Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wanapenda Fataki

Wanapenda Fataki

Wanapenda Fataki

FATAKI hulipuliwa wakati wa sherehe za kufungua maonyesho ya kilimo au Michezo ya Olimpiki. Mng’ao na rangi za fataki huonekana wakati wa kuadhimisha Siku ya Uhuru nchini Marekani, Siku ya Bastille nchini Ufaransa, na Mkesha wa Mwaka Mpya katika karibu kila jiji kubwa ulimwenguni.

Hata hivyo, wanadamu walianza kupendezwa na fataki lini? Na ni maarifa gani yanayotumiwa kutengeneza fataki maridadi?

Ni Desturi ya Mashariki

Wanahistoria wengi wanakubali kwamba Wachina walibuni fataki katika karne ya kumi hivi ya Wakati wetu wa Kawaida, wakati ambapo wanakemia wa Mashariki walipogundua kwamba kuchanganya nitrati ya potasiamu pamoja na salfa na makaa hutokeza kemikali inayolipuka. Wavumbuzi wa Magharibi kama vile Marco Polo, na labda wafanyabiashara Waarabu ndio waliopeleka kemikali hiyo Ulaya, na kufikia karne ya 14 watu wengi huko Ulaya walikuwa wanaitumia kuwatumbuiza watu.

Lakini kemikali hiyo iliyowafurahisha wengi ilibadili pia maisha ya watu wa Ulaya. Wanajeshi walitumia unga wa risasi kufyatua risasi, kulipua kuta za kasri, na kuangusha serikali zenye nguvu. Kitabu Encyclopædia Britannica kinasema: “Katika Zama za Kati huko Ulaya, vilipukaji vilivyotumiwa na wanajeshi vilipopelekwa Magharibi, fataki pia zilipelekwa, na katika Ulaya, mtaalamu wa kulipua vilipukaji alipaswa kulipua fataki wakati wa sherehe za ushindi na za amani.”

Wakati huohuo, ni kana kwamba Wachina hawakutaka sana kutumia unga wa risasi kutengeneza silaha. Katika karne ya 16, Matteo Ricci, mishonari Mjesuti Mwitaliano aliyekuwa huko China, aliandika hivi: “Wachina hawajui kutumia bunduki wala mizinga mikubwa na hawaitumii sana vitani. Hata hivyo, nitrati ya potasiamu hutumiwa sana kutengeneza fataki kwa ajili ya michezo na sikukuu. Wachina wanapenda sana maonyesho hayo . . . Ama kweli, wao ni wataalamu wa kutengeneza fataki.”

Siri ya Kutengeneza Fataki

Watengenezaji wa mapema wa fataki walihitaji ustadi na ujasiri walipotengeneza fataki mbalimbali. Waligundua kwamba chembe kubwa za unga wa risasi huungua polepole na kwamba chembe ndogo hulipuka sana. Roketi zilitengenezwa kwa kuziba ncha moja ya mti wa mwani au karatasi iliyosokotwa na kuingiza chembe kubwa za unga wa risasi kwenye sehemu ya chini. Unga wa risasi ulipowashwa moto, gesi zilizopanuka haraka zilisukumwa kutoka kwenye upande ulio wazi wa roketi na kuirusha angani. (Kanuni hiyo ya msingi hutumiwa leo kuwasafirisha watu angani.) Ncha ya juu ya roketi ilijazwa chembe ndogo za unga wa risasi ili roketi ilipuke wakati ilipofikia kikomo chake cha kuruka.

Muundo wa fataki haujabadilika sana. Hata hivyo, fataki zimeboreshwa. Hapo awali watu wa Mashariki walijua tu kutengeneza fataki nyeupe na za rangi ya dhahabu. Waitaliano walitengeneza fataki zenye rangi mbalimbali. Mwanzoni mwa karne ya 19, Waitaliano walichanganya klorati ya potasiamu na unga wa risasi na kugundua kwamba mchanganyiko huo ulibadili vyuma kuwa gesi na kutokeza mng’ao wenye rangi. Leo kabonati ya strontiamu huongezwa ili kutokeza mng’ao mwekundu. Mng’ao mweupe mwangavu hutokezwa na titani, alumini, na magnesi; mng’ao wa buluu hutokezwa na kemikali za shaba-nyekundu; mng’ao wa kijani hutokezwa na nitrati za bari; na mng’ao wa manjano hutokezwa na mchanganyiko wenye oksalati ya sodiamu.

Kompyuta pia zimeboresha tamasha za kulipua fataki. Badala ya kuwasha fataki kwa mkono, wataalamu wanaweza kupima tamasha zao kwa usahihi kwa kuwasha fataki kwa kutumia kompyuta ili zilipuke kufuatana na mdundo wa muziki.

Matumizi ya Kidini

Kama yule mishonari Mjesuti anayeitwa Ricci alivyosema, fataki zilitumiwa sana katika sherehe za kidini za Wachina. Gazeti Popular Mechanics linaeleza kwamba fataki “zilibuniwa na Wachina kufukuza mashetani kutoka kwenye sherehe za Mwaka Mpya na sherehe nyingine.” Katika kitabu chake Days and Customs of All Faiths, Howard V. Harper anasema: “Tangu zama za kale za upagani, watu wamebeba mienge na kuwasha mioto mikubwa wakati wa sikukuu zao za kidini. Si ajabu kwamba tamasha maridadi za kulipua fataki zenye kumeremeta zilihusishwa katika sikukuu hizo.”

Muda mfupi baada ya fataki kuanza kutumiwa na watu waliodai kuwa Wakristo, watengenezaji wa fataki walianza kupewa watakatifu wao. Kitabu The Columbia Encyclopedia kinasema hivi: “Inasemekana baba ya [Mtakatifu Barbara] alimfungia [Barbara] ndani ya mnara na kumuua kwa sababu alikuwa Mkristo. Kwa kuwa mzee huyo alipigwa na radi akafa, Mtakatifu Barbara akawa mtakatifu wa watu wanaotengeneza na kutumia bunduki na fataki.”

Pesa Nyingi Zinatumiwa

Iwe ni kwa ajili ya sherehe za kidini au za kilimwengu, watu wanapenda sana tamasha kubwa zaidi za kulipua fataki na fataki zinazotoa ming’ao maridadi zaidi. Akifafanua tamasha moja ya fataki nchini China katika karne ya 16, Ricci aliandika hivi: “Nilipokuwa Nankin, niliona tamasha ya fataki wakati wa kuadhimisha mwezi wa kwanza wa mwaka, ambayo ndiyo sherehe yao kubwa zaidi, na wakati huo nilikadiria kwamba walitumia unga wa risasi ambao ungeweza kutumiwa katika vita vikubwa kwa miaka kadhaa.” Alisema hivi kuhusu gharama ya fataki hizo: “Ni kana kwamba hawajali wanatumia pesa ngapi kwa ajili ya fataki.”

Mambo hayajabadilika sana tangu wakati huo. Katika sherehe moja iliyofanywa kwenye Daraja la Bandari ya Sydney mwaka wa 2000, tani 20 za fataki zililipuliwa ili kuwatumbuiza watazamaji milioni moja au zaidi waliokusanyika kando ya bandari. Pia, katika mwaka huo, dola milioni 625 zilitumiwa kutengeneza kilogramu milioni 70 hivi za fataki nchini Marekani. Bila shaka, watu wa tamaduni nyingi wangali wanapenda fataki, na bado inaweza kusemwa kuwa “ni kana kwamba hawajali wanatumia pesa ngapi kwa ajili ya fataki.”

[Picha katika ukurasa wa 23]