Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kamba-Mti Wanajua Kurudi Nyumbani
“Kamba-mti wana uwezo wa ajabu wa kujua njia ya kurudi nyumbani mwao hata baada ya kufunikwa macho, kuzungushwa huku na huko, na kutupwa mbali na makao yao,” lasema gazeti National Post la Kanada. Watafiti walikamata kamba-mti wengi karibu na visiwa vya Florida Keys na wakawaweka katika matangi yenye giza na kuwaachilia umbali wa karibu kilometa 37 kutoka mahali walipokamatwa. Kamba-mti hao walielekea upande waliokamatwa ijapokuwa macho yao yalikuwa yamefunikwa. Watafiti wanasema kwamba hiyo ndiyo njia ya hali ya juu zaidi ya kujiongoza iliyowahi kuonekana katika mnyama asiye na uti wa mgongo. “Licha ya jitihada zetu za kuwapotosha, kamba-mti walijua upande waliohitaji kuelekea ili warudi nyumbani,” alisema Dakt. Kenneth Lohmann, aliyeongoza utafiti huo. “Ebu wazia, viumbe hao wadogo wanaweza kujua mahali walipo ilhali wanadamu wangepotea kabisa.”
Hakuvunja Sheria
“Nchini Mexico, si hatia kutoroka jela,” laripoti gazeti The Korea Herald. “Sheria ya Mexico inatambua kwamba wanadamu wote wana tamaa ya kiasili ya kuwa huru, hivyo haiwahukumu kwa kutosheleza tamaa hiyo.” Wafungwa hushtakiwa tu wakivunja sheria wanapotoroka, kama vile kuwaumiza wengine, kuharibu mali, kutoa hongo, au kupanga njama za kutoroka pamoja na wafungwa wengine. Hata hivyo, kuna hatari fulani. Walinzi wa jela wanaruhusiwa kumpiga risasi mtu yeyote anayejaribu kutoroka. Jambo hilo limewafanya wafungwa watumie njia za ujanja za kutoroka. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1998, muuaji mmoja aliyehukumiwa jela alijinyima chakula na kupunguza uzito wake hadi kilogramu 50 ili mke wake ambebe na kumtoa nje kwa sanduku ambalo alitumia kubebea nguo zake chafu. Alikamatwa miezi tisa baadaye lakini akatoroka tena na hajapatikana hata leo.
Muungano wa Ulaya Utapanuka
“Miaka 50 baada ya Vita Baridi kugawanya Ulaya katika sehemu mbili, mkataa umeafikiwa . . . kuunganisha Ulaya Magharibi na Ulaya ya Kati,” lasema gazeti International Herald Tribune la Paris. Nchi kumi, zikiwemo [Jamhuri ya] Cheki, Estonia, Hungaria, Latvia, Lithuania, Malta, Poland, Saiprasi, Slovakia, na Slovenia, zikikubali mwaliko wa kujiunga na Muungano huo katika mwaka wa 2004, Muungano huo utakuwa na watu milioni 75 zaidi. Hivyo, kutakuwa na “soko moja lenye watu milioni 450” linalozalisha jumla ya dola trilioni 10.7 za Marekani. Uzalishaji huo unakaribia ule wa Marekani wa dola trilioni 11.5. Rais wa Tume ya Ulaya, Romano Prodi alitangaza hivi: “Kwa mara ya kwanza kabisa, bara la Ulaya litaungana.” Mojawapo ya matatizo mengi yanayokabili Muungano huo uliopanuliwa ni ugumu wa kufanya biashara kukiwa na lugha 21 rasmi.
Harusi za Magharibi Zinapendwa Japan
Ingawa asilimia 0.8 tu ya Wajapani ndio wanaodai kuwa Wakristo, wengi wanaiga harusi za Magharibi, yaani kuvalia joho jeupe, kuwa na mashada ya maua, na matembezi maalumu, lasema gazeti The Japan Times. Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa gazeti moja ulionyesha kwamba kati ya wenzi wa ndoa 4,132 waliofunga ndoa katika mwaka wa 2001, asilimia 61.2 waliiga harusi za Magharibi, asilimia 20.1 wakafanya harusi za Kishinto, na asilimia 0.9 wakafanya harusi za Kibudha. Ili kuiga harusi za Magharibi, kampuni zinazotayarisha harusi kwa kawaida hukodi “Wazungu ambao si makasisi,” kwani wateja hupendelea watu hao. Msemaji mmoja wa kampuni ya kutayarisha harusi alisema kwamba “vijana wengi wanaofunga ndoa wanaamini kwamba wakifunganishwa na mtu wa nchi ya kigeni, harusi yao itakuwa ya hali ya juu au hata itaheshimika.” Watu hao wanaojifanya kuwa makasisi mwishoni mwa juma, huwaapisha wale wanaofunga ndoa na kusoma vifungu vya Biblia mbele ya wasikilizaji.
