Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Hesabu Nilifurahia kusoma makala “Hesabu Huwafaidi Watu Wote.” (Mei 22, 2003) Sikuzote nimevutiwa na hesabu. Kama mlivyosema, Yehova ndiye Mhisabati Mkuu, na hapana shaka kwamba katika ulimwengu mpya sote tutajifunza mengi kuhusu hesabu. Asanteni sana kwa habari hiyo muhimu.
G. C., Uingereza
Makala hiyo ilinisaidia sana. Hesabu ndilo somo ninalochukia zaidi shuleni. Hata nikiwa makini mwalimu anapofundisha, siwezi kuelewa. Lakini baada ya kusoma makala hiyo, naona sasa ninaweza kuelewa hesabu. Asanteni kwa kuchapisha makala hiyo. Nina umri wa miaka 13.
Y. I., Japan
Makala hiyo ilinifaa sana! Nina umri wa miaka 15 na sijui hesabu sana. Ninapofanya mtihani wa hesabu, mimi hujiambia, ‘Hesabu haitanisaidia nitakapokuwa mtu mzima, hivyo hakuna haja ya kujifunza hesabu.’ Hata hivyo, baada ya kusoma makala hiyo, naona kwamba hesabu itanisaidia kwa njia nyingi. Kwa hiyo sasa nimeamua kujitahidi na sitakata tamaa. Tafadhali endeleeni kuchapisha makala nyingine kama hizo!
M. N., Japan
Minyoo Nilifurahia vibonzo vyenye kuchekesha katika makala “Minyoo wa Ajabu.” (Mei 8, 2003) Vinanisaidia kukumbuka yaliyosemwa katika makala hiyo.
M. Z., Italia
Nina umri wa miaka 11, na nimekuwa nikijiuliza kwa nini minyoo huteleza, lakini sasa ninajua sababu. Nilifikiri kwamba kuna aina moja tu ya mnyoo. Sikujua kuna zaidi ya aina 1,800 za minyoo! Endeleeni kuandika makala zenye kuelimisha kama hiyo.
T. C., Marekani
Kujeruhiwa Asanteni kwa makala “Jinsi Maisha Yangu Yalivyobadilika Nilipojeruhiwa.” (Aprili 22, 2003) Hisia zangu zinafanana na zile za Ndugu Ombeva kabisa. Ninaugua ugonjwa wa misuli na magonjwa mengine, na wakati mwingine mimi hupatwa na maumivu makali sana hivi kwamba mimi hulia. Imenibidi nimtumaini Yehova kabisa ili anipe nguvu za kuvumilia. Kama Ndugu Ombeva alivyosema, kuyatafakari maandiko yenye kufariji ni msaada mkubwa. Mume wangu pia amenitegemeza sana wakati wa taabu. Asanteni kwa makala kama hizo.
C. F., Marekani
Mume wangu ana matatizo ya mgongo kwa sababu aliumia kazini. Sisi pia tulikabili hisia zisizofaa kama zile ambazo Ndugu Ombeva alipambana nazo. Tulihuzunishwa sana na hali hiyo ambayo hatungeweza kuizuia. Nilisikia uchungu sana moyoni kuona jinsi mume wangu alivyokuwa na maumivu mengi na singeweza kufanya lolote kuyapunguza. Miaka miwili imepita sasa na bado yeye hupata maumivu lakini si kama hapo awali. Wakati huo wenye magumu, Yehova alituimarisha na anaendelea kutuhangaikia kwa upendo kupitia makala kama hiyo. Asanteni sana!
A. S., Marekani
Vijana Huuliza Nina umri wa miaka 16 na niko katika kidato cha kwanza. Ninapatwa na magumu ambayo sijawahi kupata. Nimeathiriwa sana na marika. Makala za “Vijana Huuliza” zimenisaidia kutambua umuhimu wa kusoma na kujifunza Biblia. Nathamini sana jinsi mnavyowahangaikia vijana, nami huhisi kwamba msaada mnaotoa hunilenga!
S. R., Marekani