Ni Tatizo Kubwa Kadiri Gani?
Ni Tatizo Kubwa Kadiri Gani?
MNAMO Oktoba 1997, Hollie Mullin, mtoto wa majuma matatu alipata ambukizo kwenye sikio. Kwa kuwa ambukizo halikupona baada ya siku chache, daktari alipendekeza apewe dawa ya kisasa ya kiuavijasumu (dawa ya kuua viini). Ambukizo lilitarajiwa kupona kwa urahisi lakini haikuwa hivyo. Liliendelea kila alipopewa viuavijasumu zaidi.
Katika mwaka wake wa kwanza, Hollie alikuwa ametumia viuavijasumu 17. Kisha akiwa na umri wa miezi 21, alipata ambukizo baya zaidi. Baada ya kutiwa dawa kali zaidi mishipani kwa siku 14, ambukizo lilipona hatimaye.
Visa kama hivi havijaongezeka miongoni mwa watoto na wazee pekee. Watu wa kila umri wanaugua na hata kufa kutokana na maambukizo ambayo hapo awali yalitibiwa kwa urahisi kwa kutumia viuavijasumu. Ama kwa hakika, tangu miaka ya 1950 viini sugu vimezusha matatizo makubwa katika hospitali fulani. Halafu katika miaka ya 1960 na 1970, viini vinavyokinza viuavijasumu vilienea katika jamii.
Baada ya muda, watafiti wa kitiba walisema kwamba viini vinavyokinza viuavijasumu viliongezeka hasa kwa sababu dawa hizo zilitumiwa kupita kiasi kuwatibu wanadamu na wanyama. Mnamo mwaka wa 1978, mmoja wa watafiti hao alisema kwamba viuavijasumu vinatumiwa “kupita kiasi.” Kwa hiyo, kufikia miaka ya 1990, vichwa vifuatavyo vya habari vilionekana ulimwenguni pote: “Viini Sugu Vyaibuka,” “Viini Sugu Vinatawala,” “Dawa Hatari—Kutumia Viuavijasumu Kupita Kiasi Kunasababisha Viini Sugu.”
Je, vichwa hivyo vilitia chumvi? Mashirika maarufu ya kitiba hayaoni hivyo. Katika mwaka wa 2000, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni alisema hivi katika ripoti kuhusu magonjwa ya kuambukiza: “Wanadamu wanakabili tatizo jingine mwanzoni mwa milenia mpya. Magonjwa ambayo awali yalitibiwa . . . sasa yamepata nguvu zaidi za kukinza dawa.”
Tatizo hilo ni kubwa kadiri gani? Shirika la Afya Ulimwenguni liliripoti hivi: “Tatizo hilo [la viini vinavyokinza dawa] linafanya jitihada za kutibu magonjwa ya kuambukiza zisifaulu.” Wataalamu fulani leo hata wanasema kwamba wanadamu watarudia kipindi ambacho hakukuwa na dawa za kuua viini.
Viini sugu vimewezaje kutawala ulimwengu na kukinza maendeleo tata ya kisayansi? Je, mtu anaweza kufanya lolote ili kujilinda au kuwalinda wengine? Na je, kuna matazamio ya kukomesha viini sugu? Makala zinazofuata zitajibu maswali haya.