Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Utafiti wa Chembe za Msingi Si kawaida yangu kutoa maelezo juu ya makala zenu, nimezoea makala za Amkeni! zilizoandikwa vizuri sana. Hata hivyo, sina budi kuandika na kusema kwamba zile makala zenye kichwa “Je, Sayansi Imevuka Mipaka kwa Kutumia Chembe za Msingi?” (Novemba 22, 2002) ni kielelezo bora cha makala zilizoandikwa vizuri sana kuhusu habari hiyo ngumu. Vyombo vya habari vimesema mengi kuhusu utafiti wa chembe za msingi na kuifanya habari hiyo iwe ngumu kueleweka. Makala zenu zilieleza mambo waziwazi zikizingatia masuala ya kimaadili na ya kijamii.

K. M., Marekani

Kuathiriwa na Wengine Asanteni sana kwa makala “Vijana Huuliza . . . Je, Vijana Wenzako Wanaweza Kukuathiri Sana?” (Novemba 22, 2002) Sikudhani kamwe kwamba vijana wenzangu wanaweza kuniathiri. Lakini kwetu vijana wengi wanaolewa wakiwa wachanga. Sikuzote nilitaka kuwa mseja kwa muda na kuwa mwanamke wa kiroho. Lakini watu walikuwa wakiniuliza, “Utaolewa lini?” (Nina umri wa miaka 16 tu.) Nikaanza kufikiri kwamba sipaswi kuwa mseja! Makala hii imenisaidia kuona jinsi vijana wanavyoweza kuathiri sana wenzao.

E. A., Marekani

Msaada Wakati wa Mafuriko Asanteni sana kwa makala “Upendo Waonyeshwa Kupitia Kazi Kubwa ya Kutoa Msaada.” (Novemba 22, 2002) Nilishangazwa na hasara kubwa iliyosababishwa na mafuriko huko Houston, Texas. Sikujua hali zenye kusikitisha ambazo ndugu na dada zangu Wakristo walikuwa wakikabili. Kazi ya kutoa msaada iliyofanywa kwa utaratibu imenionyesha jinsi dunia itakavyorudishwa katika hali yenye kupendeza baada ya Har-Magedoni.

M. I., Japan

Maji Machafu Nikiwa msimamizi wa mtambo wa kusafisha maji machafu, nilifurahia sana kusoma makala yenye kichwa “Maji Huenda Wapi?” (Oktoba 8, 2002) Kusafisha maji machafu huokoa maisha ya mamilioni ya watu kutokana na magonjwa. Zamani, homa ya matumbo, kipindupindu, na magonjwa mengine yanayotokana na maji yalikuwa yameenea sana ulimwenguni pote. Siku hizi, maji machafu husafishwa kwa njia ya asili, mara nyingi kwa kutumia kemikali kidogo au kwa kutotumia kemikali. Katika mtambo wangu, urujuani hutumiwa kuangamiza viini kwenye maji machafu yaliyosafishwa. Asanteni kwa kuonyesha jinsi maji machafu yanavyosafishwa ili kuokoa uhai.

E. P., Marekani

Kaharabu Nilithamini sana makala yenye kichwa “Kunaswa Katika Tone la Manjano.” (Septemba 22, 2002) Lazima nikiri kwamba sikuwa nikishughulika kamwe na kaharabu. Lakini tangu niliposoma makala hiyo, kila wakati ninapopita duka la vito, siwezi kujizuia kutazama kaharabu hiyo ya ajabu kwa makini sana—kitu ambacho nilikuwa nikifikiri ni cha kawaida na kisichovutia.

F. L., Ufaransa