Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Gari Linalotumia Mbolea
Mtu mmoja mwenye shamba huko Ufini sasa ana gari linalotumia gesi inayotokana na mbolea inayooza. Gazeti la Ufini Suomen luonto laripoti hivi: “Gari hilo linatumia gesi inayotokana na mbolea iliyosafishwa na kuwekwa katika mtambo wa kutengeneza gesi ulio kwenye shamba la mwenye gari.” Gesi ya mbolea ndiyo gesi safi zaidi inayotumiwa kuendesha magari leo, na kwa kuwa inatokana na mbolea, haiharibu mazingira. Mojawapo ya bidhaa zinazotengenezwa wakati wa uzalishaji wa gesi ya mbolea hutumiwa katika kilimo. Magari yanayotumia gesi ya asili—milioni mbili hivi ulimwenguni kote—yanaweza pia kutumia gesi ya mbolea. Nchini Sweden mabasi mengi ya jijini hutumia gesi hiyo, na vituo fulani vya mafuta vinauza gesi hiyo pamoja na mafuta mengine. Kulingana na makala hiyo, kuna faida nyingine: “Gesi ya mbolea si ghali kama petroli au dizeli.”
Jinsi Chungu Wanavyookoka Mafuriko
Chungu hufanya nini mvua inaponyesha? Ingawa si chungu wote wanaoishi ardhini, baadhi ya wale wanaoishi ardhini hutumia mbinu za ajabu ili kuokoka mafuriko, lasema gazeti The New York Times. Wataalamu wa chungu Dakt. Edward O. Wilson na Bert Holldobler wanasema kwamba aina fulani ya chungu wa misitu ya kitropiki ‘hujikinga kunapokuwa na tone moja tu [la maji] mlangoni mwa mashimo yao kwa kukimbia kotekote na kuwajulisha chungu wengine, na mara nyingi huingia huku na kutokea kule. Wao hutumia harufu kuwaongoza chungu wengine wapitie katika vijia vilivyo wazi na nyakati nyingine huwaongoza nje.’ Kwa muda usiozidi sekunde 30 wanawatahadharisha chungu wengi kundini. Gazeti The Times linaripoti kwamba kusini-magharibi mwa Marekani na kaskazini mwa Amerika Kusini, chungu fulani “hutoka shimoni wakiwa vikundi vikubwa vinavyotia ndani chungu waliokomaa, malkia na watoto wake, na kuelea kwenye maji yanayozidi kuongezeka. Wengi huokoka . . . Mwishowe chungu hao wanaoelea hujishikilia kwenye nyasi au vichaka na wale wanaookoka hurudi shimoni maji yanapopungua.”
Hasara ya Kunywa Kupindukia
Gazeti The Independent la London linaripoti hivi: “Wanawake na vijana wengi nchini Uingereza wanakufa kutokana na kunywa pombe kupindukia. Vifo hivyo vimeongezeka maradufu katika miaka 20 iliyopita, na vinasababishwa hasa na ugonjwa mbaya wa ini na kufa kwa chembe za ini.” Isitoshe, idadi kubwa zaidi ya vijana wanakufa. “Miaka kumi iliyopita wanaume na wanawake wazee zaidi waliokufa kwa sababu ya kunywa kupindukia walikuwa na umri wa miaka 70 hivi. Takwimu za karibuni zaidi za mwaka wa 1998-2000 zinaonyesha kwamba watu wazee zaidi wanaokufa wana umri wa karibu miaka 60,” inasema ripoti hiyo. Lakini kunywa kupindukia hakusababishi magonjwa tu. Gazeti Le Monde linasema kwamba nchini Ufaransa “inaonekana unywaji wa pombe unasababisha asilimia 10 hadi 20 ya misiba kazini.” Isitoshe, huko Ufaransa, kila mwaka watu 2,700 hufa na 24,000 hujeruhiwa katika misiba ya barabarani inayosababishwa na unywaji wa pombe, na asilimia 30 hivi ya vitendo vya jeuri husababishwa na zoea hilo. Unywaji wa kupindukia pia husababisha hasara kubwa ya kifedha. Gazeti Le Monde linasema kwamba nchini Ufaransa unywaji wa kupindukia ulisababisha hasara ya dola bilioni 19.2 mnamo mwaka wa 1996.
Mfadhaiko na Magonjwa
Uchunguzi mmoja uliowachunguza zaidi ya wafanyakazi 8,000 nchini Uholanzi na kuripotiwa na Shirika la Uholanzi la Utafiti wa Kisayansi ulionyesha kwamba ‘mfadhaiko unaosababishwa na kazi na uchovu huongeza uwezekano wa kupata magonjwa mabaya kama vile mafua, homa na magonjwa ya tumbo. Uchunguzi huo ulibainisha kwamba uwezekano wa watu wanaofanya kazi ngumu sana kupata mafua ulikuwa asilimia 20 zaidi ya wale wasiofanya kazi ngumu sana.’ Mambo mengine yanayosababisha magonjwa ni kama vile kufanya kazi usiku na wasiwasi unaotokana na mabadiliko katika mashirika. Ripoti hiyo inasema kwamba “wafanyakazi wa zamu wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuugua kuliko wale wanaofanya kazi mchana.”
