Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Hatari za Kufanya Mambo Mengi Wakati Uleule

Kujaribu kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja “kunaweza kukuzuia usitimize mengi na kukufanya uwe mjinga,” lasema gazeti The Wall Street Journal. “Kujaribu kufanya mambo mawili au matatu wakati uleule au haraka-haraka kwaweza kuchukua muda mrefu zaidi na kuchosha akili kuliko kufanya jambo moja kwanza.” Baadhi ya madhara ya kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja ni kusahau mambo haraka (kama yale uliyotoka kufanya au kusema), kutokuwa makini, kutokaza fikira, na dalili za mfadhaiko (kama kutopumua vizuri), na kushindwa kuwasiliana na wengine. Mtu hushindwa kufanya kazi vizuri ikiwa anahitaji kutumia sehemu zilezile za ubongo wakati mmoja, kama kuongea kwenye simu huku akimsikiliza mtoto anayeongea kwenye chumba kingine. Ni hatari kufanya mambo mengi hasa unapoendesha gari. Mambo kama vile kula au kunywa, kujaribu kuchukua kitu fulani, kuzungumza kwa shauku na abiria au kwa simu, kujipodoa, au hata kubadilisha stesheni ya redio au kifaa kingine yanaweza kukukengeusha fikira na kusababisha msiba.

Usimtikise Mtoto Kamwe!

Kumtikisa mtoto kwa nguvu husababisha mshtuko wa ghafula ambao “unaweza kumfanya avuje damu ndani ya kichwa na kuzidisha shinikizo kwenye ubongo na kuufanya uachane,” lasema gazeti Toronto Star. Kwa kuwa misuli ya mtoto haijakomaa na tishu za ubongo ni nyeti sana, “kumtikisa mtoto kwa sekunde chache kwaweza kusababisha madhara ya kudumu, kama vile, kuvimba na kuharibika kwa ubongo, mtindio wa ubongo, akili punguani, kukawiza ukuzi, upofu, uziwi, kupooza na kifo.” Daktari wa watoto katika Hospitali ya Watoto ya Ontario Mashariki, James King, amechunguza madhara ya kuwatikisa watoto. Anasema kwamba watu wanahitaji kuelimishwa, kwa kuwa mara nyingi madhara hayo hayaonekani waziwazi na huenda mtoto akadhaniwa kuwa na mafua au ugonjwa fulani wa virusi. “Watu wanapaswa kufahamu vizuri kwamba hawapaswi kamwe kumtikisa mtoto,” asema Dakt. King. “Wazazi waliopata mtoto karibuni wanapaswa kujua jambo hilo.”

Hawapendezwi na Dini

Gazeti IHT Asahi Shimbun linaripoti kwamba “inaonekana [Wajapani] wengi hawazingatii dini wanapojaribu kutatua matatizo yaliyopo sasa.” Walipoulizwa swali hili: “Je, unaamini au kupendezwa na dini?” ni asilimia 13 tu waliojibu ndiyo. Asilimia nyingine 9 ya wanaume na 10 ya wanawake walisema wanapendezwa “kidogo.” Gazeti hilo linaongeza hivi: “Wanawake wenye umri wa miaka 20 na kitu hawapendezwi na dini kwani ni asilimia 6 tu waliosema wanapendezwa na dini.” Uchunguzi huo wa kila mwaka ulionyesha kwamba asilimia 77 ya wanaume na asilimia 76 ya wanawake nchini Japan wanasema kwamba hawapendezwi kamwe na dini yoyote. Idadi ya Wajapani wanaopendezwa na dini imepungua kwa asilimia 50 hivi tangu uchunguzi wa mwisho ufanywe mwaka wa 1978. Kwa ujumla, wazee, hasa wenye umri wa zaidi ya miaka 60, ndio waliosema kwamba wanapendezwa na dini.

Kushuka Moyo Husababisha Magonjwa Mengine

“Shirika la Afya Ulimwenguni linatabiri kwamba kufikia mwaka wa 2020, mshuko wa moyo utakuwa kisababishi kikuu cha ulemavu ulimwenguni baada ya maradhi ya moyo,” lasema gazeti U.S.News & World Report. Watu wengi zaidi siku hizi hawaoni ugonjwa huo kuwa “tatizo la akili tu.” Philip Gold, msimamizi wa matibabu ya neva katika Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Akili anasema kwamba “kushuka moyo ndio ugonjwa pekee unaoathiri mwili mzima na kuzidisha karibu magonjwa mengine yote.” Kushuka moyo kwaweza hata kusababisha maradhi ya moyo na kisukari. Kwa mfano, makala hiyo inaripoti kuhusu utafiti unaoonyesha kwamba watu walioshuka moyo “wana mioyo dhaifu ambayo haiwezi kupeleka damu na oksijeni ya kutosha kupatana na mabadiliko mwilini.” Pia, “ubongo wa mtu aliyeshuka moyo hutoa ishara kwamba unahitaji nguvu zaidi, na hilo linaweza kuchochea utengenezaji wa homoni ya cortisol ambayo huongeza kiasi cha sukari katika damu.” Isitoshe, kushuka moyo huchangia ugonjwa wa mifupa na kansa. Uchunguzi unafanywa kubainisha iwapo magonjwa hayo yanaweza kupunguzwa kwa kutibu mshuko wa moyo.

