Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wakati Ambapo Viini Havitamdhuru Yeyote

Wakati Ambapo Viini Havitamdhuru Yeyote

Wakati Ambapo Viini Havitamdhuru Yeyote

VIINI ni muhimu kwa uhai. Sehemu kubwa ya udongo na ya miili yetu imefanyizwa kwa viini. Kama vile sanduku “Aina za Viini” kwenye ukurasa wa 7 linavyosema “kuna trilioni nyingi za bakteria mwilini mwetu.” Nyingi ni muhimu kwa afya. Ingawa viini vichache husababisha magonjwa, tuna hakika kwamba siku moja viini havitamdhuru mtu yeyote.

Kabla ya kuchunguza jinsi madhara ya viini yatakavyokomeshwa, hebu tuone jitihada ambazo zimefanywa hivi majuzi kupambana na viini vinavyosababisha magonjwa. Zaidi ya kuchunguza sanduku lenye kichwa “Mambo Unayoweza Kufanya,” hebu fikiria jitihada ambazo wataalamu wa afya wamefanya kupambana na viini sugu.

Mikakati ya Ulimwenguni Pote

Dakt. Gro Harlem Brundtland, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, alieleza jitihada ambazo zinafanywa. Katika ripoti inayoitwa Report on Infectious Diseases 2000, yenye kichwa “Kupambana na Viini Sugu,” alionyesha uhitaji wa kuanzisha ‘mkakati wa ulimwenguni pote wa kudhibiti viini sugu.’ Pia alieleza juu ya kuanzisha “mashirika yatakayohusisha wataalamu wote wa afya,” na akakazia hivi: “Tuna nafasi ya kuanzisha jitihada kabambe ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza.”

Mnamo mwaka wa 2001, Shirika la Afya Ulimwenguni lilichapisha hati yenye kichwa “Mkakati wa Ulimwenguni Pote wa Kudhibiti Viini Sugu.” Hati hiyo ilionyesha mambo ambayo wataalamu wa kitiba na watu kwa ujumla “wanaweza kufanya na jinsi ya kuyafanya.” Mkakati huo ulitilia maanani kuwaelimisha watu kujikinga na magonjwa, na vilevile kuwapa maagizo ya kutumia viuavijasumu na dawa nyingine za kuua viini wanapokuwa wagonjwa.

Isitoshe, wataalamu wa kitiba, yaani madaktari, wauguzi, na wafanyakazi wengine wa hospitali, walishauriwa kuchukua hatua zinazofaa ili kuzuia magonjwa yasienee. Kwa kusikitisha, uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba wataalamu wengi wa afya wanapuuza kunawa mikono au kubadilisha glavu baada ya kuwatibu wagonjwa.

Uchunguzi pia umeonyesha kwamba madaktari huwapendekezea wagonjwa viuavijasumu wakati ambapo hawavihitaji. Sababu moja ni kwamba wagonjwa huwasihi madaktari wawapendekezee viuavijasumu ili wapone haraka. Kwa hiyo madaktari hukubali maombi yao, ili kuwafurahisha. Mara nyingi madaktari hawawaelimishi wagonjwa na hawana vifaa vya kutambua viini vinavyosababisha magonjwa. Pia huenda wakawapendekezea viuavijasumu vipya na vya bei ghali ambavyo vinaweza kutibu magonjwa mengi. Na hilo huchangia tatizo la viini sugu.

Mkakati wa Shirika la Afya Ulimwenguni ulizungumzia pia hospitali, mifumo ya kitaifa ya afya, wazalishaji wa chakula, makampuni ya kutengeneza dawa, na wabunge. Ripoti hiyo ilisema kwamba wote wanapaswa kushirikiana ili kupambana na tatizo la viini sugu ulimwenguni pote. Lakini je, mpango huo utafaulu?

Vizuizi vya Mafanikio

Mkakati wa Shirika la Afya Ulimwenguni ulitaja jambo kuu linalozuia matatizo ya afya yasisuluhishwe. Jambo hilo ni pesa. Biblia inasema kwamba kupenda pesa ndiko kunakosababisha “mambo mabaya ya namna zote.” (1 Timotheo 6:9, 10) Shirika hilo linasema hivi: “Inafaa pia kuzingatia ushirikiano na makampuni ya kutengeneza dawa, na vilevile kudhibiti ushirikiano kati ya maafisa wa mauzo na wafanyakazi wa hospitali na mipango ya makampuni hayo ya kuelimisha wafanyakazi wa hospitali.”

Makampuni ya kutengeneza dawa yamesisitiza madaktari wanunue dawa zao. Sasa wanashawishi umma moja kwa moja kupitia matangazo ya biashara kwenye televisheni. Hilo limechangia matumizi ya dawa kupita kiasi, na hivyo kusababisha ongezeko la viini sugu.

Mkakati wa Shirika la Afya Ulimwenguni unasema hivi kuhusu matumizi ya dawa za kuua viini katika kutibu mifugo: “Kwa kuwa katika nchi fulani madaktari wa mifugo hupata asilimia 40 au zaidi ya mapato yao kwa kuuza dawa, hawataki kuwazuia watu kutumia dawa za kuua viini.” Kama inavyojulikana, viini sugu vimeibuka na kuongezeka kwa sababu dawa za kuua viini zinatumiwa kupita kiasi.

