Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Dhuluma Tatizo la Ulimwenguni Pote

Dhuluma Tatizo la Ulimwenguni Pote

Dhuluma Tatizo la Ulimwenguni Pote

“Ukija shuleni kesho, tutakuua.” —Mwanafunzi anayeitwa Kristen huko Kanada alipokea tisho hilo alipopigiwa simu na msichana ambaye hakutaja jina lake. *

“Kwa kawaida siathiriwi sana kihisia, lakini mambo yalizidi kiasi cha kwamba sikutaka kwenda shuleni. Niliumwa na tumbo, na kila asubuhi baada ya kula nilitapika.”—Hiromi, mwanafunzi huko Japan, anaeleza jinsi alivyodhulumiwa.

JE, UMEWAHI kudhulumiwa? Wengi wetu tumedhulumiwa, angalau wakati fulani. Huenda ni shuleni au kazini au hata nyumbani, ambapo dhuluma imezidi sana siku hizi. Kwa mfano, chanzo kimoja cha habari huko Uingereza kinakadiria kwamba asilimia 53 ya watu wazima huambiwa maneno yanayoumiza na wapenzi wao au wenzi wao wa ndoa. Wadhalimu na watu wanaodhulumiwa wanaweza kuwa wa kike au wa kiume, au watu wa tabaka lolote lile.

Ni nini maana ya kudhulumiwa? Mara nyingi dhuluma huhusisha matukio mengi madogo-madogo ambayo hufanywa kwa muda fulani bali si tukio moja au matukio machache tu. Dan Olweus, ambaye ni mtaalamu wa akili na mwanzilishi wa uchunguzi kuhusu dhuluma, anasema kwamba kwa kawaida dhuluma inahusisha kufanya ujeuri kimakusudi na kuwadhulumu watu wanyonge waziwazi.

Huenda ufafanuzi wa neno dhuluma hauhusishi aina zote za dhuluma, lakini limefafanuliwa kuwa “kutaka kumuumiza mtu mwingine kimakusudi na kumfadhaisha.” Yule anayedhulumiwa hufadhaika anapotendewa vibaya au hata kwa sababu anaogopa yale atakayotendewa. Matendo hayo ni kama vile kumdhihaki, kumchambua kila wakati, kumtusi, kumsengenya, na kumshurutisha afanye mambo asiyoweza kufanya.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 4.

Kristen, msichana aliyetajwa mwanzoni, alidhulumiwa na wanafunzi wenzake kwa miaka mingi. Alipokuwa katika shule ya msingi, wanafunzi waliomdhulumu walikuwa wakitia chingamu kwenye nywele zake, walikuwa wakimfanyia mzaha kuhusu sura yake, na kumtisha kwamba wangempiga. Alipokuwa katika shule ya sekondari, mambo yalizidi kiasi cha kwamba alipokea vitisho kupitia simu. Sasa akiwa na umri wa miaka 18, anasema hivi kwa masikitiko: “Mtu huenda shuleni kusoma, bali si kuteswa au kutishwa kwamba atauawa.”

Mtaalamu mmoja wa akili anasema hivi: ‘Watu fulani hujisikia vizuri wanapomwaibisha mtu mwingine. Hilo ni jambo la kuhuzunisha lakini la kawaida katika mahusiano ya wanadamu.’ Tabia hiyo inapozidi, huenda ikamfanya yule anayetendewa hivyo kulipiza kisasi kwa jeuri na hata kusababisha msiba. Kwa mfano, mfanyakazi mmoja wa kusafirisha abiria aliyekuwa na tatizo la usemi, alidhihakiwa na kudhulumiwa sana hivi kwamba hatimaye aliwaua wafanyakazi wenzake wanne halafu akajipiga risasi.

