Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Usisahau Kubeba Mwavuli!”

“Usisahau Kubeba Mwavuli!”

“Usisahau Kubeba Mwavuli!”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

KWA kawaida watu wengi hubeba mwavuli nchini Uingereza. Mtu hawezi kujua ikiwa kutanyesha au la. Tunapoondoka nyumbani, sisi hukumbushana, “Usisahau kubeba mwavuli!”—kisha huenda tunausahau katika basi au katika garimoshi au dukani. Naam, sisi huipuuza miavuli kwa kuwa tunaweza kununua mingine. Lakini zamani miavuli haikuwa ikipuuzwa.

Historia ya Pekee

Yaonekana kwamba miavuli ya kwanza haikuhusianishwa na mvua. Ilitumiwa na watu mashuhuri tu, nayo ilionyesha cheo na heshima. Vinyago na michoro ya maelfu ya miaka iliyopita kutoka Ashuru, Misri, Uajemi, na India huonyesha watumishi wakiwa wamebeba miavuli wakiwafunika watawala ili kuwakinga kutokana na jua. Katika Ashuru mfalme tu ndiye angeweza kuwa na mwavuli.

Mwavuli umewakilisha mamlaka sikuzote, hasa huko Asia. Cheo cha mtawala kiliongezeka kulingana na idadi ya miavuli aliyokuwa nayo, kama ilivyoonyeshwa na mfalme wa Burma aliyeitwa Bwana wa Miavuli 24. Nyakati nyingine idadi ya matabaka ilikuwa muhimu. Mwavuli wa maliki wa China ulikuwa na matabaka manne, nao wa mfalme Siam ulikuwa na matabaka saba au tisa. Hata leo bado mwavuli ni ishara ya mamlaka katika nchi fulani za Mashariki na za Afrika.

Miavuli ya Kidini

Mapema katika historia, mwavuli ulihusianishwa na dini. Wamisri wa kale waliamini kwamba mungu wa kike aitwaye Nut alikuwa akiifunika dunia nzima kwa mwili wake, kama tu mwavuli. Kwa hiyo watu walitembea chini ya miavuli yao ili awakinge. Nchini India na China, watu waliamini kwamba mwavuli uliofunguliwa uliwakilisha mbingu. Wabudha wa mapema waliutumia kama ishara ya Buddha, na miavuli iliwekwa juu ya kuba za majengo yao ya ukumbusho. Miavuli hutumiwa katika dini ya Hindu pia.

Miavuli ilienea hadi Ugiriki kufikia mwaka wa 500 K.W.K., ambapo ilitumiwa kufunika sanamu za miungu kwenye sherehe za kidini. Watumishi waliwafunika wanawake Waathene kwa miavuli, lakini ni wanaume wachache tu waliokuwa wakiitumia. Desturi hiyo ikaenea kutoka Ugiriki hadi Roma.

Kanisa Katoliki lilitumia mwavuli pamoja na mavazi yake rasmi ya sherehe. Papa akaanza kuonekana akiwa amefunikwa kwa mwavuli wa hariri wenye mistari myekundu na ya manjano, huku makadinali na maaskofu wakiwa na miavuli ya zambarau au ya kijani kibichi. Mpaka leo hii makanisa yana kiti cha papa chenye mwavuli wa rangi maalum za papa. Kardinali anayeongoza kanisa baada ya papa mmoja kufa na kabla ya mwingine kuchaguliwa huwa pia na mwavuli wa kumtambulisha wakati huo.

Kinga ya Jua Yawa Kinga ya Mvua

Wachina au huenda wanawake wa Roma ya kale ndio walioanza kuipaka miavuli yao ya makaratasi mafuta na nta ili isiharibiwe na mvua. Hata hivyo, watu wa Ulaya waliacha kutumia miavuli ili kujikinga na jua au mvua mpaka katika karne ya 16, wakati ambapo Waitaliano, na baadaye Wafaransa walipoanza tena kuitumia kwa kusudi hilo.

Kufikia karne ya 18, wanawake nchini Uingereza walianza kuibeba miavuli, ingawa bado wanaume walikataa kuibeba kwa kuwa waliiona kuwa isiyo ya lazima na ya kike. Wenye mikahawa tu ndio walioitumia kwa kuwa waliona manufaa ya kuwa na miavuli ili kuwakinga wateja kutokana na hali mbaya ya hewa wanapoelekea kwenye magari yao. Makasisi pia waliiona kuwa muhimu sana kwenye nyua za makanisa walipokuwa wakiongoza mazishi wakati wa mvua.

Msafiri na mfadhili Jonas Hanway ndiye aliyebadili matumizi ya miavuli nchini Uingereza. Inasemekana kwamba yeye ndiye mwanamume aliyekuwa na ujasiri wa kubeba mwavuli hadharani jijini London. Baada ya kuwaona wanaume wakiitumia alipokuwa katika safari zake za ng’ambo, aliazimia kuvumilia dhihaka za madereva wa magari ambao walikuwa wakimrushia kimakusudi maji ya matope walipokuwa wakimpita njiani. Hanway alionekana akiwa ameubeba mwavuli wake kwa kawaida kwa miaka 30, na kufikia wakati alipokufa mwaka wa 1786, wanaume na wanawake walikuwa wakifurahia kuibeba miavuli yao.

