA karne nyingi watu wa tamaduni mbalimbali wamekuwa na mabafu ya mvuke. Kuna aina nyingi za mabafu ya mvuke kama vile inipi la Wahindi wa Amerika Kaskazini, bania la Warusi, hamman la Waturuki, na mushiburo la Wajapan.

Pia kulikuwa na mabafu ya Roma ya kale yaliyokuwa na chumba chenye joto na chumba cha mvuke. Baadhi ya mabafu maridadi zaidi na yenye kustarehesha ya Waroma ambayo yamechimbuliwa ni yale mabafu ya Caracalla. Yalikuwa na ukubwa wa ekari 28 na yangeweza kutoshea watu 1,600.

Tunakukaribisha uchunguze aina mbili za mabafu ya mvuke ambayo bado yanatumika leo. Moja ni temescal ya Mexico. Na la pili ni sauna ya Wafini, na baada ya kusoma habari hii huenda ukataka kujaribu mabafu hayo!

Bafu la Temescal

Bafu la temescal la Mexico la kabla ya wakati wa utawala wa Hispania, lilitumiwa na Waazteki, Wazapoteki, Wamixteki, na Wamaya kwa ajili ya matibabu na kujitakasa, matambiko, kujifungua, kumzika mtu wa ukoo, na sherehe nyingine za kikabila. Neno temescal latokana na neno la Kinahuatl temazcalli, linalomaanisha “bafu.” Temescal lilikuwa jengo la matofali la mstatili au duara lenye paa la kuba. Mawe ya volkeno yalipashwa moto humo, na mvuke ulitokezwa kwa kurusha aina mbalimbali za chai za mitishamba, kama vile chai ya rosemary na ya mkalitusi, kwenye mawe hayo. Mtu aliyekuwa akioga humo alikuwa akipigwa-pigwa kwa wororo kwa mimea ya matambiko na ya dawa, hatimaye anamwagiliwa maji baridi.

Watawa wa kiume Wahispania walipinga vikali desturi hiyo kwa sababu waliona kwamba haifai kwa wanaume na wanawake kuoga pamoja. Ingawa hivyo, bafu la temescal bado linatumiwa leo katika sehemu fulani za Mexico, hasa kwa ajili ya kuoga, kuponya ugonjwa, au kupata nafuu baada ya kujifungua. Hata hivyo, watu wengi zaidi wangependa kudumisha utamaduni wa nchi hiyo kwa kuhifadhi desturi za kiroho za kale za temescal.

Sauna ya Wafini

Huenda sauna ya Wafini ndilo bafu la mvuke linalojulikana sana. “Sauna” ni neno la Kifini. Sauna imekuwapo kwa miaka 2,000 hivi. Sauna ya kale zaidi ilikuwa na shimo lenye moto ardhini ambalo halikuwa limefunikwa vizuri, lililokuwa katikati au pembeni mwa sauna.Vijumba vya sauna vikaanza kujengwa nje mapema katika karne ya 12 W.K.

Leo nchini Ufini karibu kila nyumba ina sauna iliyofunikwa kwa mbao, ambayo hupashwa moto kwa umeme au kwa kutumia kuni. Sauna zinazopashwa moto kwa kuni zinapatikana kwa wingi vibandani na sehemu za mashambani. Iwe majiko yanatumia umeme au kuni, huwa yamewekelewa mawe. Waogaji huongeza mvuke kwa kuteka maji kwa upawa na kuyamwaga juu ya mawe hayo. Tofauti kuu kati ya sauna ya Wafini na mabafu ya mvuke ya Roma au Uturuki ni kwamba sauna nyingi hufunikwa kwa mbao sikuzote na huwa na viti vya mbao. Kwa kuwa mbao hazipitishi moto vizuri, sauna yaweza kuwa na joto jingi bila waogaji kuunguzwa na viti, au kuta.

