Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Madhara ya Sura Yenye Kuvutia

Madhara ya Sura Yenye Kuvutia

Madhara ya Sura Yenye Kuvutia

BILA shaka kufuatia mitindo kwaweza kukusaidia kuboresha sura yako na kukufanya ujiamini zaidi. Vazi linalofaa linaweza kuficha kasoro fulani na hata kuboresha maumbo yako yanayopendeza. Pia linaweza kuathiri jinsi wengine wanavyokuona.

Lakini kuna madhara yanayotokezwa na mitindo, ambayo hayapaswi kupuuzwa. Wanunuzi wanaweza kunaswa katika mtego wa kununua mavazi mapya kila wakati. Kwani, viwanda huzidi kutokeza mitindo mipya. Wabuni wa mitindo hupata pesa nyingi mitindo inapopitwa na wakati. Kama alivyosema mbuni Gabrielle Chanel, “mitindo huanzishwa ili ipitwe na wakati.” Kwa hiyo, mnunuzi asiye na habari anaweza kuhisi kwamba lazima anunue mavazi mapya ili asipitwe na wakati.

Pia kuna hatari ya kunaswa na matangazo ya biashara bila kujua. Viwanda vya mitindo hutumia mamilioni ya dola kutangaza bidhaa zao, mara nyingi vikionyesha maisha ya raha ambayo eti hufurahiwa na wale wanaovaa mavazi ya viwanda hivyo. Matangazo hayo yanaweza kuwa na matokeo sana. “Hakuna kitu chenye kuvunja moyo kwa matineja kama kutokuwa na ‘chapa inayofaa’ ya viatu,” asema mwalimu mmoja nchini Hispania.

Mtego wa Mitindo

Vikundi fulani hutumia mitindo fulani ya mavazi ili kujitambulisha. Mavazi yao huenda yakaonyesha uasi, maisha ya kutojali, au hata jeuri au chuki kuelekea jamii fulani. Ingawa baadhi ya mitindo hiyo huenda ikapita kiasi au kuwa yenye kushtua, kwa kawaida wengi katika kikundi hicho huvalia mavazi ya aina moja. Hata wengine ambao hawaungi mkono malengo ya kikundi hicho wanaweza kuvutiwa na mtindo wao. Wale wanaofuata mitindo hiyo ya mavazi huenda wakawafanya wengine wawaone kuwa wanapendezwa na wanaunga mkono malengo ya kikundi hicho.

Kwa kawaida mitindo huja na kupita, mingine hutoweka baada ya miezi michache. Huenda ikatokana na mwanamuziki mashuhuri au mwanzilishi mwingine wa mitindo. Ingawa hivyo, mitindo michache tu ndiyo hudumu. Kwa mfano, jinzi za bluu zilipendwa sana miongoni mwa vijana waliokuwa wakifanya maandamano katika miaka ya 1950 na 1960. Hata hivyo, sasa mavazi hayo huvaliwa na watu wa umri mbalimbali katika hali mbalimbali.

Kuhangaikia Umbo Bora

Wale ambao huthamini sana mitindo wanaweza kuhangaikia kupita kiasi sura yao. Kwa kawaida wanamitindo huwa warefu na wembamba, na picha zao huonyeshwa daima. * Umbo “kamili” hutumiwa kuuza chochote iwe ni magari au peremende. Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Kijamii cha Uingereza chakadiria kwamba “leo wanawake wachanga huona picha nyingi zaidi za wanawake warembo sana kwa siku moja kuliko wanawake ambao mama zetu waliwaona katika maisha yao yote ya ujana.”

