Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Picha Zilizotengenezwa kwa Mawe

Picha Zilizotengenezwa kwa Mawe

Picha Zilizotengenezwa kwa Mawe

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

PICHA zilizotengenezwa kwa mawe zimeitwa “sanaa ya ajabu,” mbinu ya “ajabu” ya kupamba, na mojawapo ya “sanaa za mapambo zilizodumu tangu jadi.” Domenico Ghirlandajo, msanii Mwitaliano wa karne ya 15, alisema hiyo ndiyo “mbinu bora ya kutokeza sanaa zinazodumu milele.” Hata maoni yako kuhusu sanaa hiyo yawe nini, ina historia ya kupendeza.

Picha za mawe hupamba sehemu kama vile sakafu, ukuta, au kuba, nazo hufanyizwa kwa kupanga pamoja vipande vidogo vya mawe, vioo, au vigae. Tangu zamani, picha hizo zimetumiwa kurembesha sakafu na kuta. Tofauti na sanaa nyingine zinazoweza kuharibiwa na mvuke, picha za mawe zimetumiwa pia kupamba mabafu, madimbwi, na chemchemi za maji.

Picha zilizotengenezwa kwa mawe hutofautiana sana. Nyingine huwa sakafu za rangi moja, nyingine hufanyizwa kwa rangi nyeusi na nyeupe, nyingine huwa mapambo tata ya maua yenye rangi mbalimbali, hali nyingine huwa picha halisi zenye kuvutia.

Mwanzo na Usitawi

Haijulikani ni nani aliyebuni picha hizo. Wamisri na Wasumeria wa kale walirembesha majengo yao kwa mapambo yenye rangi mbalimbali. Hata hivyo, inaonekana sanaa hiyo ilididimia. Inasemekana kwamba sanaa hiyo ilianzia Asia Ndogo, Carthage, Hispania, Krete, Sicily, Siria, na Ugiriki. Hivyo, mwandishi mmoja alisema kwamba sanaa hiyo “ilibuniwa, ikasahauliwa, na kubuniwa tena katika sehemu mbalimbali za bonde la Mediterania katika nyakati mbalimbali.”

Picha za mawe za awali, nyingine za karne ya tisa K.W.K., zilifanyizwa kwa vijiwe laini vya duara vilivyopangwa kwa njia sahili. Wasanii walitumia vijiwe vya rangi mbalimbali. Kwa kawaida, vijiwe hivyo vilikuwa na kipenyo cha milimeta 10 hadi 20, lakini walitumia vijiwe vyenye kipenyo cha milimeta 5 kufanyiza mapambo tata. Kufikia karne ya nne K.W.K., wasanii walianza kukata vijiwe vidogo-vidogo vya duara na wakavitumia kufanya picha zivutie zaidi. Mawe ya mchemraba yalianza kutumiwa badala ya vijiwe vya duara. Mawe hayo yalikuwa na rangi mbalimbali na yalipangwa kwa urahisi na kuchongwa kwa njia maalumu. Picha zilizofanyizwa zilikuwa laini na zingeweza kusuguliwa na kutiwa nta ili zing’ae. Kufikia karne ya pili W.K., msanii angetumia hata vipande vidogo vya vioo vyenye rangi ambavyo vilitumiwa sana wakati huo.

Picha maridadi sana za mawe zilifanyizwa katika kipindi cha utamaduni wa Ugiriki (karibu na mwaka wa 300 K.W.K. hadi 30 K.W.K.). Kitabu Glossario tecnico-storico del mosaico (Faharisi ya Ustadi na Historia ya Picha za Mawe) kinasema kwamba “wasanii Wagiriki walitumia mawe madogo zaidi ya rangi mbalimbali na yenye ukubwa wa milimeta moja ya mchemraba . . . kufanyiza picha zilizokuwa bora kama michoro ya ukutani.” Rangi ilitumiwa kuonyesha mwangaza wa kadiri mbalimbali, kivuli, kina, ukubwa, na taswira.

Wasanii Wagiriki walitengeneza picha ndogo za mawe kwa kuiga picha kubwa maarufu, kisha wakazitia katika fremu zenye madoido na kuziweka katikati ya hizo picha kubwa. Baadhi ya picha hizo ndogo zilitengenezwa kwa mawe madogo sana yaliyotoshea vizuri sana hivi kwamba mtu angedhani zilichorwa kwa burashi badala ya kutengenezwa kwa mawe.

