Zawadi ya Manjano Kutoka Kaskazini
Zawadi ya Manjano Kutoka Kaskazini
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SWEDEN
‘Tutawapelekea zawadi gani kutoka nchini mwetu?’ mimi na mke wangu tulijiuliza kabla ya kuondoka Sweden ili kuwatembelea rafiki zetu huko Uingereza. Tulitaka kuifanya zawadi yetu ya jemu ya matunda ya cloudberry tuliyotengeneza wenyewe iwe yenye kuelimisha. Kwa hiyo, tuliandika kibandiko chenye maelezo yaliyotegemea mambo tunayojua na utafiti kutoka kwa vitabu vya kwetu. Tumeeleza matokeo ya utafiti wetu hapa chini.
Cloudberry Ni Matunda ya Aina Gani?
Matunda ya cloudberry, Rubus Chamaemorus katika Kilatini, hukua kwenye mimea isiyozidi urefu wa sentimeta 30. Kila mmea huchanua ua moja jeupe na kuzaa tunda moja tu. Tunda huwa jekundu na gumu linapokuwa bichi lakini linapoiva linakuwa na rangi ya manjano au ya machungwa na linakuwa laini na lenye majimaji. Jina cloudberry (tunda la mawingu), huenda lilitungwa kwa sababu kwa kawaida huko kaskazini mwa Uingereza matunda hayo hukua milimani karibu na mawingu. Unaweza pia kuyaona kwenye sehemu zenye unyevu, hasa katika maeneo mapana yasiyokuwa na miti na yale yenye majimaji kusini mwa Aktiki. Huko Sweden, matunda hayo huiva Agosti, kabla tu ya majira ya kuchipua kuanza.
Dhahabu ya Maeneo Yenye Majimaji
Kwa karne nyingi, wenyeji Walapp wamekusanya matunda hayo ili wayatumie wakati wa baridi kali. Yana vitamini C nyingi na vitamini nyingine, na kwa sababu yana kemikali ya kiasili inayoyahifadhi, jemu iliyotengenezwa kwa matunda hayo inaweza kudumu kwa miaka mingi ikiwekwa mahali baridi. Kwa kuwa walowezi wa mapema katika maeneo haya ya kaskazini walikula nyama na samaki hasa, matunda hayo yaliwapa vitamini. Si ajabu kwamba yameitwa dhahabu ya maeneo yenye majimaji!
Siku hizi, matunda mengi sana ya cloudberry hukusanywa ili yauzwe madukani na viwandani. Kwa mfano, nchini Sweden, katika mwaka mmoja, zaidi ya tani elfu moja za matunda hayo huchumwa na kuuzwa! Wafanyakazi wanaochuma matunda hayo kwa bidii, hasa wanafunzi wa shule walio likizoni, hupata pesa nyingi kwa njia hiyo. Wenyeji wa Ufini wameyasifu matunda hayo kwa kuweka picha yake kwenye sarafu mpya ya euro mbili!
Mlo Mtamu
Tunda la cloudberry lina ladha tamu na chungu yenye kuburudisha. Unaweza kupata jemu ya cloudberry, mvinyo, na vitu vingine vilivyotengenezwa nazo katika maduka ya chakula au maduka mengine katika majiji makubwa ya Ulaya na Marekani. Mara nyingi, aiskrimu ya cloudberry huliwa baada ya milo ya sherehe za kila mwaka za kuwatunukia washindi wa Tuzo ya Nobeli, inayofanywa Stockholm, Sweden. Mikahawa fulani huuza jemu iliyopashwa joto pamoja na aiskrimu ya vanila. Isitoshe, jemu hiyo huliwa kwa keki ya jibini ya Sweden au jibini ya Camembert iliyokaangwa na hutiwa pia ndani ya vitobosha kuongeza ladha. Mvinyo wa manjano wa matunda hayo hutengenezwa nchini Ufini, na divai yake imeanza kuuzwa hivi majuzi huku Sweden.
Ukitembelea mahali penye matunda hayo, yachume na ufurahie ladha yake tamu, na unaweza kuongeza sukari laini na kupaka juu krimu nyingi iliyopigwapigwa. Utagundua kwamba ni ya pekee sana kama dhahabu na huenda ukachochewa kumshukuru Muumba wako kwa zawadi hiyo yenye ladha tamu sana.