Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

St. Petersburg Ni Njia ya Urusi ya Kuelekea Ulaya

St. Petersburg Ni Njia ya Urusi ya Kuelekea Ulaya

St. Petersburg Ni Njia ya Urusi ya Kuelekea Ulaya

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI URUSI

“Nakupenda, eeh kazi ya mikono ya Petro! / Napenda umbo lako imara la mraba; / Maji ya Neva hutiririka kwa utulivu na utaratibu / Kati ya gati zake za mawe ya matale.”—ALEKSANDR SERGEYEVICH PUSHKIN.

MANENO hayo ni sehemu ya shairi maarufu la Pushkin kuhusu St. Petersburg, linalomtaja mwanzilishi wa jiji hilo na mahali ambapo limejengwa upande wa kaskazini kabisa, ambapo Mto Neva huingia kwenye Bahari ya Baltiki. Lakini huenda ukajiuliza, ‘Jiji hilo kubwa lilipataje kujengwa katika eneo lenye majimaji?’

Mwishoni mwa karne ya 17, Urusi haingeweza kusitawi kwa sababu haikuwa na njia ya kusafiri baharini. Mtawala kijana Petro Mkuu alitamani kupata njia ya baharini kuelekea Ulaya. Milki ya kale ya Uturuki ilikuwa upande wa kusini karibu na Bahari Nyeusi. Hivyo, Petro alitafuta njia upande wa kaskazini ambapo Sweden ilimiliki eneo linalopakana na Bahari ya Baltiki.

Ili kutimiza lengo lake, Petro alitangaza vita dhidi ya Sweden katika Agosti 1700. Ingawa mwanzoni alishindwa, hakukata tamaa. Katika Novemba 1702, Petro alilazimisha Sweden kuondoka eneo la Ziwa Ladoga. Ziwa hilo kubwa zaidi barani Ulaya, huungana na Bahari ya Baltiki kupitia Mto Neva, umbali wa kilometa 60 hivi kutoka St. Petersburg. Wanajeshi wa Sweden walijificha katika ngome iliyoko kwenye kisiwa kidogo karibu na mahali ambapo Mto Neva unaanzia. Petro aliiteka ngome hiyo kutoka kwa Sweden na kuiita Shlissel’burg.

Baadaye wanajeshi hao wa Sweden walipigana na Warusi katika ngome iliyoitwa Nienshants, karibu na mahali ambapo Mto Neva unatiririka kuingia katika Bahari ya Baltiki. Mnamo Mei 1703, majeshi ya Sweden yalishindwa vibaya. Ushindi huo uliwawezesha Warusi wateke eneo hilo lote. Petro alianza kujenga ngome karibu na kisiwa kilichoko karibu cha Zayachy ili kulinda eneo hilo. Hivyo katika Mei 16, 1703, miaka 300 hivi iliyopita, Petro Mkuu aliweka jiwe la msingi la ngome ambayo leo inajulikana kama Ngome ya Peter-Paul. Wengi wanakubali kwamba hiyo ndiyo tarehe ambapo St. Petersburg lilianza kujengwa. Jiji hilo lilipewa jina la mtume Petro, kwani Petro Mkuu aliamini kwamba yeye ndiye mtakatifu anayemlinda.

Jiji Kuu Laanzishwa

Tofauti na majiji mengi makuu, St. Petersburg lilipangwa na kujengwa liwe jiji kuu lenye kupendeza tangu mwanzoni. Ijapokuwa jiji hilo liko kaskazini sana kama Anchorage, Alaska, bado Petro aliamua kulijenga. Mbao zililetwa kutoka eneo la Ziwa Ladoga na Novgorod. Ili apate mawe ya kujenga, Petro alipitisha sheria fulani. Kila Mrusi aliyeleta bidhaa St. Petersburg, alipaswa kuleta pia mawe kadhaa. Halafu, Petro alipiga marufuku ujenzi wa nyumba za mawe, kwanza jijini Moscow, kisha kwenye sehemu nyingine za milki yake. Hivyo waashi wote waliokosa kazi walihamia St. Petersburg.

