Je, Hali ya Hewa Imebadilika?
Je, Hali ya Hewa Imebadilika?
“WAINGEREZA wawili wanapokutana, wao huanza kuzungumzia hali ya hewa.” Hivyo ndivyo mwandishi maarufu Samuel Johnson alivyosema kimzaha. Hata hivyo, katika miaka ya hivi majuzi, zaidi ya kuzungumzia hali ya hewa, watu ulimwenguni pote wamehangaishwa sana nayo. Kwa nini? Kwa sababu, inazidi kubadilika-badilika.
Kwa mfano, katika majira ya kiangazi ya mwaka wa 2002, bara la Ulaya lilikumbwa na mvua kubwa iliyoandamana na pepo kali. Mvua hiyo ilisababisha “mafuriko makubwa zaidi kuwahi kutokea katika Ulaya ya kati kwa zaidi ya karne moja.” Hebu ona habari zifuatazo:
AUSTRIA: “Mikoa ya Salzburg, Carinthia, na Tirol ndiyo iliyokumbwa hasa na mvua kubwa iliyoandamana na pepo kali. Barabara nyingi zilifunikwa na matope yaliyorundamana kufikia kimo cha meta 15. Katika kituo cha gari-moshi cha Südbahnhof huko Vienna, mvua ya ngurumo na radi ilisababisha msiba wa gari-moshi na watu kadhaa walijeruhiwa.”
JAMHURI YA CHEKI: “Hali ilikuwa mbaya sana huko Prague. Lakini imekuwa mbaya zaidi mikoani. Zaidi ya watu 200,000 wamehama makwao. Miji mingi imefurikwa.”
RUMANIA: “Watu kumi na wawili hivi wamekufa kutokana na dhoruba hizo tangu katikati ya mwezi wa Julai.”
UFARANSA: “Watu 23 wamekufa, 9 hawajapatikana, na wengi wameathiriwa sana . . . Watu watatu walikufa kutokana na radi Jumatatu. . . . Mzimamoto mmoja alikufa baada ya kuwaokoa wenzi wa ndoa ambao walipelekwa na maji wakiwa ndani ya gari lao.”
UJERUMANI: “Katika historia yote ya Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani, watu hawajawahi kuhama miji na vijiji kama katika ‘furiko hili kubwa kushinda yote katika miaka 100 iliyopita.’ Maelfu ya wakazi wamehama miji ya kwao. Wengi wamehama ili kuhepa hatari. Wengine walihamishwa kwa mashua au helikopta muda mfupi tu kabla ya mafuriko kutokea.”
URUSI: “Angalau watu 58 walikufa kwenye fuo za Bahari Nyeusi . . . Magari na mabasi 30 hivi bado yamo baharini, na haiwezekani kuyafikia kwani onyo limetolewa kwamba kutakuwa na dhoruba nyingine.”
Si Ulaya Peke Yake
Mnamo Agosti 2002, gazeti la Süddeutsche Zeitung liliripoti hivi: “Mvua kubwa na dhoruba zimesababisha misiba huko Amerika Kusini, Asia, na Ulaya. Siku ya Jumatano, angalau watu 50 walikufa kutokana na maporomoko ya ardhi huko Nepal. Watu wanane walikufa kutokana na tufani kusini mwa China na mvua kubwa ilinyesha katikati ya China. Mafuriko yaliyotukia China yalifanya maji ya Mto Mekong yafikie kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miaka 30 na kufunika zaidi ya nyumba 100 kaskazini-mashariki mwa Thailand. . . . Nchini Argentina, angalau watu watano walikufa maji baada ya mvua kubwa kunyesha. . . . Zaidi ya watu elfu moja wamekufa kutokana na dhoruba ambazo zimekumba China katika majira ya kiangazi.”
Ingawa sehemu nyingi za ulimwengu zilikumbwa na mafuriko, Marekani ilikumbwa na ukame. Iliripotiwa hivi: “Watu kotekote nchini wana wasiwasi kuhusu kupungua au kukauka kwa maji visimani, kupungua kwa maji mitoni, na kuongezeka kwa mioto ya misitu zaidi ya mara mbili. Kwa sababu ya kukauka kwa mimea na maeneo ya malisho, uhaba wa maji ya kunywa, mioto ya misitu na pepo kali za vumbi, wataalamu wanatabiri kwamba ukame wa mwaka wa 2002 utasababisha hasara ya mabilioni ya dola.”
Sehemu fulani za kaskazini mwa Afrika zimekumbwa sana na ukame tangu miaka ya 1960. Kulingana na ripoti mbalimbali, “mvua ilipungua kwa asilimia ishirini hadi arobaini na tisa kuliko ilivyokuwa katika miaka hamsini ya kwanza ya karne ya 20, na hivyo kusababisha njaa kubwa na vifo.”
Hali ya hewa inayoletwa na El Niño—ambayo husababishwa na kuongezeka kwa joto la maji ya upande wa mashariki wa Bahari ya Pasifiki—husababisha mafuriko mara kwa mara, na hali ya hewa isiyo ya kawaida huko Amerika Kaskazini na Kusini. * Shirika la habari la CNN linaripoti kwamba El Niño ya mwaka wa 1983/1984 “ilisababisha zaidi ya vifo 1,000 na misiba mingine karibu katika mabara yote na kuharibu mali na mifugo yenye thamani ya dola bilioni 10.” Hali hiyo ya hewa imekuwa ikitokea kwa ukawaida (kila baada ya miaka minne hivi) tangu ilipotambulishwa mara ya kwanza katika karne ya 19. Lakini wataalamu wengine wanaamini kwamba “El Niño itatokea mara nyingi zaidi” wakati ujao.
Makala moja iliyochapishwa na shirika la Marekani la usimamizi wa anga linaloitwa NASA inasema hivi: ‘Mara nyingi hali ya hewa “isiyo ya kawaida” ambayo imekuwepo, yaani, joto lisilo la kawaida na mvua inayonyesha wakati usiofaa, inasababishwa na mabadiliko ya kawaida ya hali ya hewa katika maeneo mbalimbali.’ Hata hivyo, kuna mambo yanayoonyesha kwamba huenda kuna tatizo kubwa. Shirika la mazingira la Greenpeace linatabiri hivi: “Hali mbaya za hewa kama vile tufani zenye nguvu zaidi na mvua kubwa zitaendelea kusababisha misiba kotekote duniani. Hali mbaya zaidi za ukame na mafuriko makubwa zaidi yatabadili kabisa mandhari ya Dunia na kusababisha uharibifu wa maeneo ya pwani na misitu.” Je, madai hayo ni ya kweli? Na ikiwa ni ya kweli, ni nini kinachosababisha ‘hali hizo mbaya za hewa’?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 14 Ona makala “El Niño Ni Nini?” katika gazeti la Amkeni! la Machi 22, 2000.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Mafuriko nchini Ujerumani (juu) na katika Jamhuri ya Cheki (kushoto)