Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kukabiliana na Mafuriko Huko Caucasus

Kukabiliana na Mafuriko Huko Caucasus

Kukabiliana na Mafuriko Huko Caucasus

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI URUSI

MWAKA uliopita, katika eneo la kaskazini la Caucasus huko Urusi,kiwango chamvua ambacho kwa kawaida hunyesha katika kipindi cha miezi mitatu kilinyesha kwa siku mbili tu. Mito mingi ilifurika. Hata vijito vilifurika na kufagilia mbali kila kitu. Mabwawa yalivunjika, na nyumba na majengo mengine yakaharibiwa. Ghafula, maelfu ya wakazi waliachwa bila makao. Wengi waliokawia kutoka kwenye nyumba zao waliangamia. Wengine waliduwaa tu wakitazama wapendwa wao wakisombwa na mafuriko.

Katika jiji la Nevinnomyssk, familia moja ilijaribu kutoroka kwa tingatinga lao. Hata hivyo, maji yenye nguvu yalibiringisha tingatinga hilo, na familia yote ikaangamia. Watu fulani walikufa wakijaribu kuwaokoa wengine. Kulingana na makadirio ya serikali, watu 335,000 waliathiriwa na mafuriko hayo. Zaidi ya 200 walikufa na wengi hawakujulikana walipo.

Makumi ya maelfu ya nyumba zilifurika. Mabomba ya maji safi na ya kuondoa maji machafu yaliharibiwa. Hata maiti na mizoga ya wanyama waliokufa kutokana na kimeta ilifukuliwa na mafuriko hayo yenye nguvu. Inakadiriwa kwamba mafuriko hayo yalisababisha hasara ya rubo elfu 16 milioni za Urusi, au dola milioni 500 hivi za Marekani.

Nchi hiyo maridadi na yenye rutuba ambayo husifiwa mara nyingi kwenye nyimbo na mashairi ilikuwa katika hali ya kusikitisha! Lakini, janga hilo halikuharibu upendo wa kweli.

Msaada Watolewa Haraka

Mwanzoni, hakukuwa na maji safi, umeme, gesi, wala mawasiliano ya simu. Watu hawangeweza kuwasiliana na wengine. Zaidi ya Mashahidi wa Yehova 3,000 huishi katika eneo hilo, na zaidi ya 700 huishi katika mji wa Nevinnomyssk na viunga vyake. Mara tu walipopata habari kuhusu mafuriko, Mashahidi walianzisha halmashauri za pekee za dharura ili kuwatunza walioathiriwa. Halmashauri hizo zilianza kazi hata kabla waokoaji wa serikali hawajawasili.

Katika mji mdogo wa Orbelyanovka, karibu kilometa 60 hivi kusini-mashariki ya Nevinnomyssk, maji yaliongezeka haraka. Watu wanane, wakiwemo wanawake wawili Mashahidi, walikimbilia kilima kidogo. Wanyama wadogo na nyoka wengi walikimbilia kilima hicho pia. Hivyo, watu hao wanane walipambana na nyoka hao usiku kucha.

Asubuhi iliyofuata, Mashahidi wa eneo hilo walikuwa wakitafuta njia za kuwafikia dada zao wawili Wakristo. Hatimaye, wakati wa adhuhuri, walipata mtumbwi wa mpira. Lakini kabla ya kuwaokoa akina dada hao, Mashahidi walitumia mtumbwi huo kumwokoa mzee mmoja aliyepooza. Baadaye, walipokuwa wakiwaokoa dada hao, helikopta ilikuja na kuwachukua wale wengine waliokuwa kilimani.

Baadaye siku hiyo, Mashahidi hao walitumia mtumbwi huo kuwaokoa wengine. Mashahidi walipowauliza watu hao, “Je, mnajua sisi ni nani?” watu hao walijibu: “Bila shaka nyinyi ni Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Dharura.” Walishangaa waliposikia kwamba ni Mashahidi wa Yehova.

Mashahidi wa Nevinnomyssk walinunua jiko dogo na wakatayarisha chakula kwa ajili ya wale wenye uhitaji. Zaidi ya kuleta chakula, walileta maji, nguo, na dawa. Vikundi vya Mashahidi waliojitolea vilisafisha nyumba na kuondoa takataka nyuani.

Huko Zelenokumsk, wenzi wa ndoa Mashahidi ambao wana biashara walitumia gari lao kusafirisha maji, chakula, na mavazi waliyonunua kwenye soko la jumla. Wakati mke alipoulizwa na marafiki zake kwa nini amenunua vitu hivyo, alisema kwamba vilikuwa vya kuwasaidia waamini wenzake walioathiriwa na janga hilo. Walivutiwa na ukarimu wake na wakataka pia kusaidia. Mwanamke mmoja mfanyabiashara aliwapa gunia la tambi za kula, mwingine akatoa furushi kubwa la sabuni, na wengine wakatoa magunia ya sukari.

