Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Chavuo Balaa au Muujiza?

Chavuo Balaa au Muujiza?

Chavuo Balaa au Muujiza?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

Ah-choo! Kwa mamilioni ya watu, sauti hiyo pamoja na machozi, macho yenye kuwasha, pua inayowasha na kutoa kamasi, huashiria majira ya kuchipua. Kwa kawaida mizio yao hutokana na chavuo zilizojaa hewani. Jarida BMJ (lililokuwa likiitwa British Medical Journal) lakadiria kwamba mtu 1 katika ya watu 6 katika nchi zilizositawi hupatwa na mizio ya chavuo, au mafua ya chavuo. Idadi hiyo haishangazi kwa sababu kuna chavuo nyingi sana za mimea hewani.

Wanasayansi wanakadiria kwamba misitu ya misonobari iliyo katika theluthi moja tu ya Sweden upande wa kusini hutokeza tani 75,000 hivi za chavuo kila mwaka. Mmea mmoja unaoitwa ragweed, ambao huwadhuru sana wakazi wa Amerika Kaskazini wenye mizio ya chavuo, unaweza kutokeza chembe milioni moja za chavuo kwa siku. Chavuo hizo za ragweed zimepatikana kilometa 3 angani na umbali wa kilometa 600 baharini baada ya kupeperushwa.

Lakini kwa nini chavuo huwasababishia watu fulani mizio? Kabla ya kujibu swali hilo, hebu tuzichunguze chavuo na kuona jinsi chembe hizo ndogo zilivyo na umbo la ajabu.

Chembe Ndogo za Uhai

Chavuo, yasema The Encyclopædia Britannica, “hutengenezwa katika chavulio, au sehemu ya kiume, katika mimea inayozaa mbegu na kusafirishwa kwa njia mbalimbali (upepo, maji, wadudu na kadhalika) mpaka kwenye pistili, sehemu ya kike, ambapo chembe za kiume na za kike huungana.”

Katika mimea ambayo huchanua maua, chembe za chavuo huwa na sehemu tatu tofauti—kiini cha mbegu za kiume na tabaka mbili zinazofanyiza ukuta au ganda la chembe. Lile tabaka la nje lililo gumu sana haliharibiki kwa urahisi na linaweza kustahimili asidi, alkali, na hata moto mkali. Hata hivyo, chavuo zilizo nyingi zinaweza kuota kwa siku au majuma machache tu. Lakini, ganda lake gumu linaweza kudumu kwa maelfu ya miaka bila kuoza. Kwa hiyo, chembe za chavuo zaweza kupatikana kwa wingi katika udongo. Kwa kweli wanasayansi wamejifunza mengi juu ya mimea ya dunia kwa kuchunguza chavuo zinazopatikana katika sampuli za udongo zilizotolewa kutoka katika vina mbalimbali.

Mambo ambayo wamejifunza yaweza kuwa sahihi sana kwa sababu ya maumbo ya pekee yanayopatikana kwenye ganda la nje la chembe za chavuo. Ikitegemea aina ya chavuo, ganda laweza kuwa laini, lililokunjamana, lenye alama, au lenye miiba na mafundo. “Kwa hiyo, ili kuzitofautisha, chavuo za kila mmea zaweza kutegemeka kama vile alama za vidole vya binadamu,” asema profesa wa anthropolojia Vaughn M. Bryant, Jr.

Jinsi Ambavyo Mimea Huchavusha

Mara tu chavuo inapoungana na stigma, mwishoni mwa pistili, kemikali huifanya chavuo ivimbe na kutokeza mrija unaoshuka mpaka kwenye chembe za kike. Chembe za kiume zilizo ndani ya chavuo hushuka katika mrija huo hadi kwenye chembe za kike, na kutokeza mbegu. Mbegu inapokomaa, inahitaji tu kuwa katika mazingira yanayofaa ili iote.