Watoto na Kuimba
Katika gazeti la kitiba la Gesundheit la Ujerumani, Dakt. Michael Fuchs, mtaalamu wa magonjwa ya sikio, pua, na koo wa Chuo Kikuu cha Leipzig, aliandika kwamba kuimba ni “njia muhimu ya watoto kueleza hisia zao inayowasaidia kukua.” Hata hivyo, Fuchs analalamika kwamba “aina za sauti za watoto zimepungua sana katika miaka 20 iliyopita. Sauti zao pia zimebadilika.” Fuchs anatoa sababu mbili. Kwanza, “watoto leo hawaimbi sana nyumbani. Zamani familia zilitumia wasaa wao kuimba na kucheza muziki, lakini sasa huketi na kutazama televisheni pamoja na kusikiliza muziki badala ya kuimba.” Pili, watoto wanapoimba, wao huigiza sauti mbovu za wanamuziki wa roki na waimbaji wengine mashuhuri. Fuchs anaandika hivi: “Watoto huumiza viungo vyao vya usemi wanapojaribu kuwaiga wanamuziki hao mashuhuri.” Kufanya hivyo kunaweza kukaza misuli yao ya shingo na ya koo. Isitoshe, kunaweza pia kusababisha uvimbe kwenye viungo vya usemi na kuharibu sauti zao.
Kuota Moto kwa Usalama
Jarida UC Berkeley Wellness Letter linasema kwamba “kuwasha moto jikoni au kutumia kuni kuwasha moto kunaweza kuchafua hewa ndani na nje ya nyumba na vilevile kusababisha moto.” Ili kuwasaidia watu kuepuka hatari za moto na matatizo ya kiafya yanayoletwa na uchafu huo, jarida hilo linatoa madokezo yafuatayo:
● “Dumisha bomba la moshi . . . , likiwa safi na katika hali nzuri.”
● “Fikiria kuweka kifaa cha kutambua gesi ya kaboni-monoksaidi . . . , hasa ikiwa nyumba yako haina matundu ya kutosha ya hewa.”
● “Washa mioto midogo badala ya mioto mikubwa yenye moshi.”
● “Tumia kuni zilizokauka—zilizohifadhiwa na kukaushwa angalau kwa miezi sita. Mbao ngumu huwasha moto mzuri unaodumu kwa muda mrefu.”
● “Fungua dirisha kidogo kuingiza hewa.”
● “Hakikisha kwamba jiko lako limejengwa vizuri, na liwe angalau meta moja kutoka kwa ukuta na vitu vingine vinavyoweza kushika moto.” Liweke juu ya “kifaa cha kuzuia moto ili kuzuia sakafu isishike moto.”
● “Usitumie mbao zilizotiwa dawa, mbao zilizounganishwa, mbao zilizotengenezwa kwa vibanzi, mbao zilizopakwa rangi au vanishi, karatasi zenye rangi, au plastiki. Vitu hivyo vinaweza kutoa moshi wenye sumu.”
● “Sikuzote tumia kinga ya moto unapoota moto.”
Majira ya Baridi Kali na Vitamini D
“Tunahitaji vitamini D ili kufyonza kalisi mifupani ambayo inaimarisha mifupa na kuizuia isivunjike,” laeleza jarida la Tufts University Health & Nutrition Letter. “Kwa ujumla, asilimia 90 ya vitamini D hutengenezwa kwenye ngozi yetu tunapoota jua. Lakini wakati wa majira ya baridi kali, mionzi ya jua katika maeneo yenye baridi haitoshi kutengeneza vitamini D ya kutosha. Isitoshe, watu wa umri wa makamo au wazee hawali hata kiasi cha asilimia 10 cha vitamini D ambacho hupatikana katika chakula.” Kwa hiyo Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Marekani inapendekeza kwamba wakati wa majira ya baridi kali, watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 hasa wanapaswa kula vyakula vingi zaidi vyenye vitamini D kama vile samaki wenye mafuta mengi, mafuta ya cheza au kutumia vidonge vya vitamini D, lakini wasipitishe kiwango cha mikrogramu 50 kwa siku.
Watoto Walevi wa Afrika Kusini
Gazeti The Star la Johannesburg linaonya kwamba “huenda Afrika Kusini ikawa nchi ya walevi, kwani watoto wanaanza kunywa pombe kupindukia kuanzia umri mdogo sana.” Inasemekana kwamba watoto wenye umri wa miaka tisa tu wanaenda shuleni wakiwa wamechoka sana kwa sababu ya ulevi na tabia hiyo inaongezeka. Tatizo hilo linasababishwa na nini? Polisi wanasema kwamba linasababishwa na “matangazo ya biashara [ambayo] huonyesha maisha yanayowavutia vijana.” Sababu nyingine zinazotolewa na gazeti hilo ni kupatikana kwa pombe, kukubaliwa kwa pombe katika jamii, uendekevu wa wazazi, na watoto kupewa uhuru na pesa nyingi zaidi. Mwanasaikolojia mmoja wa tiba anasema kwamba “wazazi wameachilia daraka la kuwadhibiti watoto na watu hawaheshimu mamlaka—ama kwa hakika jamii imezorota kabisa.”