Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hifadhi ya Kitaifa ya Paracas Inapendeza Sana

Hifadhi ya Kitaifa ya Paracas Inapendeza Sana

Hifadhi ya Kitaifa ya Paracas Inapendeza Sana

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Peru

KWA miaka mingi watalii kutoka sehemu zote za ulimwengu wamevutiwa na Peru. Kwa kawaida wao hutembelea Lima; Cuzco, jiji kuu la Wainka; magofu yenye kustaajabisha ya Machu Picchu; milima mirefu ya Andes; na hata kuabiri kwenye Mto Amazon. Hivi majuzi wameanza kutembelea sehemu nyingine yenye kuvutia, yaani Hifadhi ya Kitaifa ya Paracas. Hifadhi hiyo iko kilometa 250 hivi kusini ya Lima, kupitia Barabara Kuu ya Pan-American.

Hifadhi ya Kitaifa ya Paracas ina ukubwa wa ekari 800,000 kuanzia maeneo ya pwani hadi Rasi ya Paracas. Ilianzishwa mwaka wa 1975 na serikali ya Peru ili kuhifadhi wanyama wengi wanaoishi au kuhamia eneo hilo kila mwaka. Hifadhi hiyo huchangia uhifadhi wa mazingira na utalii. Zaidi ya maeneo 100 yenye vitu vya kale yamevumbuliwa, na yanaonyesha utamaduni wa Paracas wa karne nyingi zilizopita. Sili, fisi-maji, pomboo, zaidi ya aina 200 za ndege, na aina nne za kasa wanaishi katika eneo hilo la baharini.

Kwenye ramani, Rasi ya Paracas huonekana ikiwa ndogo sana ikilinganishwa na sehemu kubwa ya nchi kavu. Hivyo eneo hilo hupata pepo kali za msimu, ambazo wenyeji wa huko huziita paracas. Pepo hizo huvuma kuelekea kaskazini, na kusukuma mkondo baridi wa Peru, unaoitwa Humboldt. Kwa sababu ya maji baridi ya eneo hilo, fuo zenye kina kifupi, na kuibuka kwa maji yenye virutubisho kutoka kwenye sakafu ya bahari, rasi hiyo ni mojawapo ya sehemu yenye viumbe wengi wa baharini duniani. Bahari ya Pasifiki ina viumbe wengi, mimea, wanyama wadogo ambao huliwa na dagaa, na samaki wengine wadogo. Ndege wengi wanaoishi karibu na bahari, pengwini, na wanyama wanaoishi katika hifadhi hiyo hula viumbe hao, hasa dagaa.

Kutembelea Visiwa vya Ballestas

Safari yetu inaanzia gati za ghuba ya Paracas. Mashua nyingi ndogo za kuvua samaki zinasuka-suka bandarini zikiwa zimetiwa nanga huku ndege aina ya mwari wakiketi ndani ya mashua hizo wakijisafisha na kuwatazama watu. Mashua yetu inawasili na tunaipanda na kuvaa mavazi ya kutusaidia tusizame. Tunapotoka kwenye bandari hiyo yenye mashua nyingi, tunaenda kasi na kusisimuka tunapokata mawimbi.

Kwanza tunatia nanga karibu na ncha ya rasi hiyo. Yule anayetutembeza anatueleza kuhusu michoro mikubwa tunayoona kilimani. Inaitwa Candelabra, na huenda ukadhani inafanana na mmea wa dungusi-kakati wenye matawi matatu. Wengine wamesema kwamba hiyo ni sehemu ya michoro maarufu inayoitwa Nazca Lines. * Wengine hudhani kwamba ilichorwa na maharamia au ni ishara ya Chama cha Mason iliyotengenezwa na maaskari waliomuunga mkono kiongozi wa mapinduzi José de San Martín katika mwaka wa 1820. Haidhuru ni nani aliyeichora, michoro hiyo inastaajabisha.

