Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mawasiliano ya Viumbe na Mimea

Mawasiliano ya Viumbe na Mimea

Mawasiliano ya Viumbe na Mimea

“Bila mawasiliano, kila kiumbe angekuwa kama kisiwa kilichojitenga na visiwa vingine.”—The Language of Animals.

IWE ni msituni, mbugani, au katika bustani yako, huenda wanyama mbalimbali wanawasiliana sasa hivi. Kitabu The Language of Animals kinasema hivi: “Wanyama hutumia hisi zote kuwasiliana. Wao hutoa ishara za mwili, huketi na kusimama kwa njia maalumu; hutoa na kunusa harufu kali kama vile vicheche waliotishwa wanavyofanya, hutoa harufu isiyo kali; hutoa kilio chembamba au cha hofu, huimba; hutoa na kupokea mawimbi ya umeme; humulika-mulika; hubadili rangi; ‘hucheza dansi;’ na hata hupigapiga na kutikisa ardhi wanapotembea.” Lakini hizo ishara zote zina kusudi gani?

Wanasayansi hufahamu maana ya ishara za wanyama kwa kuwachunguza kwa makini. Kwa mfano, wamegundua kwamba kuku anapomwona adui ambaye hawezi kuruka kama vile aina fulani ya kicheche, yeye huwaonya kuku wengine kwa kutoa sauti kali ya kuk, kuk, kuk. Lakini kuku anapomwona mwewe, yeye hutoa mlio mwembamba mrefu. Katika visa vyote viwili, kuku wale wengine huitikia upesi kupatana na aina ya mlio waliosikia. Hilo huonyesha kwamba wameelewana. Ndege wengine pia wameonekana wakitoa milio kama hiyo yenye ujumbe mbalimbali.

Kitabu Songs, Roars, and Rituals kinasema kwamba “njia moja kuu ya kuchunguza mawasiliano ya wanyama ni kurekodi mlio hususa na kuwachezea wanyama mlio huo kuona kama wataitikia kwa njia inayotarajiwa.” Wakati kuku walipojaribiwa kwa milio hiyo, waliitikia kama kawaida. Mbinu hiyo imetumiwa pia kuwachunguza buibui. Watafiti walichunguza kile kinachowavutia buibui wa kike aina ya wolf kwa buibui wa kiume ambao hujaribu kuwafurahisha buibui wa kike kwa kuwapungia miguu yao ya mbele yenye manyoya-manyoya. Watafiti hao walifanya majaribio hayo kwa kupiga picha ya video ya buibui wa kiume kisha wakaondoa manyoya ya miguu katika video hiyo. Walipocheza ukanda huo wa video mbele ya buibui wa kike, buibui huyo hakuvutiwa hata kidogo. Walijifunza nini? Inaonekana buibui wa kike aina ya wolf huvutiwa tu na buibui wa kiume wanaopunga miguu yenye manyoya!

Kuwasiliana kwa Harufu

Wanyama wengi huwasiliana kwa kutokeza kemikali kali zinazoitwa pheromone. Kwa kawaida wao huzitokeza kupitia tezi maalumu, mkojo, au kinyesi chao. Wanyama kama vile mbwa na paka hutia mpaka eneo lao kama tu mwanadamu anavyoweka jina au ua kuonyesha kwamba anamiliki eneo fulani. Ijapokuwa mipaka hiyo haionekani, inawasaidia wanyama wa jamii moja kuishi mbali-mbali.

Lakini zaidi ya kutia alama eneo fulani, kemikali za pheromone hutumiwa pia kwa njia nyingine. Kemikali hizo hutoa habari nyingi ambazo wanyama wengine huchunguza na kupendezwa nazo sana. Kitabu How Animals Communicate kinasema kwamba “huenda harufu za kemikali hizo zinaonyesha umri wa mnyama, jinsia, nguvu na sifa zake nyingine, [na] kama yuko tayari kujamiiana . . . Harufu hizo ni kama kitambulisho cha mnyama.” Wanyama fulani hawapendi alama walizoziweka zichezewe, jambo ambalo watunzaji wa bustani za wanyama wanafahamu. Baada ya kusafisha vizimba au sehemu zilizotengewa wanyama, watunzaji hao wamegundua kwamba wanyama wengi hutia alama tena sehemu zao bila kukawia. Naam, “mnyama anaweza kuvurugika na kutenda kwa njia isiyo ya kawaida na hata anaweza kuwa tasa iwapo hatanusa harufu yake,” chasema kitabu kilichonukuliwa juu.

