Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wazee Wahalifu

Gazeti The Sunday Times la London linaripoti hivi: “Kitengo cha kwanza cha gereza la Uingereza kilichoundwa kipekee kwa ajili ya wazee wahalifu kimefunguliwa kwa sababu ya ongezeko la wazee wahalifu.” Kitengo hicho cha gereza la jiji la Portsmouth kina lifti, vifaa vya kufanya mazoezi vilivyorekebishwa, na wafanyakazi waliofundishwa kuwatunza wagonjwa. Uchunguzi unaonyesha kwamba wazee zaidi ya 100,000 “wameingilia—au wanafikiria—kufanya uhalifu” ili waongezee mapato wanayopata kutoka kwa serikali na malipo ya uzeeni. Wengine wameanza kuuza dawa za kulevya, kuiba madukani, kuingiza sigara na pombe kimagendo nchini Uingereza, na hata kuiba benki. Mnamo mwaka wa 1990, wazee 355 walifungwa gerezani, lakini katika mwaka wa 2000 idadi hiyo iliongezeka hadi 1,138. Mtaalamu wa uhalifu, Bill Tupman asema kwamba wengi wao hawakuwahi kuiba hapo awali lakini ‘wanataka sana kudumisha kiwango chao cha maisha. Hawa si wazee wenye mapato ya chini zaidi bali wenye mapato ya kadiri ambao walifanya kazi kwa bidii, wananchi waliotii sheria katika maisha yao yote.’

Jinsi Sili-Jike Humtambua Mtoto Wake

Sili-jike wanaporejea nyumbani baada ya majuma mengi ya kulisha baharini, ni lazima wao na watoto wao watambuane katikati ya kundi kubwa lenye kelele la mamia ya sili wakubwa na watoto. Wao hufanyaje hivyo? Kulingana na gazeti The Vancouver Sun la Kanada, “watoto hujifunza kuwatambua mama zao siku mbili tu baada ya kuzaliwa na akina mama hujifunza haraka kutambua mlio wa watoto.” Gazeti Sun linasema kwamba uchunguzi uliofanywa kwenye Kisiwa cha Amsterdam katika Bahari ya Hindi ulionyesha kwamba “mama na mtoto wanaweza kutambuana dakika saba tu baada ya mama kurudi kutoka safari yake ya baharini.” Dakt. Isabelle Charrier, aliyefanya uchunguzi huo anasema hivi: “Mama humlisha mtoto wake tu na anaweza kuwa mkali sana kuwaelekea wengine, hivyo ni muhimu sana mtoto amtambue mama yake.”

Kichina cha Mandarin na Ubongo

Hivi majuzi, mwanasaikolojia Dakt. Sophie Scott na wenzake huko London na Oxford walitumia picha za ubongo kuchunguza sehemu za ubongo zinazotumiwa kuelewa usemi. Watafiti waligundua kwamba watu wanaosema Kiingereza wanaposikia Kiingereza, kiungo fulani upande wa kushoto huanza kutenda. Lakini, kulingana na gazeti The Guardian, “watu wanaosema Kichina cha Mandarin wanaposikia lugha hiyo ikisemwa, viungo vya kulia na kushoto hutenda kwa haraka.” Kwa nini? Gazeti hilo linaeleza kwamba ‘kiungo cha kushoto huunganisha pamoja sauti ili kufanyiza maneno; na kile cha kulia hufanyiza nyimbo na lafudhi. Katika lugha ya Mandarin, maneno yaleyale yanaweza kuleta maana tofauti yakisemwa kwa sauti tofauti, kwa mfano, silabi “ma,” inaweza kumaanisha mama, kukemea, farasi au uzi wa mmea fulani,’ ikitegemea jinsi linavyosemwa. Dakt. Scott anasema hivi: “Inaonekana watu wanaosema lugha ya Mandarin hutumia kiungo cha kulia kuelewa maana ya maneno na nyimbo.”

