Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Maoni Yanayofaa Hurefusha Maisha

Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni ulionyesha kwamba wazee wenye maoni yanayofaa kuhusu maisha na uzee “waliishi miaka 7.5 zaidi ya wale wenye maoni yasiyofaa kuhusu uzee,” yasema makala katika gazeti Journal of Personality and Social Psychology. Uchunguzi huo wa miaka 23, uliofanyiwa watu 660 wenye umri wa miaka 50 na zaidi, ulithibitisha mambo mawili: Maoni yasiyofaa kuelekea uzee, “yanaweza kupunguza maisha,” na maoni yanayofaa “yanaweza kurefusha maisha.” Kwa kweli, maoni yanayofaa yanaweza kurefusha maisha kuliko vitu kama vile kiwango cha chini cha kolesteroli katika damu na shinikizo la damu linalofaa, yadokeza ripoti hiyo. Yamalizia kwa kuwahimiza watu wawe na maoni yanayofaa zaidi kuelekea wazee na kuwahusisha katika utendaji mbalimbali na “kutokazia maoni ya kawaida yasiyofaa kuhusu uzee,” yenye kudhuru ambayo watu huamini hata bila kujua.

Mifuko Hatari

Ulimwenguni pote, inakadiriwa kwamba kila mwaka wanyama, ndege, na samaki zaidi ya 100,000 hufa kwa sababu ya kula au kusakamwa na mifuko ya plastiki iliyotupwa. Huko Australia pekee, wanunuzi hutumia mifuko ya plastiki bilioni 6.9 kila mwaka, wastani wa mifuko 360 kwa kila mnunuzi. Kati ya mifuko hiyo, yakadiriwa kwamba mifuko ya plastiki milioni 25 huwa takataka. Gazeti Sunday Telegraph la Sydney liliripoti mwishoni mwa mwaka 2002 kwamba ili kupunguza vifo vya wanyama, maduka makubwa nchini Australia yangetumia mifuko mingine inayoweza kuoza badala ya kutumia mifuko ya plastiki. Ijapokuwa mifuko hiyo mipya hufanana na plastiki, imetengenezwa kutokana na wanga wa mhogo na huoza baada ya miezi mitatu. Mifuko hiyo “ndiyo ya kwanza kupatikana nchini Australia inayoweza kuoza na ambayo gharama yake inalingana na gharama ya mifuko ya kawaida ya plastiki,” asema Paul Shenston, mwenyekiti wa kikundi cha mazingira cha Planet Ark. Uchunguzi wa hivi karibuni ulionyesha kwamba “asilimia 81 ya wanunuzi ‘wanakubali kwa dhati’ kwamba mifuko inayoweza kuoza inapaswa kutumiwa.”

Aspirini na Waliofanyiwa Upasuaji wa Moyo

“Kuwapa wagonjwa aspirini saa 48 baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo kwaweza kupunguza kifo na matatizo mengine mabaya yanayohusisha moyo, ubongo, mafigo, na utumbo.” Ndivyo unavyosema uchunguzi ulioripotiwa kwenye gazeti The New York Times. Kiwango cha vifo cha wale waliopewa aspirini kilikuwa chini kwa asilimia 67 kikilinganishwa na wale ambao hawakupewa. Kiwango cha kiharusi na mishtuko ya moyo kilipungua kwa nusu, kiwango cha figo kushindwa kufanya kazi kilipungua kwa asilimia 74, na kiwango cha matatizo ya utumbo kilipungua kwa asilimia 62. Uchunguzi huo ulifanywa kwa utaratibu maalum na ulichunguza wagonjwa 5,065 ambao walitibiwa kwenye hospitali 70 katika nchi 17. Zamani, madaktari wapasuaji hawakuwaruhusu wagonjwa wao watumie aspirini kwa siku kadhaa kabla ya upasuaji au mara tu baada ya hapo, wakihofu kwamba ingewafanya wavuje damu nyingi. Hata hivyo, uchunguzi huo ulionyesha kwamba ni wagonjwa wachache tu waliovuja damu baada ya kupewa aspirini muda mfupi tu baada ya upasuaji na kwamba kiasi kidogo cha dawa kama vile aspirini ya watoto kilitosha. Inakadiriwa kwamba kufuata matokeo ya uchunguzi huo kunaweza kuokoa uhai wa watu 27,000 kila mwaka ulimwenguni pote.

Usingizi Ni Muhimu Katika Kujifunza Mbinu Mpya za Kuendesha Gari

Wanasayansi wanasema kwamba kulala vya kutosha usiku baada ya kujifunza mbinu mpya za kuendesha gari ni muhimu ili kuzikumbuka. Ijapokuwa kwa muda mrefu wamejua kulala usingizi wa kutosha ni muhimu ili kukumbuka habari na mambo mengine, bado hawakujua jinsi usingizi unavyoathiri mbinu za kuendesha gari, ambazo zinahifadhiwa katika sehemu nyingine ya ubongo. Uchunguzi mpya huko Ujerumani na Marekani unaonyesha kwamba ingawa usingizi ni muhimu katika kuhifadhi habari katika ubongo ni lazima mtu alale “katika wakati unaofaa kabisa,” lasema jarida Proceedings of the National Academy of Sciences. Watu waliofundishwa mbinu mpya jioni na wakajaribiwa tena baada ya kulala vya kutosha walifanya vyema kuliko wale waliozoezwa asubuhi na kujaribiwa baada ya muda wa saa 12 kupita kabla ya kwenda kulala.