Tunapopita rasi hiyo, tunakumbwa na mawimbi mazito. Visiwa vinang’aa kwa sababu ya jua la asubuhi. Kumbe vinang’aa kwa sababu vimefunikwa na kinyesi cha ndege wa baharini, bali si miamba wala mchanga.

Tunafika kwenye Visiwa vya Ballestas, au Visiwa vya Upinde. Wahispania waliviita hivyo kwa sababu ya njia zake zinazopita chini ya tao zilizo kama upinde. Nahodha anapunguza mwendo. Tunaona ndege wengi sana wanaotutazama kwenye miamba na juu ya kingo za visiwa hivyo, kama vile mwari, buabua, korongo, polisi, aina mbalimbali za mnandi, na hata pengwini. Ijapokuwa si rahisi kuwapata pengwini katika eneo la kitropiki, wanafurahia kuishi katika eneo hilo kwa sababu ya maji yake baridi na samaki wengi. Kisha tunawaona sili wakiota jua juu ya miamba. Sehemu kubwa ya visiwa hivyo ina miamba inayoibuka toka baharini, na tunafurahia kuona jinsi pengwini na sili wanavyojitahidi kufikia makao yao ijapokuwa kwa kawaida hawatembei kwa urahisi kwenye nchi kavu.

Yule anayetutembeza anatusisimua kwa mambo anayotuambia. Anasema: “Sili dume anaweza kuwa na uzito unaozidi kilogramu 300 na kutawala majike 20.” Ingawa sili jike ana umbo zuri, sili dume anafanana na magunia makubwa. Anatuambia kwamba madume wana nguvu na ni wakali na hupigana na dume wengine ili kulinda kundi na eneo lao. Mara nyingi anayeshindwa huuawa na kuliwa na tumbusi na tai wakubwa ambao pia huliwa na wanyama wengine katika eneo hilo la pwani. Sili hula sana, kwa kawaida yeye hula kilogramu 10 za samaki usiku mmoja. Lakini hawatushambulii, wanatutazama tu.

Nahodha wetu anatupeleka kwenye visiwa hivyo vitatu na kwenye njia za tao, na tunasikia uvundo wa kinyesi cha ndege. Yule anayetutembeza anatuambia hivi: “Popo huishi kwenye njia za tao nao huwauma-uma sili wakati wamelala.” Kwa mbali tunaona doa kubwa jeusi kwenye kisiwa kikubwa zaidi. Ni kundi la ndege aina ya mnandi wanaopenda kukaa pamoja. Wanapenda kukusanyika pamoja wakipumzika na kutoa kinyesi. Polisi wanapiga mbizi baharini huku ndege wengine wakiruka karibu nasi.

Hatimaye, tunafika kwenye ufuo mkubwa zaidi wa visiwa hivyo ambalo ndilo eneo la kuzalia. Tunafurahi kuwaona sili wengi na makundi ya watoto wao wakijinyoosha karibu na mama zao. Kuna kelele nyingi na sauti za aina mbalimbali. Tunaelezwa kwamba watoto hao hunyonya kwa miezi sita na hujifunza kuogelea wakiwa wamebebwa mgongoni na mama zao.

Tunaporudi bandarini, yule anayetutembeza anasema: “Asilimia 60 ya watoto wa sili hufa kabla hawajafikisha umri wa mwaka mmoja. Wengine hupondwa au kuuawa tu kimakusudi na madume. Wengine huzama. Hali ya hewa ya El Niño husababisha madhara pia kwa kuwalazimu dagaa wahamie kusini kwenye maji baridi sana. Sili wachanga hawana nguvu za kuwafuata sili waliokomaa kwenye maeneo hayo ya malisho.”

