Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sayari Yetu Imezorota Kadiri Gani?

Sayari Yetu Imezorota Kadiri Gani?

Sayari Yetu Imezorota Kadiri Gani?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFILIPINO

Mgonjwa yuko katika hali mahututi. Ana matatizo mengi. Ana harufu mbaya mdomoni. Ana homa kali sana. Jitihada za kuitibu hazifui dafu. Ana sumu mwilini. Anapotibiwa sehemu moja, ugonjwa unaibuka katika sehemu nyingine za mwili. Kama angekuwa mgonjwa halisi, madaktari wangesema ugonjwa wake ni hatari na wa kufisha. Kwa kukosa la kufanya, wangejaribu tu kumtuliza kadiri wawezavyo hadi afe.

LAKINI mgonjwa huyo si mwanadamu. Ni makao yetu—dunia. Mfano uliotajwa hapo juu unaeleza kinaganaga hali ya sayari yetu. Hewa chafu, ongezeko la joto duniani, maji machafu, na taka zenye sumu ni baadhi tu ya matatizo yanayoikumba dunia. Kama madaktari waliotajwa juu, wanamazingira hawana la kufanya.

Kila wakati vyombo vya habari huandika kuhusu hali mbaya ya dunia kupitia vichwa kama vile: “Kuvua samaki kwa baruti kunaiangamiza bahari.” “Huenda Mabilioni ya Waasia Wakakosa Maji Miaka 24 Ijayo.” “Tani milioni 40 za taka zenye sumu huuzwa kila mwaka ulimwenguni pote.” “Karibu thuluthi mbili ya visima 1,800 nchini Japan vina sumu.” “Shimo la Tabaka la Ozoni huko Antaktiki Limezidi na Linasababisha Wasiwasi.”

Watu fulani wamezoea kusikia habari nyingi kuhusu uharibifu wa mazingira na hata huenda wakadhani, ‘Si neno maadamu siathiriwi.’ Hata hivyo, iwe twajua au hatujui, uharibifu mkubwa wa mazingira ya dunia unaathiri watu wengi sana. Kwa kuwa sayari yetu imeharibiwa sana, yaelekea kwamba tayari maisha yetu yanaathiriwa kwa kadiri kubwa. Hivyo, sote twapaswa kuhangaikia hali ya makao yetu na jinsi ya kuyahifadhi. Tusipofanya hivyo, tutaishi wapi pengine?

Tatizo hilo ni baya kadiri gani? Dunia imeharibiwa kadiri gani? Watu wanaathiriwaje? Hebu tuchunguze mambo kadhaa yatakayotusaidia kuelewa kwa nini dunia yetu iko katika hali mahututi.

BAHARI: Samaki wamevuliwa kupita kiasi katika sehemu kubwa za bahari. Ripoti moja ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa inasema kwamba “asilimia 70 ya maeneo yenye samaki yamevuliwa sana hivi kwamba samaki wamepungua sana na hawawezi kuongezeka hata wakizaana.” Kwa mfano, idadi ya aina mbalimbali za chewa katika Bahari ya Atlantiki Kaskazini ilipungua kwa asilimia 95 kati ya mwaka wa 1989 na 1994. Hali hiyo ikiendelea, itakuwaje kwa mamilioni ya watu wanaotegemea bahari ili kupata chakula?

Isitoshe, inakadiriwa kwamba kila mwaka tani milioni 20 hadi milioni 40 za viumbe wa baharini hukamatwa na kutupwa tena baharini, kwa kawaida wakiwa wamejeruhiwa au wamekufa. Kwa nini? Wao huvuliwa pamoja na samaki lakini hawahitajiwi.

MISITU: Uharibifu wa misitu una athari nyingi. Ukataji wa miti hupunguza uwezo wa dunia wa kufyonza kaboni-dioksidi na inasemekana jambo hilo linasababisha ongezeko la joto duniani. Aina fulani za mimea, ambazo zinaweza kutumiwa kutengeneza dawa muhimu, zitatokomea. Hata hivyo, misitu inaendelea kukatwa ovyoovyo. Ama kwa hakika, misitu imeendelea kuharibiwa kwa kiwango kikubwa sana katika miaka ya majuzi. Wataalamu fulani wanahisi kwamba hali hiyo ikiendelea misitu ya kitropiki inaweza kuangamia katika muda wa miaka 20.

TAKA ZENYE SUMU: Kutupa taka hatari kwenye nchi kavu na baharini ni tatizo kubwa ambalo linaweza kudhuru sana mamilioni ya watu. Taka zenye mnururisho, vyuma vizito, na plastiki ni baadhi ya vitu vinavyoweza kusababisha ulemavu, magonjwa, au kifo kwa watu na wanyama.

KEMIKALI: Katika miaka 100 iliyopita, karibu aina 100,000 za kemikali zilianza kutumiwa. Kemikali hizo husambaa hewani, udongoni, majini, na katika chakula. Ni kemikali chache tu kati ya hizo ambazo zimechunguzwa ili ionekane kama zinawadhuru wanadamu. Hata hivyo, kemikali nyingi kati ya zile zilizochunguzwa zimegunduliwa kuwa zinaweza kusababisha kansa au magonjwa mengine.

Kuna vitu vingi zaidi vinavyohatarisha mazingira yetu: uchafuzi wa hewa, maji machafu, mvua ya asidi, na ukosefu wa maji safi. Mambo hayo machache yanaonyesha wazi kwamba dunia yetu iko katika hali mahututi. Je, mgonjwa huyo anaweza kuokolewa, au ni kuchelewa mno?