Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wanyama Wavamia Hispania

Gazeti El País la Hispania linaripoti hivi: “Zaidi ya aina 40 za wanyama wa nchi kavu, wa baharini, na wanyama warukao kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamevamia Hispania na kushambulia mimea na wanyama.” Wanyama hao wanatia ndani kambare wa Ujerumani, mwani wa Karibea, kasuku wa Argentina, na aina fulani ya kicheche wa Amerika Kaskazini. Wanyama wengi waliuzwa huko Hispania ili wawe wanyama-vipenzi au kwa sababu nyingine. Wengine walitoroka, na wengine wakaachiliwa baada ya kuwalemea wenyewe au walipoacha kuleta faida. Mwanabiolojia Daniel Sol anasema: “Mbali na kukosa makao, wanyama wa asili wanapungua hasa kwa sababu ya wanyama wageni.”

Mayai Yatibu Sumu ya Nyoka

Gazeti The Times of India linasema: “Wanasayansi Wahindi wamegundua kwamba mayai ya kuku yanaweza kutokeza molekuli zinazoweza kutibu sumu ya nyoka.” Kuku wa majuma 12 hivi hudungwa sindano “yenye sumu ya nyoka ambayo si hatari sana kwenye misuli yao” na baada ya majuma mawili au matatu wao hupewa dawa nyingine. Baada ya majuma 21, wao hutaga mayai yenye kinga za sumu. Gazeti The Times linasema kwamba watafiti wanatumaini kwamba dawa hiyo inayotokana na mayai huenda ikatumiwa badala ya ile inayotokana na farasi kwa sababu “wao huumia wakati kemikali zinazotengeneza dawa hiyo zinapotolewa mwilini mwao.” Wanasayansi nchini Australia wanasema tayari wamepata mafanikio kwa kutumia dawa hiyo mpya kwa wanyama. Dawa hiyo ya mayai ikifanikiwa kutibu wanadamu, inaweza kufaidi sana India ambako watu 300,000 huumwa na nyoka kila mwaka, na asilimia 10 kati yao hufa.

Jinsi Kipepeo Anavyoruka

Gazeti The Independent la London linasema: “Kwa miaka mingi wanasayansi wamejaribu kuelewa jinsi kipepeo anavyoruka polepole, anavyozunguka-zunguka, anavyoruka nyuma na kuruka kwa upande kwa urahisi.” Sasa watafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford wanaamini kwamba hatimaye wamegundua siri ya mdudu huyo. Wakitumia mrija maalumu uliowekwa moshi ili kuonyesha jinsi hewa inavyosonga, waliwachunguza vipepeo wa red admiral wakipepea. Vipepeo waliporuka huku na huku wakizunguka maua bandia ndani ya mrija huo, kamera zinazopiga picha nyingi haraka ambazo zinaendeshwa kwa kompyuta, zilirekodi mawimbi ya hewa karibu na mabawa yao. Watafiti hao waligundua kwamba “kipepeo haruki ovyoovyo au bila mpango, bali hutumia mfumo wa hali ya juu wa kuruka.” Wanasayansi wanatumaini kwamba ujuzi huo utawasaidia kuunda ndege yenye mabawa yasiyozidi urefu wa sentimeta kumi na inayoendeshwa kutoka mbali. Kamera zitawekwa katika ndege hizo, nazo zitatumiwa kuchunguza mapango.

Matatizo ya Usingizi Huko Italia

Katika mwaka wa 2002, zaidi ya madaktari 600 na zaidi ya wagonjwa 11,000 walihusishwa katika uchunguzi mkubwa zaidi kuhusu matatizo ya usingizi kuwahi kufanywa nchini Italia. Gazeti La Stampa linasema kwamba uchunguzi huo umefunua kwamba zaidi ya Waitaliano milioni 12 wana matatizo ya usingizi. Asilimia 65 ya waliochunguzwa husinzia asubuhi, asilimia 80 husinzia wakati wa mchana, na asilimia 46 hushindwa kukaza fikira kazini. Gazeti hilo linasema: “Kwa kuwa asilimia 22 ya misiba ya barabarani husababishwa na kusinzia, wale wanaoendesha magari wanakabili hatari kubwa.” Uchunguzi huo pia ulionyesha kwamba asilimia 67 ya watu wenye matatizo ya usingizi hawajamweleza daktari kuhusu tatizo hilo. Msimamizi wa uchunguzi huo, Mario Giovanni Terzano, alisema kwamba “angalau asilimia 20 ya watu hao hasa wanasumbuliwa na matatizo ya usingizi, na hawajui sababu.” Hata hivyo, uchunguzi wa kitiba unaweza kuonyesha tatizo lingine linalosababisha hali hiyo. Terzano alisema kwamba visababishi vingine vya matatizo ya usingizi vinatia ndani wasiwasi (asilimia 24), mambo yenye kufadhaisha (asilimia 23), na kushuka moyo (asilimia 6).