Inashangaza kwamba wanadamu ndio tisho kubwa kwa viumbe hao. Wawindaji wamewaua sili wengi ili wapate manyoya na wavuvi wamewaua kwa sababu wanawaona kuwa kizuizi. Kasa wa baharini huwindwa kwa ajili ya nyama yao inayopendwa sana na kwa ajili ya magamba yao yanayotumiwa kama mapambo. Wakusanyaji wa kinyesi cha ndege huwasumbua ndege wa eneo hilo. Pia samaki wamepungua kwa kuvuliwa kupita kiasi. Tunaambiwa kwamba sasa kuna sheria za kuwalinda wanyama. Huenda sheria hizo zitawasaidia watu waone umuhimu wa kutunza mazingira.

Historia ya Paracas

Tunatoka kwenye mashua, tayari kumaliza matembezi yetu, na tunaenda kwenye Jumba la Makumbusho la Julio C. Tello, kwenye rasi hiyo.

Mnamo mwaka wa 1925, Julio C. Tello, Mperu aliyekuwa mchimbaji wa vitu vya kale, na mshirika wake walifanya uvumbuzi wa kwanza kwenye rasi hiyo. Waliliita eneo hilo Kichwa Kirefu, kwa sababu ya mafuvu marefu ya wanadamu yaliyokuwa yamefukiwa ardhini kwenye eneo hilo lililokuwa mahame. Hayo yalikuwa mabaki ya utamaduni wa watu wa Paracas ambao wasomi wanakadiria waliishi kuanzia mwaka 1000 K.W.K. mpaka mwaka wa 200 K.W.K. Watu hao hawakuwa na lugha iliyoandikwa. Kwa hiyo, ijapokuwa inajulikana jinsi watu hao walivyorefusha mafuvu hayo, kwa kutumia mito, fimbo, na nyuzi, hakuna anayejua sababu ya kufanya hivyo. Katika eneo hilohilo, Tello aligundua mapango ya makaburi chini ya ardhi yaliyofanana na vikombe vilivyopinduliwa. Miili iliyokuwa imejikunja ambayo ilifungwa kwa vitambaa, iliwekwa karibu-karibu ili “izaliwe tena.” Pia mahindi, njugu, viazi vitamu, ala za muziki, na vifaa vilivyotumiwa wakati wa sherehe vilipatikana mapangoni.

Miaka miwili baadaye Tello na mshirika wake mwingine waligundua sehemu kubwa yenye makaburi na wakaiita Paracas Necropolis. Ilikuwa na sanda 429 zilizotumiwa kwa ajili ya maziko, nyingine zenye urefu wa zaidi ya meta 1.6. Kila moja ya miili hiyo iliyojikunja iliingizwa ndani ya kikapu. Ilifunikwa kwa vitambaa ghali vyenye rangi maridadi, madoido, na michoro yenye ishara za kidini na kimizungu.

Unaweza kuona vitambaa hivyo vya maziko pamoja na mamia ya vitu vingine vya utamaduni wa Paracas vilivyochimbuliwa kwenye Jumba la Makumbusho la Julio C. Tello.

Tunatumai kwamba safari yetu kwenye Hifadhi ya Kitaifa ya Paracas imekufanya utamani kuona vitu vyenye kuvutia huko Peru.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Hiyo ni michoro ya wanyama na maumbo ya jiometria kwenye nyanda za Nazca, Peru, na ni mikubwa sana hivi kwamba haiwezi kuonekana mtu akiwa chini. Ona makala “The Nazca Lines—A UFO Spaceport?” katika toleo la Kiingereza la Amkeni! la Januari 8, 1982.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Pengwini wa Humboldt

[Picha katika ukurasa wa 18]

Buabua

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mchoro wa Candelabra

[Picha katika ukurasa wa 18]

Vitu vinavyoonyesha utamaduni wa Paracas—vazi la maziko, mwili uliohifadhiwa, na fuvu refu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Pelican: © Archivo de PromPerú; sea lions: © Michael Tweddle/PromPerú

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Coastline: © Carlos Sala/PromPerú; flamingos: © Heinz Plenge/PromPerú; penguin: © Arturo Bullard/PromPerú

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Top left sea and tern: © Archivo de PromPerú; artifacts: Museo Nacional de Arqueología, Antropología e Historia del Perú