Dhuluma Iko Ulimwenguni Kote

Ulimwenguni kote watoto wenye umri wa kwenda shule hukabili dhuluma. Uchunguzi uliofanywa na kuchapishwa katika gazeti la Pediatrics in Review ulionyesha kwamba asilimia 14 ya watoto huko Norway huwadhulumu wengine au hudhulumiwa. Nchini Japan, asilimia 15 ya wanafunzi wa shule za msingi wanasema kwamba wao hudhulumiwa, na asilimia 17 hudhulumiwa huko Australia na Hispania. Mtaalamu mmoja anakadiria kwamba watoto milioni 1.3 hudhulumiwa au kuwadhulumu wengine nchini Uingereza.

Profesa Amos Rolider wa Chuo cha Emek Yizre’el aliwahoji wanafunzi 2,972 wa shule 21. Kulingana na gazeti The Jerusalem Post, profesa huyo aligundua kuwa “asilimia 65 walilalamika kwamba walipigwa makofi au mateke, walisukumwa, na kunyanyaswa na wanafunzi wenzao.”

Kuna mbinu mpya ya dhuluma yenye kudhuru ambayo inahusisha kutuma vitisho kwa simu za mkononi na kompyuta. Pia, vijana wanaochochewa na chuki huwadhulumu wengine kwa kuandika habari mbaya zinazotia ndani habari za kibinafsi na kuziweka kwenye Internet. Kulingana na Dakt. Wendy Craig wa Chuo Kikuu cha Queen’s huko Kanada, mbinu hiyo ya dhuluma “humdhuru sana mtoto anayedhulumiwa.”

Kazini

Wafanyakazi wengi zaidi wanalalamika kuhusu dhuluma kazini. Katika nchi fulani, inasemekana kwamba dhuluma inatukia mara nyingi zaidi kuliko ubaguzi wa rangi au kusumbuliwa kingono. Kila mwaka, asilimia 20 hivi ya wafanyakazi nchini Marekani hudhulumiwa.

Huko Uingereza, ripoti moja iliyotolewa katika mwaka wa 2000 na Chuo Kikuu cha Manchester cha Sayansi na Tekinolojia ilisema kwamba kati ya wafanyakazi 5,300 wa mashirika 70, asilimia 47 waliripoti kwamba walikuwa wameshuhudia dhuluma katika miaka mitano iliyopita. Katika mwaka wa 1996, Muungano wa Ulaya ulifanya uchunguzi katika nchi 15 ambazo ni wanachama wa muungano huo na kuwahoji wafanyakazi 15,800. Asilimia 8 ya waliohojiwa, yaani, wafanyakazi milioni 12 hivi, walisema kwamba walitishwa au kudhulumiwa.

Inaonekana aina zote za dhuluma hufanana kwa njia moja, hata iwe zinatukia shuleni au kazini—nguvu hutumiwa kumuumiza au kumwaibisha mtu mwingine. Lakini, kwa nini watu fulani huwadhulumu wengine? Matokeo ni nini? Na suluhisho ni nini?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Baadhi ya majina yamebadilishwa.

[Sanduku katika ukurasa wa 4]

Wadhalimu wa Aina Mbalimbali

Wanaotumia Jeuri: Hawa ndio rahisi kutambua. Wanapokasirika wao humpiga mtu wanayemdhulumu, humsukuma, humpiga mateke, au kuharibu mali yake.

Wanaotumia Matusi: Hawa hutumia maneno ili kuwaumiza au kuwaaibisha wengine kwa kuwabandika majina, kuwatukana, au kuwadhihaki tena na tena.

Wanaoharibu Mahusiano: Hawa hueneza uvumi mbaya kuwahusu wengine. Wanawake wanaodhulumu wengine hupenda kutumia mbinu hii.

Wanaolipiza Kisasi: Hawa ni watu ambao wamegeuka kuwa wadhalimu baada ya kudhulumiwa. Kudhulumiwa si udhuru wa kuwadhulumu wengine, bali kunatusaidia kuelewa kwa nini watu hao wamekuwa wadhalimu.

[Hisani]

Source: Take Action Against Bullying, by Gesele Lajoie, Alyson McLellan, and Cindi Seddon