Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tumefanikiwa Kadiri Gani Kuokoa Mazingira Yetu?

Tumefanikiwa Kadiri Gani Kuokoa Mazingira Yetu?

Tumefanikiwa Kadiri Gani Kuokoa Mazingira Yetu?

CHERNOBYL, Bhopal, Valdez, Kisiwa cha Three Mile. Majina hayo hutukumbusha misiba ya kimazingira ambayo ilitukia katika sehemu mbalimbali za ulimwengu. Kila moja ya misiba hiyo ilitukumbusha kwamba mazingira ya dunia yanaharibiwa.

Wataalamu na watu mmoja-mmoja wameelezea wasiwasi wao. Wengine wamechukua hatua za waziwazi kuonyesha msimamo wao. Mwingereza mmoja anayetunza maktaba alijifungilia kwenye tingatinga kwa nyororo ili kupinga ujenzi wa barabara katika eneo linalokabili uharibifu wa mazingira. Wanawake wawili Waaborijini huko Australia waliongoza kampeni ya kupinga uchimbaji wa madini ya urani katika mbuga ya kitaifa. Shughuli hizo zilisimamishwa kwa muda. Ijapokuwa jitihada hizo hufanywa kwa nia nzuri, hazijapendwa sikuzote. Kwa mfano, nahodha wa jeshi la wanamaji katika serikali ya Sovieti alihangaishwa na minururisho iliyokuwa ikivuja kutoka kwenye mitambo ya nyambizi za nyukilia zilizozama. Alipochapisha habari kuhusu maeneo ambapo nyambizi hizo zilikuwa, alikamatwa.

Mashirika mbalimbali pia yameonya kuhusu hatari zinazokumba mazingira. Mashirika hayo ni kama vile Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni; Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira; na shirika la Greenpeace. Baadhi ya mashirika hayo huripoti tu kuhusu uharibifu wa mazingira unaohusiana na kazi yao. Mengine hujitoa mhanga kutetea mazingira. Shirika la Greenpeace linajulikana sana kwa kutuma wanaharakati katika maeneo yanayokumbwa na matatizo ya mazingira na kujulisha umma kuhusu masuala kama vile ongezeko la joto duniani, viumbe walio katika hatari ya kutoweka, na hatari za wanyama na mimea iliyobadilishwa chembe za urithi.

Wanaharakati wengine husema kwamba wao “hubuni njia za kutangaza uharibifu wa mazingira ulimwenguni pote.” Ndiyo sababu wengine hujifungilia kwenye milango ya mashine za kupasua mbao ili kupinga uharibifu wa misitu ambayo imekuwapo kwa miaka mingi. Kikundi kimoja cha wanaharakati kilizusha zogo wakati nchi moja ilipovunja mkataba wa kuvua nyangumi. Wanaharakati hao walifika kwenye ubalozi wakiwa wamevalia vinyago vyenye macho makubwa ili kuonyesha kwamba matendo ya nchi hiyo yalikuwa yanatazamwa.

Matatizo ya mazingira ni mengi. Kwa mfano, watu mmoja-mmoja na mashirika yameonya mara nyingi kuhusu uchafuzi wa maji. Hata hivyo, hali ni mbaya sana. Watu bilioni moja hawawezi kupata maji safi ya kunywa. Kulingana na gazeti Time, “watu milioni 3.4 hufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayoambukizwa kupitia maji.” Tatizo jingine ni uchafuzi wa hewa. Jarida la The State of World Population 2001 linaripoti kwamba “uchafuzi wa hewa huua karibu watu milioni 2.7 hadi milioni 3.0 kila mwaka.” Linaongeza kwamba “uchafuzi wa hewa hudhuru zaidi ya watu bilioni 1.1.” Kwa mfano, linaripoti kwamba “karibu asilimia 10 ya magonjwa ya kupumua yanayowapata watoto huko Ulaya husababishwa na vichafuzi vidogo sana.” Naam, licha ya maonyo na hatua zilizochukuliwa kufikia sasa, matatizo yanayoathiri mambo ya msingi maishani yamezidi.