Kitabu The Great Soviet Encyclopedia kinasema kwamba ujenzi wa jiji hilo uliendelea “haraka isivyo kawaida ikilinganishwa na viwango vya wakati huo.” Mitaro, vigingi vya kujengea, barabara, majengo, makanisa, hospitali, na ofisi za serikali zilichipuka. Mwaka ambao jiji lilianzishwa, ujenzi wa mahali pa kutengenezea meli ulianza pia. Baadaye mahali hapo palikuja kuwa makao makuu ya bandari ya Urusi iliyoitwa Admiralty.

Ujenzi wa jumba la kifalme lililotumiwa na watawala katika majira ya kiangazi ulianza mwaka wa 1710. Mnamo mwaka wa 1712, makao makuu ya Urusi pamoja na ofisi nyingi za serikali, yalihamishwa kutoka Moscow hadi St. Petersburg. Jumba la kwanza la kifalme lililojengwa kwa mawe lilikamilishwa katika mwaka wa 1714 na lingalipo hata leo. Jumba hilo lilijengwa kwa ajili ya mtawala wa kwanza wa jiji, Aleksandr Menshikov. Mwaka huo pia, Kanisa Kuu la Peter-Paul lilijengwa ndani ya ngome yenye jina hilo. Mnara wa kanisa hilo unaonekana waziwazi katika jiji hilo. Jumba la kifalme lililotumiwa katika majira ya baridi kali lilijengwa karibu na Mto Neva, na lilijengwa tena mara kadhaa. Jumba la kifalme la majira ya baridi kali lenye vyumba 1,100 lilijengwa baadaye na bado lipo. Leo katika jumba hilo lenye kupendeza kuna jumba maarufu la makumbusho linaloitwa Hermitage.

Katika miaka kumi ya kwanza, St. Petersburg lilipanuka kwa haraka sana hivi kwamba inasemekana kulikuwa na majengo 34,500 hivi katika jiji hilo kufikia mwaka wa 1714! Bado majumba ya kifalme na majengo mengine makubwa yaliendelea kujengwa. Athari kubwa ya dini nchini Urusi inaonekana katika majengo hayo.

Mfano mmoja ni wa Kanisa Kuu la Kazan lenye umbo la nusu mviringo na nguzo nyingi upande wa mbele. Umbo lake lenye kuvutia limefanya barabara ya Nevsky Prospekt ionwe kuwa mojawapo ya barabara za fahari zaidi ulimwenguni. Baadaye ujenzi wa Kanisa Kuu la St. Isaac ulianza. Karibu nguzo 24,000 zilichimbiwa chini katika eneo lenye majimaji ili kuliimarisha jengo, na kilogramu 100 za dhahabu safi zilitumika kufunika paa lake kubwa.

Majengo ya maeneo yaliyo karibu na St. Petersburg pia yanavutia. Katika kiunga cha Peterhof, kinachoitwa Petrodvorets leo, ujenzi wa Jumba Kuu la Kifalme ulianza katika mwaka wa 1714. Hayo yalikuwa makao ya Petro. Wakati uo huo, mke wa Petro alijengewa Jumba la Kifalme la Catherine lenye fahari katika mji ulio karibu wa Tsarskoe Selo, ambao leo unaitwa Pushkin. Baadaye katika karne hiyo, majumba mawili makubwa ya kifalme yalijengwa katika viunga viwili vya kusini, Pavlovsk na Gatchina.

Umaridadi wa jiji hilo jipya pia uliimarishwa sana na madaraja mengi yaliyojengwa kwenye mito na mitaro mingi iliyopo. Hivyo St. Petersburg limeitwa “Venice la Kaskazini.” Wasanifu wa majengo kutoka Italia, Ufaransa, na Ujerumani walifanya kazi pamoja na wenzao wa Urusi wenye ustadi kuunda jiji ambalo kitabu The Encyclopædia Britannica kinasema ni “mojawapo ya majiji ya Ulaya yenye kuvutia na yenye fahari zaidi.”

Lilidumu Licha ya Taabu

Wapinzani wa Petro hawakuwa na habari kwamba Warusi wangelilinda jiji hilo kwa ujasiri mwingi. Kitabu Peter the Great—His Life and World kinasema hivi: “Tangu Petro Mkuu alipofika kwa mara ya kwanza mahali ambapo Mto Neva unaingia baharini, eneo na jiji lililojengwa hapo limebaki mikononi mwa Warusi daima.”

