Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuabiri kwa Kutegemea Maji, Anga, na Upepo

Kuabiri kwa Kutegemea Maji, Anga, na Upepo

Kuabiri kwa Kutegemea Maji, Anga, na Upepo

JE, UNAOGOPA kuanguka kutoka ukingoni mwa dunia? Pengine huogopi. Hata hivyo, katika nyakati za kale mabaharia fulani waliogopa kuanguka. Wengi wao waliabiri karibu na nchi kavu. Lakini mabaharia wengine jasiri walishinda woga wao na kuabiri kwenye bahari kuu.

Miaka 3,000 hivi iliyopita mabaharia kutoka Foinike walifunga safari kutoka bandari za kwao kwenye ufuo wa mashariki wa Mediterania ili wakafanye biashara Ulaya na Afrika Kaskazini. Katika karne ya nne K.W.K., mvumbuzi mmoja Mgiriki aliyeitwa Pytheas aliabiri kuzunguka Uingereza na huenda alifika Iceland. Na muda mrefu kabla ya meli za Ulaya kuingia Bahari ya Hindi, mabaharia Waarabu na Wachina kutoka Mashariki tayari walikuwa wameabiri kwenye bahari hiyo. Mzungu wa kwanza kuabiri hadi India, Vasco da Gama, alifika huko salama salimini akisaidiwa na nahodha Mwarabu, Ibn Majid, aliyeongoza meli za Da Gama kwa siku 23 zilipokuwa zikivuka Bahari ya Hindi. Manahodha hao wa zamani walipataje njia baharini?

Kukisia Kuliwaokoa

Mabaharia wa kale walitegemea makisio. Nahodha alihitaji kujua mambo haya matatu: (1) mwanzo wa safari, (2) mwendo wa meli, na (3) mwelekeo. Ilikuwa rahisi kujua mwanzo wa safari. Lakini mwelekeo ungeweza kujulikanaje?

Mwaka wa 1492, Christopher Columbus alitumia dira ili kujua upande aliokuwa akielekea. Lakini dira zilianza kutumiwa barani Ulaya katika karne ya 12 W.K. Bila dira, manahodha waliabiri kwa kutegemea jua na nyota. Mawingu yalipowazuia kuona, manahodha walifuata mawimbi mazito ya bahari yaliyosababishwa na upepo. Walichunguza jinsi mawimbi hayo yalivyosonga kupatana na kuchomoza na kutua kwa jua na nyota.

Walikadiriaje mwendo? Njia moja ilikuwa kwa kukadiria muda ambao meli ilichukua kupita kitu kilichotupwa mbele yake. Njia nyingine ya baadaye iliyokuwa sahihi zaidi ilitia ndani kuangusha baharini kipande cha ubao kilichofungwa kwa kamba iliyotiwa mafundo kwenye visehemu vinavyotoshana. Meli ilipokuwa ikienda, ubao huo uliokuwa ukielea ulivuta kamba kutoka melini. Baada ya muda fulani hususa, kamba hiyo ilirudishwa melini na mafundo yakahesabiwa. Idadi ya mafundo ilionyesha mwendo wa meli, yaani, maili za kibaharia kwa saa, kipimo kinachotumika hata leo hii. Baada ya kujua mwendo wa meli, nahodha angeweza kuhesabu umbali ambao ilikuwa imesafiri kwa siku moja. Kisha alichora mstari kwenye ramani ya bahari kuonyesha umbali aliokuwa amesafiri.

Bila shaka, mikondo ya bahari na upepo ungeielekeza meli upande usiofaa. Kwa hiyo, pindi kwa pindi nahodha alihesabu na kurekodi kiasi ambacho angehitaji kugeuza usukani wa meli ili ielekee upande unaofaa. Kila siku, aliendelea mahali alipoachia—akipima, kuhesabu na kuchora safari yake kwenye ramani. Mwishowe, meli ilipotia nanga, mistari aliyochora kila siku kwenye ramani ilifanyiza rekodi yenye kudumu ya jinsi meli hiyo ilivyofika mwisho wa safari yake. Kwa kukisia, Columbus alisafiri kutoka Hispania hadi Amerika Kaskazini na kurudi tena zaidi ya miaka 500 iliyopita. Ramani zake zilizochorwa kwa uangalifu huwawezesha manahodha wa leo kufuatia safari yake ya ajabu.

