Kutembelea Chemchemi za Maji ya Moto za Japan
Kutembelea Chemchemi za Maji ya Moto za Japan
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI JAPAN
UNAPOSIKIA juu ya Japan, wewe hufikiria nini? Je, ni mlima mkubwa wa Fuji? Je, ni gari-moshi la umeme linalokwenda kasi? Je, ni jiji kubwa la Tokyo? Kuna mambo mengine ya kupendeza nchini Japan. Kila mwaka, mamilioni ya watu hutembelea chemchemi za maji ya moto za Japan zinazoitwa onsen ambazo hutumiwa kwa matibabu au kwa starehe. Katika mwaka mmoja hivi karibuni, inakadiriwa kwamba watu milioni 140 walitembelea hoteli moja yenye chemchemi ya maji ya moto nchini Japan. Kwa nini chemchemi hizo zinapendwa sana?
Historia ya Chemchemi Hizo
Kwa karne nyingi, Wajapani wamefurahia kuoga ndani ya chemchemi za maji ya moto. Maandishi ya tangu karne ya nane W.K. yanataja chemchemi hizo. Inaonekana kwamba mtawala wa karne ya 16 aliyeitwa Takeda Shingen aliona chemchemi hizo kuwa muhimu kwa tiba. Baada ya vita, yeye na maaskari
wake walioga katika chemchemi za maji ya moto ili kuponya majeraha ya panga, mifupa iliyovunjika, na mikwaruzo. Pia maji hayo yalitumiwa kupunguza mfadhaiko na kuwatayarisha tena kwa ajili ya vita.Ama kwa hakika, maaskari hao walikabili hatari ya kushambuliwa ghafula bila silaha walipokuwa wanaoga. Ili kuepuka tatizo hilo, Takeda Shingen alitumia chemchemi za mbali zilizojificha, ambazo baadaye ziliitwa chemchemi zilizojificha za Shingen. Chemchemi hizo zinatumiwa hata leo na wanariadha, kama vile wanamwereka wa sumo na wachezaji wa besiboli kwa kuwa wanaamini kwamba zinaweza kuimarisha miili yao kwa ajili ya mashindano.
Mandhari za Pekee
Chemchemi za maji ya moto zinafaana na mandhari ya Japan. Kuna volkano 245 hivi katika visiwa vya Japan na 86 zinaweza kulipuka. Volkano hizo ni ishara ya mambo yanayoendelea chini ya ardhi. Kuna nini huko?
Visiwa vya Japan viko juu ya mahali ambapo miamba mikubwa ya dunia inakutana. Inasemekana kwamba miamba huyeyuka mahali hapo. Volkano ziko juu ya sehemu hiyo. Maji yaliyomo ardhini hupashwa joto na kufyonza madini kutoka kwenye miamba iliyoyeyuka, na kububujika yakiwa chemchemi za maji ya moto. Basi si ajabu kwamba kitabu The Hot Springs of Japan kinasema: “Hakuna nchi ulimwenguni yenye chemchemi za asili za maji ya moto kama Japan.” Isitoshe, uchunguzi uliofanywa mwaka wa 1998 ulionyesha kwamba kuna chemchemi 2,839 za maji ya moto nchini Japan.
Chemchemi za maji ya moto za Japan huwa na miundo, ukubwa, maumbo, na rangi mbalimbali. Shirika la Mazingira la Japan limegawanya chemchemi hizo katika vikundi tisa kulingana na madini yaliyomo ili kuonyesha faida zake za kitiba. Kwa kawaida, majina ya chemchemi hizo huonyesha jinsi zilivyo. Kwa mfano, chemchemi zenye madini ya chuma zinaweza kuacha rangi nyekundu na ya machungwa kwenye taulo yako. Hivyo, neno “nyekundu” huwa sehemu ya jina lake. Chemchemi zilizo na chumvi nyingi huitwa chemchemi za chumvi. Je, ungependa
kuoga katika chemchemi za mkunga? Labda jambo hilo halikuvutii. Lakini usijali. Chemchemi hizo hazina mikunga. Zinaitwa hivyo kwa sababu watu wanapooga humo, ngozi yao huteleza kama mkunga kwa sababu ya madini yaliyomo.Mazingira Maridadi
Kuoga ndani ya maji ya moto katika mazingira maridadi yenye milima, mabonde, mito, fuo za bahari, na nyanda huvutia sana na ni jambo lisilosahaulika kwa urahisi. Kwa kuwa chemchemi nyingi za maji ya moto nchini Japan ziko nje, watu hutazama mandhari maridadi wanapooga. Anga la buluu nzito hutanda juu ya chemchemi hizo kama dari, na kandokando kuna milima iliyo kama kuta. Sauti za ndege wanaoimba kama kwaya husikika asubuhi na vilevile mvumo wa kijito kinachotiririka taratibu. Ama kweli, hatuwezi kuelezea mandhari zote zenye kuvutia sana zinazopatikana huko.
Je, unapenda kuoga chini ya poromoko la maji? Unaweza kufurahia jambo hilo. Maji yanayoporomoka yatakanda mwili wako unapofurahia mtindo
huo mwingine wa kuoga wa Wajapani. Hata unaweza kuoga pangoni, ambamo mna maji yenye madini yanayobubujika kutoka chini sana miambani. Chemchemi nyingine ziko kwenye ufuo ambako unaweza kuona jua likizama kwa uzuri, hali nyingine ziko karibu na mito.Ukiamua kuoga katika chemchemi yoyote ile, jambo moja ni hakika: Maji ya moto ya chemchemi yatakupumzisha na hekaheka za kila siku, angalau kwa kitambo kidogo. Utaburudishwa kabisa na pengine utafahamu vizuri maisha ya Wajapani. Hivyo, ukipata nafasi ya kutembelea Japan, jitahidi juu chini ufike kwenye onsen—chemchemi za maji ya moto!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]
CHEMCHEMI ZA MAJI YA MOTO NA WATAWALA
Maji yenye madini yalipendwa sana katika enzi ya Edo (mwaka wa 1603-1867). Madikteta wa kijeshi waliwatumia watu kusafirisha maji hayo katika mapipa ya mbao yaliyobebwa mabegani kwa milingoti kuanzia Atami mpaka Edo (Tokyo), umbali wa kilometa 110. Kwenye sehemu mbalimbali njiani, wabebaji wengine walipokezwa maji hayo yaliyopendwa sana. Hivyo, maji hayo yenye madini yalisafirishwa haraka. Maji yalichotwa kwenye chemchemi yakiwa moto sana. Baada ya safari ya kuchosha ya saa 15 hivi, maji hayo yalipoa kiasi cha kumburudisha mtawala alipokuwa anaoga katika kasri yake huko Edo!
[Hisani]
A Chronological Table of the History of Atami
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]
Taratibu za Onsen
Kulingana na desturi, mtu hujipaka sabuni, hujiosha, na kujimwagilia maji kabisa kabla ya kuingia ndani ya chemchemi za maji ya moto. Kisha hujitumbukiza ndani ya maji safi yenye madini. * Inafaa uingie polepole, kwa kuwa baadhi ya chemchemi hizo huwa moto sana. Unapomaliza, usioshe madini yaliyo mwilini mara moja. Jipanguse tu kwa taulo. Inasemekana kwamba madini yanayopenya ndani hulainisha ngozi.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 22 Jambo jingine la pekee ni kwamba kuna chemchemi za umma za wanaume na nyingine za wanawake.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Watu hufurahia maji ya moto mwaka mzima
[Hisani]
Fall: Yubara, Okayama Prefecture; winter: The Mainichi Newspapers
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Hakkoda Onsen Yusen