Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matatizo ya Wakulima Yanasababishwa na Nini?

Matatizo ya Wakulima Yanasababishwa na Nini?

Matatizo ya Wakulima Yanasababishwa na Nini?

“Wafanyakazi wanaopokea simu katika kituo cha kushughulikia mfadhaiko wa wakulima wamezoezwa kukusaidia kukabiliana na matatizo yako. Sisi ni wakulima au tulikuwa wakulima kama wewe, na tunaelewa magumu yanayokumba familia za mashambani. Tunaweza kukujulisha kwa watu wanaoweza kukusaidia. . . . Hatutafichua habari zozote utakazotuambia.”—Kutoka kwa kituo cha Internet cha serikali ya Kanada.

WATAALAMU wengi wa afya wametambua kwamba mfadhaiko ni mojawapo ya matatizo ya wakulima. Ili kuwasaidia wakulima wakabiliane nao, kuna wanasaikolojia wanaoshughulikia mfadhaiko wa wakulima, na wanapanga mikutano ya kuwashauri wakulima na kuwapa namba za simu wanazoweza kupiga ili wapate msaada.

Jane, ambaye ni mke wa mkulima, huhudhuria mkutano wa kupata mashauri Alhamisi usiku. Jane anasema hivi: “Ninahudhuria kwa sababu mume wangu alijiua. Sikuzote alipenda sana kulima shamba letu, na ninadhani alijiua kwa sababu hakufaulu katika kilimo.”

Watu wengi wamegundua kwamba kuna ongezeko kubwa la wakulima wanaotaka msaada kwa sababu ya mfadhaiko. Matatizo ya wakulima yanasababishwa na nini?

Misiba ya Asili na Magonjwa

Kituo cha Internet cha serikali kilichonukuliwa pale mwanzoni kinasema: “Kuna mambo mengi ambayo mkulima hawezi kuyadhibiti maishani mwake, kama vile hali ya hewa, bei za mazao, viwango vya riba, na kuharibika kwa vifaa. Hata kuamua mambo kama vile mazao utakayopanda au kuuza shamba au kuwapa wakopeshaji shamba hilo kwa muda kunaweza kusababisha mfadhaiko, kwani unaweza kupata hasara au faida ikitegemea uamuzi uliofanya.” Matatizo hayo yanapozidishwa na hatari ya ukame mkali, magonjwa, au uwezekano wa kupoteza shamba, mfadhaiko unaweza kumlemea mkulima sana.

Kwa mfano, ukame unaweza kusababisha hasara maradufu. Mkulima Howard Paulsen alisema kwamba ukame wa mwaka wa 2001, ambao ulikuwa mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya ukame kuwahi kutukia huko Kanada, uliathiri mimea na mifugo yake. Hakukuwa na malisho ya mifugo au mazao ya kuvuna, kwa hiyo ilibidi wakulima wanunue chakula cha mifugo. Alisema hivi: “Tayari nimetumia dola 10,000 za Kanada kununua chakula cha mifugo na sasa ninawalisha chakula ambacho wanapaswa kula wakati wa baridi kali. Ukifanya hivyo, huwezi kupata faida yoyote hata kutoka kwa mifugo wenyewe.” Katika sehemu nyingine, mafuriko yameharibu kabisa mashamba mengi na mavuno yote.

Kuzuka kwa ugonjwa wa midomo na miguu mwaka wa 2001 kulikuwa tu mojawapo ya matatizo ambayo wakulima Waingereza walikumbwa nayo hivi karibuni, kutia ndani kichaa cha ng’ombe na homa ya nguruwe. Mbali na kuharibu uchumi na kusababisha hofu, magonjwa hayo yanasababisha matatizo mengi zaidi. Gazeti Agence France-Presse lilisema hivi: “Wanaume wakakamavu wa mashambani ambao hawatokwi na machozi ovyoovyo, wameonekana wakilia wanapowatazama wataalamu wa mifugo wa serikali wakiteketeza marundo ya mifugo ambao wametumia maisha yao yote kuzalisha.” Baada ya ugonjwa wa midomo na miguu kuzuka, polisi hata walianza kuwapokonya bunduki wakulima waliokusudia kujiua. Wakulima wengi waliofadhaika walipiga simu wakiomba mashauri.