Picha za Mawe za Waroma

Mara nyingi inasemekana kwamba picha za mawe ni sanaa za Waroma kwa sababu zimepatikana kwa wingi nchini Italia na katika majimbo ya Milki ya Roma. Chapisho moja linasema hivi: “Vijia vingi sana vilivyopambwa kwa picha za mawe vimepatikana katika majengo ya wakati wa Waroma kaskazini mwa Uingereza, Libya, katika pwani ya Atlantiki, na jangwa la Siria. Kwa kuwa sanaa hiyo ya ajabu inahusiana sana na kuenea kwa utamaduni wa Waroma, nyakati nyingine vijia hivyo hutumiwa kuthibitisha kwamba Waroma waliishi katika eneo fulani.”

Hata hivyo, picha za mawe zenye rangi mbalimbali hazikufaa sana nyakati za Waroma. Kwa sababu ya ukuzi mkubwa wa miji katika karne ya kwanza W.K., picha nyingi za mawe za bei nafuu zilihitajiwa haraka. Hivyo picha za mawe zilizokuwa tu na rangi nyeusi na nyeupe zilianza kutengenezwa. Kulingana na Enciclopedia dell’arte antica (Ensaiklopidia ya Sanaa ya Kale), picha hizo zilitengenezwa kwa wingi sana hivi kwamba “nyumba zote za matajiri katika majiji yote ya milki hiyo zilikuwa na picha za mawe.”

Picha za mawe zinazofanana zimepatikana katika sehemu tofauti-tofauti. Hiyo inaonyesha kwamba wasanii walitembelea sehemu mbalimbali au labda vitabu vyenye michoro ya picha hizo vilitumiwa katika maeneo tofauti-tofauti. Kama mtu angetaka, angeagiza picha ndogo ya mawe ambayo imetengenezwa kwenye karakana ya msanii, kisha ingesafirishwa hadi mahali pa ujenzi kwa jukwaa la marumaru au la udongo wa mfinyanzi na kusimamishwa. Kazi iliyosalia ingekamilishwa mahali pa ujenzi.

Mpango mzuri ulihitajiwa ili kutengeneza mapambo na fremu za picha. Msanii alihakikisha kwamba msingi na sehemu ya juu ya picha ilikuwa laini na bapa. Kisha tabaka jembamba la saruji laini lilitandazwa kwenye sehemu ndogo, ambayo huenda ilikuwa na ukubwa usiozidi meta moja ya mraba, ili picha iwekwe hapo kabla saruji haijakauka. Picha hiyo ilichorwa kwenye saruji ili imwongoze msanii. Mawe ya mchemraba yalikatwa ifaavyo na msanii alianza kuyapanga mahali pake.

Jiwe moja baada ya jingine lilipangwa, na yote yakaunganishwa kwa kufinyiliwa kwenye saruji. Baada ya kumaliza sehemu moja, msanii alitandaza saruji kwenye sehemu nyingine na kurudia utaratibu huo. Wasanii stadi walitengeneza sehemu tata zaidi, huku wasaidizi wao wakishughulikia zile sehemu rahisi.

Picha za Mawe za Jumuiya ya Wakristo

Picha za mawe zilianza kutiwa katika makanisa ya Jumuiya ya Wakristo katika karne ya nne W.K. Mara nyingi picha hizo zilionyesha hadithi za Biblia na zilitumiwa kuwafundisha waabudu. Taa zenye kumwekamweka ziliangaza dhahabu na vipande vya vioo vyenye rangi na hivyo kutokeza mazingira yasiyo ya kawaida. Kitabu Storia dell’arte italiana (Historia ya Sanaa ya Italia) kinasema: “Sanaa ya picha za mawe ilifaa maoni ya wakati huo ambayo yaliathiriwa sana na . . . falsafa mpya za Plato. Sanaa ya picha za mawe ilifanya vitu visivyo na uhai viwe na uhai, nuru, na umbo kamilifu.” * Mambo hayo yalikuwa tofauti sana na ibada sahili iliyofundishwa na mwanzilishi wa Ukristo, Yesu Kristo!—Yohana 4:21-24.