Hali ya Ndoa Huathiri Moyo

Gazeti The Daily Telegraph la London linasema “uchunguzi unaonyesha kwamba hali ya ndoa inaweza kuamua wapo mtu aliyefanyiwa upasuaji wa moyo atapona.” Dakt. James Coyne wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania, Marekani, anasema kwamba ndoa yenye furaha inaweza kumchochea mgonjwa apone, lakini “mseja aliyefanyiwa upasuaji wa moyo anaweza kupona haraka kuliko mgonjwa mwenye matatizo ya ndoa.” Dakt. Coyne na wenzake waliwapiga picha za video wenzi waliokuwa wakibishana nyumbani, na wakagundua kwamba wagonjwa wa moyo waliokosana na wenzi wao walikabili hatari mara mbili zaidi ya kufa katika muda wa miaka minne kuliko wale wenye amani. Profesa wa soshiolojia katika Chuo Kikuu cha Chicago, Dakt. Linda Waite anasema kwamba kuwa na ndoa yenye furaha “ni sawa na kula vizuri, kufanya mazoezi, na kutovuta sigara.”

“Miti ya Fidla” Inatoweka

“Mbao maalumu zinahitajiwa ili kutengeneza ala bora za kupiga fidla, lakini mbao hizo zinazidi kupungua,” lasema gazeti la sayansi la Ujerumani natur & kosmos. Jina la mti unaotoa mbao hizo ni Caesalpinia echinata, na unaitwa pia Pernambuco au pau brasil. Unapatikana sana katika misitu ya pwani ya Brazili. Lakini misitu hiyo imepungua sana kwa sababu ya shughuli za kilimo. Sasa ni asilimia 4 tu ya misitu hiyo inayobaki na mti huo umetiwa katika orodha ya mimea iliyo katika hatari ya kutoweka. Isitoshe, miti iliyoishi kwa miaka 20 au zaidi ndiyo iliyo na mbao za manjano au za kahawia na nyekundu zinazofaa kutengeneza ala za kupiga fidla. Makala hiyo inamnukuu fundi stadi wa ala za fidla, Thomas Gerbeth, akisema kwamba hakuna kifaa kingine kinachoweza kutumiwa kwa sababu “vifaa visivyo vya asili si bora kama mbao za mti huo.” Sasa mafundi na wanamuziki wa fidla wanatetea kuhifadhiwa kwa “mti wa fidla.”

Ugonjwa wa Kale Ungalipo

“Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni zinaonyesha kwamba katika mwaka wa 2002, zaidi ya watu 700,000 waliambukizwa ugonjwa wa ukoma ulimwenguni pote,” lasema gazeti El País la Hispania. Tangu nyakati za Biblia, ukoma umekuwa ugonjwa wa kutisha. Lakini ukoma wa leo unaweza kutibiwa. Kwa hakika, karibu watu milioni 12 wamepona ukoma katika muda wa miaka 20 iliyopita. Hata hivyo, mtafiti Jeanette Farrell anasema “bado hatuwezi kusema kwamba ukoma umetoweka kabisa.” Madaktari hawajafaulu kukomesha ugonjwa huo, na bado kuna wengi wanaoshikwa na ugonjwa huo. Nchi ambazo zingali na watu wengi wenye ukoma ni Brazili, India, Madagaska, Msumbiji, Myanmar, na Nepal. Wanasayansi wanatumaini kwamba kwa sababu kuna habari mpya kuhusu chembe za urithi, watapata chanjo inayofaa ya ukoma.

“Wavulana Wengi Sana Wanazaliwa” China

“Kulingana na sensa ya tano ya China, uwiano wa wavulana kwa wasichana wanaozaliwa ni 116.9 kwa 100 ikilinganishwa na uwiano wa 113.8 kwa 100 katika mwaka wa 1990,” lasema gazeti la China Today. “Uwiano huo unapita kwa mbali ule wa kawaida wa dunia wa 105 kwa 100, na unaonyesha kwamba wavulana wengi zaidi wanazaliwa nchini China.” Inatabiriwa kwamba wakati ujao, wanaume Wachina wapatao milioni 50 hawatapata wenzi wa ndoa watakapofikisha umri wa kuoa. Makala hiyo inaongeza hivi: “Zheng Zizhen, msimamizi wa Taasisi ya Jimbo la Guangdong ya Soshiolojia na Takwimu za Idadi ya Watu, alinukuliwa akisema kwamba uwiano huo usio wa kawaida utaathiri jamii na maadili ya Wachina.”