Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kucheza Dansi Pamoja na Korongo

Kucheza Dansi Pamoja na Korongo

Kucheza Dansi Pamoja na Korongo

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

KATIKA jiji la Pusan la Korea Kusini, unaweza kutazama dansi ya kipekee ya kitamaduni. Wanaume wanaocheza dansi hiyo huvalia kanzu nyeupe na kofia ndefu nyeusi, hupunga mikono, huzunguka na huinama, na hata kusimama kwa mguu mmoja.

Wamejifunza dansi hiyo ya pekee isiyo na mpango maalumu kwa kuwaiga korongo wenye taji jekundu. Kwa mamia ya miaka, korongo hao wamekuwa wakihamia Korea Kusini kila mwaka ili kuepuka majira ya baridi kali katika maeneo yao ya kuzalia. Wakazi wa nchi hiyo walivutiwa sana na dansi ya pekee ya korongo hao hivi kwamba walibuni dansi ya kitamaduni kwa kuwaiga ndege hao.

Watu wanaopenda maumbile, huko Hokkaido, Japan, umbali wa kilometa 1,500 kutoka Korea, humiminika kwenye Mbuga ya Kushiro Shitsugen ili kutazama dansi ya korongo hao. Kikundi kimoja cha korongo wenye taji jekundu huko Japan sasa kina mamia ya ndege kwa sababu korongo hao hulishwa katika majira ya baridi kali. Inavutia sana kuwatazama ndege hao wenye rangi nyeupe na nyeusi wakicheza kwa shauku katika theluji. Mwandishi wa gazeti National Geographic, Jennifer Ackerman, anatumia neno aware la Kijapani anapoeleza jinsi anavyovutiwa na korongo hao. Anasema kwamba neno hilo linafafanua “hisia zinazochochewa na kitu maridadi kinachodumu kwa muda mfupi sana.”

Watu wamevutiwa na korongo tangu siku za kale na korongo hupatikana katika mabara yote ila Amerika ya Kusini na Antaktika. Picha za ndege hao zimechorwa kwenye kuta za mapango barani Afrika, Australia, na Ulaya. Katika Mashariki ya Asia, ambako korongo ni mfano wa maisha marefu na furaha, wasanii hupenda kuchora picha za ndege hao. Yaelekea korongo huonwa kuwa mfano wa furaha ya ndoa kwa sababu korongo huwa na mwenzi mmoja tu maishani. Kwa hiyo, mara nyingi kanzu za arusi huwa na picha za korongo. Watu wa Korea wanaona ni muhimu kuwahifadhi korongo hao kwa sababu wao ni wa pekee na maridadi sana. Noti za Japan za yen 1,000 zina picha ya korongo wanaocheza dansi. Na miaka 2,500 iliyopita Wachina walibuni “dansi ya korongo weupe.” Huenda watu wanapendezwa na korongo kwa sababu ndege hao wanapenda sana kucheza dansi.

Dansi ya Korongo

Aina zote 15 za korongo hucheza dansi. Hata vifaranga ambao hawajafikia umri wa siku mbili hujitahidi kucheza. Kitabu Handbook of the Birds of the World kinaeleza kwamba “ndege wengine hucheza dansi pia, lakini hawachezi mara nyingi kama korongo wala . . . hawachezi kwa madaha sana.” Dansi ya korongo ni yenye kubadilika-badilika na ya fahari sikuzote, tukizingatia jinsi ambavyo ndege hao wakubwa hujiendesha kwa madaha na kurukaruka juu sana wakiwa wameyakunjua mabawa. Kitabu Handbook of the Birds of the World kinaongeza kwamba dansi ya korongo “huchezwa katika hatua mbalimbali zinazohusisha kuinama, kurukaruka, kukimbia, kupaa, na kutua.” Na kama wanadamu, korongo wachache wanapoanza kucheza dansi wote wengine hujiunga nao. Huko Afrika watu wamewaona korongo 120 wa kijivu wenye taji wakicheza pamoja wakiwa wawili-wawili.

Kwa nini korongo hucheza? Je, wanacheza ili wapate mazoezi ya mwili, kwa ajili ya mawasiliano au kuonyesha kwamba wako tayari kujamiiana, kwa sababu wametishwa, au kwa sababu wanafurahia maisha? Hatujui ikiwa korongo hucheza dansi kwa sababu hizo zote au mojawapo tu. Ni wazi kwamba korongo hupenda kucheza dansi wakiwa wawili-wawili, nao hucheza wakiwa tayari kujamiiana. Lakini, hata korongo wachanga hucheza dansi, na kwa kawaida hao ndio wanaocheza kwa shauku zaidi. Kitabu Handbook of the Birds of the World kinamalizia kwa kusema kwamba “inavutia sana kuwatazama korongo wanapocheza dansi, hata sababu yao ya kucheza iwe nini.”

