Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Dhuluma Baadhi ya Visababishi na Matokeo

Dhuluma Baadhi ya Visababishi na Matokeo

Dhuluma Baadhi ya Visababishi na Matokeo

KWA NINI mtoto huanza kuwadhulumu wengine? Ikiwa umewahi kudhulumiwa, huenda ukasema kwamba, “Hata sababu iwe nini hakuna udhuru wa kumdhulumu mwingine.” Na huenda maoni yako ni sawa. Lakini kuna tofauti kubwa kati ya udhuru na sababu. Sababu zinazomfanya mtoto awadhulumu wengine hazifanyi tabia yake mbaya ikubalike, lakini zinaweza kutusaidia kuielewa. Na ni muhimu sana kuelewa kwa nini anatenda hivyo. Kwa nini?

Methali moja ya kale inasema hivi: “Ufahamu wa mtu hakika hupunguza hasira yake.” (Mithali 19:11, NW) Tukikasirishwa na tabia ya mdhalimu tunaweza kukata kauli kimakosa, na hivyo kufadhaika sana na hata kumchukia. Lakini tukiielewa tabia yake tunaweza kupunguza hasira yetu. Hilo linaweza kutusaidia kuwa na maoni yanayofaa tunapotafuta masuluhisho. Kwa hiyo, hebu tuchunguze visababishi kadhaa vya tabia hiyo mbaya.

Kwa Nini Watu Huwadhulumu Wengine?

Wadhalimu wengi huiga mfano mbaya wa wazazi wao au walipuuzwa kabisa na wazazi wao walipokuwa watoto. Wengi wana wazazi ambao si wachangamfu, wasiojali, au ambao wamewawekea watoto wao mfano mbaya kwa kushughulikia matatizo kwa hasira na jeuri. Huenda watoto ambao wamelelewa kwa njia hiyo wasione kwamba wanawadhulumu wengine kwa maneno na matendo yao ya jeuri. Huenda hata wakafikiri kwamba tabia yao ni sawa kabisa.

Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 16 ambaye alidhulumiwa na baba yake wa kambo na vilevile na wanafunzi wenzake shuleni, alibadilika kuwa mdhalimu alipofika darasa la saba. Anasema hivi: “Nilikuwa na hasira nyingi; nilimdhulumu mtu yeyote tu. Kuhisi uchungu si jambo dogo. Mtu anapoumizwa, yeye hutaka kuwaumiza wengine pia.” Ijapokuwa kwa kawaida wasichana wanaowadhulumu wengine hawatumii jeuri, wao huwadhulumu wengine kwa sababu wamekasirika. *

Shule nyingi huwa na wanafunzi wengi ambao wamelelewa kwa njia zinazotofautiana sana. Kwa kusikitisha, watoto fulani huwa wajeuri kwa sababu wamefundishwa nyumbani kwamba kuwatisha wengine na kuwatusi ndizo njia bora za kupata wanachotaka.

Inasikitisha kwamba mara nyingi njia hizo hufaulu. Shelley Hymel, ambaye ni mshauri msaidizi kwenye Chuo Kikuu cha British Columbia, Kanada, amechunguza tabia za watoto kwa miaka ishirini. Anasema hivi: “Kuna watoto ambao wanajua jinsi ya kupata wanachotaka, na inasikitisha kwamba wao hufanikiwa wanapowadhulumu wengine. Wao hufaulu kupata wanachotaka, yaani, wanapata mamlaka, hadhi na umashuhuri.”

Ukosefu wa mwongozo ni jambo jingine linalofanya dhuluma iongezeke. Watu wengi wanapodhulumiwa huhisi kwamba hakuna mtu anayeweza kuwasaidia na inasikitisha kwamba hali huwa hivyo mara nyingi. Debra Pepler, mkurugenzi wa Kituo cha LaMarsh cha Utafiti Kuhusu Jeuri na Masuluhisho ya Ugomvi kwenye Chuo Kikuu cha York huko Toronto, alifanya uchunguzi kuhusu wanafunzi wa shule na akagundua kwamba walimu hutambua na kukomesha karibu asilimia 4 tu ya visa vya dhuluma.

Hata hivyo, Dakt. Pepler anaamini kwamba ni muhimu kukomesha hali hiyo. Anasema hivi: “Watoto hawawezi kutatua tatizo hilo kwa sababu linahusu nguvu, na mdhalimu hupata nguvu zaidi kila mara anapomdhulumu mtu.”

Kwa hiyo, kwa nini visa vingi vya dhuluma haviripotiwi? Ni kwa sababu wale wanaodhulumiwa huamini kwamba wakiripoti jambo hilo, huenda mambo yakawa mabaya zaidi. Hivyo, vijana wengi huwa na wasiwasi kwa kadiri fulani na hukosa usalama katika miaka yao ya shule. Ni nini matokeo ya hali hiyo?

Athari za Kimwili na Kihisia

Ripoti ya shirika moja la wataalamu wa akili huko Marekani inasema kwamba kila siku zaidi ya watoto 160,000 hukosa kwenda shule kwa sababu wanaogopa kudhulumiwa. Huenda wale wanaodhulumiwa wakaacha kuzungumza juu ya shule au juu ya somo fulani au shughuli fulani hususa ya shuleni. Huenda wakajaribu kuchelewa kwenda shuleni kila siku au kuhepa masomo fulani au hata kutoa udhuru ili wasiende shuleni.

Watoto wanaodhulumiwa wanaweza kutambuliwaje? Huenda wakanuna, wakakasirika haraka, wakavunjika moyo, wakaonekana wachovu, au wakajitenga. Wanaweza kuwadhulumu watoto wenzao nyumbani au marafiki zao. Watoto wanaoshuhudia wengine wakidhulumiwa huathiriwa pia. Hali hiyo huwaogopesha sana na hudhoofisha uwezo wao wa kujifunza.

