Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Yaani Kunanyesha Tena?

Yaani Kunanyesha Tena?

Yaani Kunanyesha Tena?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI IRELAND

“Ah! Yaani kunanyesha tena?”

Je, umewahi kusema hivyo? Tuseme ilitukia hivyo wakati wa kiangazi ukiwa kwenye sehemu maridadi ya Pwani ya Bahari ya Atlantiki huko Ireland. Huenda ulitamani kuwe na jua ili ufurahie mandhari hayo maridadi, lakini kukawa na pepo kali na mvua kubwa. Wakati huo ni rahisi kusahau kwamba mvua ni baraka. Bila mvua, sisi wala mandhari hayo maridadi hayangekuwapo kamwe!

Baada ya mvua kubwa kunyesha, mvua hunyesha tena na tena. Kwa nini? Kwa sababu ya mzunguko wa ajabu wa maji. Kuchunguza kwa ufupi hatua tatu muhimu za mzunguko huo unaoendeleza uhai, yaani mvukizo, mtonesho, na mvua, hutuonyesha kwamba huo si mfumo uliofanyizwa kiholela. Kitabu kimoja kinaeleza kwamba ni utaratibu tata unaofuata “sheria zisizobadilika.”

Mvukizo

Karibu asilimia 97 ya maji duniani yanapatikana baharini. Maji yaliyosalia yanapatikana katika mito ya barafu, maziwa, na visima vya chini ya ardhi. Bila shaka, hatuwezi kunywa maji ya bahari. Kama vile yule baharia mwenye taabu alivyosema katika shairi linaloitwa “Shairi la Baharia wa Kale,” * baharini kuna ‘maji, maji, kila mahali, lakini hakuna hata tone moja la kunywa.’

Kabla maji ya baharini yaweze kunywewa, hatua nyingi huhusika. Kwanza yanakuwa mvuke. Joto la jua huvukiza maji yanayotoshea kilometa 400,000 za mchemraba kutoka nchi kavu na baharini kila mwaka. Nyakati za kale, mtu mmoja aliyeitwa Elihu alimsifu Mungu kwa kutokeza utaratibu huo akisema: “Yeye huyavuta kwake maji ya bahari, na kutoka ukungu hufanya matone ya mvua.”—Ayubu 36:27, Biblia Habari Njema.

Angahewa ni “eneo tata sana,” lenye urefu wa zaidi ya kilometa 400. Maji ya mvua hufanyizwa kilometa 10 mpaka 20 kutoka duniani. Kitabu Our Fragile Water Planet hufafanua sehemu hiyo kuwa “eneo linalopakana na uso wa dunia, lenye mawingu, mvua, theluji, tufani, na vimbunga.”

Hewa hubeba maji mengi zaidi kadiri inavyokuwa na joto jingi zaidi. Ndiyo sababu nguo zilizooshwa hukauka haraka siku yenye joto na upepo. Angahewa la maeneo ya tropiki ndilo lenye maji mengi zaidi. Kwa hiyo huenda ukauliza, ‘Maji hayo yote hufikaje kwenye maeneo mengine ambako yanahitajiwa?’ Ni kupitia pepo kali zinazozunguka dunia. Pepo hizo hufanyizwa kutokana na jinsi ambavyo dunia inazunguka mhimili wake na kwa sababu sehemu fulani za dunia hupata joto jingi kuliko nyingine, hivyo angahewa huwa na upepo daima.

Angahewa lina makundi makubwa ya hewa. Makundi hayo ya hewa huwa na karibu kiwango kilekile cha joto. Ni makubwa kadiri gani? Yanaweza kufikia ukubwa wa kilometa milioni kadhaa za mraba. Makundi ya hewa yenye joto hufanyizwa kwenye maeneo ya Tropiki, na yale yenye hewa baridi hufanyizwa kwenye maeneo ya Aktiki na Antaktiki. Makundi hayo ya hewa husafirisha maji mengi katika angahewa.

