Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wanyama Walevi

Kulingana na ripoti kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni, si wanadamu pekee ambao hulewa wanapokunywa pombe. Hivi majuzi, tembo waliolewa baada ya kunywa pombe katika kijiji cha Assam, India, waliharibu majengo. Huko Bosnia, dubu aliyezoea kunywa pombe iliyobaki kwenye mikebe iliyotupwa, alitamani kupata pombe zaidi. Wanavijiji walipochoshwa na usumbufu wa dubu huyo mlevi, walianza kumpatia pombe isiyolewesha na wakafanikiwa kumdhibiti. Ingawa bado dubu huyo anafurahia kinywaji chake, sasa si mkali kama alivyokuwa awali. Huko kaskazini mwa California, ndege waliolewa kwa kula matunda yanayokua kando ya barabara walishambulia magari. Jambo hilo lilisuluhishwa kwa kuikata miti inayozaa matunda hayo. Nyuki waliolewa baada ya kunywa maji yaliyochacha ya maua hupanda juu ya miti au kuanguka chini, wasijue njia ya kurudi kwenye mizinga. Wale wanaofaulu kufika mizingani hushambuliwa na nyuki walinzi ambao hujitahidi kuzuia nyuki wengine wasiambukizwe ulevi.

Samaki Kutoka Juu

Mamia ya samaki wadogo waliotoka Ziwa Dojran au Ziwa Korónia, walipatikana katika kijiji cha Koróna, laripoti gazeti la Ugiriki Eleftherotypia. “Wanakijiji waliwapata samaki walioanguka kutoka juu wakiwa wametapakaa kila mahali.” Kulingana na mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya hewa ya Thessalonica, Christos Balafoutis, hilo halikuwa jambo jipya. Mawingu ya dhoruba katika hali fulani ya hewa hutokeza upepo wa kisulisuli ambao hubeba maji pamoja na samaki na vyura kutoka ziwani. Ripoti hiyo inasema kwamba “upepo huo unaweza kuyabeba maji hayo juu sana na kuyapeleka mbali sana.” Baadaye samaki hao huanguka chini upepo huo wa kisulisuli unaposhindwa kuwashikilia zaidi.

Mahangaiko ya Vijana

“Wazazi wana wasiwasi mwingi kwamba vijana wao watatumia dawa za kulevya hivi kwamba wanashindwa kutambua matatizo mazito ya kihisia na kiakili yanayowakumba watoto wao,” lasema gazeti The Times la London. Kati ya wazazi zaidi ya 500 na vijana zaidi ya 500 waliohojiwa katika uchunguzi mmoja, asilimia 42 ya wazazi wanaamini kwamba utumizi wa dawa za kulevya ndilo tatizo kubwa zaidi ambalo watoto wao wanakabili. Lakini ni asilimia 19 tu ya vijana wanaoona kuwa dawa za kulevya ni tatizo kubwa. Asilimia 31 ya vijana wanahangaikia marafiki na familia zao, na asilimia 13 wanaogopa kudhulumiwa shuleni. Mkurugenzi wa shirika lililofanya uchunguzi huo ambalo hutoa ushauri kupitia simu, Justin Irwin, alisema kwamba wazazi wanakosa kutambua matatizo ya kiakili na kihisia ya vijana wao. Aliwatolea wazazi mwito huu: “Acheni kukisia tu. Oneni mambo kihalisi.”

Madhara ya Kutolala vya Kutosha

“Asilimia tisa ya Wapolandi hulala kwa muda unaopungua saa tano kila siku,” laripoti gazeti Wprost la Warsaw. “Mtu 1 kati ya 3 hulala kwa muda usiozidi saa 6.5 kila siku nchini Marekani na Uingereza.” Kulingana na Michał Skalski wa kliniki moja inayoshughulikia matatizo ya usingizi nchini Poland, “watu ambao hawalali vya kutosha huwa na mfadhaiko sikuzote.” Gazeti Wprost laripoti kuhusu uchunguzi mmoja uliofanywa nchini Japan unaoonyesha kwamba “watu wanaolala kwa muda wa saa tano au chini ya hapo, wana uwezekano mara mbili zaidi wa kupata mshtuko wa moyo kuliko wale wanaolala kwa muda wa saa nane kila siku.” Isitoshe, uchunguzi mwingi ambao umefanywa nchini Marekani unaonyesha kwamba kutolala vya kutosha kunaweza kusababisha kisukari na magonjwa mengine. Ripoti hiyo inasema kwamba kutolala vya kutosha “huathiri ujenzi na uvunjaji wa glukosi” na kuchangia “ongezeko la unene.” “Wakati ambapo umechoka, mwili wako hujaribu kuongeza nishati,” laeleza gazeti American Fitness. “Watu ambao hawalali vya kutosha hula na kunywa zaidi ili wakae macho. Kwa hiyo, ikiwa umepunguza uzito wako na hutaki kuwa mnene tena, lala zaidi.”