Kushindania Jengo Refu Zaidi Duniani

Gazeti The Wall Street Journal linasema kwamba “kwa mara nyingine tena, wataalamu wa kupanga miji ulimwenguni pote wanashindana kujenga jengo refu zaidi duniani.” Tayari jengo lenye urefu wa meta 508, linalopita majengo ya Twin Towers huko New York City kwa karibu meta 90, linajengwa huko Taipei, Taiwan. Wakati huohuo, huko Shanghai, China, kuna mipango ya kujenga jengo lenye urefu wa meta 492 litakaloitwa Kituo cha Biashara Ulimwenguni. Maafisa wa Shanghai wanasema kwamba jengo hilo litakuwa refu kuliko lile la Taiwan, kwa sababu lile la Taiwan litakuwa na mnara wa kusambaza mawimbi ya televisheni wenye urefu wa meta 50. Isitoshe, huko Seoul, Korea Kusini, jengo la kituo cha biashara ya kimataifa litakuwa na urefu wa meta 540. Kisha, wengine wanapendekeza kujenga jengo refu zaidi duniani huko New York City mahali pa lile lililobomolewa katika mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11. Gazeti hilo linasema hivi: “Haingefikiriwa kwamba mashindano ya kujenga majengo marefu zaidi yangerejea haraka hivi baada ya mashambulizi ya mwaka wa 2001.”

Vijana Wenye Hasira Huhatarisha Moyo

Gazeti The Gazette la Montreal linaripoti hivi: “Wachunguzi wamegundua kwamba watoto na vijana wenye hasira kali wana uwezekano wa karibu mara tatu zaidi wa kupata ugonjwa fulani kuliko wale ambao hawana hasira kali—hali inayoweza kusababisha ugonjwa wa moyo.” Watafiti Wamarekani na Wafini waliochunguza viwango mbalimbali vya hasira katika vijana na watoto 134, waligundua kwamba asilimia 22 ya wale wenye hasira walikuwa katika hatari ya kuugua ugonjwa wa moyo kuliko wale wasio na hasira nyingi. Dakt. Kristen Salomon, mmoja wa wale waliochapisha matokeo ya uchunguzi huo alisema hivi: “Watu hawaamki asubuhi moja na kujipata wakiugua ugonjwa wa moyo wakiwa na umri wa miaka 50. Ugonjwa wa moyo huanza mtu akiwa mdogo.”

Je, Ndiye Ndege Mzee Zaidi Nchini Uingereza?

Gazeti The Times la London linaripoti kwamba “ndege mzee zaidi nchini Uingereza bado ananawiri, akiwa na umri wa miaka 52 na amesafiri umbali wa kilometa milioni nane.” Ndege huyo mdogo mweusi na mweupe aina ya Manx shearwater, “kwanza alitiwa alama ya kumtambulisha katika Mei 1957, alipokuwa na umri wa miaka sita hivi.” Alionekana tena katika mwaka wa 1961, 1978, na 2002, na baada ya hapo wataalamu wa ndege hawakutazamia kumwona tena. Lakini katika mwaka wa 2003, ndege huyo alionekana tena katika pwani ya Wales Kaskazini. Shirika la Uingereza la Elimu ya Ndege linasema kwamba ndege huyo amesafiri umbali wa kilometa 800,000 kwenda na kurudi kutoka Amerika Kusini. Kuongezea safari zake za kawaida za kulisha za kilometa 1,000, wanasayansi wanasema kwamba amesafiri zaidi ya kilometa milioni nane. Graham Appleton wa Kituo cha Kuchunguza Ndege cha Bardsey huko Wales Kaskazini anasema hivi: “Ndege huyo mzee ametiwa alama ya kumtambulisha mara nne; ambalo tena ni jambo la kushangaza. Alama zile nyingine zote zilikuwa zimechakaa.”

Vipindi vya Watoto vya Televisheni Vinatoweka Hispania

Gazeti la kila siku la Hispania, El País, linasema kwamba “vipindi vya televisheni vya alasiri vya watoto vinatoweka.” Manuel Cereijo, msemaji wa Kituo cha Kitaifa cha Televisheni cha Hispania, anasema kwamba “watoto si watazamaji wa kawaida wa televisheni hivi kwamba wawe na vipindi vyao wakati wa alasiri.” Hata hivyo, jambo hilo halimfurahishi Lola Abelló, mkurugenzi wa Chama cha Wanafunzi na Wazazi cha Hispania, ambaye anasema hivi: “Watoto hutazama kipindi chochote ambacho wanaletewa.” Ripoti hiyo inasema kwamba mtoto mmoja kati ya 3 nchini Hispania ana televisheni katika chumba chake cha kulala, hivyo watoto wenye umri wa miaka 4 hadi 12 hawaongei kuhusu katuni tena bali wanaongea kuhusu waimbaji mashuhuri na vipindi vya watu wazima. Abelló anasema kwamba “jambo hilo linasikitisha kwani watoto hawaishi maisha ya utotoni tena. Wanatazama habari za watu wazima wakiwa wachanga mno.”