Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Ndoto ya Kupata Njia ya Kaskazini-Magharibi Imetimia?

Je, Ndoto ya Kupata Njia ya Kaskazini-Magharibi Imetimia?

Je, Ndoto ya Kupata Njia ya Kaskazini-Magharibi Imetimia?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFINI

KWA kawaida watu huona kwamba ongezeko la joto duniani husababisha hasara. Lakini huenda likatimiza ndoto ya mabaharia wengi ya kupitia Njia ya Kaskazini-Magharibi. Kulingana na gazeti Science, huenda njia hiyo inayounganisha Bahari ya Atlantiki na Pasifiki na inayopita juu ya bara la Amerika Kaskazini itaanza kutumiwa na meli karne hii. Linaelezea hivi: “Njia hiyo itapunguza safari ya kutoka Ulaya hadi Asia kupitia Mlango-Bahari wa Panama [kwa kilometa 11,000] na itapunguza safari hiyohiyo kupitia Rasi ya Horn [kwa kilometa 19,000] kwa ajili ya meli za mafuta zisizoweza kupitia kwenye rasi hiyo.”

Uwezekano wa kupitia mlango huo ulitabiriwa zaidi ya miaka 500 iliyopita. Jitihada za mapema za kupata njia ya kaskazini zilifanywa punde baada ya Christopher Columbus kuvumbua bara la Amerika. Mnamo mwaka wa 1497, Mfalme Henry wa 7 wa Uingereza alimtuma John Cabot kutafuta njia ya baharini inayoelekea Mashariki. Kama Columbus, Cabot aliabiri magharibi kutoka Ulaya, lakini baadaye akaelekea kaskazini. Cabot alipotia nanga, labda huko Newfoundland, Amerika Kaskazini, alikuwa na hakika kwamba amewasili Asia. Ingawa baadaye ilitambuliwa kwamba kulikuwa na bara la Ulimwengu Mpya kati ya Ulaya na Asia, jitihada za kutafuta njia ya kaskazini kuelekea Mashariki ziliendelea. Je, bara hilo lililovumbuliwa lingeweza kufikiwa kutoka kaskazini?

Kizuizi cha Barafu

Ilionekana rahisi kupata na kupitia Njia ya Kaskazini-Magharibi. Hata hivyo, haikuwa rahisi kwani hali mbaya za Aktiki zilifanya safari hiyo iwe ngumu kuliko ilivyotarajiwa. Kizuizi kikubwa kilikuwa barafu. James P. Delgado aliandika hivi katika kitabu chake Across the Top of the World: “Barafu hiyo iliachana na kuruhusu meli ziingie kisha iliungana na kunasa meli na mabaharia kama mtego, na wakati mwingine iliwaponda.”

Sir Martin Frobisher alikumbana na barafu alipokuwa akiongoza kikundi cha kwanza kilichosafiri kaskazini ya bara la Amerika Kaskazini ili kutafuta Njia ya Kaskazini-Magharibi kupitia eneo la Aktiki. Kikundi hicho chenye meli mbili na mashua moja kiliondoka London mwaka wa 1576. Frobisher alikutana pia na Wainuit, wenyeji wa eneo la Aktiki. Kwanza alifikiri walikuwa sili au samaki, “lakini walipokaribia aligundua kwamba walikuwa wanaume katika mashua za ngozi,” chasema kitabu kimoja kuhusu safari ya Frobisher. Kwa ujumla, Frobisher alisafiri mara tatu hadi Aktiki, lakini hakufaulu kupata Njia ya Kaskazini-Magharibi. Angalau Frobisher alifaulu kurudi nyumbani bila kuumia katika safari zake zote. Haikuwa hivyo kwa wavumbuzi wengine waliokuwa wakitafuta njia hiyo ya kihekaya. Eneo la Aktiki lilikuwa balaa kwa wengi kwa sababu ya barafu, baridi, na uhaba wa chakula. Na bado, baada ya Frobisher, meli nyingi na maelfu ya wanaume waliabiri kaskazini wakijaribu kuvuka barafu hiyo.

Franklin Alienda Wapi?

