Maamuzi Yanayoathiri Afya Yako
Maamuzi Yanayoathiri Afya Yako
MARA nyingi ni vigumu kula vizuri na kudumisha afya. Kwa sababu ya magumu ya leo, watu hupenda kununua chakula kilichopikwa badala ya kupika nyumbani, na wanapenda kutazama televisheni na kutumia kompyuta badala ya kufanya mazoezi. Kwa sababu hiyo, watu wazima na watoto wengi zaidi wanaweza kujiletea matatizo makubwa ya afya.
Gazeti la Asiaweek linasema kwamba huko Asia, “watu wengi huugua ugonjwa wa kisukari kwa sababu wao hula chakula chenye mafuta mengi na hawafanyi mazoezi ya mwili.” Jambo linalotia wasiwasi ni kwamba watu wengi wenye umri mdogo hupata ugonjwa huo. Gazeti la The Globe and Mail linasema kuwa nchini Kanada “watafiti wamegundua kwamba ni mtoto mmoja tu kati ya saba anayekula matunda na mboga za kutosha [na] kwamba ni nusu tu ya watoto wanaocheza kiasi cha kutokwa na jasho.” Kwa sababu hiyo, “kuna uwezekano mkubwa kwamba vijana hao watapata magonjwa ya moyo kabla hawajafika umri wa miaka 30,” gazeti hilo linasema.
Wataalamu wa usingizi vilevile wanasema kwamba watu wazima huenda wakahitaji kulala kwa muda wa saa nane hivi kila usiku na labda vijana wanahitaji kulala kwa muda mrefu zaidi. Uchunguzi mmoja uliofanywa kwenye Chuo Kikuu cha Chicago ulionyesha kwamba wavulana wenye afya waliolala kwa muda wa saa nne tu katika siku sita mfululizo walianza kuonyesha dalili za magonjwa ambayo kwa kawaida yanawapata wazee. Watu wengi hukesha kwa sababu ya kazi, masomo ya shule, au raha, lakini jambo hilo linaweza kuwadhuru badala ya kuwanufaisha. James Maas, mtaalamu wa usingizi wa Chuo Kikuu cha Cornell cha New York, anasema hivi: ‘Ni afadhali sana mtu awe chonjo na mbunifu kuliko kuwa mzembe ili asijikute akisinzia anapoendesha gari kwenye barabara kuu.’
Bila shaka kuna mambo mengine pia yanayoathiri afya yetu. Kwa mfano, kuwa mchangamfu kunaweza kutunufaisha kiafya. Na kuwa na kusudi maishani kunaweza kututia moyo tufanye maamuzi yatakayotusaidia kudumisha afya nzuri.