Watu wengi wamechanganyikiwa. Habari nyingi zaidi kuhusu masuala ya kimazingira zinapatikana kuliko wakati mwingine wowote. Watu wengi na mashirika mengi yana nia ya kusafisha mazingira kuliko wakati mwingine wowote. Serikali zimeanzisha idara za kutatua matatizo hayo. Tuna tekinolojia ya hali ya juu zaidi ya kusaidia kukabiliana na matatizo hayo. Lakini, mambo hayajaboreka. Kwa nini?

Hatua Moja Mbele, Hatua Mbili Nyuma

Maendeleo ya kiviwanda yalikusudiwa kurahisisha maisha yetu na yamefanya hivyo kwa njia fulani. Hata hivyo, “maendeleo” hayohayo ndiyo yanayozidisha matatizo ya mazingira. Tunafurahia mavumbuzi na maendeleo ya kiviwanda, lakini mara nyingi utengenezaji wa vitu na jinsi tunavyovitumia kumeharibu sehemu fulani za dunia yetu.

Mfano mmoja ni magari. Magari yamerahisisha na kuharakisha usafiri. Watu wengi hawangependa kurudi kwenye enzi ya farasi na magari ya kukokotwa. Hata hivyo, usafiri wa kisasa umeleta matatizo mengi. Moja ni kuongezeka kwa joto duniani. Wanadamu wamekuwa wakichafua hewa kwa kutumia vitu vinavyotoa mamilioni ya tani za gesi. Inasemekana kwamba gesi hizo zinasababisha ongezeko la joto angani. Katika karne iliyopita, joto liliongezeka sana. Shirika la Marekani la Kulinda Mazingira linaripoti kwamba “miaka 10 yenye joto zaidi katika karne ya 20 ilikuwa katika miaka 15 ya mwisho ya karne hiyo.” Wanasayansi fulani wanaamini kwamba katika karne ya 21, joto la wastani duniani litaongezeka kwa nyuzi 1.4 hadi 5.8 za Selisiasi.

Inatazamiwa kwamba ongezeko la joto litasababisha matatizo mengine. Theluji imepungua katika sehemu ya kaskazini ya dunia. Mapema katika mwaka wa 2002, bamba la barafu lenye ukubwa wa kilometa 3,250 za mraba liliporomoka huko Antaktika. Katika karne hii, huenda kiwango cha maji baharini kikaongezeka sana. Kwa kuwa thuluthi moja ya idadi ya watu duniani wanaishi karibu na bahari, huenda wakapoteza nyumba na mashamba yao. Yaelekea pia matatizo makubwa yatazuka katika majiji ya pwani.

Wanasayansi wanaamini kwamba ongezeko la joto litasababisha ongezeko la mvua na mara nyingi kutakuwa na hali mbaya ya hewa. Watu fulani wanaonelea kwamba dhoruba kali kama ile iliyowaua watu 90 na kuharibu miti milioni 270 huko Ufaransa katika mwaka wa 1999 ni baadhi tu ya matatizo yanayotarajiwa. Watafiti wengine wanaonelea kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yatasababisha kuenea kwa magonjwa kama vile malaria, kidingapopo, na kipindupindu.

Uvumbuzi wa magari unaonyesha matokeo mbalimbali ya maendeleo ya kitekinolojia—ingawa yanafaidi watu kwa ujumla, yanaweza kusababisha matatizo mengi yanayoathiri shughuli nyingi maishani. Jarida la Human Development Report 2001 linatoa taarifa hii mwafaka: “Kila uvumbuzi wa kitekinolojia huleta manufaa na hatari, na nyingine hazitarajiwi.”

Watu hutazamia kwamba tekinolojia itasuluhisha matatizo ya mazingira. Kwa mfano, kwa muda mrefu wanamazingira wamepinga matumizi ya dawa za kuua wadudu. Wakati mimea iliyobadilishwa chembe za urithi ilipozalishwa ili kupunguza au kukomesha matumizi ya dawa za kuua wadudu, ilionekana hilo ni suluhisho tosha. Lakini, mahindi aina ya Bt ambayo yalizalishwa ili kuwakomesha wadudu wavamizi bila kutumia dawa yalipochunguzwa, iligunduliwa kuwa yanaweza pia kuua vipepeo aina ya monarch. Hivyo, nyakati nyingine “masuluhisho” hayafui dafu na yanaweza kusababisha matatizo zaidi.