Idadi ya viuavijasumu vinavyotengenezwa ni kubwa ajabu. Nchini Marekani pekee, kilogramu zipatazo milioni 20 hutengenezwa kila mwaka! Kati ya viuavijasumu vyote ambavyo hutengenezwa ulimwenguni, karibu nusu tu ndivyo hutumiwa kuwatibu wanadamu. Nusu inayosalia hunyunyiziwa mimea au hulishwa wanyama. Viuavijasumu huchanganywa na chakula cha mifugo ili kuharakisha ukuzi.

Jukumu la Serikali

Umalizio wa Mkakati wa Shirika la Afya Ulimwenguni unasema hivi: “Nchi mojamoja zina jukumu kubwa la kutekeleza mkakati huu. Serikali zina daraka muhimu sana.”

Kwa hakika, serikali kadhaa zimeanzisha miradi ya kudhibiti viini sugu, huku zikitilia maanani ushirikiano nje na ndani ya nchi zao. Miradi hiyo inahusisha kuchunguza matumizi ya dawa za kuua viini na viini sugu, kuboresha njia za kudhibiti magonjwa, kutumia vizuri dawa za kuua viini katika tiba na kilimo, kufanya utafiti ili kuelewa jinsi viini vinavyokuwa sugu, na kubuni dawa mpya. Kulingana na Report on Infectious Diseases 2000 ya Shirika la Afya Ulimwenguni, haielekei mradi huo ungetekelezwa. Kwa nini?

Ripoti hiyo ilisema kwamba “serikali fulani hazitaki kutilia maanani afya ya umma.” Iliongezea hivi: “Magonjwa—na viini sugu—huenea kunapokuwa na vita, umaskini, uhamaji mkubwa na uharibifu wa mazingira, wakati ambapo watu wengi huwa katika hatari ya kuambukizwa magonjwa.” Kwa kusikitisha, serikali za wanadamu hazijafaulu kamwe kusuluhisha matatizo hayo.

Hata hivyo, Biblia inatueleza kuhusu serikali ambayo itasuluhisha matatizo yanayosababisha magonjwa na vilevile kukomesha kabisa magonjwa. Labda unafikiri kwamba viini fulani vitaendelea kuleta madhara siku zote, lakini kuna sababu nzuri za kuamini kwamba haitakuwa hivyo wakati ujao.

Wakati Ambapo Viini Havitadhuru

Zamani sana, nabii Isaya anayetajwa katika Biblia alizungumzia serikali yenye uwezo unaopita wa wanadamu na akamtambulisha mtawala wa serikali hiyo. Hebu ona unabii wake unavyosema: “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.”—Isaya 9:6, italiki ni zetu.

Mtoto huyo, au mfalme, ambaye atapokea utawala ni nani? Hebu ona jinsi alivyotambulishwa hata kabla hajazaliwa. Malaika Gabrieli alimwambia bikira Maria hivi: “Tazama! utachukua mimba katika tumbo lako la uzazi na kuzaa mwana, nawe itakupasa kumwita jina lake Yesu. Huyu atakuwa mkubwa . . . , na hakutakuwa na mwisho wa ufalme wake.”Luka 1:31-33.

Yesu alipokuwa mtu mzima, alionyesha kwamba yeye ndiye Mtawala aliyeahidiwa wa Ufalme wa Mungu. Yesu alitembea kotekote akihubiri “habari njema ya ufalme” na akaonyesha nguvu zake za kukomesha magonjwa yote. Biblia inasema kwamba “umati mkubwa ukamkaribia yeye, ukiwa pamoja na watu waliokuwa vilema, walioharibika viungo, walio vipofu, mabubu, na wengi wa hali tofauti, nao wakawatupa kabisa miguuni pake, naye akawaponya; hivi kwamba umati ukahisi mshangao ulipoona mabubu wakisema na vilema wakitembea na vipofu wakiona.”—Mathayo 9:35; 15:30, 31.

Naam, Yesu aliponya magonjwa yote. Hata aliwafufua watu fulani waliokuwa wamekufa! (Luka 7:11-17; 8:49-56; Yohana 11:38-44) Ni kweli kwamba wale walioponywa na hata wale waliofufuliwa walikufa hatimaye. Hata hivyo, miujiza ya Yesu ilionyesha yale ambayo atawafanyia wanadamu wanaoishi duniani wakati ujao chini ya utawala wa Ufalme. Biblia inaahidi kwamba wakati huo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24; Ufunuo 21:3, 4.

Leo, kama sote tujuavyo sana, mtu yeyote anaweza kuwa mgonjwa na kufa. Viini hudhuru mamilioni ya watu na mara nyingi husababisha kifo. Hata hivyo, mwili wa mwanadamu umeumbwa kwa njia ya ajabu sana hivi kwamba wengine hushangaa ni kwa nini watu huwa wagonjwa. Daktari Lewis Thomas aliandika kuhusu umuhimu wa bakteria na akasema kwamba magonjwa hutokea “kwa sadfa tu.” Aliongeza hivi: “Huenda kinga za mwili za wagonjwa zina kasoro fulani.”

