Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Desturi ya Kale ya Piñata

Desturi ya Kale ya Piñata

Desturi ya Kale ya Piñata

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

WATOTO wanafanya sherehe mtaani. Tunawasikia wakipiga kelele: “Dale! Dale! Dale!” (Piga! Piga! Piga!) Tunachungulia uani na kuona punda aliyetengenezwa kwa karatasi yenye rangirangi akining’inia kati ya miti miwili. Mtoto aliyefunikwa macho anampiga punda huyo kwa fimbo akijaribu kumtoboa. Wageni wanashangilia. Hatimaye, punda anatoboka, na peremende, matunda, na vitu vya kuchezea vinamwagika. Wote wanacheka waking’ang’ania vitu hivyo na wanafurahi sana. Tunaambiwa kwamba punda huyo anaitwa piñata na kwamba ni desturi kumtoboa kwenye karamu za huku Mexico na katika baadhi ya nchi za Amerika Kusini.

Hatujui kwa nini desturi ya piñata inapendwa na watu wengi. Ilianzaje? Je, kumtoboa piñata kuna maana yoyote ya pekee? Tuliamua kuchunguza.

Jinsi Piñata Ilivyoanza

Watu wengi wanasema kwamba huenda Wachina ndio wa kwanza kutumia kitu kilichofanana na piñata katika sherehe zao za Mwaka Mpya, ambazo pia ziliashiria mwanzo wa majira ya kuchipua. Walitengeneza sanamu za ng’ombe, fahali, na nyati wakitumia karatasi yenye rangi iliyojazwa aina tano za mbegu. Fimbo zenye rangi zilitumiwa kutoboa sanamu hizo. Karatasi yenye rangirangi iliyokuwa imefunika sanamu hizo, iliteketezwa na majivu yake yakahifadhiwa ili yalete bahati njema mwaka uliofuata.

Inaaminika kwamba katika karne ya 13, msafiri wa Venice, Marco Polo, alianzisha desturi hiyo ya China nchini Italia. Halafu ilipewa jina lake la sasa kutokana na neno la Kiitalia pignatta, linalomaanisha chungu chepesi. Chungu hicho kilijazwa vitu visivyo na thamani kubwa, vito, au peremende badala ya mbegu. Baadaye desturi hiyo ilisambaa hadi Hispania. Katika kila Jumapili ya kwanza ya Kwaresima, * watu walitoboa piñata. Inaonekana mishonari Wahispania ndio walioanzisha desturi ya piñata nchini Mexico mwanzoni mwa karne ya 16.

Hata hivyo, haikosi mishonari walishangaa (kama sisi) kuwakuta watu wa Mexico wakifuata desturi hiyo pia. Waazteki walisherehekea sikukuu ya kuzaliwa kwa mungu wao wa jua na vita aitwaye Huitzilopochtli kwa kuweka chungu juu ya kigingi kilichokuwa ndani ya hekalu lake mwishoni mwa mwaka. Chungu hicho kilirembeshwa kwa manyoya yenye rangirangi na kujazwa vito vingi vidogo. Kisha chungu hicho kilipasuliwa, na vito vilivyomwagika vikawa matoleo kwa sanamu ya mungu huyo. Wamaya pia walicheza mchezo ambapo watu waliofunikwa macho walipiga chungu cha udongo kilichoning’inizwa kwa kamba.

Mishonari Wahispania walitumia piñata kama mbinu ya kuwahubiria Wahindi, na iliwakilisha pia jitihada za Wakristo za kumshinda Ibilisi na dhambi. Piñata ya awali ilikuwa chungu chenye umbo la nyota kilichofunikwa kwa karatasi yenye rangirangi na nyuzi ziliwekwa kwenye ncha zake saba. Inasemekana kwamba ncha hizo ziliwakilisha dhambi saba zinazoweza kusababisha kifo, yaani pupa, ulafi, uzembe wa kiroho, kiburi, wivu, hasira, na harara. Kupiga piñata mtu akiwa amefunikwa macho kulionyesha kwamba mtu ana imani kali na azimio la kushinda vishawishi au uovu. Vitu vilivyokuwa ndani ya piñata vilikuwa zawadi ya kazi yake.

Piñata ya Leo

Baadaye, piñata ikawa sehemu ya sherehe za posada * katika majira ya Krismasi na bado iko hivyo hata leo. (Piñata yenye umbo la nyota huwakilisha nyota ambayo iliwaongoza wanajimu hadi Bethlehemu.) Kutoboa piñata huwa jambo muhimu sana wakati wa sherehe za sikukuu ya kuzaliwa. Ama kweli, piñata zimekuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa Mexico hivi kwamba nchi hiyo inauza sanamu hizo katika nchi nyingine.

Tuligundua kwamba kwa watu wengi nchini Mexico, desturi ya piñata haina maana yoyote ya kidini, na wengi wao huiona kuwa tafrija tu. Kwa hakika, piñata hutumiwa katika sherehe nyingi nchini Mexico, si katika sherehe za posada ama sikukuu za kuzaliwa tu. Na piñata huuzwa zikiwa na maumbo mengi tofauti-tofauti mbali na umbo la kawaida la nyota. Wakati mwingine hizo hutengenezwa zikiwa na umbo la wanyama, maua, au wanadamu.

Wakristo wanapaswa kujali dhamiri za wengine wanapoamua kutumia piñata katika sherehe zao. (1 Wakorintho 10:31-33) Jambo kuu ni jinsi watu wa kwenu wanavyoiona leo, si kile ilichomaanisha miaka mingi iliyopita. Ni kweli, watu wa maeneo mbalimbali wanaweza kuwa na maoni yanayotofautiana. Hivyo ni vizuri kuepuka kulifanya jambo hilo kuwa suala kubwa. Biblia inasema hivi: “Acheni kila mmoja afulize kutafuta sana, si faida yake mwenyewe, bali ya mtu yule mwingine.”—1 Wakorintho 10:24.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Katika dini nyingine, kama vile Katoliki, Kwaresima ni kipindi cha siku 40 cha kutubu mwishoni mwa sherehe za Juma Takatifu la Pasaka.

^ fu. 11 Nchini Mexico, sherehe za posada ni sherehe za siku tisa kabla ya Krismasi ambazo huonyesha Yusufu na Maria wakitafuta posada, yaani malazi. Piñata hutobolewa kila usiku kwa siku tisa kuonyesha kwamba sherehe imemalizika.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Unapoamua kutumia “piñata” kwenye sherehe, fikiria dhamiri za wengine

[Picha katika ukurasa wa 23]

“Piñata” huwa na maumbo na ukubwa mbalimbali