Je, Serikali Zinaweza Kusaidia?

Kwa kuwa uharibifu wa mazingira ni tatizo kubwa, ni lazima serikali za ulimwengu zishirikiane ili kupata suluhisho linalofaa. Wawakilishi fulani wa serikali wamependekeza mabadiliko yanayoweza kusaidia kuhifadhi mazingira. Hata hivyo, mara nyingi hawajafanikiwa sana.

Mfano mmoja ni kongamano la kimataifa lililofanywa nchini Japan mnamo mwaka wa 1997. Mataifa yalibishana kuhusu mkataba wa kupunguza gesi zinazosemekana zinasababisha ongezeko la joto duniani. Hatimaye, bila kutarajiwa, yalikubaliana. Makubaliano hayo yaliitwa Mkataba wa Kyoto. Maeneo yaliyoendelea, kama vile Muungano wa Ulaya, Japan, na Marekani yalipaswa kupunguza utoaji wa gesi kwa wastani wa asilimia 5.2 kufikia mwaka wa 2012. Ilionekana jambo hilo lingefaulu. Hata hivyo, mapema katika mwaka wa 2001, serikali ya Marekani ilisema kwamba ingejiondoa kwenye Mkataba wa Kyoto. Jambo hilo liliwashangaza wengi, kwa sababu Marekani, ambayo ina chini ya asilimia 5 ya idadi ya watu ulimwenguni, inatoa robo ya gesi hizo. Isitoshe, serikali nyingine zimesitasita kabla ya kukubali mkataba huo.

Mfano huo unaonyesha jinsi ambavyo ni vigumu kwa serikali kusuluhisha matatizo ya mazingira. Ni vigumu kukutanisha serikali mbalimbali, na ni vigumu kwa serikali hizo kukubaliana juu ya jinsi ya kushughulikia matatizo ya mazingira. Hata mikataba inapotiwa sahihi, baadaye nchi fulani hazitekelezi ahadi zao. Nchi nyingine huona ni vigumu kutekeleza mikataba hiyo. Wakati mwingine, serikali na mashirika huona kwamba hayawezi kukubali gharama za kusafisha mazingira. Wakati mwingine, tatizo huwa ni pupa, kwani mashirika makubwa ya kibiashara hushawishi serikali zisitekeleze makubaliano yatakayopunguza faida zao. Makampuni na mashirika mengine yametumia ardhi vibaya bila kufikiria matokeo ya wakati ujao.

Jambo linalofanya tatizo hilo kuwa baya zaidi ni kwamba wanasayansi hawakubaliani kuhusu athari za uchafuzi wa mazingira. Kwa hiyo, wapangaji wa mikakati hawana uhakika kuhusu mambo ambayo watafanya kudhibiti ukuzi wa uchumi ili kuzuia uharibifu wa mazingira kwani hawajui tatizo hilo ni kubwa kadiri gani.

Wanadamu wamo taabani. Kila mtu anajua kuna tatizo na kwamba linahitaji kutatuliwa. Mataifa fulani yanafanya jitihada kabambe lakini matatizo ya mazingira yanaendelea kuongezeka. Je, dunia itaharibiwa kiasi cha kutoweza kukaliwa na wanadamu? Hebu tuchunguze swali hilo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

KELELE

Mojawapo ya mambo yanayoharibu mazingira ni kelele. Wataalamu wanasema kwamba kelele ni tatizo kwa sababu zinaweza kusababisha uziwi, mfadhaiko, kupanda kwa shinikizo la damu, kukosa usingizi, na uchovu. Watoto wanaosomea katika shule zilizo kwenye maeneo yenye kelele wanaweza kupata matatizo ya kusoma.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

UHARIBIFU WA MISITU WASABABISHA UVAMIZI WA PANYA

Wakati miji 15 huko Samar, Ufilipino, ilipovamiwa na panya wengi, chanzo kimoja cha serikali kilisema kwamba uvamizi huo ulisababishwa na uharibifu wa misitu. Ukataji wa miti ulisababisha kupungua kwa vyakula vya panya na wanyama wanaokula panya. Panya walihamia maeneo yenye watu wengi wakitafuta chakula.