Ubuni mwingine wa ajabu ni jinsi ambavyo mvuke husonga katika angahewa. Mvuke huondoa joto kutoka kwenye maeneo yenye joto jingi, kama vile maeneo ya Tropiki, hadi maeneo yenye baridi. La sivyo, joto lingeendelea kuongezeka zaidi na zaidi katika maeneo fulani ya dunia.

Mtonesho

Naam, mvuke ni muhimu katika angahewa, lakini ikiwa ungebaki huko juu haungetufaidi. Kwa mfano, angahewa la Jangwa la Sahara lina mvuke mwingi sana, lakini eneo hilo ni kame. Mvuke hurudi duniani kwa njia gani? Kwanza, hubadilika na kuwa maji.

Unapochemsha maji kwenye sufuria iliyofunikwa, mvuke hubadilika kuwa matone ya maji unapofika kwenye kifuniko kilicho baridi. Jambo hilohilo hutukia hewa inapopoa wakati inapoendelea kupaa kwenye maeneo yenye baridi. Ni nini hufanya hewa ipae? Hilo linaweza kutukia wakati kundi la hewa yenye joto linapoinuliwa juu zaidi na kundi la hewa baridi lililo zito zaidi. Wakati mwingine hewa husukumwa juu na milima. Nyakati nyingine, hasa katika maeneo ya tropiki, hewa baridi huinua hewa yenye joto.

Huenda ukauliza, ‘Lakini, mvuke unapopoa unajikusanya wapi?’ Angahewa lina chembechembe nyingi ndogo sana kama za moshi, vumbi, na chumvi ya bahari. Mvuke unapopoa, unafanyiza matone ya maji kwenye chembechembe hizo. Kisha matone hayo madogo ya maji hufanyiza mawingu.

Hata hivyo, maji hayo hayaanguki mara moja duniani. Kwa nini? Labda unajiuliza hilo linawezekanaje kwani uzito wa maji unazidi uzito wa hewa mara 800. Hiyo ni kwa sababu kila tone la maji ni dogo na jepesi sana hivi kwamba linaweza kuelea hewani. Elihu, aliyetajwa mapema, alistaajabishwa na jambo hilo la kupendeza kuhusu mzunguko wa maji alipoeleza jinsi “mawingu yanavyoelea angani” na kusema kwamba ni “kazi za ajabu za yule [Muumba] aliye mkamilifu wa maarifa!” (Ayubu 37:16, BHN) Je, hushangazwi kujua kwamba wingu dogo jepesi linaloelea angani linaweza kuwa na tani 100 mpaka 1,000 za mvuke?

Mvua

Mawingu mengi hayatokezi mvua. Ni rahisi kueleza jinsi maji yanavyofanyizwa kwenye angahewa na jinsi mawingu yanavyoelea angani. Lakini mwandishi mmoja anasema “ugumu ni kueleza jinsi maji yanavyorudi chini” tena.—The Challenge of the Atmosphere.

Tone moja la mvua linaweza kufanyizwa na “matone ya mawingu milioni moja au zaidi.” Inaonekana hakuna anayejua kabisa jinsi matone hayo madogo ya mawingu hufanyiza tani bilioni moja hivi za maji zinazoanguka duniani kila dakika na kila siku. Je, matone ya mawingu huungana na kufanyiza matone makubwa ya mvua? Nyakati nyingine yanafanya hivyo. Jambo hilo linaelezea jinsi matone ya mvua hufanyizwa katika maeneo fulani kama vile ya Tropiki. Lakini halielezei “fumbo la jinsi ambavyo matone ya mvua hufanyizwa” katika maeneo mengine kama vile Pwani ya Bahari ya Atlantiki huko Ireland.

