Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ndege Mwenye Kumeremeta Anayejionyesha

Ndege Mwenye Kumeremeta Anayejionyesha

Ndege Mwenye Kumeremeta Anayejionyesha

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

TAUSI hujitokeza mbele ya pazia maridadi sana kama mhusika mkuu katika mchezo mpya wa kuigiza. Manyoya yake yenye fahari, yenye urefu mara tano zaidi ya mwili wake, huinuka na kung’aa katika mwangaza wa jua.

Onyesho hilo lenye kupendeza hutukia wakati tausi anapotafuta mwenzi. Linapokaribia kwisha, manyoya yake ya mkia huanza kutetemeka na kutokeza sauti ya mkwaruzo inayomsaidia kufanikiwa. Ama kweli, tausi wa kike hawezi kukosa kuvutiwa na onyesho hilo ambalo limetajwa kuwa ‘tangazo la kuvutia zaidi ulimwenguni.’

Hata hivyo, tausi wa kiume hajionyeshi mbele ya tausi wa kike tu. Kitabu Wonders of Peacocks kinasema: “Wataalamu wa viumbe wamesema kwamba tausi hujionyesha mara nyingi na kwa muda mrefu mbele ya watu wengi kuliko mbele ya tausi wa kike.” Huenda msemo wa kwamba tausi anaringa unatokana na tabia yake ya kutanua manyoya yake maridadi.

Si vibaya kwa tausi kujionyesha, kwani onyesho lake huvutia sana. Mkia wake mrefu huwa na manyoya yenye urefu mbalimbali na madoadoa yanayomeremeta. Hilo humwezesha kuyatanua kama feni. Manyoya yake huwa na rangi ya shaba-nyekundu, shaba-nyeusi, manjano, au bluu nzito ya kijani na zambarau ikitegemea miale ya jua.

Katika nchi za Magharibi, huenda watu wakafikiri kwamba tausi ni ndege maridadi anayewafurahisha watu tu na hana faida nyingine. Hata hivyo, huko India mahali anapotoka, wenyeji humpenda sana kwa sababu hula swila wachanga na nyoka wengine wenye sumu. Kwa kuwa inaonekana sumu ya swila haimdhuru tausi, katika nchi za Mashariki yeye humwakilisha mungu na huhusianishwa na hali ya kutokufa.

Yapata miaka 3,000 iliyopita, tausi alipendwa sana katika Mashariki ya Kati. Mfalme Sulemani alinunua tausi kutoka nchi nyingine pamoja na vitu vingine vyenye thamani kama vile ‘dhahabu, fedha, na pembe za tembo.’ (1 Wafalme 10:22) Kitabu The Natural History of the Bible kinasema: “Huenda Tausi walionunuliwa na Sulemani ndio waliokuwa wa kwanza katika nchi za Mediterania.” Karne kadhaa baadaye, Aleksanda Mkuu alivutiwa sana na tausi hivi kwamba aliwakataza askari wake wasiwaue.

Hata leo watu wengi huvutiwa na maonyesho ya pekee ya tausi. Na hatupaswi kumpuuza Mwanzilishi wa maonyesho hayo. Kama vile kazi ya msanii inavyoonyesha kwamba yeye ni stadi, ndivyo kiumbe huyo maridadi sana anavyoonyesha usanii usio na kifani wa Muumba.

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 17]

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Cortesía del Zoo de la Casa de Campo, Madrid