Kuzorota kwa Uchumi

Kumekuwa pia na mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Jalada la nyuma la kitabu Broken Heartland linasema hivi: “Kati ya mwaka wa 1940 hadi katikati ya miaka ya 1980, gharama za uzalishaji katika eneo kuu la kilimo la Marekani ziliongezeka mara tatu, gharama za vifaa ziliongezeka mara nne, malipo ya riba yaliongezeka mara kumi, faida zilipungua kwa asilimia 10, idadi ya wakulima ilipungua kwa thuluthi mbili, watu walihama maeneo mengi ya mashambani, biashara zilifungwa, na uchumi ukazorota.”

Kwa nini faida zinapungua na gharama zinaongezeka? Katika ulimwengu wa leo ulio kama kijiji, wakulima wanaathiriwa na hali za masoko ya kimataifa. Kwa hiyo wakulima hujikuta wakishindana na wazalishaji wa chakula katika maeneo ya mbali sana. Ni kweli kwamba masoko mapya ya bidhaa za kilimo yameanzishwa kwa sababu ya biashara ya kimataifa, lakini masoko ya kimataifa yanaweza kubadilika ghafula. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1998, wakulima kadhaa wa nafaka na wafugaji wa nguruwe nchini Kanada walikuwa karibu kufilisika wakati wateja wao huko Asia walipokumbwa na matatizo ya kiuchumi.

Wakazi wa Mashambani Wanahama

Profesa Mike Jacobsen wa Chuo Kikuu cha Iowa, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mashambani, anasema kwamba matatizo ya wakulima yanawaathiri pia wakazi wote wa mashambani. Anasema hivi: “Mashambani ni mahali panapowafaa watoto, ni mahali safi, ambapo watu wangependa kuoa na kulea watoto. Shule za mashambani ni nzuri na salama. Naam, huo ndio ukweli wa mambo. Lakini, uchumi wa miji ya mashambani unategemea hasa mashamba madogo yanayomilikiwa na familia mbalimbali.” Hivyo, matatizo ya wakulima yamefanya hospitali, shule, mikahawa, maduka, na makanisa ya mashambani yafungwe. Jamii zenye umoja, ambazo hufanya maisha ya mashambani yavutie, zinatoweka.

Basi, haishangazi kwamba gazeti Newsweek lilisema kwamba karibu asilimia 16 ya Wamarekani wanaoishi mashambani ni maskini hohehahe. Geoffrey Lawrence anasema hivi katika ripoti yenye kichwa “Matatizo ya Mashambani Huko Australia”: “Ukosefu wa kazi na umaskini umeongezeka sana mashambani kuliko mjini.” Familia nyingi, na hasa familia za vijana, zimelazimika kuhamia mjini kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi. Sheila, anayeisaidia familia yao kulima shamba lao, anauliza hivi: “Hali ikiendelea hivi, je, kweli kutakuwa na wakulima?”

Kwa kuwa vijana wengi sana wamehamia mijini, wakazi wengi wa miji ya mashambani ni wazee. Hivyo, hakuna vijana wa kufanya kazi wala watu wa kuwatunza wazee ambao wanahitaji sana msaada. Ndiyo sababu mabadiliko hayo ya haraka yamewafanya wazee wachanganyikiwe na kuogopa.

Kwa hiyo, matatizo ya wakulima yanasababisha matatizo makubwa kila mahali. Yanatuathiri sote. Hata hivyo, kama makala ifuatayo itakavyoonyesha, tunaweza kutumaini kwamba matatizo ya wakulima yatakoma.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Katika ulimwengu wa leo ulio kama kijiji, wakulima wanaathiriwa na hali za masoko ya kimataifa

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Hali ikiendelea hivi, je, kweli kutakuwa na wakulima?”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

KULIMA KWA MBOLEA YA KIASILI

Chakula kilichozalishwa kwa mbolea ya kiasili kinazidi kupendwa. Huko Kanada, wanunuzi wa chakula hicho wanaongezeka kwa karibu asilimia 15 kila mwaka.