Kemikali za pheromone ni muhimu hata kwa wadudu. Kwa mfano, aina fulani ya kemikali hizo huwachochea wadudu kuhama kwa wingi na kushambulia. Aina nyingine huwasaidia kutambua mahali chakula kipo au mahali pa kujenga makao. Hizo zinatia ndani kemikali zinazowachochea kujamiiana, na viumbe fulani huchochewa sana nazo. Nondo wa hariri wa kiume wana vipapasio viwili vidogo vyenye manyoya mengi madogo-madogo. Vipapasio hivyo vinaweza kutambua hata molekuli moja ya kemikali ambayo humchochea nondo wa kike kujamiiana! Nondo wa kiume anapotambua molekuli 200 za nondo wa kike, ataanza kumtafuta. Hata hivyo, si viumbe tu wanaowasiliana kwa kutumia kemikali.

Jinsi Mimea Inavyowasiliana

Je, ulijua kwamba mimea inaweza kuwasiliana na mimea mingine na hata kuwasiliana na wanyama fulani? Gazeti la Discover linasema kuwa watafiti huko Uholanzi waligundua kwamba maharagwe aina ya lima yanapovamiwa, huwa yanatoa kemikali ambayo huwavutia wadudu wengine ambao hushambulia wale wadudu wavamizi. Vivyo hivyo, mimea ya mahindi, tumbaku, na pamba, inapovamiwa na viwavi, hutoa kemikali zinazomvutia nyigu, ambaye ni adui mkubwa wa viwavi. Mtafiti mmoja alisema hivi: “Mimea haisemi tu, ‘Nimevamiwa,’ inasema pia yule aliyeivamia. Huo ni mfumo tata na wa ajabu sana.”

Mawasiliano baina ya mimea yanastaajabisha pia. Kulingana na gazeti Discover, watafiti ‘wameona miti ya willow, mipopla, miti ya alder, na mibetula ikisikiliza miti mingine ya aina yake, na mimea ya shayiri ikisikiliza mimea mingine ya shayiri. Mimea iliyoharibiwa, iwe ni kwa kuliwa na viwavi, kuvamiwa na kuvu au wadudu waharibifu, ilitoa kemikali ambazo inaonekana zilitahadharisha mimea ya karibu ili ianze kujikinga mapema.’ Hata miti isiyo ya jamii moja imewasiliana kwa njia hiyo ili kutoa tahadhari.

Mmea huanza kujikinga unapovamiwa au unapotahadharishwa kuhusu uvamizi. Kinga za mmea zinatia ndani kemikali zenye sumu zinazowaua wadudu wavamizi au zinazowafanya washindwe kumeng’enya mmea huo. Huenda katika siku za usoni utafiti kuhusu njia hiyo ya mawasiliano utatokeza habari zenye kustaajabisha, na huenda nyingine zitafaidi kilimo.

Kuwasiliana kwa Nuru

Mtaalamu wa uhusiano wa viumbe na mazingira, Susan Tweit, aliandika hivi katika makala iliyohusu vimulimuli: “Taa zao ndogo zinazoning’inia hewani na zinazomweka-mweka chini ya nyota zilirembesha sana mtaa wetu.” Tweit anasema kwamba wadudu hao wa jamii ya mbawakawa humulika “ili kuonya na vilevile kutuma na kupokea habari kutoka kwa mdudu wa kike au wa kiume wanapotaka kujamiiana.” Nuru yao huwa ya rangi ya kijani, ya manjano, na ya machungwa. Kwa kuwa kwa kawaida vimulimuli wa kike hawaruki sana, nuru nyingi tunayoona ni ya vimulimuli wa kiume.—Ona sanduku “Mwangaza wa Kimulimuli Usio na Joto.”

