Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Msiba Baharini na Uharibifu wa Pwani

Msiba Baharini na Uharibifu wa Pwani

Msiba Baharini na Uharibifu wa Pwani

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

MELI ya mafuta inayoitwa Prestige ilitoboka na ikaanza kuvuja mafuta ilipokabili mawimbi makubwa katika Novemba 13, 2002. Tukio hilo liliharibu sana mazingira na kusababisha hasara kubwa ya kifedha. Jitihada za kuokoa meli hiyo ziliambulia patupu na baada ya siku sita, tani 20,000 hivi za mafuta zilikuwa zimemwagika. Hatimaye meli hiyo ilivunjika na kuzama umbali wa kilometa 200 hivi kutoka pwani ya Hispania.

Meli hiyo ilizama ikiwa na zaidi ya tani 50,000 za mafuta ndani yake, na tani 125 hivi za mafuta ziliendelea kumwagika kila siku. Mafuta yaliyomwagika yaliendelea kusonga hadi pwani bila kuzuilika. Mafuta hayo mazito na yenye sumu yaliharibu sana mazingira.

Harufu ya mafuta hayo iliwafanya watu kadhaa waliojitolea kusafisha fuo washindwe kuendelea na kazi hiyo. Isitoshe, mafuta hayo yakawa kama mawimbi ya lami yanayosonga-songa, ambayo yalijibandika kwenye miamba, kama chingamu nyeusi. Michel Girin, mkurugenzi wa Kituo cha Habari na Utafiti wa Uchafuzi wa Maji, alisema hivi: “Huo ni mojawapo ya misiba mikubwa zaidi ya umwagikaji wa mafuta kuwahi kutukia.”

Jitihada Kubwa

Mamia ya wavuvi walijitahidi kuondoa mafuta yaliyomwagika baharini ambayo yaliharibu biashara ya uvuvi. Wavuvi hao walijitahidi sana kukusanya na kuondoa mafuta kabla hayajafika ufuoni na kuharibu mojawapo ya maeneo yenye samaki wengi zaidi duniani. Watu wengine walitoa mafuta yaliyoganda kwa mikono. Mvuvi mmoja anayeitwa Antonio alieleza hivi: “Ilikuwa kazi ngumu sana lakini sisi tuliokuwa na mashua ndogo hatukuwa na namna nyingine.”

Wavuvi hao walifanya kazi kwa jasho baharini huku maelfu ya watu kutoka sehemu zote za Hispania wakijitolea kusafisha fuo. Wakiwa wamevalia vinyago na nguo nyeupe ilionekana kana kwamba walikuwa wamejikinga na mashambulizi ya viini hatari. Lakini kazi yao ilikuwa ya kuondoa mafuta kwa kuyakusanya katika ndoo. Kama vile wale wavuvi, baadhi ya watu waliojitolea walitumia mikono kuondoa mafuta yaliyokuwa yamechafua fuo.

Hasara

Rafael Mouzo, aliye meya wa Corcubión katika sehemu ya kaskazini ya Galicia, ambako ufuo uliharibiwa na mafuta, alisema hivi: ‘Nilifikiri ningekufa kwa sababu ya huzuni nilipoona yale mawimbi meusi yaliyorusha mafuta kwenye gati mjini Muxía. Mafuta hayo yaliyomwagika yameathiri kazi ya watu wengi sana katika mji wetu.’

Jambo linalosikitisha ni kwamba mbuga mpya ya wanyama ya Hispania inayoitwa Las Islas Atlánticas (Visiwa vya Atlantiki), iliathiriwa sana na mafuta hayo. Makundi makubwa ya ndege wa baharini walikuwa na viota kwenye visiwa hivyo vitano vilivyo karibu na Galicia, ambavyo vilikuwa safi sana kabla ya msiba huo. Eneo hilo lilikuwa na viumbe wengi wa baharini.

Mapema mwezi wa Desemba, asilimia 95 ya ufuo wa mbuga hiyo ilikuwa imechafuliwa kwa mafuta. Wataalamu wa ndege walikadiria kwamba ndege 100,000 hivi wangeathiriwa. Wapiga mbizi hata waliona mabonge makubwa ya mafuta yaliyoganda yakiruka-ruka chini ya bahari na kuharibu makao ya viumbe wa baharini.

Jay Holcomb, aliyeanzisha kituo cha kuwaokoa ndege alisema hivi: “Kwa kawaida ndege hufa maji au kutokana na baridi. Mafuta hupenya ndani ya manyoya, na kufanya yasiweze kukinga baridi au kuzuia maji. Isitoshe, mafuta hayo huwafanya wazame, kama tu nguo zilizolowa maji zinavyoweza kumfanya mtu anayeogelea azame. . . . Inafurahisha sana kuwaokoa baadhi ya ndege, hata kama ni wachache.”

‘Misiba Inayotazamiwa’

Ulimwengu unategemea mafuta ili kupata nishati, lakini ili kupunguza gharama, mara nyingi mafuta husafirishwa katika meli ambazo hazidumishwi vizuri. Kwa hiyo, gazeti la The New York Times lilisema kwamba “misiba kama hiyo inatazamiwa.”

Prestige ni meli ya tatu ya kubeba mafuta ambayo imezama nje ya pwani ya Galicia katika miaka 26 iliyopita. Yapata miaka kumi iliyopita meli Aegean Sea ilizama karibu na La Coruña, kaskazini mwa Galicia na tani 40,000 za mafuta zilimwagika. Sehemu fulani za ufuo huo bado zinaathiriwa na msiba huo. Kisha meli inayoitwa Urquiola ilizama katika eneo hilohilo mwaka wa 1976, na zaidi ya tani 100,000 za mafuta zilimwagika.

Kwa sababu ya msiba uliotukia hivi majuzi, Muungano wa Ulaya umeazimia kupiga marufuku meli zenye kubeba mafuta zisizo na viunzi viwili. Hata hivyo, matokeo yataonyesha kama jambo hilo litaweza kulinda fuo za Ulaya zinazopatwa na msiba tena na tena.

Ni wazi kwamba serikali za wanadamu hazijaweza kuondoa uchafuzi duniani, kama vile mafuta yaliyomwagika, takataka zenye sumu, au uchafuzi wa hewa. Hata hivyo, Wakristo wanatazamia wakati ambapo Ufalme wa Mungu utahakikisha kwamba dunia itageuzwa kuwa paradiso ambayo haitachafuliwa tena kamwe.—Isaya 11:1, 9; Ufunuo 11:18.

[Picha katika ukurasa wa 20, 21]

Meli Prestige ilizama ikiwa na tani 50,000 za mafuta

[Hisani]

AFP PHOTO/DOUANE FRANCAISE