Kijiti cha Kusugua Meno
Kijiti cha Kusugua Meno
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ZAMBIA
AFRIKA—bara lenye watu wenye meno ya kupendeza lakini lenye miswaki michache inayotengenezwa viwandani! Hilo lawezekanaje? Kwa wengi, siri ya tabasamu hiyo yenye kuvutia ni kipande kidogo cha mti—kijiti cha kutafunwa!
Vijiti vya kutafunwa vilitumiwa zamani na Wababiloni na baadaye Wamisri, Wagiriki, na Waroma. “Miswaki” hiyo midogo ya vijiti pia ilipatikana kwa wingi Uarabuni kabla ya enzi za Uislamu. Kijiti hicho cha kutafunwa kiliacha kutumiwa na wengi barani Ulaya miaka 300 hivi iliyopita, hata hivyo, bado kinatumiwa na watu wengi katika sehemu za Afrika, Asia, na Mashariki ya Kati.
Huko Mashariki ya Kati, vijiti hivyo hutokana hasa na mti unaoitwa mswaki. Midimu na michungwa hutumiwa Afrika Magharibi, na barani Hindi mikilifi hasa ndiyo hutumiwa. Afrika Mashariki karibu aina 300 za miti hutumiwa kutengeneza miswaki. Kijiti hicho husuguaje meno?
Kinapotafunwa, nyuzinyuzi zilizo mwishoni mwa kijiti hicho hulegea, na kufanyiza “brashi” ngumu. Kuendelea kukitafuna huondoa uchafu katikati ya meno na huchochea mzunguko wa damu kwenye fizi. Pia, kukitafuna huongeza mate, ambayo huusafisha mdomo na kuondoa viini pamoja na kuvizuia visiongezeke humo. *
Lakini kijiti cha kutafunwa si mswaki wa kawaida tu. Matawi na mizizi ya miti fulani huwa na kemikali ambazo hupunguza kufanyizwa kwa ukoga kwenye meno. Baadhi ya vijiti huwa na kemikali zinazozuia viini na kuvu. Vijiti vya mswaki, vilivyotajwa mapema, vinaweza kuzuia vidonda mdomoni. Huko Namibia, vijiti vya mti fulani unaoitwa muthala huzuia kuongezeka kwa viini vinavyosababisha kuoza kwa meno, magonjwa ya fizi, na maumivu ya koo. Mswaki huo wa asili unaweza pia kuzuia mashimo kwenye meno na pia kuimarisha fizi na mizizi ya meno. Kampuni fulani sasa hutengeneza dawa za meno zenye nyuzi na utomvu kutoka katika mimea hiyo.
Bila shaka, watu fulani hupendelea kutumia mswaki wa kawaida. Ukichagua kuutumia mswaki wa kawaida au kutumia kijiti, kama watu wa kale walivyofanya, uhakika ni kwamba: Usafi wa meno ni muhimu kwa afya ya mtu.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 6 Bila shaka, chakula kinachofaa ni muhimu pia. Watu wa mashambani barani Afrika mara nyingi hula nafaka na mboga kuliko wenzao wanaoishi mijini. Pia wao hawatumii sukari, vyakula vya viwandani, na soda kwa wingi—vitu ambavyo hufanya meno yaoze.
[Picha katika ukurasa wa 11]
Baadhi ya miswaki hutokana na mkilifi
[Hisani]
William M. Ciesla, Forest Health Management International, www.forestryimages.org