Ama kweli, kitabu kilichonukuliwa hapo juu kinasema kwamba “tangu zamani za kale, wavamizi wenye majeshi yenye nguvu walioingia Urusi hawakuweza kuiteka bandari ya Petro katika Bahari ya Baltiki, ingawa Wanazi walizingira jiji hilo kwa muda wa siku 900 katika Vita vya Pili vya Ulimwengu. Watawala waliojaribu kuivamia bandari hiyo ni Charles wa 12, Napoleon, na Hitler lakini hawakufaulu kuiteka.” Katika kipindi hicho kirefu ambacho Wanazi walizingira jiji hilo, watu milioni moja hivi walikufa. Wengi walikufa kutokana na baridi na njaa ya mwaka wa 1941/1942 wakati baridi ilipokuwa nyuzi 40 za Selsiasi chini ya kipimo cha kuganda. Katika kipimo hicho, nyuzi za Selsiasi na Fahrenhaiti hulingana.

Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilipoanza katika mwaka wa 1914, jina la jiji hilo lilibadilishwa kuwa Petrograd. Wakati kiongozi wa kwanza wa Muungano wa Sovieti Vladimir Lenin alipokufa katika mwaka wa 1924, jina hilo lilibadilishwa kuwa Leningrad. Hatimaye, katika mwaka wa 1991, Muungano wa Sovieti ulipovunjika, jiji hilo lilianza kuitwa St. Petersburg tena.

Jinsi Ambavyo Limefaidi Ulimwengu

Kupatana na amri ya Petro, Chuo cha Sayansi cha Urusi kilianzishwa katika jiji hilo mnamo mwaka wa 1724, na Chuo cha Sanaa katika mwaka wa 1757. Petro alikufa katika mwaka wa 1725 akiwa na umri wa miaka 52. Wachoraji Warusi Karl Bryullov na Ilya Repin wa karne ya 19, walisomea katika jiji hilo na baadaye wakatambuliwa ulimwenguni pote.

Mnamo mwaka wa 1819, Chuo Kikuu cha Taifa cha St. Petersburg kilianzishwa, na baadaye vyuo vingine vya masomo ya juu vilianzishwa pia. Mwishoni mwa karne ya 19, Mrusi Ivan Pavlov, mshindi wa Tuzo ya Nobeli na mtaalamu wa mifumo ya mwili alivumbua kwamba wanyama wanaweza kufundishwa kuhusianisha jambo moja na jingine wanapochochewa kwa njia fulani. Yeye aliishi St. Petersburg. Pia ni katika jiji hilo ambapo mwanakemia Mrusi Dmitry Mendeleyev alibuni jedwali ya elementi au kama inavyojulikana huku Urusi, jedwali ya Mendeleyev.

Sanaa ya jiji hilo pia ilivutia watu ulimwenguni pote. Mnamo mwaka wa 1738, chuo cha kujifunza kucheza dansi kinachojulikana ulimwenguni pote cha Mariinsky Ballet kilianzishwa. Punde si punde majumba ya muziki, dansi, na uigizaji, yalirembesha jiji hilo. Watunzi maarufu wa muziki waliishi St. Petersburg, kama vile Pyotr Ilich Tchaikovsky. Yeye anajulikana kwa miziki inayopendwa kama vile Sleeping Beauty, Swan Lake, The Nutcracker, na muziki wake maarufu 1812 Overture.

Washairi wengi maarufu na waandishi wa Urusi pia waliishi St. Petersburg. Kijana Aleksandr Sergeyevich Pushkin alikuwa “mshairi maarufu zaidi [wa Urusi] na mwanzilishi wa fasihi ya kisasa ya Urusi.” Yeye huonwa kuwa Shakespeare wa Urusi, na vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha zote kuu, kutia ndani shairi lililonukuliwa kwa sehemu mwanzoni mwa makala hii kuhusu jiji alilohamia. Pia kuna Dostoyevski, ambaye kitabu The Encyclopædia Britannica kinasema “anaonwa kuwa mmoja wa waandishi bora wa riwaya waliowahi kuishi.”

Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba kile ambacho St. Petersburg lilipokea kutoka Ulaya, limelipia mara nyingi tangu lianzishwe. Wakazi wake wamefaidi ulimwengu kisanaa kwa miaka mingi.