Safari za Korongo

Mara nyingi unaweza kuwasikia korongo kabla hujawaona. Unaweza kusikia mlio wao mrefu kama wa tarumbeta, hata ingawa huenda wakawa mbali sana. Yaelekea mlio huo huwasaidia kuambatana katika safari zao ndefu za kuhama. Aina nyingi za korongo huhama maeneo ya kaskazini ya kuzalia. Kabla ya majira ya baridi kali kuanza huko Kanada, Skandinavia, au Siberia wao husafiri mwendo mrefu sana hadi sehemu za joto za China, India, Marekani (Texas), au eneo la Mediterania. Safari hizo za korongo ni hatari na zenye kuchosha. Korongo fulani wanaotoka Ulaya na Asia wameonekana wakiruka kwenye mwinuko wa meta 10,000 hivi walipokuwa wakivuka milima ya Himalaya wakielekea India. Korongo huruka wakiwa wamejipanga kwa muundo wa herufi ya V na wakifikia hewa yenye joto wao hutumia nafasi hiyo kunyiririka mbali iwezekanavyo bila kutumia mabawa. Hata hivyo, wanapovuka bahari na maziwa ni lazima watumie mabawa. *

Kwa miaka 20 hivi, Juan Carlos Alonso, mtaalamu wa ndege Mhispania, amechunguza safari za wale korongo 70,000 wa Asia na Ulaya wanaohamia Hispania kila mwaka. Anasema hivi: ‘Baadhi ya ndege hutiwa alama mguuni na wengine wanawekwa vifaa vya kupokea na kupasha habari ili tujue mahali walipo wanaposafiri. Mimi husisimuka sana ninapomwona ndege huku Hispania, niliyemtia alama mguuni huko Ujerumani Kaskazini alipokuwa mdogo. Kwa mamia ya miaka, korongo wamepitia sehemu zilezile wanapohama. Mmoja aliyetiwa alama nchini Ufini, alipatikana Ethiopia, na baadhi ya korongo kutoka Siberia huhamia Mexico.’

Wamelindwa na Mwanadamu Wasitoweke Kabisa

Kwa sasa, aina 9 kati ya zile aina 15 za korongo zinakabili uwezekano wa kutoweka kabisa. Hali ya korongo aina ya whooping wa Amerika Kaskazini ni mbaya zaidi. Kulikuwa na ndege 14 tu wa aina hiyo mwaka wa 1938. Hata hivyo, kwa sababu ya mipango ya kuzalisha korongo hao wakiwa wamefungiwa, na kulinda makao yao porini, idadi yao imeongezeka polepole kufikia zaidi ya 300. Wataalamu wa maumbile huzalisha vifaranga kisha huwapeleka kwenye maeneo ya porini yaliyolindwa. Hivi majuzi ndege ndogo zimetumiwa kwa mafanikio kuwaongoza korongo wachache wachanga aina ya whooping hadi eneo wanalopaswa kuhamia kabla ya majira ya baridi kali kuanza. Wanasayansi nchini Urusi hutumia mbinu kama hizo kuwalinda korongo wa Siberia ili wasitoweke kabisa.

Simulizi moja linalovutia sana kuhusu jinsi korongo walivyosaidiwa linatoka nchini Japan. Korongo wachache wenye taji jekundu huko Hokkaido hawakuhama kwa ukawaida kwa sababu ndege hao waliweza kupata chakula wakati wa majira ya baridi kali kandokando ya vijito vilivyokuwa karibu na chemchemi za maji ya moto. Hata hivyo, katika majira ya baridi kali ya mwaka wa 1952 hata vijito hivyo vilifunikwa kwa barafu na ilionekana kama korongo hao 30 wangekufa wote. Lakini watoto wa shule wa hapo walitawanya mahindi kwenye barafu iliyofunika vijito na ndege hao wakanusurika. Tangu wakati huo, korongo hao wamelishwa kwa ukawaida, na idadi ya ndege katika kundi hilo imeongezeka kufikia 900 hivi. Hiyo ni karibu thuluthi ya korongo wote wenye taji jekundu wanaopatikana ulimwenguni pote.

Wakati Ujao Usiojulikana

Kama vile aina nyingine nyingi za ndege, korongo wameathiriwa kwa sababu makao yao yenye majimaji na mbuga yamepunguka sana. Korongo wamelazimika kuzoea kukaa karibu na wanadamu. Kwa kawaida wao hupenda kukaa mbali na wanadamu, lakini wasiposumbuliwa wanaweza kuzoea kukaa karibu na watu. Nchini India, korongo aina ya sarus, ambaye ni mrefu zaidi kati ya ndege wote wanaoruka, amezoea kuzaa kwenye vidimbwi vya vijiji. Korongo wengine ambao wamezoea kukaa karibu na wanadamu hula kwenye mashamba wanapokuwa wakihama au wakiwa katika eneo wanalohamia katika majira ya baridi kali.

Inatumainiwa kwamba jitihada za kuwahifadhi korongo katika nchi nyingi zitazuia ndege hao wenye madaha wasitoweke kabisa. Ingehuzunisha sana ikiwa wakati ujao watu hawataweza kufurahia dansi ya korongo au kusikia milio yao wanapoelekea sehemu za kusini za dunia kabla ya majira ya baridi kali kuanza sehemu za kaskazini.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Maelfu ya korongo kutoka Asia na Ulaya hupita nchi ya Israel wanapohama kabla ya majira ya baridi kali kuanza katika maeneo yao ya kuzalia na wanaporudi kwenye maeneo hayo. Wengine wao pia huhamia nchi hiyo. Jioni-jioni katika sehemu ya kaskazini ya Bonde la Yordani, watu wanaweza kuona vikundi vya korongo wakipita Mlima Hermoni uliofunikwa kwa theluji. Lakini mandhari hiyo yenye kuvutia huonekana kwa muda mfupi tu.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Korongo wenye taji jekundu, Asia

[Picha katika ukurasa wa 16]

Picha kwenye chombo kilichotengenezwa Korea

[Picha katika ukurasa wa 16]

Korongo weusi na weupe wenye manyoya masikioni

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Korongo wa kawaida wa Ulaya wanaposafiri

[Picha katika ukurasa wa 17]

Korongo wenye taji