Kinachoendelea Kazini

Gazeti London Magazine liliwahoji watu 511 kuhusu kinachoendelea kazini katika siku ya kawaida. Gazeti The Daily Telegraph la London liliripoti kwamba nusu ya watu hao walisema kwamba walikunywa pombe wakiwa kazini, asilimia 48 waliiba, na karibu thuluthi moja walitumia dawa haramu. Isitoshe, asilimia 42 “walifikiria kumuua tajiri wao,” karibu thuluthi moja “walitazama picha chafu kwenye Internet,” “asilimia 62 walitongozwa na wafanyakazi wenzao, na karibu mtu 1 kati ya 5 alifanya ngono ofisini.” Asilimia 36 ya wafanyakazi hao walidanganya kwenye barua zao za kuomba kazi, asilimia 13 walisema wangefanya ngono na tajiri wao ili wapandishwe cheo, na asilimia 45 wangemchongea mfanyakazi mwenzao ili wapandishwe cheo. Kulingana na daktari wa akili Philip Hodson, tabia hizo husababishwa hasa na chuki kuwaelekea wenye mamlaka. Alisema hivi: “Tuko tayari kufanya jambo lolote ili tupate cheo. Heshima, cheo, na hadhi ndiyo mambo tunayoona kuwa muhimu zaidi.”

Wanamichezo Wanakufa Ghafula

Wakati watu watatu wenye umri wa miaka 50 na kitu walipokufa ghafula siku moja kutokana na mshtuko wa moyo baada ya kukimbia mbio za masafa marefu katika sehemu mbalimbali za Japan, madaktari wa wanamichezo walitoa tahadhari. Dakt. Masatoshi Kaku, mwenyekiti wa Chuo cha Michezo cha Kobe aliandika hivi katika gazeti Asahi Shimbun: “Asilimia 80 hivi ya vifo vya ghafula husababishwa na magonjwa ya moyo. . . . Zaidi ya asilimia 90 ya watu waliokufa walikuwa wamepewa vyeti na madaktari kuonyesha kwamba wana afya bora.” Dakt. Kaku anapendekeza kwamba moyo wa mtu uchunguzwe anapokuwa akifanya mazoezi bali si wakati amepumzika. Pia anasema kwamba mtu hapaswi kujikaza sana na anapendekeza watu waache kufanya mazoezi mara tu wanapopata mafua, wanapochafukwa na moyo, au kusikia kizunguzungu. Anasema hivi: “Kuondoka uwanjani kabla mbio hazijamalizika si jambo la kuaibikia.” Halafu anaongeza: “Wanariadha huona kwamba kumaliza mbio ni muhimu zaidi, lakini wanapaswa kubadili maoni yao ikihitajika.”

Umuhimu wa Mazungumzo ya Familia

“Mazungumzo ya familia yamezorota na kuwa ‘manung’uniko nyakati zote’ hivi kwamba watoto hawawezi kuzungumza vizuri,” laripoti gazeti The Times la London. Mkurugenzi wa shirika la Uingereza linalodumisha viwango vya elimu, Alan Wells, anasema jambo hilo linasababishwa na tabia ya watoto ya “kutazama televisheni, kutumia kompyuta, na familia kukosa nafasi ya kula pamoja.” Wells anasema kwamba jambo hilo pia linatokana na ongezeko la familia zenye mzazi mmoja ambazo hazina babu na nyanya, na wazazi kukosa kuwasomea watoto wao. Anaamini kwamba hiyo ndiyo sababu watoto wanaoanza kwenda shuleni wakiwa na umri wa miaka minne au mitano “hawawezi kuongea kwa ufasaha wala kuzungumza kwa njia inayoeleweka” kama zamani. Wells anapendekeza kuwe na mitaala ya kuwafundisha wazazi jinsi ya kuwasiliana na watoto wao.

Maisha Bora

Uchunguzi uliofanywa na shirika la kibinafsi la utafiti la Australia unaonyesha kwamba “katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, asilimia 23 ya Waaustralia wenye umri wa miaka 30 hadi 59 wameacha kazi zenye mshahara mnono ili waishi maisha sahili zaidi,” laripoti gazeti The Sydney Morning Herald. Mbinu hiyo inatumiwa na watu wengi zaidi wanaotaka kuishi maisha bora na kuwa pamoja na watoto wao kwa muda mrefu zaidi. Gazeti Herald linasema kwamba wafanyakazi hao “wanaanza kufanya kazi ambazo hazidai muda mwingi na ambazo hazilipi mshahara mkubwa, wanapunguza saa wanazofanya kazi au kuacha kazi kabisa.” Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Dakt. Clive Hamilton, anasema hivi: “Watu hao wanaona uhai kuwa muhimu kuliko pesa. Ni watu ambao hawajioni kuwa wameshindwa; ni watu wa kawaida ambao wanataka kupunguza mapato yao ili waishi maisha yenye usawaziko zaidi.”