Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mbegu Kubwa Zaidi Ulimwenguni

Mbegu Kubwa Zaidi Ulimwenguni

Mbegu Kubwa Zaidi Ulimwenguni

Miaka mingi iliyopita watu walivutiwa na mbegu kubwa ajabu iliyosukumwa na maji hadi kwenye fuo za visiwa vya Maldives na Indonesia. Hadithi mbalimbali kuhusu chanzo chake zilisambazwa. Watu fulani walidhani kwamba ilitokana na mti uliokua ndani ya maji. Ndiyo sababu iliitwa Coco-De-Mer, au nazi ya baharini. Mbegu hiyo hata ilidhaniwa kuwa tunda lililokatazwa ambalo Adamu alikula katika shamba la Edeni. Hata hivyo, ukweli ulibainika katikati ya karne ya 18. Mbegu hiyo ya ajabu ilitokana na mchikichi unaopatikana katika visiwa vya Ushelisheli katika Bahari ya Hindi.

Nazi hizo hupatikana kwa wingi huko Vallée de Mai, kwenye kisiwa cha Praslin. Michikichi hiyo inaweza kufikia urefu wa meta 30 na inakadiriwa kwamba inaishi kwa mamia ya miaka. Jambo moja la kustaajabisha kuhusu miti hiyo ni kwamba kuna ya kiume na ya kike. Ili mti wa kike uzae matunda ni lazima uchavushwe na mti wa kiume. Kwa hiyo, ili iendelee kuzaana ni lazima kuwe na miti ya kiume na ya kike iliyokomaa.

Mti wa kike una tunda la pekee sana. Tunda hilo linapokuwa mtini hufanana na moyo mkubwa wa rangi ya kijani. Lakini ndani kuna mbegu iliyogawanywa katika sehemu mbili za mviringo ambazo zinaweza kuwa na uzito wa kilogramu 20. Matunda mengine yana mbegu zaidi. Basi si ajabu kwamba kitabu The Guinness Book of Records kinasema kwamba mbegu ya Coco-De-Mer ndiyo kubwa zaidi ulimwenguni.

Mtu anapoona vichala vya tunda hilo kubwa kama mwamba, hakosi kustaajabia sana kazi hiyo ya ajabu ya uumbaji. Lakini ni hatari sana kusimama chini ya mti huo. Vichala vyake vinaweza kuwa na uzito wa kilogramu 180. Hata hivyo, hakuna ripoti zozote zinazoonyesha kwamba mtu fulani aliwahi kujeruhiwa na tunda hilo. Walakini si jambo la hekima kutembelea Vallée de Mai wakati wa dhoruba kali. Ni bora kutazama miti hiyo wakati hali ya hewa ni shwari.