Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Muujiza wa Namaqualand wa Kila Mwaka

Muujiza wa Namaqualand wa Kila Mwaka

Muujiza wa Namaqualand wa Kila Mwaka

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

Maua ya rangi mbalimbali yamepamba sehemu zote za uwanda. Mara nyingi wageni husisimuka sana wanapoona muujiza wa kila mwaka wa Namaqualand. Mtalii mmoja anasema: “Nilipoona maua hayo kwa mara ya kwanza, nilifikiri ni lava inayotiririka kutoka kwenye mashimo, na kurembesha kila sehemu kwa rangi ya machungwa inayong’aa.”

Lakini ni nini ambacho hufanya maua hayo yapendeze wakati yanapochipuka? Namaqualand ni eneo kubwa lenye ukame kwenye pembe ya kaskazini-magharibi ya Afrika Kusini. Mto Orange unapita upande wa kaskazini wa eneo hilo mbele ya milima. Eneo la Namaqualand ni kubwa kuliko Uswisi (karibu kilometa 50,000 za mraba) na linafika umbali wa kilometa 200 hivi kusini, zaidi ya nusu ya umbali wa kufika Cape Town. Katika miezi mingi, joto la eneo hilo kame hufikia nyuzi 40 Selsiasi wakati wa mchana na nyuzi 8 Selsiasi chini ya kipimo cha mgando wakati wa usiku. Kwa kuwa eneo la Namaqualand halina mito mingi na maji ya chini ya ardhi, halipendezi isipokuwa wakati wa muujiza wa kila mwaka!

Kila mwaka mara tu baada ya mvua, mwanzoni mwa Agosti mpaka katikati ya Septemba, nyanda kame za Namaqualand huchipua maua mengi kwa ghafula. Mashamba huota maua ya rangi ya machungwa, manjano, waridi, nyeupe, nyekundu, buluu, na zambarau. Kwa kuwa maua hayo huwepo kwa majuma machache tu kila mwaka, wageni kutoka sehemu zote za ulimwengu huwa wametarajia kipindi hicho kwa hamu ili watazame maua hayo maridadi.

Maua hayo huchipuka kwa sababu ya mvua na mwangaza wa kutosha wa jua. Kisha watu hutamani pepo za mashariki zisivume, kwa kuwa zitanyausha maua hayo na kuyafanya yasiwe maridadi.

Muujiza huo wa Namaqualand pia hutokana na wingi wa mbegu zinazozalishwa. Hata hivyo, maua mengi hayachipuki kila mwaka isipokuwa tu hali ya hewa iwe nzuri. Ingawa mbegu nyingine huota baada ya mwaka mmoja, nyingine huota baada ya misimu kadhaa kukiwa na hali zinazofaa kwa ajili ya ukuzi. Mgeni mmoja anasema: “Mbegu nyingine hulindwa na utaratibu fulani unaozizuia kuota kabla ya kukomaa. Badala ya kuchipuka mvua inaponyesha mara moja wakati wa kiangazi, mbegu hizo huota wakati wa baridi na unyevu, hali ambazo huziwezesha kukua na kunawiri katika eneo hilo kavu.”

Ikitegemea kiasi cha mvua na kusipokuwa na pepo kali, maua huchipuka kwa njia tofauti kila mwaka, huku miaka mingine kukiwa na maua yenye kupendeza kuliko miaka mingine. Kitabu Namaqualand—South African Wild Flower Guide, kinasema: “Kwa kuwa kila aina ya maua inahitaji kiasi tofauti cha joto ili iote, na mvua huanza kunyesha kati ya Aprili na Julai (miezi ambayo huwa na kiasi tofauti cha joto) aina tofauti-tofauti huota kila mwaka, ikitegemea wakati mvua inapoanza.”

Kuna maua ya kila aina—zaidi ya aina 4,000, na kila moja lina muundo, rangi, na njia tofauti ya kuota! Katika sehemu fulani, mtu anaweza kuona aina 10 mpaka 20 za maua katika eneo la meta moja ya mraba. Eneo hilo lenye kupendeza ni maridadi kuliko mchoro mzuri sana wenye rangi mbalimbali. Hata maneno makubwa hayatoshi kuelezea umaridadi wa Namaqualand.

Wasanii, washairi, na waandishi huchochewa na maua hayo yenye kustaajabisha. Mshairi wa Afrika Kusini, D. J. Opperman, alisema: “Ilikuwa siku kubwa ya kupanda mbegu duniani ambapo . . . mfuko bora wa Bwana ulitoboka na mbegu za thamani zikamwagika.” Mtu mmoja aliyevutiwa sana aliandika hivi: “Ni kana kwamba upinde wa mvua ulipitia jangwani na kuacha rangi kila mahali.” Mgeni mmoja alisema: “Uzuri huo usio na kifani humfanya mtu athamini ukarimu na hekima nyingi ya Muumba wetu, Yehova.”

Zaidi ya yote, umaridadi wa muujiza wa kila mwaka wa Namaqualand unatuhakikishia kwamba Muumba anaweza kutumia taratibu za uumbaji kurudisha Paradiso duniani pote ili watumishi waaminifu na wenye shukrani waifurahie milele. (Zaburi 37:10, 11, 29) Kisha, duniani pote, “jangwa litafurahi na kuchanua maua.”—Isaya 35:1, Biblia Habari Njema.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mashamba makubwa yenye ukubwa wa kilometa 50,000 za mraba huchanua maua