Katika karne ya 19, Jeshi la Wanamaji la Uingereza lilipanga safari kubwa za kutafuta Njia ya Kaskazini-Magharibi. Safari moja ilikumbwa na msiba mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya safari za Aktiki. Sir John Franklin, baharia mwenye ujuzi wa eneo la Aktiki, alichaguliwa kuongoza safari hiyo. Meli mbili kubwa zilizokuwa na injini za mvuke zilitumiwa. Meli zote mbili ziliendeshwa na mabaharia wenye ujuzi zaidi katika jeshi hilo na wakapewa vitu ambavyo wangetumia kwa miaka mitatu. Isitoshe, walipewa vitu vya kuwastarehesha. Kwa mfano, meli hizo zilikuwa na maktaba kubwa na zana za muziki. Afisa mmoja aliyekuwa kwenye safari hiyo aliandika hivi: “Hakuna kitu muhimu ambacho hakipo na sidhani kwamba ningeongeza kitu chochote hata kama ningeruhusiwa kuzunguka London kwa saa moja au mbili!” Safari hiyo ilianzia Uingereza mnamo Mei 1845, na Julai walikuwa wamefika Ghuba ya Baffin.

Mwaka mmoja ukapita. Mwaka wa pili ukapita. Hatimaye, miaka mitatu iliyokuwa imepangiwa kwa ajili ya safari hiyo ikapita, lakini hakukuwa na habari zozote kuhusu safari ya Franklin. Kupotea kwa meli hizo mbili na mabaharia wake kuliwafanya wengi wasafiri kuelekea Aktiki. Nyingi za safari hizo zilifunua mengi kuhusu safari ya Franklin na fumbo la Njia ya Kaskazini-Magharibi.

Nahodha Robert McClure aliongoza mojawapo ya meli mbili zilizotumwa kumtafuta Franklin. Ziliondoka London mnamo mwaka wa 1850 na zilipitia Pasifiki kuelekea pwani ya kaskazini ya Amerika kupitia Mlango wa Bering. McClure aliacha meli moja na kusafiri kwa ushujaa kuelekea Bahari ya Aktiki. Muda si muda alifika mahali ambapo Mzungu yeyote hakuwa amefika. Baada ya kukabili hatari nyingi, hatimaye aliwasili kwenye pwani ya Kisiwa cha Banks, ambako aligundua jambo la kupendeza. Kisiwa hicho ni kilekile ambacho Edward Parry alikuwa ameona miaka mingi mapema alipokuwa akitafuta Njia ya Kaskazini-Magharibi kutoka upande wa mashariki. Iwapo McClure angefika upande wa pili wa kisiwa hicho, angekuwa amepitia Njia yote ya Kaskazini-Magharibi!

Lakini meli yake ilinaswa na barafu. Miaka miwili baadaye, McClure na mabaharia wenzake walikuwa bado wamekwama humo. Hata hivyo, walipokuwa wamekata tamaa, waliona wanaume kwa mbali wakija kwenye meli yao. Ulikuwa kama muujiza. Nahodha Henry Kellett, aliyeongoza safari nyingine, alipata ujumbe ambao McClure aliacha katika Kisiwa cha Melville na akawatuma wanaume kumwokoa McClure na watu wake. Mabaharia wa McClure, waliokuwa karibu kufa, waliingizwa katika meli ya Kellett na kurudishwa nyumbani kupitia njia ya mashariki. Kumbe, Kellett alikuwa amefika kwenye pwani ya kaskazini ya Amerika kupitia Atlantiki! Kulingana na kitabu The New Encyclopædia Britannica, McClure “alikuwa mtu wa kwanza kupitia Njia ya Kaskazini-Magharibi, ingawaje alitumia zaidi ya meli moja na hata alitembea umbali fulani.”

Lakini safari ya Franklin ilipatwa na nini? Kuna maelezo mbalimbali kuhusu mambo yaliyotukia baada ya mwaka wa 1845. Meli zote mbili za safari hiyo zilikwama kwenye barafu katika Mlango wa Victoria. Miezi 18 baada ya meli hizo kukwama kwenye barafu, wanaume kadhaa walikuwa wamekufa, kutia ndani Franklin. Wale waliookoka waliamua kuacha meli hizo na kutembea kwa miguu kuelekea kusini, lakini walikufa njiani kwa kuwa tayari walikuwa wanyonge. Hakuna aliyeokoka katika safari hiyo. Basi matokeo ya safari hiyo hayajulikani. Hata inasemekana kwamba wanaume hao walikufa haraka kwa sababu ya sumu ya madini ya risasi yaliyotokana na mikebe ya vyakula.

