Kile Ambacho Watoto Wanahitaji
Kile Ambacho Watoto Wanahitaji
TANGU mtoto anapozaliwa, anahitaji kutunzwa kwa wororo. Anahitaji kupapaswa kwa wororo na kukumbatiwa. Madaktari fulani wanaamini kwamba saa 12 za kwanza za maisha yake ni muhimu sana. Wanasema kwamba mara tu baada ya kuzaliwa, kile ambacho mama na mtoto wanahitaji na wanataka sana ni “kupapasana, kukumbatiana, kutazamana na kusikilizana, bali si kulala wala kula.” *
Kwa kawaida wazazi humshika, humpakata, humpapasa, na kumkumbatia mtoto wao. Naye mtoto huanza kuwa na uhusiano wa karibu na wazazi wake na huitikia wanapomjali. Uhusiano huo ni wenye nguvu sana hivi kwamba wazazi hujitoa mhanga kumtunza mtoto lolote liwalo.
Kwa upande mwingine, mtoto anaweza kudhoofika na kufa wazazi wasipomjali. Hivyo, madaktari fulani husema kwamba mtoto anapaswa kuletwa kwa mama yake mara tu anapozaliwa. Wanapendekeza kwamba anapaswa kuwa na mama yake angalau dakika 30 mpaka 60 za kwanza kabisa za maisha yake.
Ingawa watu fulani husisitiza kwamba mama na mtoto wake wawe pamoja mara tu baada ya kuzaliwa, jambo hilo
haliwi rahisi katika hospitali nyingine. Mara nyingi watoto hutenganishwa na mama zao kwa sababu inahofiwa kwamba watoto wataambukizwa magonjwa. Hata hivyo, uthibitisho unaonyesha kwamba mtoto anapokuwa na mama yake haielekei ataambukizwa ugonjwa hatari. Kwa hiyo, hospitali nyingi zaidi zinawaruhusu akina mama kuwa na watoto wao kwa muda mrefu zaidi baada ya kuzaliwa.Kuhangaikia Uhusiano Wako na Mtoto
Akina mama fulani hawavutiwi na watoto wao wanapowatazama kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo, wanajiuliza, ‘Je, nitampenda mtoto wangu?’ Ni kweli kwamba si mama wote wanaowapenda watoto wao mara tu wanapowaona. Lakini hakuna haja ya kuwa na wasiwasi.
Hata mama asipovutiwa na mtoto wake mara moja, anaweza kuvutiwa naye baadaye. Mama mmoja mwenye uzoefu anasema: “Uhusiano wako pamoja na mtoto wako hauathiriwi unapomtazama baada ya kujifungua.” Hata hivyo, ikiwa wewe ni mjamzito na una wasiwasi kuhusu uhusiano wako wa baadaye pamoja na mtoto wako, itafaa uzungumze na daktari wako mapema. Mweleze unataka kuwa na mtoto wako wakati gani na kwa muda gani.
“Tafadhali Ongea Nami!”
Inaonekana kuna wakati ambapo huwa rahisi kwa watoto kujifunza mambo fulani. Baada ya muda inakuwa vigumu kujifunza mambo hayo tena kwa urahisi. Kwa mfano, mtoto mchanga hujifunza lugha moja au zaidi kwa urahisi. Lakini anapofikia umri wa miaka mitano hivi, inakuwa vigumu kujifunza lugha.
Inakuwa vigumu hata zaidi kwa mtoto kujifunza lugha fulani anapofikia umri wa miaka 12 mpaka 14. Kulingana na daktari wa mfumo wa neva wa watoto, Peter Huttenlocher, wakati huo “ukubwa na idadi ya viunganishi vya neva katika sehemu za ubongo zinazoshughulikia lugha hupungua.” Basi, miaka michache ya kwanza maishani ni muhimu katika kujifunza lugha!
Watoto huwezaje kuzungumza, jambo ambalo ni muhimu sana katika ukuzi wa akili yao? Hasa kwa kuongea na wazazi. Watoto huchochewa hasa na sauti za watu. Barry Arons wa Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts anasema, “mtoto . . . huiga sauti ya mama yake.” Hata hivyo, watoto hawaigi sauti zote. Arons anasema kwamba mtoto “haigi kelele za kitanda chake zinazosikika wakati uleule mama yake anapozungumza.”