Sauna ni sehemu kubwa ya utamaduni wa Wafini hata inakadiriwa kwamba kuna sauna 1 kwa kila Wafini 3. Wafini wengi hutumia sauna mara moja kwa juma. Mara nyingi wengi hutumia sauna kila siku wanapokuwa likizoni kando ya ziwa wakati wa majira ya kiangazi! Kwa kawaida waogaji hutumia sauna yenye joto kisha huogelea kwenye maji baridi ya ziwa. Kwa wale ambao hupenda kufanya hivyo kwa mwaka mzima, kuna sauna za kutosha karibu na maji yaliyoganda, ambapo huwa na shimo katika barafu kwa ajili ya wale ambao wangependa kujitumbukiza humo kifupi.

Manufaa za Afya za Bafu la Mvuke

Kwa muda mrefu, Wafini wamekuwa wakisema kwamba sauna ni nzuri kwa afya. Methali moja ya Kifini husema: “Sauna ni dawa ya maskini.” Kwa kweli, zaidi ya kuwa bafu, sauna pia ilikuwa hospitali ya aina fulani na wadi ya kujifungua mpaka katika karne ya 19.

Kwa kawaida watu hukaa kwenye sauna kwa dakika 10 hadi 15 kukiwa na joto la nyuzi Selsiasi 80 hadi 100. Wengi hutumia sauna, kisha hupumzika au kuoga kabla ya kurudi tena katika sauna. Kwa sababu ya joto, damu huzunguka vizuri zaidi, vitundu kwenye ngozi hufunguka, na takataka kama vile asidi laktiki hutoka mwilini na kumfanya mtu ahisi akiwa safi kabisa. Mara nyingi watu hutumia sauna ili kuondoa maumivu baada ya mazoezi na kutuliza mizio, mafua, na maumivu yanayosababishwa na yabisi kavu. Ijapokuwa kuna maoni tofauti kuhusu manufaa hayo ya afya, watu wanaopenda sauna husema kwamba sauna humfanya mtu ahisi vizuri, akiwa mwepesi na safi. Watu fulani hupenda kutumia sauna mwishoni mwa siku ili wapumzike na kutulia. Wengine huonelea kwamba badiliko la joto na baridi huwatia nguvu na kwa hiyo hupenda kuitumia mchana. *

Sauna zinazidi kupendwa na watu wengi zaidi ulimwenguni pote, hasa katika hoteli na mahali pa michezo. Tahadhari: Kwa kusikitisha, katika nchi fulani neno “sauna” hutumiwa kurejezea madanguro. Kwa hiyo, hakikisha kwamba sauna unayoenda inatumika kwa makusudi yanayofaa.

Katika sehemu fulani sauna hazifanyi kazi vizuri. Kwa mfano, kumwaga maji kwenye jiko ambalo halina mawe ya kutosha kwaweza kutokeza mvuke mwingi ghafula ambao unaweza kudhuru. Pia, maji yanaweza kuingia kwenye moto au nyaya za umeme na kuliharibu jiko. Kwa hiyo, sikuzote hakikisha kwamba maagizo yamefuatwa na sauna hudumishwa ikiwa safi na yenye hewa ya kutosha. Ikiwa kuna sauna inayotimiza matakwa hayo katika ujirani wenu, huenda ukataka kujaribu bafu hilo la kisasa lililoanza zamani za kale.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 14 Ikiwa wewe ni mzee au mjamzito au una matatizo ya moyo, mwone daktari kabla ya kutumia sauna.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Madokezo ya Kutumia Sauna

● Kabla ya kutumia sauna epuka kunywa pombe na kula sana.

● Oga kwanza.

● Kalia taulo.

● Kumbuka kwamba sehemu ya chini haina joto jingi kama sehemu ya juu.

● Badili kiwango cha mvuke kwa kunyunyiza mara kwa mara kiasi kidogo cha maji kwenye mawe yaliyo juu ya jiko.

● Usishindane na waogaji wengine ili kuona ni nani anayeweza kuvumilia joto jingi sana au kukaa katika sauna kwa muda mrefu sana.

● Maliza kwa kuoga kwa maji baridi.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Mabafu ya Caracalla ya Roma

[Hisani]

Courtesy of James Grout/ Soprintendenza Archeologica di Roma

[Picha katika ukurasa wa 21]

Bafu la mvuke la “temescal”