Msaada Kutoka Mbali

Kwa kuwa Mashahidi wengi nchini Urusi walitaka kujua jinsi ambavyo wangewasaidia watu walioathiriwa na mafuriko hayo, hazina maalumu ilianzishwa kwa ajili ya wale waliopenda kusaidia. Hata wafanyakazi wa kujitolea katika Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, karibu na St. Petersburg, walisaidia. Wengine walinunua vitu vipya kwa ajili ya walioathiriwa na mafuriko. Mmoja alisema hivi: “Nimetoa vitu vyangu bora zaidi kwa sababu angalau nina kitu, lakini ndugu na dada zetu hawana chochote.”

Kituo cha Usimamizi kilituma pia barua kwa makutaniko 150 hivi ya Mashahidi wa Yehova jijini St. Petersburg na Moscow, na kueleza jinsi ambavyo akina ndugu wangeweza kuchanga pesa, chakula, na nguo. Ingawa kuna matatizo ya kiuchumi nchini Urusi na Mashahidi wengi ni maskini, walitoa michango mingi sana. Michango yao inatukumbusha jinsi Wakristo maskini wa Makedonia walivyotoa michango kuwasaidia ndugu na dada zao huko Yudea.—2 Wakorintho 8:1-4.

Baada ya vitu vilivyochangwa kupangwa vizuri kwenye vituo vya kupokea, vilipakiwa katika malori na kupelekwa kwenye eneo lililokumbwa na janga hilo. Mbali na vitu hivyo vilivyochangwa, Kituo cha Usimamizi kilinunua tani kumi za chakula, jozi 500 za mashuka, na bidhaa za usafi, na vilevile vifaa na nguo za kazi kwa ajili ya usafi. Malori sita ya tani 50 yalisafirisha bidhaa hizo za msaada hadi eneo la kaskazini la Caucasus.

Ukarimu Ulitoa Ushahidi

Watu walivutiwa na kazi ya Mashahidi ya kusafisha eneo lililoathiriwa na mafuriko. Mfano mmoja ni katika jiji maridadi la Kislovodsk, ambako kuna Mashahidi zaidi ya 300. Mashahidi hao waliomba kazi kwenye baraza la jiji na wakaonyeshwa eneo la kusafisha.

Mnamo Juni 28, saa mbili asubuhi, Mashahidi wapatao 150, kutia ndani familia nzima-nzima, walikuja na vifaa tayari kuanza kazi. Baadhi yao walichukua likizo isiyo na malipo ili wafanye kazi hiyo. Muda mfupi baadaye, gari moja lililombeba naibu wa kwanza wa meya liliwasili. Naibu huyo aliuliza hivi, “Hawa ni nani?”

Aliambiwa, “Ni Mashahidi wa Yehova. Wamekuja kusafisha jiji baada ya msiba.”

Alishangaa kuona watu wengi sana, na akasema, “Wamefanya vyema kuja! Asanteni! Inapendeza sana!”

Baadaye, kabla tu ya chakula cha mchana, afisa mwingine wa jiji alikuja kwa gari lake. Alishuka na kwenda mahali Mashahidi walipokuwa. Alisema hivi: “Tumekuwa tukitazama kazi yenu na tumeshangaa sana. Hatujawahi kamwe kuwaona watu wanaofanya kazi kama nyinyi. Tayari mmefanya kazi kubwa sana!”

Wakati huohuo, mama mmoja mzee aliyekuwa akitembea alisimama na kuuliza, “Kwa nini watu hawa wanafanya kazi kwa bidii sana?” Alipoambiwa ni Mashahidi wa Yehova wanawasaidia wakazi wa jiji, machozi yalimtiririka. Alisema hivi: “Nyinyi ni waamini wa kweli. Watu wazuri hujulikana wakati wa msiba.” Mwanamke mwingine alisema hivi: “Hilo ni jambo zuri sana! Sijaona jambo kama hilo kwa muda mrefu.”

Siku iliyofuata gazeti la Na Vodakh liliwasifu Mashahidi wa Yehova likisema kwamba walikuwa wamesafisha zaidi ya tani 100 za udongo jijini. Maafisa wa jiji la Kislovodsk waliwaandikia Mashahidi barua ya shukrani wakisema: “Msaada wenu mkubwa umelirembesha jiji tena . . . Bila shaka, mtapata sifa kubwa kutoka kwa wageni wengi wanaotembelea jiji letu.”

Ingawa janga lililokumba eneo la kaskazini la Caucasus lilisababisha hasara kubwa na matatizo mengi, Mashahidi wa Yehova walikuwa tayari kuwaonyesha upendo waamini wenzao na majirani. Walifurahi hasa kwa sababu wanajua kwamba matendo ya upendo kama hayo humtukuza Yehova, Muumba wetu.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Bahari Nyeusi

MILIMA YA CAUCASUS

Nevinnomyssk

Orbelyanovka

Zelenokumsk

Kislovodsk

Bahari ya Caspian

[Hisani]

Globe: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mashahidi walinunua jiko hili na wakatayarisha chakula kwa ajili ya wenye uhitaji

[Picha katika ukurasa wa 17]

Shahidi huyu alitumia gari la familia yao kupeleka chakula na misaada

[Picha katika ukurasa wa 18]

Maafisa wa jiji la Kislovodsk waliwashukuru Mashahidi kwa kusaidia kusafisha jiji lao