Wazazi katika sehemu mbalimbali huzungumza na watoto wao kwa njia moja. Mzazi anapozungumza kwa upendo, mpigo wa moyo wa mtoto huongezeka. Inaaminika kwamba jambo hilo humsaidia mtoto kuhusianisha vitu na majina yake. Ni kana kwamba mtoto anasema: “Tafadhali ongea nami!”
“Tafadhali Nitazameni!”
Imegunduliwa kwamba katika mwaka wa kwanza au baadaye, mtoto huwa na uhusiano wa karibu na mtu anayemlea, hasa mama yake. Mtoto anapokuwa na uhusiano huo
mzuri, anapatana na watu wengine kuliko watoto ambao hawana uhusiano mzuri na wazazi wao. Uhusiano huo unapaswa kusitawishwa kabla mtoto hajafikia umri wa miaka mitatu.Ni nini kinachoweza kutukia mtoto anapopuuzwa wakati huo ambapo akili yake inaweza kuathiriwa kwa urahisi? Martha Farrell Erickson aliyewachunguza akina mama 267 na watoto wao kwa miaka zaidi ya 20, anasema: “Mtoto anapopuuzwa, pole kwa pole yeye hukosa uchangamfu na hatimaye anashindwa kuchangamana na wengine au kujifunza mambo mengine.”
Akielezea maoni yake kuhusu matokeo mabaya ya kumpuuza mtoto, Dakt. Bruce Perry, wa Hospitali ya Watoto ya Texas anasema: “Kama ningeombwa nichague kati ya kumvunja mtoto wa miezi 6 mifupa yake yote au kumpuuza kwa miezi miwili, ningesema afadhali avunjwe mifupa yake yote.” Kwa nini? Perry anaonelea kwamba “mifupa inaweza kupona, lakini mtoto akipuuzwa kwa miezi miwili, akili yake itachanganyikiwa daima.” Watu fulani hudai kwamba madhara hayo yanaweza kutibiwa. Hata hivyo, uchunguzi wa kisayansi unaonyesha kwamba malezi yafaayo ni muhimu kwa akili ya mtoto.
Kitabu Infants kinasema, “kwa ujumla [watoto] hutaka kupenda na kupendwa.” Mtoto anapolia, mara nyingi anawasihi wazazi wake hivi: “Tafadhali nitazameni!” Inafaa wazazi wamshughulikie kwa njia ya upendo. Kwa njia hiyo mtoto ataanza kujua kwamba anaweza kuwaeleza wengine mahitaji yake. Atajifunza kuchangamana na wengine.
‘Si Nitamharibu Mtoto?’
Huenda ukajiuliza, ‘Nikimhangaikia mtoto kila anapolia, si nitamharibu?’ Labda. Watu wana maoni tofauti kuhusu jambo hilo. Kwa kuwa kila mtoto ni tofauti, wazazi wanapaswa kuamua njia nzuri ya kumlea. Hata hivyo, uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba mtoto aliyezaliwa hivi karibuni akiwa na njaa, maumivu, au akikasirika, homoni za mfadhaiko hutokezwa mwilini. Yeye huonyesha mfadhaiko wake kwa kulia. Inasemekana kwamba mzazi anapoitikia na kumhangaikia mtoto, anaanza kusaidia ubongo wake kutokeza chembe zitakazomsaidia kujua jinsi ya kujituliza. Pia kulingana na Dakt. Megan Gunnar, mtoto anayehangaikiwa anapolia, hutokeza homoni chache za mfadhaiko za cortisol. Hata anapokasirika, yeye hujituliza haraka.
Erickson anasema: “Watoto wanaohangaikiwa haraka na kwa ukawaida wanapolia, hasa katika miezi 6 hadi 8 ya kwanza, hawalii sana kama wale wanaopuuzwa.” Pia ni muhimu kuitikia kwa njia mbalimbali. Ukiitikia
kwa njia moja kila wakati, kama vile kwa kumlisha au kumpakata, ataharibika. Wakati mwingine inatosha kuongea tu anapolia. Au kumsogelea na kuzungumza polepole sikioni mwake kunaweza kusaidia. Kwa upande mwingine, kupapasa mgongo au tumbo lake kunaweza kusaidia pia.“Kazi ya mtoto ni kulia tu.” Huo ni msemo wa Mashariki. Kulia ndiyo njia ya mtoto ya kueleza anachotaka. Ungehisije ikiwa ungepuuzwa kila unapoomba kitu fulani? Basi, mtoto ambaye anahitaji kutunzwa atahisije akipuuzwa kila anapolia? Lakini ni nani anayepaswa kumshughulikia?