Mitishamba Hatari
“Watu wengi wanaamini kimakosa kwamba dawa ya mitishamba haina madhara kwa sababu inatokana na mimea,” laripoti gazeti El Financiero la Mexico City. Kulingana na Abigail Aguilar Contreras wa Taasisi ya Mexico ya Masilahi ya Jamii, kujitibu kwa kutumia mitishamba kunaweza kuwa hatari. Gazeti hilo lasema kwamba “utumizi mbaya wa mitishamba unaweza kudhuru mwili na hata kuua kwani ina dawa zinazosababisha uzoefu au zile zinazolevya.” Mfano mmoja ni mmea wa manjano wa oleander, unaotumiwa kupunguza uzito. Mmea huo unaweza kusababisha kuhara na kutapika na kudhuru moyo. Kwa hiyo, ni vizuri kumuuliza mtaalamu wa mitishamba unapotaka kutumia dawa ya mitishamba.
Biashara ya Hisa Inakuwa Zoea Sugu
Daktari mmoja Mjerumani anawatibu watu wanaofanya biashara ya hisa kupita kiasi, laripoti gazeti Die Welt la Hamburg. Kulingana na Joachim Otto, ambaye huwashauri watu walio na mazoea sugu, watu hao wanavutiwa na “uwezekano wa kupata pesa haraka.” Wazoefu hao walijihusisha katika biashara ya hisa “kwa kuhofia kwamba wangepoteza pato la mwaka,” lakini walishindwa kujidhibiti na kuwa wazoefu kwa sababu ya “kuuza na kununua hisa haraka, kujasiria kufanya biashara, na msisimko wa daima.” Sasa wengi wao wana madeni makubwa. Bila wake zao kujua, baadhi yao wamepoteza akiba zao zote na kuweka rehani nyumba zao. Wengi hutafuta matibabu wakati tu wanapotambua kwamba familia zao haziwezi kuvumilia tabia yao tena.
Mapacha Waliozaliwa Miaka Tofauti
“Mapacha wawili Caleigh na Emily Johnson wanafanana katika mambo mengi lakini walizaliwa katika siku tofauti—na miaka tofauti,” laripoti gazeti Daily News la New York. “Caleigh alizaliwa Des. 31 saa 5:24 usiku. Emily alizaliwa Jan. 1 saa 6:19 usiku.” Mama yao, Dawn Johnson, wa Barnegat, New Jersey, alifurahi sana. Alisema hivi: “Ingawa ni mapacha, nilitaka kila mmoja awe tofauti na yule mwingine, na ikawa hivyo tangu wazaliwe.” Mapacha hao walitarajiwa kuzaliwa katika Februari 2, lakini walizaliwa mwezi mmoja mapema.
Lugha ya Internet Inatumiwa Darasani
“Maneno yaliyofupishwa ya Kiingereza yanayotumiwa katika Internet na wakati wa kutuma ujumbe kwenye simu yanaathiri somo la Kiingereza shuleni,” lasema gazeti Toronto Star. Walimu fulani wanaamini kwamba “tekinolojia mpya inaathiri jinsi watoto wanavyoandika na kufikiri.” Wanafunzi wameanza kutumia lugha mpya ya maneno yaliyofupishwa ya Kiingereza. Maneno hayo hutumiwa wakati wa kutuma ujumbe kwenye Internet au kupitia simu za mkononi. Sasa wanafunzi wanatumia maneno hayo yaliyofupishwa wanapofanya kazi za shule.
Uvumbuzi Mpya Kuhusu Kahawa
“Kahawa iliyoondolewa kafeini si bora kwa afya kushinda kahawa ya kawaida na inaweza kuwafanya wanywaji wasilale usiku mzima kama kahawa ya kawaida,” lasema gazeti The Times la London. Watafiti katika Hospitali ya Chuo Kikuu, huko Zurich, Uswisi, wanasema kwamba aina zote za kahawa huathiri moyo na mfumo wa neva karibu kwa njia ileile, na huenda kuna kemikali nyingine inayosababisha matatizo mbali na kafeini. Kiongozi wa utafiti huo Dakt. Roberto Conti alisema hivi: “Hadi sasa tumedhania kwamba kafeini ndiyo inayoathiri moyo mtu anapokunywa kahawa, lakini tumegundua kwamba hata wale wanaokunywa kahawa iliyoondolewa kafeini bado wanapatwa na matatizo yaleyale. Jambo hilo linaonyesha kwamba tunajua machache sana kuhusu athari za kinywaji hicho kinachojulikana sana na kinachotumiwa na watu wengi zaidi duniani.”