Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutembelea Maporomoko Makubwa ya Maji

Kutembelea Maporomoko Makubwa ya Maji

Kutembelea Maporomoko Makubwa ya Maji

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ZAMBIA

KUFIKIA mwaka wa 1855, mishonari na mvumbuzi Mskoti David Livingstone alikuwa amesafiri kwa miaka mingi barani Afrika—bara ambalo halikuwa limejulikana na watu wa mabara mengine wakati huo. Aliposafiri mashariki kwenye mto mkubwa wa Zambezi, wenyeji walisema kwa shauku kwamba kuna maporomoko makubwa ya maji mbele. Wenyeji waliyaita Mosi-oa-Tunya, yaani “Moshi Unaonguruma,” kwa sababu ya kelele na mvuke mwingi uliotokezwa nayo.

Livingstone alitaka sana kuyaona maporomoko hayo ambayo sasa yanaitwa Maporomoko ya Maji ya Victoria. Aliandika hivi baada ya kuyaona kwa mara ya kwanza: “Nilisogea polepole kwenye ncha ya korongo, nikatazama chini kwenye korongo hilo ambalo lilikuwa limeanzia ukingo mmoja hadi ukingo wa pili wa mto mpana wa Zambezi, nami nikaona mto huo wenye upana wa maelfu ya meta ukiporomoka meta 30 kisha upana wake ukapungua ukawa meta 15 au 20.”

Wakati ambapo maji yamejaa kabisa, Maporomoko ya Maji ya Victoria yaliyo katika nchi ya Zambia na Zimbabwe huonwa kuwa maporomoko makubwa zaidi duniani! Wakati huo lita 545,000,000 za maji huporomoka meta 108 kila dakika kwenye korongo kubwa. Kisha maji yote ya Mto Zambezi hupita haraka kwenye korongo lenye kina kirefu linalojipinda-pinda lisilozidi upana wa meta 65. Mandhari hayo ya pekee hufanya Maporomoko ya Maji ya Victoria yavutie kwelikweli.

Eneo linalozunguka maporomoko hayo ni maridadi sana pia. Ni sehemu ya mbuga ya kitaifa yenye miti na mimea mbalimbali ya kupendeza, na wanyama wa kustaajabisha kama vile viboko, tembo, twiga, nyumbu, punda-milia, na hata simba. Ndege maridadi kama vile tai na vipanga hujenga makao yao kwenye miamba.

Kama Livingstone alivyosema, “hakuna kitu kilicho maridadi hivyo nchini Uingereza. Hakuna Mzungu yeyote aliyekuwa ameona kitu kama hicho; lakini haikosi malaika waliona mandhari hayo ya kupendeza walipokuwa wakiruka.” Ingawa karibu miaka 150 imepita tangu Livingstone alipoyaona maporomoko hayo kwa mara ya kwanza na kuyaita Maporomoko ya Maji ya Victoria kutokana na jina la Malkia Victoria wa Uingereza, mamia ya maelfu ya watu kutoka ulimwenguni pote huyatembelea kila mwaka ili wajionee umaridadi wake.

Ama kweli, kama inavyosemwa, Maporomoko ya Maji ya Victoria ni mojawapo ya mambo ya kustaajabisha ulimwenguni. Lakini maporomoko mengi yasiyojulikana sana yaliyo kwenye mito mingi mikubwa ya Zambia, yanapendeza sana pia. Tafadhali jiunge nasi tunapotembelea baadhi yake.

Maporomoko ya Maji ya Ngonye

Siku moja yenye joto katika mwezi wa Novemba, miaka miwili hivi kabla ya kuona Maporomoko ya Maji ya Victoria kwa mara ya kwanza, Livingstone alifika kwenye Maporomoko ya Maji ya Ngonye, yanayoitwa pia Sioma. Aliandika: “Visiwa vilivyo juu ya maporomoko hayo vimefunikwa kwa majani yenye uzuri usio na kifani. Nilipokuwa kwenye mwamba unaotokeza kwenye maporomoko, mandhari hayo yalinivutia kuliko yoyote niliyowahi kuona.” Wageni wanaotembelea Maporomoko ya Maji ya Ngonye leo wanakubali maelezo hayo ya Livingstone.

Livingstone alisema: “Mto huo unapoteremka chini kwa kilometa nyingi, unapitia sehemu nyembamba isiyozidi meta mia moja. Maji hayo husukasuka na kupinduka-pinduka hivi kwamba hata mwogeleaji stadi anaweza kushindwa kuelea.”