Ni Nani Anayepaswa Kumtunza Mtoto?
Sensa ya hivi karibuni nchini Marekani, ilionyesha kwamba asilimia 54 ya watoto hutunzwa kwa kadiri fulani na watu ambao si wazazi wao tangu wanapozaliwa mpaka wanapofikia darasa la tatu. Katika familia nyingi wazazi wote hufanya kazi ili kupata riziki. Hata hivyo, akina mama wengi hupewa likizo ya kujifungua, ikiwezekana, ili kuwatunza watoto wao kwa majuma au miezi kadhaa. Lakini ni nani atakayemlea mtoto baadaye?
Ni wazi kwamba hakuna sheria kali kuhusu jambo hilo. Hata hivyo, ni vizuri kukumbuka kwamba mtoto anahitaji msaada wakati huo muhimu. Wazazi wote wawili wanahitaji kufikiria jambo hilo kwa uzito. Wanapofanya uamuzi wanapaswa kufikiria njia mbalimbali za kushughulikia hali hiyo.
Dakt. Joseph Zanga, wa Chuo cha Marekani cha Tiba ya Watoto, anasema: “Imeonekana kwamba hata kuwaacha watoto watunzwe na walezi bora zaidi hakuwezi kuchukua mahali pa mama na baba.” Wataalamu fulani wamesema kwamba watoto wanaopelekwa kwenye vituo vya utunzaji hawawi na walezi wao kwa muda wa kutosha.
Kwa kuwa wanatambua mahitaji ya watoto wao, akina mama fulani wanaofanya kazi wameamua kuacha kazi ili kuwa na watoto wao badala ya kuwaachia wengine wawatunze. Mwanamke mmoja alisema: “Nimepata uradhi ambao naamini singepata kwa kufanya kazi nyingine yoyote.” Bila shaka, matatizo ya kiuchumi hayawezi kuwaruhusu akina mama wote wafanye hivyo. Wazazi wengi wanalazimika kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya utunzaji, hivyo wao hufanya jitihada nyingi ili kuwa pamoja na watoto na kuwahakikishia upendo wao. Pia, wazazi wengi wasio na mwenzi ambao wanafanya kazi hulazimika kuwapeleka watoto wao kwenye vituo hivyo na hujitahidi sana kuwalea, nao wanapata matokeo mazuri.
Kulea watoto kunaweza kufurahisha, hata kusisimua. Lakini ni kazi ngumu. Unawezaje kufaulu?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Katika mfululizo huu, Amkeni! linaelezea maoni ya wataalamu maarufu wa utunzaji wa watoto kwani habari hizi zinaweza kuwasaidia na kuwaelimisha wazazi. Lakini tunapaswa kuelewa kwamba maoni hayo yanaweza kubadilika baada ya muda fulani, tofauti na kanuni za Biblia ambazo Amkeni! huunga mkono kwa ukamili.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Watoto Wanyamavu
Madaktari fulani huko Japan wanasema kwamba idadi ya watoto ambao hawalii au kutabasamu imeongezeka. Daktari wa watoto, Satoshi Yanagisawa, anawaita watoto wanyamavu. Kwa nini watoto huacha kuonyesha hisia zao? Madaktari fulani wanaamini kwamba hali hiyo hutokea kwa sababu watoto wanapuuzwa na wazazi wao. Nadharia moja inasema kwamba mtoto anapopuuzwa mara nyingi au kueleweka vibaya anapolia, hatimaye anaacha kuonyesha hisia zake.
Kulingana na Dakt. Bruce Perry, daktari mkuu wa akili kwenye Hospitali ya Watoto ya Texas, mtoto anapopuuzwa wakati anapohitaji msaada, sehemu ya ubongo inayomchochea kuwa mwenye huruma huenda isisitawi. Anapopuuzwa kabisa anaweza kushindwa kuonyesha huruma katika maisha yake yote. Dakt. Perry anaamini kwamba huenda hali hiyo ikamfanya mtoto awe mzoefu wa dawa za kulevya na mjeuri anapobalehe.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Uhusiano kati ya mzazi na mtoto huimarika wanapowasiliana