Ingawa mimea fulani ambayo huzaa mbegu huwa ya kiume tu au ya kike tu, mimea mingi huwa na chavuo na pia chembe za kike. Baadhi ya mimea hujichavusha yenyewe huku mingine ikichavushana kwa kuhamisha chavuo hadi kwa mimea mingine ya aina yake au ya jamii moja. Mimea ambayo huchavushana “kwa kawaida huepuka kujichavusha yenyewe kwa kuangusha chavuo zake kabla au baada ya sehemu yake yenyewe ya kike kuwa tayari kuzipokea,” yasema Britannica. Mimea mingine huwa na kemikali inayoiwezesha kutofautisha chavuo zake na zile za mmea mwingine wa aina yake. Inapotambua chavuo zake, inazimaliza nguvu, mara nyingi, kwa kuzuia ukuzi wa mrija wa chavuo.

Katika sehemu yenye mimea mbalimbali, hewa inaweza kuwa na mchanganyiko wa chavuo nyingi. Mimea huchujaje chavuo inazohitaji? Mimea fulani hutumia kanuni tata za mwendo wa vitu hewani. Kwa mfano, hebu fikiria misonobari.

Kuvuna Upepo

Sonobari za kiume hukua katika vishada na zinapokomaa, huachilia chavuo nyingi sana hewani. Wanasayansi wamegundua kwamba sonobari za kike kwa kushirikiana na majani yaliyo kama miiba yanayozizingira, huelekeza upepo katika njia ambayo chavuo zilizo hewani huzunguka na kuanguka kuelekea sehemu za kike za sonobari. Katika sonobari za kike magamba hufunguka kidogo na kutengana ili kufunua sehemu hizo.

Mtafiti Karl J. Niklas alichunguza sana jinsi chavuo za msonobari husafiri hewani kwa njia ya ajabu. Aliandika hivi katika gazeti Scientific American: “Uchunguzi wetu unaonyesha kwamba umbo la pekee la sonobari za kila jamii ya mmea huelekeza hewa kwa njia ya pekee . . . Vivyo hivyo, kila aina ya chavuo ina ukubwa, umbo na uzito wa pekee unaoifanya chavuo isafiri hewani kwa njia ya pekee.” Mbinu hizo hufanikiwa kadiri gani? Niklas asema hivi: “Sonobari nyingi tulizochunguza zilichuja chavuo ‘zake’ zenyewe kutoka hewani wala si chavuo za jamii nyingine ya mimea.”

Bila shaka si mimea yote inayochavushwa kwa kuchuja hewa—na hiyo ni habari njema kwa watu wenye mizio! Mimea mingi hutumia viumbe.

Hushawishiwa na Mbochi

Mimea ambayo huchavushwa na ndege, mamalia wadogo, na wadudu mara nyingi hutumia vitu kama kiopoo, miiba, au nyuzi zenye kunata ili kushikiza chavuo kwenye mwili wa kiumbe anayetafuta mbochi. Kwa mfano, nyuki mwenye manyoya huenda akajikuta amebeba chavuo 15,000 mara moja!

Kwa kweli, nyuki ndio wachavushaji wakuu wa mimea inayochanua maua. Mimea hiyo humthawabisha nyuki kwa kumpa mbochi na chavuo ale, naye nyuki hupata protini, vitamini, madini, na mafuta kutoka kwenye chavuo. Katika ushirikiano huo wa ajabu, nyuki wanaweza kutembelea zaidi ya maua 100 katika safari moja, lakini watakusanya chavuo, mbochi, au zote mbili kutoka katika jamii moja tu ya mimea mpaka wawe wamekusanya kiasi cha kutosha au ziishe. Tabia hiyo ya ajabu, ya kisilika huhakikisha kwamba uchavushaji unafanywa ifaavyo.

Hupumbazwa na Maua

Badala ya kutoa mbochi, mimea fulani hutumia udanganyifu mkubwa kuwashawishi wadudu ili waichavushe. Mfano mmoja ni aina ya okidi inayokua Australia Magharibi. Ua la okidi hiyo lina petali ambayo, hata kwa binadamu, hufanana kabisa na nyigu mnene wa kike asiye na mabawa. Ua hilo hata hutoa kemikali inayovutia nyigu wa kiume kama ile ambayo hutolewa na nyigu halisi wa kike! Juu ya nyigu huyo bandia kuna vifuko vyenye kunata vilivyojaa chavuo.