Kuna jamii 1,900 za vimulimuli, na kila jamii ina njia yake ya pekee ya kumulika-mulika. Wengine humulika-mulika mara tatu kila baada ya sekunde moja hivi au wanaweza kumulika-mulika kwa muda mrefu zaidi au mfupi zaidi. Kimulimuli wa kiume anapotafuta mwenzi, yeye hurukaruka akimulika-mulika kwa njia ya kumvutia mwenzi. Gazeti Audubon linasema kwamba “kimulimuli wa kike hutambua ishara hiyo,” kisha “yeye huitikia kwa kumulika mara moja kwa wakati barabara kabisa kulingana na desturi ya jamii yake, kana kwamba anasema ‘Niko hapa.’” Kimulimuli wa kiume hupokea mwaliko wake na kuruka hadi alipo.

Ndege Huwasiliana kwa Nyimbo

Katika kitabu chake The Life of Birds, David Attenborough anasema hivi: “Hakuna sauti ya mnyama yeyote inayoweza kufananishwa na wimbo wa ndege kwa urefu, unamna-namna, na utata wake. Nyimbo za ndege hazitokei kooni bali katika kiungo fulani kilicho ndani sana kwenye kifua cha ndege, karibu na mahali ambapo koromeo hugawanyika kabla ya kuingia mapafuni.

Ndege hurithi nyimbo fulani na hujifunza nyimbo nyingine kutoka kwa wazazi. Hivyo, ndege wanaweza kupata lafudhi ya eneo fulani. Kitabu The Life of Birds kinasema hivi: “Ndege wanaoitwa blackbird waliotokana na wale waliopelekwa Australia katika karne ya kumi na tisa ili kuwaburudisha Wazungu waliokuwa wamehamia huko, sasa wana lafudhi nzito ya Australia.” Inasemekana nyimbo za ndege anayeitwa lyrebird ndizo tamu na tata zaidi kati ya nyimbo zote za ndege na kwamba ndege huyo amejifunza karibu nyimbo zote hizo kutoka kwa ndege wengine. Ama kwa hakika, ndege wa lyrebird wana kipaji cha kuiga kwani wanaweza kuiga milio yoyote wanayoisikia kutia ndani ala za muziki, mbwa wanaobweka, milio ya ving’ora, kelele za shoka, na hata kelele za kamera! Na wanaiga milio hiyo ili kumvutia mwenzi.

Ndege wanaoitwa kigogota, ambao kwa kawaida hutumia mdomo wao kutafuta chakula, huwasiliana na ndege wengine kwa kugongesha mdomo wao kwenye tawi au gogo lenye uwazi. Attenborough anasema kwamba hata wengine “hutumia ala mpya za muziki kama vile . . . , paa la mabati au bomba la moshi la mabati.” Ndege pia huwasiliana kwa kutumia ishara fulani inayoambatana na nyimbo au bila nyimbo. Kwa mfano, wanaweza kuwasiliana kwa kutanua manyoya yao yenye rangi maridadi.

Aina moja ya kasuku-kishungi huko Australia huonyesha kwamba anamiliki eneo fulani kwa kugongagonga vitu, kuimba, kuchezesha mwili, na kuonyesha manyoya yake. Yeye hukata tawi linalofaa kisha hulikamata kwa mguu wake na kulitumia kupiga-piga gogo. Wakati huohuo, yeye hutanua mabawa yake na kishungi chake, hutikisa kichwa chake huku na huku, na kutoa milio mikali. Ama kweli, hiyo ni tamasha yenye kupendeza sana!

Milio ya ndege fulani hutambuliwa na wanyama wengine. Hebu ona mfano huu wa yule ndege anayeitwa kiongozi, ndege mdogo anayepatikana hasa Afrika. Kupatana na jina lake, ndege huyo humwongoza nyegere kwa mlio wake mkali hadi kwenye mti ulio na mzinga wa nyuki. Ndege huyo anapotua kwenye mti au karibu na mti, yeye hutoa mlio tofauti kana kwamba anasema, “Nimepata asali!” Nyegere hufika kwenye mti huo na kupasua shina lake kwa kucha zake, kisha yeye hufurahia mlo huo mtamu.