Safari ya Kwanza Kufaulu

Ingawa Njia ya Kaskazini-Magharibi iligunduliwa, haikutumiwa na meli hadi karne ya 20. Kijana Roald Amundsen aliongoza kikundi cha watu saba kutoka Norway katika safari hiyo. Walitumia mashua ndogo ya kuvua samaki iliyoitwa Gjøa, iliyokuwa tofauti kabisa na meli kubwa za vita za Uingereza. Mashua hiyo ndogo iliyoelea kwa urahisi ilifaa kusafiri katika Bahari ya Aktiki ambayo ina njia nyingi nyembamba, miamba, na sehemu zenye vina vifupi. Mnamo Juni 16, 1903, Amundsen na kikundi chake walianza safari yao ndefu kutoka Oslo kuelekea eneo la Aktiki la Amerika Kaskazini kupitia mashariki. Zaidi ya miaka miwili baadaye, katika Agosti 27, 1905, mabaharia hao waliona meli ya kuwindia nyangumi ambayo ilikuwa imefika kwenye Bahari ya Aktiki, ikitumia njia ya magharibi kupitia Mlango wa Bering. Amundsen aliandika hivi kuhusu tukio hilo: “Njia ya Kaskazini-Magharibi ilikuwa imepatikana. Ndoto yangu ya tangu utotoni ilitimia wakati huo . . . Nililia machozi.”

Hata hivyo, kufikia sasa haijawa rahisi kwa meli kupitia njia hiyo kwa ukawaida. Tangu nyakati za Amundsen, meli kadhaa zimepita juu ya bara la Amerika Kaskazini, lakini bado safari hiyo si rahisi. Hata hivyo, huenda jambo hilo likabadilika.

Suluhisho Lisilotarajiwa?

Barafu ya Aktiki inayeyuka haraka sana. Kwa sababu hiyo, katika mwaka wa 2000, meli ya polisi ya Kanada iliabiri katika Njia ya Kaskazini-Magharibi kwa mwezi mmoja hivi. Gazeti The New York Times lilipomhoji nahodha wake, Sajini Ken Burton, baada ya safari hiyo, alisema alishangaa kwa sababu hawakutatizwa na barafu. Burton alisema: “Kulikuwa na miamba kadhaa ya barafu, lakini haikuwa hatari. Tuliona mabamba fulani ya barafu lakini yote yalikuwa madogo na yalikuwa vipande-vipande kwa hiyo tuliweza kuyazunguka.” Kulingana na gazeti Science, “barafu ya Aktiki imepungua kwa asilimia 5 katika miaka 20 iliyopita, ni nyembamba, na inatabiriwa kwamba barafu hiyo itazidi kupungua kadiri joto la dunia linavyoongezeka.” Makala hiyo inataja ripoti iliyotolewa na Tume ya Marekani ya Kuchunguza Aktiki ambayo inakadiria kwamba katika miaka kumi ijayo Njia ya Kaskazini-Magharibi “huenda itatumiwa angalau kwa mwezi mmoja wakati wa kiangazi na meli zisizo na vifaa vya kuvunja barafu.”

Inashangaza kwamba “kwa kukaa nyumbani na kutumia mabilioni ya tani za fueli za visukuku,” ndoto ya wanadamu ya kutimiza jambo ambalo wamejitahidi kufanya kwa muda mrefu itatimia, lasema gazeti Science. Hata hivyo, watafiti wana wasiwasi kuhusu jinsi kuyeyuka kwa barafu na safari nyingi za meli zitakavyoathiri dubu weupe, sili wenye pembe, na wenyeji wa Aktiki. Isitoshe, huenda Njia ya Kaskazini-Magharibi ikaleta migogoro ya kisiasa. Njia hiyo italeta matokeo gani mengine? Tutaona.

[Ramani katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Safari ya Martin Frobisher 1578

Safari ya John Franklin 1845-1848

Safari ya Robert McClure 1850-1854

Safari ya Roald Amundsen 1903-1905

(Mstari wa nukta unaonyesha safari ya nchi kavu)

Ncha ya Kaskazini

URUSI

ALASKA, MAREKANI

KANADA

GREENLAND

[Picha katika ukurasa wa 23]

John Cabot

[Hisani]

Culver Pictures

[Picha katika ukurasa wa 23]

Sir Martin Frobisher

[Hisani]

Painting by Cornelis Ketel/Dictionary of American Portraits/Dover Publications, Inc., in 1967

[Picha katika ukurasa wa 23]

Sir John Franklin

[Hisani]

National Archives of Canada/C-001352

[Picha katika ukurasa wa 23]

Robert McClure na meli yake “Investigator” (chini)

[Hisani]

National Archives of Canada/C-087256

National Archives of Canada/C-016105

[Picha katika ukurasa wa 23]

Roald Amundsen

[Hisani]

Brown Brothers

[Picha katika ukurasa wa 24]

Ongezeko la joto duniani linafanya njia zenye barafu ziweze kutumiwa

[Hisani]

Kværner Masa-Yards

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

From the book The Story of Liberty, 1878