Haikuwa rahisi kutumia miavuli ya mvua wakati huo. Miavuli hiyo ilikuwa mizito, mikubwa, na isiyopendeza. Hariri au turubali iliyopakwa mafuta na viunzi na mipini yake ya mianzi au ya mifupa ya nyangumi iliifanya kuwa migumu kufungua ilipokuwa imeloa, nayo ilikuwa ikivuja. Hata hivyo, bado ilizidi kupendwa na wengi hasa kwa kuwa ilikuwa rahisi kununua mwavuli kuliko kukodi gari wakati mvua iliponyesha. Kukawa na ongezeko la watengenezaji wa miavuli na maduka ya miavuli, nao wenye kuibuni wakaanza kuboresha mitindo yake. Katikati ya karne ya 19, Samuel Fox aliunda mwavuli aina ya Paragon, ambao ulikuwa na kiunzi cha feleji, chepesi lakini kigumu. Vitambaa vyepesi kama vile hariri, pamba, na kitani kilichopakwa nta vikaanza kutumiwa badala ya vile vitambaa vya kale vya turubali. Huo ukawa mwavuli wa kwanza wa kisasa.

Kifaa cha Mapambo

Mwavuli ukawa maarufu sana kama kifaa cha mapambo cha wanawake Waingereza wanaopenda mitindo. Kadiri mitindo ilivyobadilika miavuli yao midogo ikazidi kuwa mikubwa na yenye vitambaa vya hariri na atlasi zenye rangi mbalimbali nyangavu. Mara nyingi ilifanana na nguo zao nayo ilirembeshwa kwa lesi, matarizi, utepe, na hata manyoya. Katika karne ya 20, hakuna mwanamke yeyote mstaarabu aliyetaka kutunza ngozi yake ambaye angeonekana bila mwavuli.

Katika miaka ya 1920, watu wakaanza kupenda ngozi iliyobadilika rangi kwa sababu ya jua, na hivyo wakaacha kutumia miavuli. Kisha wanaume wangwana wa jijini wakaanza kuvaa kofia na kubeba mwavuli mweusi, uliotumiwa pia kama bakora ya kutembelea kwa madaha.

Baada ya vita ya pili ya ulimwengu, tekinolojia mpya iliboresha mitindo ya miavuli, kama vile ile miavuli midogo ambayo hukunjika, pamoja na vitambaa vya nailoni, poliesta, na plastiki visivyoweza kupenywa na maji. Bado kuna maduka machache ambayo hutengeneza kwa mikono miavuli mizuri ya bei ghali. Lakini leo, viwanda hutengeneza kwa wingi kwa gharama ya chini miavuli yenye rangi na ukubwa mbalimbali, kama vile miavuli mikubwa inayoweza kuwafunika watu wawili na ile inayoweza kutumiwa katika bustani na miavuli midogo ya sentimeta 15 inayokunjika na kutoshea vizuri ndani ya kibeti.

Ingawa wakati mmoja miavuli ilionwa kuwa kitu cha starehe na cha watu wenye vyeo, siku hizi miavuli inaweza kupatikana kwa bei rahisi, nayo ni baadhi ya vitu ambavyo hupotezwa sana. Miavuli husaidia sana kukabiliana na hali ya hewa popote ulimwenguni, na katika nchi nyingine watu wameanza tena kuitumia kujikinga na jua kwa kuwa maonyo mengi yanatolewa kuhusu hatari za miale ya jua. Kwa hiyo unapoondoka nyumbani leo huenda wewe pia utakumbushwa: “Usisahau kubeba mwavuli!”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]

Kununua na Kuutunza Mwavuli

Amua ikiwa unataka mwavuli ambao ni rahisi kubeba au mwavuli wa kudumu. Mwavuli mdogo unaokunjika ambao unatoshea katika mfuko mkubwa una viunzi vichache lakini hauwezi kustahimili upepo mkali. Kwa upande mwingine, huenda mwavuli wa kawaida usiokunjika ukagharimu pesa nyingi zaidi lakini kwa kawaida hustahimili hali ya hewa na hudumu kwa muda mrefu. Kwa kweli, mwavuli mzuri unaweza kudumu kwa muda mrefu. Wowote ule utakaochagua, ulinde usipatwe na kuvu au kutu kwa kuuacha ukiwa umefunguka ili ukauke kabisa kabla ya kuufunga tena. Kuutia kwenye kifuko cha nje kutaudumisha ukiwa safi.

[Picha katika ukurasa wa 19]

Mtumishi amfunika mfalme Mwashuru

Mwanamke wa Ugiriki ya kale akiwa na mwavuli

[Hisani]

Drawings: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck

[Picha katika ukurasa wa 20]

Mwavuli wa miaka ya 1900

[Hisani]

Culver Pictures