Hata hivyo, gazeti Pediatrics in Review lasema hivi: “Tokeo baya zaidi la dhuluma miongoni mwa wale waliodhulumiwa na katika jamii ni jeuri, na hiyo inatia ndani kujiua na kuwaua wengine. Watoto wanaodhulumiwa huhisi kwamba hawana nguvu kabisa hivi kwamba wengine wao huamua kujiua au kuwaua wengine.”

Dakt. Ed Adlaf, mtafiti na profesa wa afya ya umma kwenye Chuo Kikuu cha Toronto, anasema kuwa “kuna uwezekano mkubwa kwamba wadhalimu au wanaodhulumiwa wataumia kihisia sasa na baadaye.” Katika mwaka wa shule wa 2001, zaidi ya wanafunzi 225,000 huko Ontario walihojiwa, na kati ya robo na thuluthi ya wanafunzi hao walidhulumiwa au kuwadhulumu wengine. Mwanafunzi 1 kati ya 10 alikuwa amefikiria sana kujiua.

Mtu anapodhulumiwa sana anaweza kuacha kujiamini, kupatwa na magonjwa hatari, na hata kushindwa kuendelea na kazi. Huenda watu wanaodhulumiwa wakaumwa na kichwa, wakakosa usingizi, wakawa na wasiwasi, na hata kushuka moyo. Wengine hupata ugonjwa fulani unaosababishwa na mfadhaiko. Ijapokuwa mtu anapoumizwa kimwili anaweza kuhurumiwa sana, mambo huwa tofauti anapoumizwa kihisia. Watu hawawezi kujua kwa urahisi kwamba anaumia. Kwa hiyo badala ya kumhurumia, huenda marafiki na watu wa familia wakachoshwa na malalamiko yake.

Wadhalimu pia huathiriwa na dhuluma. Wasipokomeshwa wanapokuwa wadogo, huenda wakawadhulumu wafanyakazi wenzao wanapokuwa watu wazima. Miradi fulani ya uchunguzi inaonyesha kwamba watu waliokuwa wadhalimu walipokuwa watoto walikuwa na tabia hiyohiyo hata walipokuwa watu wazima. Pia, kuna uwezekano mkubwa kwamba watakuwa wahalifu.

Jinsi Familia Inavyoathiriwa

Dhuluma inayotukia kazini huathiri muungano na amani katika familia. Mtu anayedhulumiwa kazini anaweza kuchochewa kuwaumiza watu wa familia yake na wasielewe kwa nini anafanya hivyo. Isitoshe, hilo linaweza kumfanya mwenzi wake wa ndoa au mtu mwingine katika familia hiyo amuunge mkono na kujaribu kulipiza kisasi isivyofaa. Kwa upande mwingine, mwenzi wake wa ndoa anaweza kumlaumu kwamba amesababisha tatizo hilo. Visa hivyo vya dhuluma vinapoendelea, hata wenzi ambao hapo awali walijitahidi kusaidia hushindwa kuvumilia hali hiyo. Kadiri miaka inavyopita, familia hizo hukabili uwezekano mkubwa wa kuvunjika.

Nyakati nyingine, dhuluma inaweza kusababisha mtu apoteze kazi na kukosa riziki, kutengana, talaka, au hata kujiua. Kati ya nusu na thuluthi mbili ya Waaustralia waliodhulumiwa wakiwa kazini walisema kwamba jambo hilo liliathiri mahusiano yao pamoja na watu walio karibu sana nao kama vile wapenzi wao, wenzi wao wa ndoa, au familia zao.

Hasara za Dhuluma

Dhuluma inayotukia kazini huwasababishia waajiri hasara. Mtu anayewadhulumu wengine kazini anaweza kuwa mwajiri anayesema mambo ya kuumiza au mfanyakazi anayepanga njama, na anaweza kuwa mwanamume au mwanamke. Watu wa aina hiyo huwadhibiti wengine kupita kiasi, huzingatia mambo madogo-madogo, na kuwadharau wengine kwa kusema mambo ya kuwavunja moyo au kwa kuwachambua kila wakati, na mara nyingi huwaaibisha mbele ya watu. Mara nyingi wadhalimu hawatambui ujeuri wao wala kuomba radhi kwa ajili ya tabia yao. Mara nyingi wao huwadhulumu wafanyakazi wenye bidii, waaminifu, na wanaopendwa sana na wafanyakazi wengine.

Kwa kawaida wafanyakazi wanaodhulumiwa hawafanyi kazi vizuri. Wafanyakazi wengine wanaoshuhudia dhuluma hiyo huathiriwa pia na hushindwa kufanya kazi vizuri. Dhuluma inaweza kuwafanya wafanyakazi wasiwe waaminifu kwa mwajiri wao na wasifanye kazi kwa bidii. Ripoti moja inasema kwamba dhuluma husababisha hasara ya dola bilioni tatu kila mwaka katika Muungano wa Uingereza. Na inasemekana kwamba tabia hiyo husababisha zaidi ya asilimia 30 ya magonjwa yanayotokana na mfadhaiko.

Ama kweli, dhuluma huathiri watu ulimwenguni pote. Lakini, je, kuna jambo linaloweza kufanywa ili kudhibiti na kukomesha tatizo hilo?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Kwa kawaida, wasichana huwadhulumu wenzao kwa kujitenga nao na kueneza uvumi. Hata hivyo, inaonekana sasa wasichana wengi wanatumia jeuri pia.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Inasikitisha kwamba dhuluma ni jambo la kawaida kazini

[Picha katika ukurasa wa 7]

Watu wanaodhulumiwa kila wakati wanaweza kufadhaika na kuhisi upweke