Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Majengo ya Kale Yenye Jina la Mungu

Majengo ya Kale Yenye Jina la Mungu

Majengo ya Kale Yenye Jina la Mungu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SLOVENIA

Kwa karne nyingi, makanisa na nyumba za watawa zilijengwa milimani kotekote Ulaya. Majengo hayo yana kuta pana na nzito, tao zilizopindwa za tangu Zama za Kati na mitindo maridadi ya karne za baadaye. Kwa kupendeza, ndani ya majengo hayo mna Tetragramatoni—zile herufi nne za Kiebrania zinazowakilisha jina la Mungu.

Kwa mfano, fikiria Stična, mojawapo ya majengo ya watawa ya kale zaidi ya utaratibu wa Cistercian, lililoko nchini Slovenia. Lilijengwa mwaka wa 1135, miaka 40 hivi baada ya utaratibu wa watawa wa Cistercian kuanzishwa nchini Ufaransa. Ingawa jengo hilo limebadilishwa mara nyingi, bado lina mtindo wa awali wa karne ya 9 na madoido ya karne za baadaye. Sehemu ya ndani imepambwa kwa michoro na sanamu. Madhabahu ya upande mmoja yamerembwa kwa herufi kubwa za dhahabu za Tetragramatoni na kuzungushiwa pete ya fedha.

Mji wa Slovenj Gradec unatajwa kwa mara ya kwanza katika maandishi ya karne ya kumi. Hospitali ya kanisa ya Kigothi ilijengwa huko mwaka wa 1419. Ukuta wote wa ndani umepambwa kwa picha ya karne ya 15 inayoonyesha mandhari 27 za Biblia. Picha ya kwanza ni ya ufufuo wa Lazaro na ya mwisho ni ya Pentekoste. Katika sehemu nyingine ya jengo hilo, jina la Mungu limeandikwa kwa maandishi meusi ya Kiebrania kwenye rangi ya dhahabu.

Mji wa Radovljica uko katika eneo la kaskazini-magharibi la nchi. Katika karne ya 15, eneo hilo dogo lilizungukwa na kuta na handaki, na lilikuwa na kasri, kanisa, na majengo mengine. Bamba la dhahabu katika madhabahu moja ya kanisa lina Tetragramatoni.

Karibu na kijiji kidogo cha Podčetrtek, kuna nyumba ya watawa ya tangu karne ya 17. Ukichunguza kwa makini ndani ya nyumba utaona jina la Mungu kwenye picha.

Tetragramatoni inapatikana katika majengo mengine mengi ya kale ya Slovenia. Hivyo, watalii wanapofurahia ufundi na sanaa za kale, wanaweza kuona kwamba wakazi wa kale wa huko walijua jina la Mungu.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Madhabahu ya nyumba ya watawa ya Stična

[Picha katika ukurasa wa 31]

Ndani ya kanisa la Sveti Duh huko Slovenj Gradec

[Hisani]

Slovenj Gradec - Cerkev Sv. Duha, Slovenija