Kuwasiliana Ndani ya Maji

Tangu vifaa vya kusikiliza sauti majini vilipovumbuliwa, watafiti wameshangazwa na sauti nyingi sana zinazotoka baharini. Sauti hizo ni kama vile mivumo, milio kama ya paka na hata milio myembamba, nazo ni nyingi sana hivi kwamba waendeshaji wa nyambizi wamezitumia kufunika sauti za nyambizi. Hata hivyo, samaki wana milio maalumu. Katika kitabu Secret Languages of the Sea, mtaalamu wa viumbe wa baharini Robert Burgess anasema hivi: “Samaki mmoja ‘anapokoroma, anapowika, na anapobweka,’ na kurudia milio hiyohiyo, huenda samaki mwingine akaitikia kwa ‘kupiga mdomo wake’ na ‘kutoa sauti ya mkwaruzo’ ili yule mwingine aitikie.”

Kwa kuwa samaki hawana viungo vya usemi, wao hutoaje sauti? Burgess anasema kwamba wengine hutumia misuli “iliyo kwenye kuta za vifuko vyao vya hewa kutetemesha kuta hizo hadi vifuko hivyo” vinapolia kama ngoma. Samaki wengine husaga meno yao au hufunga na kufungua mashavu yao kwa kishindo. Je, wao “huropoka” tu? La. Burgess anasema kwamba samaki hutoa sauti “kuwavutia wale wa jinsia tofauti, kutafuta njia, kujikinga na maadui, kuwasiliana juu ya mambo ya kawaida, na kutisha.”

Samaki pia wanaweza kusikia sauti vizuri. Jamii nyingi za samaki zina masikio ya ndani na vilevile mstari ulio kandokando ya mwili wao ambao una chembe zinazohisi shinikizo. Mstari huo wa chembe unaweza kuhisi shinikizo la mawimbi yanayotokezwa na sauti inayopita majini.

Wawasiliani Stadi Zaidi Duniani

Profesa wa lugha Noam Chomsky aliandika hivi: “Tunapojifunza lugha ya mwanadamu tunakaribia kufahamu utu wa mwanadamu, sifa hususa za kiakili ambazo kulingana na ujuzi wetu wa sasa ni mwanadamu tu aliye nazo.” Barbara Lust, profesa wa lugha na ukuzi wa mwanadamu, alisema: “Watoto walio na umri wa miaka 3 huwa tayari na ujuzi mwingi sana kuhusu muundo wa lugha, ambao ni tata na sahihi sana hivi kwamba si rahisi kueleza jinsi wanavyoupata.”

Hata hivyo, Biblia inaeleza vizuri kwa nini wanadamu wana uwezo wa ajabu wa kufahamu lugha. Inaeleza kwamba Muumba, Yehova Mungu, ndiye aliyewapa zawadi hiyo, na aliwaumba kwa “mfano” wake. (Mwanzo 1:27) Lakini sifa za Mungu zinaonekanaje katika uwezo wetu wa kuwasiliana?

Kwa mfano, hebu fikiria uwezo wa kutunga majina. Profesa wa mawasiliano ya maneno Frank Dance aliandika kwamba wanadamu “tu ndio viumbe wanaoweza kutunga majina.” Maandiko yanaonyesha kwamba uwezo huo umetoka kwa Mungu. Mwanzoni mwa simulizi la uumbaji, Biblia inasema kwamba Mungu aliita “nuru Mchana, na giza akaliita Usiku.” (Mwanzo 1:5) Kulingana na Isaya 40:26, yaonekana Mungu alizipatia nyota zote majina. Hiyo ilikuwa kazi ya ajabu sana!