Maporomoko ya Maji ya Lumangwe

Maporomoko mengi ya maji ya Zambia yako mbali na hayajaharibiwa na wanadamu. Yana ukubwa mbalimbali. Maporomoko ya Maji ya Lumangwe yanafanana na yale ya Victoria, ingawa ni madogo. Lakini si madogo sana. Poromoko moja la maji lina urefu wa meta 30 hivi na upana wa zaidi ya meta 100. Hata kuna msitu mdogo wa mvua unaositawi kutokana na ukungu wa poromoko hilo.

Maporomoko ya Maji ya Kalambo

Maporomoko ya Maji ya Kalambo ndiyo marefu zaidi nchini Zambia, nayo hutiririka kutoka nyanda ya juu hadi Bonde Kuu la Ufa la Afrika. Yanaporomoka kwa zaidi ya meta 200 kwenye miamba mikubwa mahali ambapo kongoti wakubwa huzaana wakati wa kiangazi.

Kitabu National Monuments of Zambia kinasema hivi: “Kalambo ndiyo maporomoko ya maji ya pili kwa urefu barani Afrika ambayo yanatiririka moja kwa moja [ya kwanza yakiwa Maporomoko ya Tugela nchini Afrika Kusini] na ya kumi na mbili kwa urefu ulimwenguni—urefu wake unazidi ule wa Maporomoko ya Victoria mara mbili.”

Ingawa ni vigumu kuyafikia maporomoko hayo, mwandishi wa huko, C. A. Quarmby, anasema kwamba Kalambo ni “mojawapo ya mandhari ya Afrika yasiyoweza kusahaulika.” Anatabiri hivi: “Itachukua muda mrefu kabla ya sehemu hiyo kutembelewa na watalii wengi. . . . Ni wachache tu wanaofanikiwa kufika Kalambo.”

Ama kwa hakika, maporomoko mengi ya maji na sehemu nyingine za kuvutia nchini Zambia ziko katika sehemu zisizofikika kwa urahisi. Kitabu National Monuments of Zambia kinasema kwamba sehemu nyingine “zilizo kwenye barabara mbovu zinaweza tu kufikiwa kwa gari aina ya Land-rover na nyingine kwa miguu.” Bila shaka, hilo linachangia kufanya sehemu hizo kuwa za pekee. Hata hivyo, wageni wanakaribishwa. Bwana Kagosi Mwamulowe, mwanajiolojia wa Tume ya Kuhifadhi Mirathi ya Kitaifa ya Zambia, anaeleza kwamba kusudi lao ni kuwawezesha watu wafurahie sehemu hizo maridadi na kuzihifadhi.

Hazina Kubwa Zaidi ya Zambia

Katika kitabu chake Zambia, mwandishi Richard Vaughan anasema hivi: “Zambia ni nchi yenye sehemu nyingi maridadi sana na nyingi hazijulikani na wageni wala Wazambia wenyewe. . . . Nchi hiyo ina maziwa, mito, misitu, na milima mbalimbali.” Lakini hazina kubwa zaidi ya nchi hiyo inapatikana kwingineko.

Vaughan anasema hivi: “Wazambia wanajulikana kwa uchangamfu, shauku, na uvumilivu wao.” Mwandishi mwingine, David Bristow, alisema kwamba “jambo la pekee zaidi kuhusu Zambia ni watu wake ambao wana joto kama jua la Afrika.” Tuna hakika kwamba utakubaliana na kauli hizo utakapotembelea sehemu hii maridadi ya ulimwengu.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 18]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

TANZANIA

JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

ANGOLA

ZAMBIA

MAPOROMOKO YA KALAMBO

MAPOROMOKO YA LUMANGWE

Lusaka

MAPOROMOKO YA NGONYE

MAPOROMOKO YA VICTORIA

ZIMBABWE

MSUMBIJI

BAHARI YA HINDI

[Picha]

Ingawa ni madogo, Maporomoko ya Lumangwe ni kama ya Victoria

Maporomoko ya Ngonye—“mara nyingi utajipata peke yako ukiwa hapa”

Maporomoko ya Kalambo yanazidi urefu wa Maporomoko ya Victoria mara mbili

[Hisani]

Lumangwe and Ngonye Falls: Marek Patzer/www.zambiatourism.com; map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Maporomoko ya Victoria—“Moshi Unaonguruma”

[Hisani]

Marek Patzer/www.zambiatourism.com