Kuabiri kwa Kutegemea Anga

Mabaharia wa kale walitumiaje mwezi, jua na nyota kuongoza meli zao? Kuchomoza na kutua kwa jua kulionyesha upande wa mashariki na magharibi. Wakati wa mapambazuko, mabaharia wangeweza kujua umbali ambao jua limesonga kwa kulinganisha umbali wake na nyota ambazo bado hung’aa alfajiri. Usiku, wangeweza kujua mwelekeo wao kwa kuchunguza Polaris—Nyota ya Kaskazini—ambayo huonekana juu ya Ncha ya Kaskazini baada ya giza kuingia. Upande wa kusini zaidi, kikundi cha nyota nyangavu kinachoitwa Msalaba wa Kusini kiliwasaidia kupata Ncha ya Kusini. Kwa hiyo kwenye usiku usio na mawingu, mabaharia wangeweza kuchunguza wanakoelekea kwa kutegemea mwezi, jua au nyota.

Lakini waliongozwa na vitu vingine vya angani mbali na vitu hivyo. Kwa mfano, Wapolinesia na mabaharia wengine kutoka Pasifiki, wangeweza kusoma anga la usiku kama ramani ya barabara. Mojawapo ya mbinu walizotumia ilihusisha kufuata nyota ambayo walijua iliibuka au kutua kwenye upeo wa macho upande waliokuwa wakielekea. Mabaharia hao walichunguza pia mipangilio mingine ya nyota usiku kucha ili kuhakikisha kwamba walikuwa wakielekea upande unaofaa. Ikiwa walikuwa wakielekea upande usiofaa, walibadili mwelekeo kwa kuchunguza mpangilio wa nyota.

Mbinu hiyo ilitegemeka kwa kadiri gani? Wakati ambapo mabaharia Wazungu walikuwa wakisafiri karibu na nchi kavu wakiogopa kuanguka ukingoni mwa dunia tambarare, yaelekea mabaharia wa Pasifiki walikuwa wakifunga safari ndefu za baharini katikati ya visiwa vidogo. Kwa mfano, zaidi ya miaka 1,500 iliyopita, Wapolinesia waliondoka katika Visiwa vya Marquesas na kuelekea kaskazini wakivuka Bahari kubwa ya Pasifiki. Kufikia wakati walipowasili kwenye ufuo wa Hawaii, walikuwa wamesafiri kilometa 3,700! Hadithi za kisiwani humo husimulia juu ya safari za Wapolinesia kati ya Hawaii na Tahiti. Wanahistoria fulani husema kwamba masimulizi hayo ni hekaya tu. Lakini, mabaharia wa siku hizi wamefunga safari hiyohiyo kwa kutegemea nyota, mawimbi mazito ya baharini, na mambo mengine ya asili—bila kutumia vifaa.

Kuendeshwa kwa Upepo

Meli zenye matanga zilitegemea upepo. Upepo mwanana kutoka nyuma ulikisukuma chombo vyema, lakini upepo kutoka mbele ulipunguza sana mwendo wa mashua. Ukosefu wa upepo, kama ilivyokuwa mara nyingi katika eneo la ikweta, ulifanya meli zisimame. Baada ya muda, mabaharia wakavumbua upepo wa baharini uliowasaidia waanzishe njia kuu za meli katika bahari kuu. Mabaharia walitumia vizuri upepo huo.

