Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Ukahaba wa Watoto Sijui nielezeje shukrani zangu kwa ajili ya mfululizo wa makala “Ukahaba wa Watoto Ni Hali Inayosikitisha.” (Februari 8, 2003) Makala hizo zilieleza kinaganaga uovu huo. Naona makala hizo zinapaswa kuchapishwa tena katika magazeti ya kawaida ili watu wengi zaidi wajue kwamba utumwa huo upo.
M. K., Jamhuri ya Cheki
Siria Asanteni kwa ajili ya makala “Historia Inayopendeza ya Siria.” (Februari 8, 2003) Kusema kweli, sipendi historia hata kidogo. Lakini makala hiyo ilinisaidia niwazie majiji mbalimbali ambayo mtume Paulo alitembelea na njia alizopitia. Habari kama hizo hutusaidia tuelewe zaidi hali ambazo watumishi wa Mungu walikabili zamani.
T. S., Marekani
Kudumisha Afya Bora Nawashukuru kwa madokezo yote kuhusu mazoezi na kupunguza uzito ambayo mmechapisha katika makala za “Kuutazama Ulimwengu.” Nilifurahia hasa ile habari yenye kichwa “Kudumisha Afya Bora.” (Februari 8, 2003) Ilisema kwamba hata mazoezi mepesi yanaweza kuboresha afya yako. Habari hiyo ilinisaidia kwa sababu ninatumia dawa ambayo inanifanya nichoke haraka na inanibidi nifanye mazoezi kwa muda mfupi. Asanteni kwa dokezo hilo ambalo ni muhimu kwa afya.
G. P., Marekani
Fumbo la Kujaza Maneno Nawashukuru kwa sababu ya fumbo la kujaza maneno katika magazeti yenu. Nayapenda mafumbo hayo sana! Ni yenye kusisimua, kuelimisha, na hunistarehesha jioni.
J. G., Marekani
Sikuzote mimi hufurahia kujaza mafumbo, na mlipoanza kuyachapisha katika Amkeni! niliyatarajia kwa hamu. Mwanzoni, nilisoma maandiko mengi ili nipate majibu, lakini sasa ninaweza kujibu maswali mengi bila kuangalia maandiko! Kwa njia hiyo, nimejua maandiko mengi na watu wanaotajwa katika Biblia.
E. G., Marekani
“Amkeni!” linajibu: Katika lugha fulani makala “Je, Wajua?” huchapishwa badala ya fumbo la kujaza maneno.
Tabasamu Familia yangu na marafiki walinibandika jina Tabasamu. Hata nilipewa picha yangu yenye maneno haya: “Ukimwona mtu yeyote asiyetabasamu, mpe tabasamu yako.” Hata hivyo, nilishuka moyo sana kwa sababu familia yetu ilikumbwa na misiba hivi majuzi. Makala “Manufaa ya Tabasamu” (Januari 22, 2003) ilibadili mtazamo wangu. Sasa naweza kuwafurahisha watu tena kwa tabasamu yangu. Namshukuru Yehova kwa kunisaidia nibadili mtazamo wangu kupitia makala hiyo.
O. F., Nigeria
Takataka Katika mfululizo “Je, Tutazama Katika Takataka?” (Agosti 22, 2002), mlinukuu makadirio ya shirika moja la mazingira la Italia yaliyoonyesha muda ambao vitu mbalimbali huoza baharini. Naamini kwamba kadirio linaloonyesha kuwa mikebe huoza baada ya miaka 500 si sahihi hata kidogo. Kwenye maji yenye chumvi ya Hifadhi ya Wanyama ya Kisiwa cha Pelican, huko Florida, nimeona mikebe mingi ya alumini na bati ambayo huvunjika-vunjika ninapoipiga teke kwa viatu vyangu. Sidhani mikebe hiyo imedumu kwa zaidi ya miaka kumi. Yeyote mwenye mashua ya alumini anajua vizuri kwamba maji ya chumvi huozesha alumini.
S. S., Marekani
“Amkeni” linajibu: Ni kweli kwamba makadirio mengine ni ya zamani. Hata hivyo, kitabu “Elements of Marine Ecology,” cha R. V. Tait na F. A. Dipper, kinasema kwamba mikebe ya alumini inaweza kuoza baada ya miaka 80 hadi 100 na ile ya bati miaka 50 hadi 100. Mikebe ya chuma iliyo majini huenda isioze haraka kama ile inayopigwa na hewa kwenye nchi kavu.