Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mtoto Wako Anapopata Homa

Mtoto Wako Anapopata Homa

Mtoto Wako Anapopata Homa

“Nasikia vibaya!” Mtoto wako anapolalamika hivyo, mara moja unachunguza joto lake la mwili. Ikiwa ana homa, huenda ukawa na wasiwasi.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Watoto cha Johns Hopkins huko Baltimore, Maryland, Marekani, asilimia 91 ya wazazi waliamini kwamba “hata homa kidogo tu inaweza kusababisha angalau tatizo moja kama vile mshtuko wa moyo au kuharibu ubongo.” Uchunguzi huo unaonyesha kwamba “asilimia 89 ya wazazi waliwapa watoto wao dawa za kupunguza homa kabla ya joto la mwili wa mtoto kufikia nyuzi 102 za Fahrenhaiti (nyuzi 38.9 za Selsiasi).”

Je, unapaswa kuwa na wasiwasi mtoto wako anapopata homa? Na ni zipi njia bora za kuitibu?

Umuhimu wa Homa

Homa husababishwa na nini? Ingawa kwa kawaida joto la mwili huwa nyuzi 37 za Selsiasi (linapopimwa kwenye mdomo), linabadilika-badilika kwa nyuzi moja au zaidi siku inapoendelea. * Kwa hiyo joto la mwili wako linaweza kuwa chini asubuhi na kuwa juu jioni. Sehemu fulani inayoitwa hypothalamus, iliyoko chini ya ubongo, hudhibiti joto la mwili. Homa hutokea wakati mfumo wa kinga unapotokeza vitu fulani katika damu vinavyoitwa pyrogen, labda unaposhambuliwa na bakteria au virusi. Hiyo hufanya hypothalamus iongeze joto la mwili.

Ingawa homa inaweza kusababisha maumivu na kupunguza maji mwilini, si kwamba ni mbaya. Kulingana na Taasisi ya Mayo ya Elimu na Utafiti wa Kitiba, homa husaidia mwili sana kuondoa bakteria na virusi. “Virusi vinavyosababisha mafua na magonjwa mengine ya kupumua husitawi wakati wa baridi. Homa kidogo inaweza kusaidia mwili kuondoa virusi hivyo.” Taasisi hiyo inasema kwamba “haifai kutibu homa kidogo kwani inaweza kudhoofisha kinga ya mtoto.” Hospitali moja nchini Mexico hata hutibu magonjwa fulani kwa kuongeza joto la mgonjwa.

Dakt. Al Sacchetti wa Chuo cha Marekani cha Madaktari wa Dharura anasema: “Mara nyingi homa si ugonjwa lakini inaweza kuwa dalili ya ugonjwa. Hivyo mtoto anapokuwa na homa, unapaswa kuzingatia afya yake badala ya kuwa na wasiwasi kuhusu joto lake.” Chuo cha Marekani cha Tiba ya Watoto kinasema: “Hupaswi kumpa mtoto wako dawa akiwa na kiwango cha joto cha nyuzi 101 za Fahrenhaiti (38.3 za Selsiasi) ila tu ikiwa anaumwa au hupatwa na mpapatiko mara kwa mara. Hata joto la mwili wake likiwa juu zaidi hilo si hatari, isipokuwa awe na mpapatiko au ugonjwa mwingine hatari. Ni vizuri kumfahamu. Ikiwa anakula na kulala vizuri, anacheza vizuri, basi hahitaji matibabu yoyote.”

Kutibu Homa Isiyo Kali

Haimaanishi kwamba huwezi kufanya lolote kumsaidia mtoto wako. Madaktari fulani hutoa madokezo yafuatayo ya kutibu homa isiyo kali: Hakikisha chumba cha mtoto hakina joto sana. Mvishe mavazi mepesi. (Mavazi mazito yanaweza kuongeza homa.) Mpe mtoto vinywaji kama vile maji, maji ya matunda yenye maji mengi, na supu, kwa sababu homa inaweza kumfanya aishiwe na maji. * (Vinywaji vyenye kafeini kama vile kola au chai isiyo na maziwa, vinaweza kumfanya apoteze maji zaidi.) Watoto wachanga wanapaswa kuendelea kunyonyeshwa. Epuka vyakula ambavyo havisagiki kwa urahisi kwani homa hupunguza utendaji tumboni.