Makanisa ya Byzantium yana picha za mawe zenye kuvutia sana. Majengo mengine ya ibada yana picha za mawe katika kuba na kuta nyingi za ndani. Huko Ravenna, Italia, mtu anaweza kuona zile zinazoitwa “picha bora za mawe za Ukristo” ambazo zimezingirwa kwa rangi ya dhahabu inayomaanisha nuru ya kimungu na mambo yasiyoeleweka.

Katika Zama za Kati, picha za mawe ziliendelea kutumiwa sana katika makanisa ya Ulaya Magharibi na sanaa za hali ya juu zikatokezwa katika nchi za Kiislamu. Katika kipindi cha usitawi wa sanaa huko Italia, karakana zilizoshirikiana na makanisa makubwa, kama vile St. Mark huko Venice na St. Peter huko Roma, zilikuwa vituo vya utengenezaji wa picha hizo. Wapata mwaka wa 1775, wasanii wa Roma walijifunza kukata vipande vidogo vya vioo vilivyoyeyushwa ambavyo vilikuwa na rangi mbalimbali. Hivyo, wangeweza kuiga michoro na kutengeneza picha ndogo sana za vipande vya vioo.

Mbinu za Sasa na Matumizi Yake

Wasanii wa leo hutengeneza picha za mawe katika karakana. Wao hutumia gundi kubandika vipande vya vioo kwenye karatasi yenye mchoro, huku upande wa juu wa vioo ukiangalia chini. Visehemu vya picha hupelekwa mahali pa ujenzi na upande wa chini wa vioo hivyo hufinyiliwa katika saruji. Saruji inapokauka, karatasi na gundi huondolewa kwa maji, na upande wenye picha huonekana waziwazi. Mbinu hiyo ni rahisi na haichukui wakati mwingi, lakini picha hizo hazing’ai kama zile picha za Zama za Kati.

Hata hivyo, katika karne ya 19, majumba mengi ya mabaraza ya majiji, kumbi za michezo ya kuigiza, makanisa, na majengo mengine yalipambwa kwa njia hiyo. Isitoshe, mbinu hiyo imetumiwa sana katika majumba ya makumbusho, vituo vya ardhini vya magari ya moshi, maduka makubwa, na bustani na viwanja katika Jiji la Mexico, Moscow, Israel, na Japan. Picha laini zenye maumbo mbalimbali zimetumiwa pia kupamba kuta nzima za majengo ya kisasa.

Msanii na mwanahistoria wa sanaa Mwitaliano wa karne ya 16, Giorgio Vasari aliandika hivi: “Picha za mawe ndizo picha zinazodumu zaidi. Picha nyingine huchakaa baada ya muda, lakini picha za mawe huendelea kung’aa hata zinapozeeka.” Naam, tunavutiwa na ustadi mkubwa uliotumiwa kutengeneza picha nyingi za mawe. Ama kweli, picha za mawe zinavutia sana!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 18 Falsafa mpya za Plato zilifundisha mambo yasiyo ya kimaandiko kama vile kutokufa kwa nafsi.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ramani ya Yerusalemu (karne ya sita W.K.)

[Hisani]

Garo Nalbandian

[Picha katika ukurasa wa 16]

Aleksanda Mkuu (karne ya pili K.W.K.)

[Hisani]

Erich Lessing/Art Resource, NY

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kuba la Rock, Yerusalemu (lilijengwa mwaka wa 685-691 W.K.)

[Picha katika ukurasa wa 17]

“Dionysos,” Antioch (wapata mwaka wa 325 W.K.)

[Hisani]

Museum of Art, Rhode Island School of Design, by exchange with the Worcester Art Museum, photography by Del Bogart

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mawe ya mchemraba, vijiwe vya duara, na vioo vyenye rangi bado vinatumiwa kutengeneza picha za kisasa

[Picha katika ukurasa wa 18]

Picha za mawe huko Lynn Heritage State Park, Massachusetts

[Hisani]

Kindra Clineff/Index Stock Photography

[Picha katika ukurasa wa 18]

Picha za mawe huko Barcelona zilizotengenezwa na Antoni Gaudí (mwaka wa 1852-1926)

[Hisani]

Foto: Por cortesía de la Fundació Caixa Catalunya