Baada ya Mungu kumuumba Adamu, mojawapo ya kazi za kwanza alizompa ilikuwa kuwapa wanyama majina. Ilimbidi Adamu awe macho na awe mbunifu sana katika kazi hiyo! Baadaye, Adamu alimwita mke wake Hawa. Kisha, Hawa akamwita mwana wake wa kwanza Kaini. (Mwanzo 2:19, 20; 3:20; 4:1) Tangu wakati huo, wanadamu wamejitoa mhanga kutunga majina ya kila kitu, hasa kwa ajili ya mawasiliano. Naam, hebu wazia jinsi ambavyo ingekuwa vigumu kuwasiliana ikiwa hakungekuwa na majina.

Licha ya kuwa na uwezo na tamaa ya kutunga majina, wanadamu wana njia nyingine nyingi za kuwasiliana, na nyingine hazihusishi kuongea. Ama kweli, tunaweza kuwaeleza wanadamu wenzetu jambo lolote lile, iwe ni jambo tata au hisia zetu za kutoka moyoni. Lakini, kama tutakavyoona katika makala inayofuata, kuna njia moja ya mawasiliano iliyo bora kuliko zote.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

MWANGAZA WA KIMULIMULI USIO NA JOTO

Zaidi ya asilimia 90 ya nishati ya taa fulani za balbu hubadilika kuwa joto. Lakini kimulimuli hutumia asilimia 90 hadi 98 ya nishati ya umeme kutokeza mwangaza, huku kiasi kidogo sana cha nishati kikibadilika kuwa joto. Ndiyo sababu inasemekana kwamba mwangaza huo hauna joto lolote. Mwangaza wa kimulimuli hutokezwa kupitia utendaji tata sana wa kemikali ambao hutukia katika chembe za pekee zinazoitwa photocyte. Neva huanzisha au kusimamisha utendaji wa chembe hizo.

[Hisani]

John M. Burnley/Bruce Coleman Inc.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Jinsi Unavyoweza Kuboresha Uwezo Wako wa Kuwasiliana

1. Sikiliza kwa makini wengine wanapozungumza, na usitawale mazungumzo. Watu wanaweza kupuuza neno lililotamkwa vibaya au kosa la kisarufi, lakini hawawezi kumchangamkia mtu anayetaka kuzungumza bila kusikiliza. Biblia inasema uwe “mwepesi sana juu ya kusikia, wa polepole juu ya kusema.”—Yakobo 1:19.

2. Jitahidi kujua mambo yanayotukia kawaida maishani. Soma habari mbalimbali, lakini uchague unachosoma kwa busara. Unapozungumzia yale uliyojifunza, uwe mwenye kiasi na mnyenyekevu.—Zaburi 5:5; Mithali 11:2.

3. Jifunze maneno mapya unayoweza kuyatumia, bali si maneno magumu ya kujionyesha. Watu walisema hivi kumhusu Yesu: “Hajasema kamwe mtu mwingine kama hivi.” (Yohana 7:46) Lakini, hata watu “wasio na elimu na wa kawaida tu” walielewa maneno ya Yesu kwa urahisi.—Matendo 4:13.

4. Zungumza waziwazi, na utamke maneno kwa usahihi. Lakini epuka kuvuta maneno kupita kiasi au kujifanya. Tunapozungumza kwa njia inayoeleweka wazi na kuepuka kumezameza au kukatakata maneno, yale tunayosema yataheshimiwa na tutakuwa tukiwajali wale wanaotusikiliza.—1 Wakorintho 14:7-9.

5. Tambua kwamba uwezo wako wa kuwasiliana ni zawadi kutoka kwa Mungu. Hilo litakusaidia kuheshimu uwezo huo.—Yakobo 1:17.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Nondo wa hariri wana vipapasio vinavyopokea ujumbe haraka sana

[Hisani]

Courtesy Phil Pellitteri

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kigogota

[Picha katika ukurasa wa 7]

Ndege wa paradiso

[Hisani]

© Michael S. Yamashita/CORBIS

[Picha katika ukurasa wa 7]

Aina moja ya kasuku-kishungi

[Hisani]

Roland Seitre