Katika eneo hilo, matone ya mawingu hayaungani tu, bali yanafanyiza madonge madogo ya barafu kwa njia zisizoeleweka. Madonge hayo huungana na kufanyiza “mojawapo ya vitu vya ajabu zaidi vya uumbaji,” yaani, chembe za theluji. Chembe za theluji huanguka duniani zinapokuwa kubwa na nzito kuliko pepo zinazoinuka. Kunapokuwa na baridi sana, mabilioni ya chembe hizo huanguka zikiwa theluji. Lakini zinapopitia kwenye hewa yenye joto, chembe hizo za theluji huyeyuka na kufanyiza matone ya maji. Hivyo, mvua ya theluji haifanyizwi na matone ya maji yaliyoganda. Badala yake, mvua nyingi inayonyesha katika maeneo yenye joto la wastani huanza ikiwa theluji, kisha huyeyuka inapokuwa ikinyesha.

Kwa hiyo baada ya maji kusafiri maelfu ya kilometa na kupitia hatua nyingi tata ambazo kwa sasa hazieleweki vizuri, mvua hunyesha tena. Ni kweli kwamba mara kwa mara mvua inaweza kuathiri mipango na shughuli zako. Lakini mfumo huo wa kuvutia hutuwezesha tupate maji sikuzote. Ama kweli, mvua ni baraka. Hivyo, unapogongwa na tone la mvua usoni, hapana shaka utathamini zawadi hiyo kutoka kwa Mungu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Lililoandikwa na mshairi Mwingereza Samuel Taylor Coleridge.

[Sanduku/Mchoro katika ukurasa wa 14]

Jinsi Mvua ya Mawe Hufanyizwa

Kitabu Weather kinasema kwamba “mvua ya mawe hutokezwa kiajabu na mawingu makubwa ya ngurumo na radi.” Matone ya maji yanapofanyizwa kwenye chembe ndogo za mawingu ya ngurumo na radi, nyakati nyingine hewa inayoinuka huyasukuma kwenye sehemu zenye baridi zaidi za wingu. Katika hali hizo zenye baridi, matone mengine huungana na tone hilo la mvua na kuganda mara moja. Utaratibu huo hujirudia-rudia na tone la mvua lililoganda husonga-songa juu na chini ya wingu hilo. Kila mara, tone hilo lililoganda hupata tabaka jipya la barafu na kuwa zito zaidi, likizidi kupata matabaka kama ya kitunguu. Mwishowe, tone hilo huwa zito sana hivi kwamba haliwezi kuinuliwa tena na hewa iliyo katika wingu. Hivyo, linaanguka duniani likiwa jiwe la mvua. Kitabu Atmosphere, Weather and Climate, kinasema: “Wakati mwingine, kila jiwe katika mvua ya mawe linaweza kuwa kubwa sana, likiwa na uzito wa kilogramu 0.76.”

[Mchoro]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

mvua ya mawe

↑ hewa inayoinuka

eneo la mgando .........................

↓ hewa inayoshuka

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

Je, Ulijua?

Kwa wastani, maji yaliyo kwenye angahewa ulimwenguni pote yanatosha mvua ya karibu siku kumi tu.

Ngurumo moja ya radi wakati wa kiangazi inaweza kutoa nishati mara kumi na mbili zaidi ya nishati ya bomu lililolipuka huko Hiroshima wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Ngurumo 45,000 hivi za radi hutukia kila siku duniani.

Angahewa halipashwi joto moja kwa moja na jua. Sehemu kubwa ya joto hupenya angahewa hadi duniani. Joto linalorudi kutoka duniani ndilo hupasha joto angahewa.

Maji ndicho kitu ambacho hupatikana kwa wingi duniani na wakati uleule kupatikana katika namna tatu tofauti, yaani yakiwa barafu, majimaji, na mvuke.

Ukungu ni wingu linalotokea ardhini.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Asilimia 97 ya maji ya dunia yanapatikana baharini

Joto la jua huvukiza maji

Mvuke hubadilika kuwa matone na kufanyiza mawingu

Matone ya mvua na chembe za theluji yanapatikana baharini

Matone ya mvua na theruji