Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Madini Yanayometameta Kama Mbalamwezi

Madini Yanayometameta Kama Mbalamwezi

Madini Yanayometameta Kama Mbalamwezi

Mnamo Aprili 2000, wachimba-migodi karibu na Chihuahua, Mexico, walilipua shimo la meta 300 chini ya ardhi wakitafuta madini yenye thamani. Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 40 anayeitwa Eloy Delgado alikuwa akijikakamua kupitia kijia chembamba alipoona pango lenye fuwele kubwa zinazopitisha mwanga. Alisema hivi: “Lilikuwa jambo lenye kuvutia sana. Ni kana kwamba mwangaza ulirudishwa na kioo kilichovunjika.” Mtu mwingine alisema kuwa ‘madini hayo yanametameta kama mbalamwezi.’

Inasemekana kwamba fuwele hizo ndizo kubwa zaidi ulimwenguni. Baadhi ya fuwele hizo ni kubwa kama miti ya misindano iliyokomaa kwani zina urefu wa meta 15 na uzani wa zaidi ya kilogramu 10,000! Jeffrey Post, msimamizi wa madini kwenye Taasisi ya Smithsonian huko Washington, D.C., alisema hivi: “Inasisimua kuona fuwele kubwa na zilizokamilika jinsi hiyo.” Alisema kwamba fuwele nyingi huwa ndogo sana kiasi cha kwamba zinaweza kutoshea mkononi mwako.

Gazeti Smithsonian la Aprili 2002 lilisema hivi lilipokuwa likizungumzia jinsi fuwele hizo zilivyofanyizwa: “Maji yenye salfa nyingi yaliyokuwa ndani ya mapango hayo yalianza kumomonyoa kuta za chokaa na kiasi kikubwa sana cha kalisi kikatokezwa. Halafu kalisi hiyo iliungana na salfa na kufanyiza fuwele nyingi ajabu.”

Ingawa halijoto na kiasi cha unyevu ndani ya mapango hayo zinafaa fuwele hizo, wanadamu wanaweza kuumia sana wanapoingia humo. Halijoto humo zinakaribia nyuzi 65 za Selsiasi na kiasi cha unyevu ni asilimia 100. Mvumbuzi Richard Fisher, ambaye ni mtu wa kwanza wa Amerika Kaskazini kutembelea mapango hayo, anasema hivi: “Mtu anapoingia ndani ya lile pango kubwa anahisi kana kwamba yumo ndani ya tanuru.” Pia anasema kwamba mtu anaweza kuvumilia hali hizo kwa dakika sita hadi kumi tu. Baada ya hapo, haiwezekani tena kustahimili hilo joto kali na unyevu mwingi.

Uvumbuzi wa fuwele hizo kubwa unatukumbusha jinsi dunia ilivyojaa vitu vingi vya kustaajabisha, na yaonekana kuna vingi ambavyo havijavumbuliwa bado. Pasina shaka unakubaliana na mtunga-zaburi aliyesema hivi: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.”—Zaburi 104:24.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

All pictures: © Richard D. Fisher