Picha hizo nyingi zaweza kuwa na madhara. Kwa mfano, nchini Marekani uchunguzi ulionukuliwa katika Newsweek ulionyesha kwamba asilimia 90 ya matineja wazungu hawaridhiki na umbo lao. Baadhi yao wanaweza kufanya chochote ili wawe na ‘umbo kamili.’ Hata hivyo, Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Kijamii chadai kwamba chini ya asilimia 5 ya wanawake ndiyo inayoweza kufikia uzito na wembamba unaopendekezwa na vyombo vya habari. Isitoshe, kuhusudu maumbo membamba sana kumefanya mamilioni ya wanawake vijana wawe watumwa. Kumewafanya baadhi yao wawe na tatizo la kujinyima chakula. * Mwanamitindo Mhispania, Nieves Álvarez, aliyekuwa na tatizo la kujinyima chakula, akiri hivi: “Niliogopa sana kunenepa kuliko nilivyoogopa kifo.”

Ni kweli kwamba, matatizo ya kula kama vile kujinyima chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida, yanaweza kusababishwa na mambo mbalimbali. Hata hivyo, Madaktari Anne Guillemot na Michel Laxenaire wanasema hivi: “Kuhusudu wembamba kumechangia tatizo hilo kwa kiasi fulani.”

Ni wazi kwamba, mitindo ina mafaa na madhara. Hutosheleza tamaa ya msingi ya wanadamu ya kutaka kupendeza na kuwa na mavazi mapya. Lakini mitindo inayopita kiasi inaweza kumfanya mtu avae mavazi ambayo huwafanya wengine wawe na maoni mabaya. Na tukiiona sura kuwa muhimu kupita kiasi, tunaweza kuwa na maoni yasiyofaa kwamba ubora wetu hutegemea ‘sura’ yetu badala ya sifa zetu za moyoni. “Lazima tuanze kuthamini zaidi uwezo wa mtu na utu wake wa ndani, badala ya sura yake tu,” asema Álvarez, aliyenukuliwa awali. Lakini huenda itachukua muda kabla ya watu kuanza kuwa na maoni hayo. Basi, tunawezaje kuwa na maoni yanayofaa kuelekea mitindo?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Kwa kawaida wanamitindo hutazamiwa kuwa na urefu wa “angalau meta 1.74, wembamba sana, wenye midomo mikubwa, mashavu yenye kupendeza, macho makubwa, miguu mirefu na iliyonyooka, pua ambayo si kubwa sana,” laripoti gazeti Time.

^ fu. 10 Shirika la Kitaifa la Marekani la Ugonjwa na Matatizo ya Kujinyima Chakula linakadiria kwamba watu milioni 8 huwa na ugonjwa wa kujinyima chakula nchini Marekani peke yake na kwamba wagonjwa kadhaa walio mahututi hufa. Walio wengi kati yao (asilimia 86) walianza kuwa na matatizo ya kula kabla ya kufikia umri wa miaka 21.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Je, kwa Kweli Mtu Anaweza Kuvaa Vazi Hilo?

Majumba ya mitindo ya New York, Paris, na Milan huonyesha mavazi ya wabuni bora zaidi kila majira ya kuchipua na majira ya majani kupukutika. Mbali na bei ghali za mavazi hayo, mingi ya mitindo hiyo huwa isiyofaa au isiyoweza kuvaliwa. “Mitindo inayopita kiasi, na ya kiajabu unayoona kwa kweli haikubuniwa ili ivaliwe na watu wa kawaida,” asema mbuni Mhispania, Juan Duyos. “Kusudi la maonyesho ya mitindo laweza kuwa kuvuta uangalifu kwa mbuni au kwa jina la kampuni fulani, kuliko kuuza mavazi hayo. Kwa mfano, mavazi yenye kuvutia ambayo hutangazwa sana katika vyombo vya habari yanaweza kuwafanya watu wanunue mavazi au marashi yenye jina la mbuni fulani.”

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kufuatia mitindo kwaweza kugharimu sana

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kufuatia mtindo fulani wa mavazi kwaweza kumtambulisha mtu kuwa mshiriki wa kikundi fulani

[Picha katika ukurasa wa 7]

Watu fulani wametumbukia katika tatizo la kujinyima chakula