Wakati wa Kukumbuka

Katika juma la Mei 24 hadi Juni 1, mamia ya maelfu ya wageni walimiminika St. Petersburg kusherehekea miaka 300 tangu lianzishwe. Walipofikiria matokeo ya kazi nyingi ya kulijenga, wengi walifurahia umaridadi wa jiji hilo na historia yake yenye kupendeza.

Juma moja tu mapema, Mashahidi wa Yehova wengi walitembelea St. Petersburg wakati ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi ilipowekwa wakfu. Majengo hayo yaliyopanuliwa yako viungani mwa jiji hilo. Siku iliyofuata, karibu watu 9,817 walikutana katika Uwanja wa Kirov huko St. Petersburg kusikiliza marudio ya programu ya wakfu na ripoti zenye kutia moyo kuwahusu Mashahidi wa Yehova katika nchi nyingi.

Kuna Mengi Sana ya Kuona

Kuna mambo mengi sana ya kuona jijini St. Petersburg hivi kwamba watu wanaotembea huku hushindwa waanzie wapi. Hali huwa hivyo pia katika jumba la makumbusho la Hermitage. Inakadiriwa kuwa iwapo mtu angetumia dakika moja kutazama kitu kimoja kati ya maelfu ya vitu vilivyo katika vyumba vya jumba hilo, ingemchukua miaka mingi kuvitazama vyote.

Wengine huona jambo lenye kuvutia zaidi jijini St. Petersburg kuwa maonyesho yake ya dansi. Kwa mfano, kuna Ukumbi wa Maonyesho wa Mariinsky ambao umerembeshwa kwa taa maridadi sana na kuta za ndani zinazometameta ambazo zimerembeshwa kwa kilogramu 400 hivi za dhahabu. Ukiwa umeketi katika ukumbi huo, unaweza kutazama baadhi ya dansi bora zaidi duniani.

Ukitembea kwenye jiji hili lenye wakazi milioni tano, unaweza kuona majengo maridadi karibu na Mto Neva. Ukiamua kusafiri kwa gari la moshi linalopita kwenye reli ya chini ya ardhi ambayo ni mojawapo ya reli zenye kina kirefu zaidi duniani, unaweza kufurahia safari hiyo yenye kupendeza. Kila siku, zaidi ya watu milioni mbili hutumia reli hiyo yenye umbali wa kilometa 98 hivi wanaposafiri kati ya vituo vyake zaidi ya 50. Baadhi ya vituo hivyo ni kati ya vile maridadi zaidi duniani. Katika mwaka wa 1955, wakati njia hiyo ilipofunguliwa, gazeti The New York Times lilisema kwamba vituo hivyo ni “majumba ya kifalme ya chini ya ardhi ya karne ya ishirini.”

Pasina shaka utasisimuka kutembelea St. Petersburg. Utafurahia kujua jinsi lilivyoanzishwa, lilivyopanuka, na vilevile utavutiwa na umaridadi, sanaa, utamaduni, elimu, na muziki wake ambao umedumu tangu jadi. Haidhuru mtu anavutiwa na nini katika jiji hili, mgeni yeyote atakubaliana na kitabu kinachosema kwamba St. Petersburg ni “mojawapo ya majiji maridadi zaidi barani Ulaya.”

[Picha katika ukurasa wa 23]

Petro Mkuu, mwanzilishi wa jiji la St. Petersburg

[Picha katika ukurasa wa 24]

Ngome ya Peter-Paul na kanisa lake kuu ambapo ujenzi wa St. Petersburg ulianzia

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Jumba la kifalme lililotumiwa katika majira ya baridi kali karibu na Mto Neva, ambapo leo kuna jumba la makumbusho la Hermitage (kulia kabisa)

[Hisani]

The State Hermitage Museum, St. Petersburg

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Jumba Kuu la Kifalme

[Picha katika ukurasa wa 25]

Jiji hili limeitwa “Venice la Kaskazini”

[Picha katika ukurasa wa 26]

Ukumbi wa Maonyesho wa Mariinsky unaojulikana ulimwenguni pote

[Hisani]

Steve Raymer/National Geographic Image Collection

Photo by Natasha Razina

[Picha katika ukurasa wa 26]

Njia za chini ya ardhi za St. Petersburg zimetajwa kuwa “majumba ya kifalme ya chini ya ardhi”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Top picture: Edward Slater/Index Stock Photography; painting and emblems: The State Hermitage Museum, St. Petersburg