Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

‘Hoteli ya Hali ya Juu’

‘Hoteli ya Hali ya Juu’

‘Hoteli ya Hali ya Juu’

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

KUNA watu wengi ambao, kama mimi, wanaweza kuchagua kulala jangwani wakitazama nyota badala ya kulala katika hoteli ya hali ya juu. Ndivyo nilivyohisi baada ya kutembelea kusini mwa Tunisia, huko Afrika Kaskazini. Nikiwa huko nilifurahia kustarehe katika hema la wachungaji wanaohamahama jangwani, ambalo huonwa kuwa hoteli ya hali ya juu.

Katika historia yote ya wanadamu, mamilioni ya watu kutoka nyika za Asia, jangwa la Sahara, na Amerika Kaskazini wameishi katika “hoteli” kama hizo. Ingawa makabila mengi yamelazimika kuacha kuishi kwenye mahema yao katika karne iliyopita, maelfu ya wahamaji bado wanaishi jangwani. Mtu hawezi kusahau ukarimu wao.

“Nyumba ya Manyoya”

Ili kufika kwenye kambi ya wahamaji, inayoitwa douar huko Afrika Kaskazini, mimi na yule anayenitembeza tunasafiri kwa gari kuukuu aina ya Land Rover. Baada ya kuwaomba wachungaji watuonyeshe njia, mwishowe kwa mbali tunaona maumbo ya mahema meusi na ya kahawia. Mara tu tunapotoka kwenye gari, tunavutiwa na jinsi jangwa hilo lilivyotulia. Wabedui wanasema kwamba utulivu huo hupumzisha akili. Tunasalimiwa kwa uchangamfu na mkaribishaji wetu anayetualika ndani ya hema lake. Lina urefu wa meta 12, upana wa meta 5 na kimo cha meta 2. Tunaingia kwenye sehemu iliyotengewa wanaume na wageni na tunakalia mikeka maridadi. Sehemu ile nyingine ya hema, ambayo hufunikwa kwa pazia kunapokuwa na wageni, hutumiwa na familia na ndio jikoni. Tunapozungumza, mke wa mkaribishaji wetu anatuletea chai ya kienyeji ya mnanaa, huku binti zake wakikanda unga jikoni ili kutayarisha keki. Mikate hiyo mitamu inapikwa kwenye chombo cha udongo kilichowekwa juu ya mawe karibu na moto.

Tunapoendelea na mazungumzo, ninamuuliza mkaribishaji wangu jinsi paa na kuta za hema hutengenezwa. Ananijibu kwa uchangamfu. Kuta hazijaundwa kwa kitambaa kimoja, bali zimeundwa kwa vipande vingi vya vitambaa vilivyounganishwa vyenye urefu wa meta 15 hivi na upana wa sentimeta 50 hivi. Mahema makubwa yana vipande 12 au 13. Vitambaa hivyo hutengenezwaje?

Alasiri moja yenye jua kali, namwona binti mmoja wa mkaribishaji wangu akiketi mchangani mbele ya hema akisokota uzi kwa ustadi kutokana na manyoya ya mnyama. Uzi huo hufumwa na kutengeneza vitambaa kwenye kitanda cha mfumi kilichowekwa ardhini. Nyuzi hazikazwi sana ili kuruhusu hewa iingie. Hata hivyo, kunaponyesha, nyuzi hufura na kuzuia maji yasipenye. Ama kweli, jina la Kiarabu la hema bait esh-shaar, linalomaanisha “nyumba ya manyoya,” linafaa.

Kutunza Hema

Hema hudumu kwa muda gani? Wahamaji hutunza sana nyumba zao za jangwani. Mkaribishaji wangu ananiambia kwamba wanawake wa nyumba yake hutengeneza angalau kitambaa kimoja kila mwaka. Kwa kawaida, kila mwaka kitambaa kilichochakaa zaidi hubadilishwa na kingine kipya. Hivyo, ukuta wenye vitambaa vinane utarekebishwa kabisa baada ya miaka minane. Katika sehemu nyingine, vitambaa hufumuliwa na kugeuzwa ili upande wa ndani ambao haujachakaa uangalie nje.

Hema hutegemezwa na nini? Katikati ya hema kuna vigingi vinne vya mti wa apricot, ijapokuwa miti mingine pia hutumiwa. Vigingi viwili vya katikati vina urefu wa meta 2.5. Upande mmoja wa kila kigingi hupigiliwa ardhini, na ule mwingine huingizwa kwenye mtambaapanya uliorembeshwa, wenye urefu wa sentimeta 45 mpaka 60. Mtambaapanya umejipinda kidogo, na kufanya sehemu ya juu ya hema ifanane na nundu ya ngamia. Sehemu za kando na sehemu ya nyuma ya hema imetegemezwa kwa vigingi vidogo. Tunaenda nje kuona jinsi hema inavyofungiliwa. Tunaona kamba zilizotengenezwa kwa manyoya ya mbuzi hutumiwa kufungilia vipande vya mbao ardhini.

Nyuma ya hema, kuna ua wa miti midogo iliyokauka ili kuzuia wanyama wa mwituni. Punda wa familia amefungwa karibu na hema. Karibu na hapo, kwenye boma la duara, kuna kundi la kondoo na mbuzi linalochungwa na mabinti wa mkaribishaji wangu.

Maisha Sahili

Kufikia sasa, mikate iko tayari na inatiwa katika mafuta ya zeituni yanayoifanya iwe na ladha nzuri. Ninapotazama makao hayo, ninapendezwa na maisha sahili ya wahamaji. Wana vyombo vichache tu kama vile kabati la mbao, mifuko, mikeka, na mablanketi yaliyofumwa. Mabinti wa mkaribishaji wangu wanafurahia kunionyesha kifaa kidogo wanachotumia kuchana na kusokota uzi. Zaidi ya hayo, hawana vitu vingi sana. Hilo linanikumbusha maneno ya hekima ya yule mchungaji mshairi Daudi, aliyeishi kwa muda fulani kwenye mahema: “Mmoja anarundika vitu wala hajui ni nani atakayevikusanya.”—Zaburi 39:6.

Wahamaji wengi ni washairi na wanapenda mashindano ya mashairi labda kwa sababu ya kuchochewa na mazingira yao. Pia wanapenda sana hadithi na methali. Kwa upande wangu, ninanukuu baadhi ya methali za Maandiko Matakatifu zilizojaa hekima kamilifu ya “Yeye anayetandaza mbingu kama shashi bora, anayezitandaza kama hema la kukaliwa ndani.” (Isaya 40:22) Wakati wangu wa kuondoka umewadia. Nawashukuru sana wakaribishaji wangu kwa ukarimu wao na ninajiuliza ni lini nitarudi tena kwenye “hoteli hiyo ya hali ya juu.”

[Picha katika ukurasa wa 26]

Keki zikipikwa katika joko la udongo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Musée du Sahara à Douz, avec l’aimable autorisation de l’Agence de mise en valeur du patrimoine et de promotion culturelle de Tunisie; camels: ZEFA/ROBERTSTOCK.COM