Ama kweli, watu wenye mfumo wa kinga wenye nguvu mara nyingi hawapati magonjwa yanayosababishwa na bakteria au hawaugui magonjwa hayo kamwe. Walakini, watu wote huzeeka na kufa hatimaye. Biblia inasema kwamba dhambi ambayo wanadamu walirithi kutoka kwa mwanadamu wa kwanza mkamilifu, Adamu, ndiyo inayosababisha magonjwa na kifo. Biblia inasema kwamba “kupitia mtu mmoja dhambi iliingia katika ulimwengu na kifo kupitia dhambi, na hivyo kifo kikasambaa kwa watu wote kwa sababu wote walikuwa wamefanya dhambi.”—Waroma 5:12.

Hata hivyo, Mungu alimtuma Mwana wake duniani ili atoe uhai wake mkamilifu uwe fidia ya kuwakomboa wanadamu kutokana na matokeo ya dhambi. (Mathayo 20:28) Biblia inaeleza hivi: “Mshahara ambao dhambi hulipa ni kifo, lakini zawadi ambayo Mungu hutoa ni uhai udumuo milele kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu.” (Waroma 6:23; 1 Yohana 5:11) Wakati wa utawala wa Ufalme wa Mungu, watu wataponywa kupitia dhabihu ya fidia ya Kristo. Kisha viini vyote, hata vile vinavyosababisha magonjwa leo, havitamdhuru mtu yeyote.

Si ni jambo linalofaa kujifunza kuhusu serikali ya Ufalme iliyoahidiwa katika Biblia, ambayo itasuluhisha matatizo ya wanadamu? Mashahidi wa Yehova wangependa kukusaidia ujifunze mengi.

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

Mambo Unayoweza Kufanya

Unaweza kufanya nini ili kupunguza uwezekano wa kuathiriwa na viini sugu? Shirika la Afya Ulimwenguni limetoa madokezo kadhaa. Kwanza, lilidokeza mambo tunayoweza kufanya kupunguza magonjwa na kuzuia maambukizo yasienee. Pili, lilieleza jinsi watu wanavyoweza kutumia vizuri dawa za kuua viini.

Njia bora ya kupunguza na kuzuia magonjwa yasienee ni kujitahidi juu chini kutunza afya. Unaweza kufanya nini ili kujikinga na magonjwa?

Madokezo ya Kujikinga na Magonjwa

1. Jitahidi kadiri uwezavyo kufanya mambo haya matatu: kula vizuri, kufanya mazoezi ya kutosha, na kupumzika vya kutosha.

2. Dumisha usafi. Wataalamu wa afya husema kwamba kunawa mikono ndiyo njia bora ya kujikinga na magonjwa au kuepuka kueneza maambukizo.

3. Hakikisha kwamba chakula mnachokula na familia yako ni salama. Hakikisha mikono yako na mahali unapotayarishia chakula ni safi. Pia, hakikisha kwamba unatumia maji safi kunawa mikono na kusafisha chakula. Kwa kuwa viini huzaana ndani ya chakula, pika nyama kabisa. Hifadhi vyakula vizuri.

4. Katika maeneo ambayo magonjwa hatari huenezwa na wadudu wanaoruka, epuka kuwa nje usiku au mapema asubuhi wakati ambapo wadudu ni wengi. Jikinge kwa chandarua sikuzote.

5. Kupata chanjo kunaweza kuimarisha mfumo wako wa kinga ili upambane na viini vinavyopatikana mahali unapoishi.

Kutumia Dawa za Kuua Viini

1. Omba mashauri ya daktari kabla ya kununua au kutumia viuavijasumu au dawa yoyote ya kuua viini. Dawa zinazouzwa na wachuuzi mara nyingi huwafaidi wauzaji badala ya wanunuzi.

2. Usimsihi daktari akupendekezee viuavijasumu. Ukifanya hivyo, huenda akakupendekezea kwa sababu hataki kumpoteza mteja. Kwa mfano, mafua husababishwa na virusi, na viuavijasumu haviponyi mafua. Kumeza viuavijasumu unapokuwa na virusi kunaweza kuua bakteria muhimu, na labda kufanya viini sugu viongezeke.

3. Usiwe na zoea la kutumia dawa mpya kabisa kwani huenda isikufae na huenda ukatumia pesa nyingi isivyo lazima.

4. Pata habari kuhusu dawa yoyote kutoka kwa mtu mwenye kutegemeka: Inatibu nini? Inaweza kuleta madhara gani? Inapaswa kutumiwa na dawa gani, ni mambo gani mengine yanayoweza kuifanya iwe hatari?

5. Iwapo kweli unahitaji kutumia viuavijasumu, inapendekezwa utumie dozi nzima, hata ukihisi nafuu kabla ya kuimaliza. Dawa za mwisho za dozi humaliza kabisa maambukizo.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Wakati wa utawala wa Mungu wenye uadilifu, watu watafurahia kuishi bila viini vyovyote vinavyodhuru