Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mafuta Ni Muhimu Maishani Mwako

Mafuta Ni Muhimu Maishani Mwako

Mafuta Ni Muhimu Maishani Mwako

JE, UMEWAHI kuwazia jinsi maisha ya watu wengi yangekuwa bila mafuta na bidhaa zake? * Mafuta hutumiwa kulainisha magari, baiskeli, vigari vya watoto, na mashine nyingine zinazozunguka. Mafuta hupunguza msuguano na hivyo kuzuia mashine zisiharibike haraka. Lakini yana matumizi mengine.

Mafuta hutumiwa kuendesha ndege, magari, na mifumo ya kupasha joto. Vipodozi, rangi, wino, dawa, mbolea, plastiki na vitu vingine vingi hutengenezwa kwa bidhaa za mafuta. Maisha ya watu wengi yangebadilika sana kama mafuta hayangekuwapo. Basi si ajabu kwamba kitabu kimoja kinasema kwamba mafuta na bidhaa zake “zinatumiwa kwa njia nyingi sana labda kuliko kitu kingine chochote ulimwenguni.” Mafuta hupatikanaje? Mafuta hutoka wapi? Wanadamu wameyatumia kwa muda mrefu kadiri gani?

Biblia inatuambia kwamba zaidi ya miaka elfu mbili kabla ya Kristo, Noa alifuata maagizo ya Mungu akajenga safina kubwa na alitumia lami—labda iliyotokana na mafuta—kuzuia maji yasipenye. (Mwanzo 6:14) Bidhaa za mafuta zilitumiwa na Wababiloni kutengeneza matofali yaliyokaushwa kwenye tanuru, zilitumiwa na Wamisri kuhifadhi maiti, na watu wengine wa kale walizitumia katika matibabu.

Ni nani angedhani kwamba bidhaa hiyo ingekuwa muhimu sana leo? Hakuna mtu anayeweza kubisha kwamba maendeleo ya sasa viwandani yanategemea mafuta.

Mafuta yalipata umaarufu yalipoanza kutumiwa kuwasha taa. Katika karne ya 15, mafuta yaliyotoka kwenye visima visivyo na kina kirefu yalitumiwa kuwasha taa huko Baku, jiji kuu la Azerbaijan. Katika mwaka wa 1650, visima vya mafuta visivyo na kina kirefu vilichimbwa huko Rumania, ambako mafuta yalitumiwa kuwasha taa. Kufikia katikati ya karne ya 19, biashara ya mafuta ilikuwa imesitawi sana huko Rumania na katika nchi nyingine za Ulaya Mashariki.

Nchini Marekani, harakati za kutafuta chanzo cha nuru nyangavu zaidi katika miaka ya 1800, zilifanya kikundi cha wanaume waanze kutafuta mafuta. Wanaume hao walikata kauli kwamba iliwabidi kuchimba mafuta ili wapate mafuta ya taa yanayotosheleza wateja. Kwa hiyo, katika mwaka wa 1859, kisima cha mafuta kilichimbwa huko Pennsylvania. Jitihada za kutafuta mafuta ya taa zikapamba moto. Ikawaje?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Nyakati nyingine mafuta huja juu ya ardhi kupitia mianya. Yanaweza kuwa majimaji au mazito kama lami, bereu, au bitumeni.

[Sanduku katika ukurasa wa 3]

MAFUTA NI NINI?

Mafuta ni mchanganyiko mzito wa asili wa gesi na umajimaji wa haidrojeni na kaboni ambao unapatikana ardhini, unashika moto kwa urahisi, na una rangi nyeusi na manjano. Mchanganyiko huo unaweza kutenganishwa katika visehemu kama vile gesi ya asili, petroli, nafta, mafuta ya taa, mafuta ya kulainisha, nta, na lami, na hutumiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali.