Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Jamii Mpya za Ndege Zagunduliwa

Gazeti The Independent la London linasema kwamba “jumla ya jamii mpya 28 [za ndege] zimezungumziwa katika majarida ya kisayansi tangu mwaka wa 1998, na huenda jamii zaidi zikagunduliwa na kuongeza idadi ya ndege ulimwenguni hadi 9,700 hivi.” Kulingana na Steve Gantlett, mhariri wa gazeti Birding World, “jamii nyingi zimegunduliwa kwa sababu wataalamu wa ndege wanaweza kufika sehemu nyingi ambazo hawangeweza kufika makumi ya miaka iliyopita.” Anasema ugunduzi huo “unaonyesha kwamba wamekuwa stadi zaidi katika kutambua ndege mbalimbali kwa milio yao—njia pekee inayotumiwa mara nyingi kuwatambua ndege katika misitu ya mvua yenye msongamano wa miti.” Wanasayansi wanaamini kwamba jamii nyingi zaidi zitagunduliwa. Hata hivyo, huenda uharibifu wa mazingira ukahatarisha jamii zilizogunduliwa karibuni “kwa sababu zina ndege wachache na zinapatikana katika maeneo machache,” laeleza gazeti The Independent. 

Samaki Wenye Makelele

Gazeti The West Australian linaripoti kwamba watafiti wa Taasisi ya Australia ya Sayansi ya Baharini wamegundua kwamba samaki “kama vile damselfish, kifuu, na dagaa-donzi . . . huwasiliana kwa kukoroma, kulia, na kupiga mbinja.” Uchunguzi huo unaonyesha jinsi samaki wadogo hujua njia ya kurudi nyumbani kwenye tumbawe wanaposukumwa mbali na maji. Watafiti wa taasisi hiyo walinasa sauti ndani ya matumbawe na wakacheza sauti hizo karibu na samaki. Mwanasayansi Dakt. Mark Meekan aliliambia gazeti hilo kwamba “samaki wengi wadogo walipatikana kwenye sehemu hizo za uchunguzi ambako sauti hizo zilichezwa kuliko katika sehemu ambazo hazikuwa na makelele ya samaki na hilo linaonyesha [kwamba] samaki huvutiwa na sauti hususa.” Watafiti wamegundua kwamba sauti fulani za samaki waliokomaa zinaweza kusikika umbali wa kilometa 15. Meekan anasema kwamba “wakati wa alfajiri na jioni sauti za samaki huwa kubwa sana kama makelele ya mashabiki wengi kwenye uwanja wa mpira.” Hata hivyo, wanadamu hawawezi kusikia sauti hizo.

Je, Ni Hasara Kupunguza Uzito?

Gazeti International Herald Tribune la Paris linasema kwamba “katika mwaka wa 2002, watu milioni 231 hivi katika Muungano wa Ulaya walijaribu kupunguza uzito kwa kudhibiti ulaji wao.” Ripoti ya kikundi cha Datamonitor kinachochunguza maendeleo ya viwanda, inasema kwamba mwaka jana watu huko Ulaya walitumia dola bilioni 100 kununua bidhaa za kupunguza uzito—“kiasi kinacholingana na mapato ya Morocco kwa mwaka mmoja.” Hata hivyo, “watu wasiozidi milioni 4 ndio hufaulu kupunguza uzito kwa kipindi kinachozidi mwaka mmoja,” na “chini ya asilimia mbili ya watu wanaopunguza uzito ndio hufaulu kupunguza uzito kabisa barani Ulaya,” lasema gazeti hilo. Wajerumani ndio waliotumia pesa nyingi zaidi kununua bidhaa za kupunguza uzito, karibu dola bilioni 21, na Waingereza walitumia dola bilioni 16 hivi. Waitaliano walitumia karibu dola bilioni 15 na Wafaransa karibu dola bilioni 14. Gazeti Tribune linasema kwamba kulingana na kikundi cha Datamonitor, “watu wanaopunguza uzito wanapaswa kufahamu kwamba kudhibiti ulaji pekee hakuwezi kusuluhisha kabisa tatizo la kunenepa kupita kiasi.”

Matatizo ya Vijana wa Miaka 20

Gazeti Gießener Allgemeine la Ujerumani linasema kwamba “vijana wenye umri wa miaka 20 na kitu” wanapaswa “kuishi raha mstarehe. Wakati huo kijana huwa amebalehe kabisa na huwa hajaanza kukabili matatizo yanayowakumba watu wa makamo.” Lakini badala ya kuishi raha mstarehe, vijana wengi wenye umri wa miaka 20 na kitu wanakabili matatizo. Gazeti hilo linasema kwamba “vijana wanakuwa na wasiwasi kuhusu maisha yao wanapokaribia kumaliza masomo yao.” Mwanasaikolojia Christiane Papastefanou kutoka Mannheim anasema kwamba maendeleo ya kijamii katika miaka ya majuzi ndiyo yanayochangia wasiwasi huo. Isitoshe, kwa kuwa siku hizi kuna kazi mbalimbali za kufanya na njia mbalimbali za kuishi, vijana fulani huogopa kufanya uamuzi usiofaa. Hata hivyo, Papastefanou aliyenukuliwa na gazeti hilo la Ujerumani anasema kwamba maamuzi yanaweza kubadilishwa, na si kosa “kubadili maamuzi mara kwa mara.”