Bila shaka, ikiwa upepo huo haukuvuma ifaavyo, ungeweza kuleta taabu na kifo. Kwa mfano, katika mwaka wa 1497, Da Gama alipoanza kuabiri kutoka Ureno hadi Pwani maarufu ya Malabar huko India, upepo ulimsukuma hadi Atlantiki ya Kusini na kumrudisha upande wa kusini-mashariki na kuzunguka Rasi ya Tumaini Jema barani Afrika. Lakini katika Bahari ya Hindi, alikumbana na upepo wa msimu ambao huvuma upande tofauti kila msimu. Mwanzoni mwa kila mwaka upepo wa msimu wa kiangazi hutoka kusini-magharibi mwa Bahari ya Hindi, na kwa miezi mingi husukuma vitu vyote vinavyoelea kuelekea Asia. Majira ya kupukutika yanapoelekea kwisha, upepo wa majira ya baridi kali huanza kuvuma. Huvuma kwa nguvu kutoka kaskazini-mashariki kurudi Afrika. Lakini Da Gama aliondoka India mwezi wa Agosti na punde si punde akakumbana na upepo uliokuwa ukivuma upande usiofaa. Badala ya kuvuka kuelekea mashariki kwa siku 23 kama ilivyo kawaida, safari yake ilichukua karibu miezi mitatu. Kwa sababu ya kuchelewa huko, chakula kilipungua, na watu wake wengi wakafa kwa sababu ya kiseyeye.

Mabaharia wenye busara walioabiri katika Bahari ya Hindi walijifunza kuchunguza kalenda na vilevile dira. Meli zilizokuwa zikielekea mashariki kupitia Rasi ya Tumaini Jema zilipaswa kuanza safari ya kuelekea India mapema wakati wa kiangazi, la sivyo, zingengoja kwa miezi mingi upepo unaovuma upande ufaao. Kwa upande mwingine, manahodha wa meli walikuwa wakiondoka India kuelekea Ulaya mwishoni mwa majira ya kupukutika ili wasikabili upepo wa msimu wa kiangazi. Kwa hiyo, Bahari ya Hindi ilikuwa kama njia ya kuelekea upande mmoja tu kwa wakati—mara nyingi safari za baharini kati ya Ulaya na Pwani ya Malabar huko India zilikuwa zikielekea upande mmoja tu kwa wakati mmoja.

Safari Zaendelea

Wakati ulipita, na mwishowe maendeleo yalifanywa katika kuabiri. Mashine zilianza kupunguza uhitaji wa kutegemea macho na kukisiakisia. Kifaa cha Astrolabe na kifaa sahihi zaidi cha sextant—ambavyo hupima umbali wa jua au nyota kutoka kwenye upeo wa macho—viliwawezesha mabaharia kujua mahali walipokuwa kaskazini au kusini mwa ikweta. Marine chronometer—saa yenye kutegemeka ambayo ingeweza kutumika baharini—iliwawezesha kujua mahali walipokuwa upande wa mashariki au magharibi. Vifaa hivyo vilikuwa sahihi zaidi kuliko kukisia.

Leo, dirajiro huonyesha kaskazini bila kutumia kidole cha sumaku. Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Setilaiti unaweza kuonyesha mahali hususa ambapo meli ipo kwa kubonyeza tu vidude vichache. Mara nyingi kompyuta ndogo hutumiwa badala ya ramani za karatasi. Naam, kuabiri kumekuwa jambo la kisayansi. Lakini maendeleo hayo yote hutufanya tuthamini zaidi ujasiri na ustadi wa mabaharia wa kale ambao waliendesha vyombo vyao katika bahari kubwa wakitegemea tu ujuzi wao wa maji, anga, na upepo.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 12, 13]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Makisio

Makisio yalirekodiwa kwa uangalifu kwa ajili ya safari za baadaye

1 Mwanzo

2 Mwendo Wakadiriwa kwa kutumia kipande cha

ubao, kamba iliyofungwa mafundo

kwenye visehemu vinavyotoshana, na

kipima-wakati

3 Mwelekeo Wakadiriwa kwa kuangalia

mikondo, nyota, jua, na upepo

[Picha]

Dira

“Sextant”

[Picha katika ukurasa wa 14]

Vifaa bora vya kisasa hufanya kuabiri leo kuwe jambo la kisayansi

[Hisani]

Kværner Masa-Yards