Chakula hicho huzalishwaje? Ripoti ya Idara ya Kilimo, Chakula na Maendeleo ya Mashambani ya Alberta inasema kwamba “chakula hicho huzalishwa bila kutumia kemikali na hilo linaboresha hali ya udongo, linachangia ongezeko la aina mbalimbali za mimea, linaboresha afya ya mifugo, na kuhifadhi mazingira.”

Wakulima wanaotumia mbolea ya asili wanasema kwamba kilimo hicho kinatofautiana sana na uzalishaji wa chakula kwenye mashamba makubwa. Katharine Vansittart anaandika hivi katika gazeti Canadian Geographic: “Watu wenye mashamba makubwa huwa na zoea la kupanda mimea ya aina moja tu ambayo huzalishwa hasa kwa kutumia mashine, mbolea nyingi za kemikali na dawa nyingi za kuua wadudu. Mbali na kwamba chakula hicho kina mabaki ya kemikali, kiasi cha virutubisho hupungua mazao yanapovunwa kabla hayajakomaa ili yasafirishwe kwenye masoko ya mbali. Huenda pia kikatiwa gesi, nta, au mnururisho wa nyukilia ili kisiharibike.”

Ni nani wanaonunua chakula hicho? Ripoti ya Alberta inasema kwamba wanunuzi ni “vijana na akina mama wanaojali afya na wazee waliozaliwa baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu. . . . Lakini havinunuliwi tu na watu wanaopenda vyakula vya kiasili.”

Hata hivyo, si kila mtu anayesadiki kwamba chakula kilichozalishwa kwa mbolea ya kiasili ni bora. Gazeti Canadian Geographic linasema: “Kwa kuwa vyakula vinavyozalishwa kwa njia hiyo huuzwa kwa bei ghali, wachambuzi hutilia shaka umuhimu wake bila kuzingatia uthibitisho wa kisayansi unaoonyesha faida zake. Wengine wanasema kwamba maskini hawawezi kukinunua.” Watetezi wa chakula hicho hudai kwamba watu wa matabaka yote wataweza kukinunua iwapo kutakuwa na mabadiliko ya ulaji, uuzaji, na usafirishaji wake. Kutokana na maoni hayo mbalimbali na uthibitisho wa sayansi, inaonekana mjadala kuhusu chakula kinachozalishwa kwa mbolea ya kiasili hautaisha karibuni.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

DAWA ZA KUWAUA WADUDU HUWAHANGAISHA WAKULIMA

Wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea yameharibu asilimia 75 ya mazao katika sehemu fulani ulimwenguni. Inaonekana suluhisho ni kupanda mimea zaidi. Gazeti Globe and Mail laripoti hivi: “Wakulima wa Kanada wamejaribu kutatua tatizo hilo kwa kutumia njia za kilimo zinazokusudiwa kuongeza mazao ili wauze mazao mengi zaidi.” Hata hivyo, Terence McRae wa shirika la kimazingira la Kanada anaonya hivi: “Mengi ya mabadiliko hayo yamezidisha hatari za kimazingira zinazosababishwa na kilimo.”

Vipi matumizi ya dawa za kuua wadudu? Jambo hilo pia huwahangaisha wakulima kwa sababu bado kuna ubishi kuhusu ubora wa dawa hizo na hatari zake kwa afya. Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni ilikiri kwamba kufikia sasa hakuna habari kamili kuhusu hatari za dawa nyingi za wadudu na sumu iliyo katika dawa hizo. Hatari nyingine zinaweza kutokea chakula kinapoliwa. Wanyama hula mimea iliyopuliziwa dawa hizo. Halafu wanadamu hula wanyama hao.

[Hisani]

USDA Photo by Doug Wilson