Mara nyingi mtoto hupewa dawa za dukani za kutuliza maumivu kama vile acetaminophen au ibuprofen joto lake linapopita nyuzi 38.9 za Selsiasi. Hata hivyo, ni muhimu kufuata maagizo yaliyo kwenye kibandiko. (Watoto walio na umri wa chini ya miaka miwili wasipewe dawa zozote bila idhini ya daktari.) Dawa za kupunguza homa haziui virusi hivyo, hazitibu mtoto mafua au magonjwa mengine kama hayo, ingawa zinaweza kupunguza maumivu. Wataalamu wengine wamependekeza kwamba watoto walio chini ya umri wa miaka 16 wasipewe aspirini ili kutuliza homa, kwani inaweza kusababisha ugonjwa hatari wa Reye. *

Homa inaweza kutulizwa pia kwa kumwosha mtoto. Mweke ndani ya beseni yenye maji kidogo yaliyo vuguvugu na umwoshe kwa sifongo. (Usitie dawa yenye alkoholi kwenye maji hayo kwani inaweza kumdhuru.)

Sanduku lililoonyeshwa linadokeza wakati unaofaa kumwona daktari. Inafaa uombe ushauri wa daktari iwapo unaishi katika maeneo ambayo watu huugua sana kidingapopo, Ebola, homa ya matumbo, au homa ya manjano.

Kwa vyovyote vile, jambo unalopaswa kuzingatia ni kumpunguzia mtoto wako maumivu. Kumbuka, haielekei kwamba homa itasababisha ugonjwa wa mfumo wa neva au kifo. Ingawa homa inatisha wakati inaposababisha mpapatiko, mara nyingi inafifia baadaye.

Bila shaka kuzuia ni bora kuliko kuponya, hivyo njia bora zaidi ya kumkinga mtoto wako na magonjwa ni kumfundisha kuhusu usafi. Watoto wanapaswa kufundishwa kunawa mikono mara kwa mara, hasa kabla ya kula, baada ya kwenda kujisaidia, baada ya kuwa mahali penye watu wengi, au baada ya kumshika mnyama. Mtoto wako anapopata homa hata baada ya jitihada hizo zote, usiwe na wasiwasi. Kama tulivyoona, unaweza kumsaidia mtoto wako apate nafuu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Hali ya joto huwa tofauti ikitegemea mahali ambapo limepimiwa na pia kifaa kilichotumiwa.

^ fu. 10 Ona gazeti la Aprili 8, 1995, la Amkeni!, ukurasa wa 11, kwa habari zinazohusu kutengeneza mchanganyiko unaoweza kutumiwa ikiwa mtu mwenye homa anaharisha au kutapika.

^ fu. 11 Ugonjwa wa Reye ni ugonjwa hatari wa mfumo wa neva ambao unaweza kuwapata watoto baada ya kushambuliwa na virusi.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Mwone Daktari Iwapo Mtoto Wako Mwenye Homa . . .

▪ Ana umri wa miezi mitatu au chini na joto lake ni nyuzi 38 za Selsiasi au zaidi

▪ Ana umri wa kati ya miezi mitatu na sita na joto lake ni nyuzi 38.3 za Selsiasi au zaidi

▪ Ana umri unaozidi miezi sita na joto lake ni nyuzi 40 za Selsiasi au zaidi

▪ Anakataa kunywa chochote na anaonekana ameishiwa na maji

▪ Ana mpapatiko au hatulii hata kidogo

▪ Homa yake imedumu kwa zaidi ya saa 72

▪ Analia tu au anaonekana amechanganyikiwa

▪ Ana vipele, ana ugumu wa kupumua, anaharisha, au anatapika sana

▪ Shingo yake ni ngumu au ana maumivu makali kichwani

[Hisani]

Source: The American Academy of Pediatrics