Swara wa Saiga Wako Karibu Kutoweka

Gazeti New Scientist linasema: “Katika mwaka wa 1993, swara wa saiga zaidi ya milioni moja walipatikana katika nyika ya Urusi na Kazakhstan. Leo, idadi ya swara hao haizidi 30,000.” Ripoti hiyo inasema kwamba wanyama hao wanaangamizwa na “wawindaji-haramu. Wanabiolojia wanasema kwamba idadi ya wanyama hao imepungua sana na kwa muda mfupi kuliko ya wanyama wengine wakubwa.” Kwa nini wanawindwa? Mapema katika miaka ya 1990, wahifadhi wa mazingira walihangaikia kutoweka kwa vifaru na kuwachochea watu watumie pembe za saiga kutengeneza dawa ya kienyeji ya Kichina badala ya pembe za kifaru. Kwa kuwa swara hao walikuwa wametoweka nchini China, wale wa katikati ya Asia ndio waliowindwa. Katika muda wa miaka mitano (1993-1998), idadi ya swara ilipungua kwa asilimia 50 hivi, na kwa asilimia 97 kufikia mwaka wa 2002. Katika Kazakhstan ya Kati, wamepungua kwa asilimia 99. Swara 4,000 tu ndio wamebaki huko. Mtaalamu wa wanyama, Abigail Entwistle wa Shirika la Kimataifa la Wanyama na Mimea, anasema: “Tunafikiri tuna miaka miwili tu ya kuokoa jamii hiyo.”

Fikira, Hisia, na Afya

Gazeti Wprost la Poland lilisema kwamba mambo tunayofikiri yanaweza kuathiri sana afya yetu kuliko ilivyodhaniwa. Linaongeza hivi: “Fikira na hisia huathiri viungo na mifumo yote muhimu ya mwili, kama vile mfumo wa neva, wa kinga, wa homoni, wa mzunguko wa damu, na wa uzazi.” Hivyo, Profesa Marek Kowalczyk wa Taasisi ya Jeshi ya Usafi na Magonjwa huko Warsaw, asema “watu wanaokabili mfadhaiko maishani hupata mafua na homa mara nyingi kuliko wengine.” Pia anasema kwamba uwezekano wa wanawake walioshuka moyo kupata mimba hupungua kwa asilimia 50. Gazeti hilo pia linaripoti kwamba ijapokuwa mfadhaiko hausababishi kansa, “unaweza kuharakisha kuenea kwa kansa iliyojificha.” Hasira pia hudhoofisha afya, kwa kuwa inaaminiwa kwamba watu wakali na wajeuri hupata magonjwa ya moyo zaidi, hivyo wanaweza kupata mshtuko wa moyo.

Biashara ya Pembe za Tembo

Katika miaka kumi tu, kuanzia mwaka wa 1979 mpaka 1989, idadi ya tembo wa Afrika ilipungua kwa zaidi ya asilimia 50. Sababu moja ni kwamba bidhaa zilizotengenezwa kwa pembe za tembo zilihitajika sana. Sababu nyingine ni kwamba wawindaji-haramu walipata silaha kali. Hivyo, mnamo mwaka wa 1989 Mkataba wa Kupinga Biashara ya Kimataifa ya Viumbe na Mimea Inayokabili Hatari ya Kutoweka ulipiga marufuku kabisa biashara ya pembe za tembo. Hata hivyo, gazeti African Wildlife linasema kwamba hivi majuzi mkataba huo uliruhusu Afrika Kusini, Botswana, na Namibia kuuza tani 60 za pembe za tembo. Wawindaji-haramu walinyang’anywa pembe hizo au zilitolewa kutoka kwa wanyama waliokufa. Makala hiyo ilisema kwamba nchi nyingine mbili zilikatazwa kuuza pembe hizo kwa sababu “hazikutoa uhakikisho wa kutosha kwamba zingezuia uuzaji haramu wa pembe za tembo.”