Nyigu wa kiume akivutiwa na harufu ya kemikali hiyo bandia, humkamata nyigu huyo bandia na kujaribu kuruka “naye.” Hata hivyo, anapoondoka, mwendo wake humgeuza yeye pamoja na mwenzake na kumwingiza kwenye vile vifuko vyenye kunata vya chavuo. Baada ya kugundua kosa lake, nyigu wa kiume humwachilia yule nyigu bandia, ambaye huwa ameungana na ua hilo kwa njia inayomwezesha kurudi mahali pake, kisha nyigu huyo wa kiume huruka na kwenda zake, lakini baadaye hujikuta akiwa amepumbazwa tena na ua lingine la okidi. Hata hivyo, yeye huchavusha okidi hiyo kwa chavuo alizobeba kutoka katika ua la kwanza.

Lakini ikiwa manyigu halisi wa kike wanapatikana, manyigu wa kiume huchagua mmoja wao badala ya yule nyigu bandia. Kwa kufaa basi, okidi huchanua maua yake majuma kadhaa kabla ya manyigu wa kike kuibuka kutoka katika hali yao ya kuwa mabuu ardhini, na hivyo maua hayo hufaidika kwa muda.

Mizio Husababishwa na Nini?

Kwa nini watu fulani hupata mizio kutokana na chavuo? Chembe ndogo za chavuo zinapokwama puani, zinanaswa na utando wa kamasi lenye kunata. Kisha huingia kooni na mtu huzimeza au hukohoa na kuzitoa, mara nyingi bila madhara yoyote. Hata hivyo, nyakati nyingine chavuo huchochea mfumo wa kinga.

Tatizo husababishwa na protini ya chavuo. Kwa sababu fulani, mfumo wa kinga wa mtu mwenye mizio huiona protini ya chavuo fulani kuwa tishio. Miili hufanya chembe fulani zinazopatikana mwilini zitoe kiasi kikubwa sana cha histamini. Histamini huifanya mishipa ya damu ilegee na kupitisha vitu kwa urahisi hivi kwamba huvuja umajimaji wenye chembechembe nyingi za kinga. Katika hali za kawaida chembe hizo huhamia mahali penye madhara au ambukizo ambapo husaidia kuondoa wavamizi hatari. Hata hivyo, kwa watu wenye mizio, chavuo huufanya mwili utende kana kwamba kuna ambukizo na kusababisha pua iwashe na kutoa kamasi, tishu zivimbe, na machozi kutoka.

Watafiti huamini kwamba watu hurithi mizio kutoka kwa wazazi wao, hata ingawa huenda mizio hiyo isisababishwe na vitu vilevile. Uchafuzi unaweza pia kutokeza mizio. “Huko Japan uchunguzi ulionyesha kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mizio ya chavuo na kuwa karibu na maeneo yenye hewa iliyojaa chembe za moshi wa dizeli,” likasema gazeti la BMJ. “Uchunguzi wa wanyama unadokeza kwamba chembe hizo huongeza mizio.”

Jambo la kupendeza ni kwamba dawa zinazoitwa antihistamines zinaweza kupunguza matatizo ya watu wenye mizio. * Dawa hizo huzuia athari za homoni ya histamini. Hata hivyo, licha ya kwamba chavuo husumbua, mtu hana budi kustaajabia hekima inayoonekana katika ubuni na usambazaji wa chembe hizo ndogo sana za uhai. Bila chembe hizo, dunia nzima ingekuwa jangwa tu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 29 Zamani, dawa za antihistamines zilikuwa zikisababisha usingizi na kuufanya mdomo ukauke. Dawa za karibuni zaidi zimepunguza athari hizo.

[Mchoro katika ukurasa wa 24, 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Pistili

Chembe ya kike

Kifuko cha chembe za kike

Mrija wa chavuo

Stigma

Chembe ya chavuo

Stameni

Chavulio

Petali

[Hisani]

NED SEIDLER/NGS Image Collection

[Picha katika ukurasa wa 25]

Aina mbalimbali za chavuo zinavyoonekana kwa hadubini

[Hisani]

Pollen grains: © PSU Entomology/PHOTO RESEARCHERS, INC.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Sehemu ya okidi inayofanana na nyigu wa kike

[Hisani]

Hammer orchid images: © BERT & BABS WELLS/OSF

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Pollen grains: © PSU Entomology/PHOTO RESEARCHERS, INC.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Pollen grains: © PSU Entomology/PHOTO RESEARCHERS, INC.