“Hataki Tena Kuwa Mkatoliki”

Huko Italia, Mkatoliki aliyebatizwa ambaye “hataki tena kuwa Mkatoliki” sasa anaweza kuondoka, laripoti gazeti Il Sole-24 Ore. Hapo awali, maombi ya jina kuondolewa kwenye orodha ya waliobatizwa yalikataliwa kwa msingi wa kwamba “yangeharibu historia ya Kanisa.” Hata hivyo, baada ya watu kadhaa kuomba waondolewe kwenye orodha ya kanisa, mdhamini anayelinda habari za kibinafsi aliagiza orodha ya kanisa ya waliobatizwa irekebishwe na kuongezwa taarifa hii: “Hataki tena kuwa Mkatoliki.” Tayari mdhamini huyo amewaagiza makasisi wa parokia wakubali maombi ya angalau waumini watatu.

Nyumba Zaongezeka kwa Sababu ya Familia Zilizovunjika

Uchunguzi wa kimataifa uliofanywa chini ya uongozi wa Dakt. Jianguo Liu wa Chuo Kikuu cha Michigan State, Marekani, ulionyesha kwamba hata katika nchi ambazo idadi ya watu inapungua, nyumba zinaongezeka familia zinapovunjika na watoto kuanza kuishi peke yao. Kadiri nyumba zaidi zinavyojengwa kwa ajili ya idadi hiyo ya watu, miji inapanuka na mazingira yanazidi kuharibika. “Kwa mfano, nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala, hujengwa kwenye ardhi yenye ukubwa uleule, kwa kiasi kilekile cha vifaa, na hutumia kiasi kilekile cha fueli iwe na watu wawili au wanne,” laripoti New Scientist. Wachunguzi wanatabiri kwamba ikiwa hali itaendelea hivyo, kutakuwa na nyumba milioni 233 zaidi kufikia mwaka wa 2015.

Akina Mama Vijana

Huko Mexico asilimia ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 10 na 19 wanaopata mimba “imeongezeka kwa asilimia 50 katika miongo mitatu iliyopita,” lasema gazeti Cambio la Mexico City. Ongezeko hilo limetukia licha ya kampeni za kupanga uzazi na elimu ya ngono katika shule za umma. Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa afya unafunua kwamba “vijana wanaovuta sigara, au kutumia dawa fulani haramu wana mwelekeo wa kufanya ngono wakiwa na umri mdogo kwa kiwango kinachozidi mara nne ya wale wasiotumia vitu hivyo.” Isitoshe asilimia 30 ya akina mama vijana hupata mtoto wa pili bila mpango, kabla ya mwaka mmoja kwisha tangu kuzaliwa kwa mtoto wa kwanza na asilimia 50 hujifungua mtoto wa pili kabla ya miaka miwili kwisha. Pamoja na matatizo yanayohusiana na utineja na mimba za kabla ya utineja, asilimia 60 ya akina mama hao vijana hulazimika kuwalea watoto wao bila baba.

Asidi Yaharibu

Karibu asilimia 65 ya vitabu na hati zilizochapishwa kati ya mwaka wa 1875 na 1960 ambazo zimehifadhiwa katika maktaba ya kitaifa huko Paris ziko katika hatari ya kuharibiwa, laripoti gazeti Le Monde. Vitabu na hati hizo zinaharibiwa polepole na asidi salfuriki, ambayo hufanya kurasa zikauke na kuchanika. Vitabu 20,000 hivi huondolewa asidi kila mwaka na huduma za maktaba ya Kitaifa, kwa gharama ya dola 7 hadi 8 kwa kitabu. Tangu miaka ya 1980, vitabu vingi vimechapishwa kwa karatasi zisizo na asidi.

Wamebatizwa, Lakini Hawatendi

“Hispania bado ni taifa la [Wakatoliki] waliobatizwa, lakini wengi wao ni Wakatoliki wasiotenda,” laripoti gazeti la Kihispania la El País. Wakati wa utawala wa kimabavu wa Jenerali Franco, “Katoliki ilikuwa dini rasmi ya taifa, na dini nyingine zote zilipigwa marufuku na kunyanyaswa. Katika sehemu za mashambani, ilikuwa lazima kuhudhuria Misa kila Jumapili, na wale waliojaribu kukiuka sheria hiyo ya kanisa wangetozwa faini au kuadhibiwa,” lasema gazeti hilo. Siku hizi, hali imebadilika sana. Utafiti uliofanywa na Kituo cha Uchunguzi wa Masuala ya Kijamii (CIS katika Kihispania), ulionyesha kwamba asilimia 18.5 ya Wahispania huhudhuria Misa kwa ukawaida. “Kanisa Katoliki liliokoka vita vya [wenyewe kwa wenyewe] na utawala wa kimabavu wa Franco, lakini uchunguzi wa CIS unaonyesha kwamba ni vigumu sana sasa kulirudisha katika hali ya awali,” lasema El País.