Mafuta Je, Yatakwisha?
Mafuta Je, Yatakwisha?
“Bila [nishati] viwanda haviwezi kufanya kazi . . . Magari, malori, magari ya moshi, meli na ndege haziwezi kutengenezwa . . . Bila nishati, nyumba hazingalikuwa na joto wala taa, chakula hakingepikwa. . . . Bila nishati tungerudia Enzi ya Mawe.”—Kutoka kwa “Ripoti ya Marekani ya Nchi Zenye Mafuta Duniani ya Mwaka wa 2000.”
WATAALAMU wa nishati wanasema kwamba huenda mafuta yatakwisha hatimaye. Baadhi yao wanakadiria kwamba hifadhi za mafuta ulimwenguni zitadumu kwa miaka 63 hadi 95 zaidi. Kwa sasa, vyanzo vingine vya nishati vinatumika na baadhi yake vimetumiwa kwa makumi ya miaka. Vyanzo vifuatavyo vya nishati vinadumu au vinaweza kutumiwa tena: nishati ya jua, upepo, mawimbi, maji, na joto la bahari. Lakini kwa sasa kuna matatizo makubwa ya uzalishaji na usambazaji wa nishati hizo.
Kutarajia kutumia vyanzo vya nishati vinavyodumu baada ya vyanzo vingine vya nishati kwisha ni hatari. Kampuni za mafuta ziko tayari kutumia vizuri wakati mfupi unaobaki kabla ya mafuta kwisha. Lakini, inatarajiwa kwamba matatizo ya kijamii na ya kimazingira yanayosababishwa na mafuta yataendelea kuwapo kadiri mafuta yanavyopatikana. Hata hivyo, matatizo hayo hayasababishwi na mafuta. Pupa ya wanadamu na tamaa ya kutawala ndiyo imesababisha matatizo hayo.
Inatia moyo kwamba hali ya wakati ujao ya mafuta na hata ya vyanzo vingine vyote vya nishati haitegemei mataifa. Inategemea Muumba na Mtunzaji wa dunia, Yehova Mungu, ambaye ameahidi kwamba hivi karibuni matatizo yote ya kimazingira na ya kijamii yanayosababishwa na matumizi na uharibifu wa rasilimali za dunia yatakoma. (Ufunuo 4:11) Kama Biblia inavyosema, hivi karibuni Mungu ‘atawaharibu wale wanaoiharibu dunia.’ Utawala mwadilifu wa Mungu utaleta “mbingu mpya na dunia mpya,” ulimwengu ambao hautakuwa na choyo wala dhuluma, na rasilimali za dunia zitatumiwa bila ubinafsi kwa faida ya wanadamu wote watiifu.—Ufunuo 11:18; 21:1-4.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Vyanzo vingine vya nishati vyatia ndani vifaa vinavyotumia nishati ya jua kutokeza umeme na vinu vya upepo