[Hisani]

© Michael Harvey/Panos Pictures

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

JE, WAMEATHIRIWA NA TAKA ZENYE SUMU?

Michael, aligunduliwa kuwa na aina fulani ya kansa alipokuwa na umri wa miezi mitatu na nusu. Iwapo ni yeye peke yake, hilo halingesababisha hangaiko kubwa. Hata hivyo, baadaye iligunduliwa kwamba karibu watoto 100 zaidi wa eneo hilo waliugua kansa pia. Jambo hilo liliwashtua wazazi wengi. Wengine walifikiri kwamba idadi hiyo kubwa ya watoto wenye kansa ilisababishwa na kampuni za kemikali za eneo hilo. Uchunguzi ulionyesha kwamba kampuni moja ya kutupa takataka ilikuwa imetupa mapipa yenye umajimaji wenye sumu yaliyotoka kwenye mojawapo ya kampuni hizo za kemikali. Walitupa mapipa hayo kwenye shamba moja lililotumiwa kufugia kuku zamani na nyakati nyingine walimwaga sumu hiyo. Watafiti waligundua sumu hiyo katika visima vya maji vya eneo hilo. Wazazi wanafikiri kwamba huenda sumu hiyo ndiyo imesababisha watoto wao kuugua kansa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

KEMIKALI ZENYE SUMU

Baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, tani 120,000 za kemikali zenye sumu, hasa phosgene na sumu ya mvuke, zilipakiwa ndani ya meli na kuzamishwa baharini, nyingine kaskazini-magharibi mwa Ireland Kaskazini. Wanasayansi Warusi wameonya kwamba kuna hatari ya kemikali hizo kuvuja.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

UCHAFUZI WA HEWA HUUA

Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kwamba kila mwaka asilimia 5 hadi 6 ya vifo vyote duniani husababishwa na uchafuzi wa hewa. Inaripotiwa kwamba huko Ontario, Kanada, wakazi hupata hasara ya dola bilioni 1 kila mwaka kutokana na matatizo ya afya na kukosa kufika kazini kwa sababu ya uchafuzi wa hewa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

MATUMBAWE YANAANGAMIA

Wavuvi fulani Kusini-Mashariki mwa Asia hutumia umajimaji wa sianidi kuwalevya samaki ili wawakamate kwa urahisi. Samaki hutoa sumu hiyo mwilini, kwa hiyo bado wanaweza kuliwa. Hata hivyo, sumu hiyo hubaki baharini na kuangamiza matumbawe.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

JE, TUFUNIKE PUA?

Gazeti Asiaweek linaripoti kwamba katika majiji ya Asia hewa huchafuliwa hasa na moshi wa magari. Injini za malori na pikipiki ndizo husababisha uchafuzi mwingi, na hutoa kiasi kikubwa cha vichafuzi vidogo sana. Vichafuzi hivyo husababisha matatizo mengi ya afya. Gazeti hilo linasema: “Mtaalamu maarufu wa athari za uchafuzi nchini Taiwan, Dakt. Chan Chang-chuan, anasema moshi wa malori husababisha kansa.” Ili kujilinda, watu fulani katika majiji ya Asia hufunika fua kwa vitambaa. Je, vinasaidia? Dakt. Chan anasema: “Vitambaa vya kufunika pua havisaidii. Vichafuzi vingi vya hewa huwa vya gesi na ni vidogo sana hivi kwamba vitambaa vya kawaida haviwezi kuzuia vichafuzi visipenye. Isitoshe, . . . vinapitisha hewa. Kwa hivyo vinapumbaza tu.”

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kupanda miti ili kuokoa mazingira

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]

AFP/Getty Images; top left: Published with the permission of The Trustees of the Imperial War Museum, London (IWM H 42208); top right: Howard Hall/howardhall.com