Teknolojia Mpya Inayotambua Wanafunzi Wasiokuwepo

Toleo la Kiingereza la gazeti El País la Hispania linasema kwamba “kuna teknolojia mpya inayowawezesha walimu watume ujumbe kwa wazazi wakati wanafunzi wanapokosa kwenda shuleni.” Shule 200 huko Hispania zina programu mpya ya kompyuta inayowawezesha walimu kutuma matokeo ya mtihani, rekodi za wasiokuja shuleni, na adhabu ambazo wanafunzi wanapewa. Kila asubuhi, walimu hurekodi majina ya wanafunzi wakitumia kifaa kidogo cha mkononi. Halafu, kifaa hicho huunganishwa na kompyuta ambayo huchanganua habari hizo. Gazeti hilo linasema kwamba “nyakati nyingine mfumo huo hupeperusha ujumbe kwenye simu za mkononi za wazazi.” Hivyo teknolojia hiyo inaweza kutambua idadi ya wanafunzi wasiokuwepo, jambo ambalo halikuwezekana awali. Kulingana na toleo la Kihispania la El País, shule nyingine 400 zinataka kutumia mfumo huo wa kompyuta.

Kurekebisha Nyumba Kunaweza Kumdhuru Mtoto

Jarida Medi-Netz la Ujerumani linasema kwamba “mtoto anaweza kupata matatizo ya kupumua au hata kuugua ugonjwa unaoathiri mfumo wa kupumua katika miezi ya kwanza ya maisha yake ikiwa wazazi watarekebisha nyumba akiwa tumboni au muda mfupi baada ya kuzaliwa. Sasa imegunduliwa kwamba mfumo wa kinga wa mtoto huathiriwa pia, hata akiwa tumboni, na hivyo anakabili hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya kuambukiza na mizio.” Watafiti katika kliniki na taasisi kadhaa nchini Ujerumani waligundua kwamba kemikali zinazowadhuru watoto ni kama zile zinazotoka kwenye gundi, mazulia, rangi, na fanicha mpya. Jarida Medi-Netz linasema kwamba “kemikali zinazotoa mvuke hudhoofisha chembe za mfumo wa kinga zinazotulinda na mizio.” Ripoti kama hiyo katika gazeti la GEO inapendekeza kwamba wazazi wasirekebishe nyumba “hadi mtoto anapofikia umri wa miaka miwili” mfumo wake wa kinga unapokuwa imara zaidi.

Klabu za Michezo na Vileo

Kituo cha Internet cha Shirika la Habari la Ufini kinasema “vijana ambao ni wanachama wa klabu za michezo hunywa pombe zaidi na kulewa zaidi kuliko vijana wengine.” Uchunguzi huo uliochapishwa na Kituo cha Utafiti wa Afya katika Chuo Kikuu cha Jyväskylä, ulisema kwamba “mara nyingi matangazo ya biashara na wadhamini huhusianisha pombe, sigara, na michezo,” lasema gazeti Helsingin Sanomat la Helsinki. “Vijana huwaiga wanariadha mashuhuri wenye umri mkubwa. Vijana huwaona mabingwa wa michezo wakinyunyiziana mvinyo na kuvuta sigara katika sherehe za ushindi.” Tatizo lingine ni kunusa tumbaku. Gazeti hilo linasema kwamba “chini ya asilimia 4 ya wavulana wenye umri wa miaka 15 ambao si wanachama wa klabu za michezo walinusa tumbaku kila juma, lakini karibu asilimia 10 ya wale ambao ni wanachama walifanya hivyo.”

Kupepesa Macho

Gazeti El País la Hispania linaeleza kwamba “maelfu ya vikundi zaidi ya 30 vya neva vinahitajika ili kupepesa macho.” Vikundi hivyo vya neva ambavyo huunganisha “kigubiko cha jicho na ubongo,” vimechunguzwa kwa makini kuliko wakati mwingine wowote na kikundi cha wanasayansi wa neva wa Hispania, ambao walichunguza wanyama. Kwa nini vigubiko vya macho vinahitaji neva nyingi na tata jinsi hiyo? Kwa sababu macho hayafumbwi kwa njia ileile au kwa sababu ileile nyakati zote. Watu hupepesa macho mara 15 hivi kwa dakika ili yasikauke. Macho hujifumba ghafula kitu kinapoyakaribia na tunaweza pia kuyafumba kimakusudi. Vilevile tunaweza kuyafumba kidogo ikitegemea jinsi tunavyohisi au tunaweza kuyafumba kabisa kwa vipindi mbalimbali.

Jinsi Kompyuta Zinavyoathiri Mazingira

Gazeti New Scientist linasema kwamba “kwa kuwa kompyuta za kisasa ni safi na zenye kung’aa, mtu hawezi kujua kwamba zinaathiri mazingira.” Gazeti hilo lasema kwamba kutengeneza kifaa kinachoweza kuhifadhi habari kwenye kompyuta kwa miaka minne, “huhitaji nishati ya visukuku inayozidi uzito wa kifaa hicho mara 800.” Wachanganuzi huko Japan, Ufaransa, na Marekani wanakadiria kwamba utengenezaji na matumizi ya kifaa cha aina hiyo cha megabaiti 32 chenye uzito wa gramu mbili, huchukua angalau kilogramu 1.6 za nishati ya visukuku, kilogramu 32 za maji na gramu 72 za kemikali zenye sumu kama vile amonia na asidi ya haidrokloriki. Wachanganuzi hao walikata kauli hii: “Vifaa hivyo vidogo huathiri sana mazingira.”